Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rorya
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninaanza kukushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi jioni ya leo kuwa mchangiaji wa kwanza katika Hotuba ya Waziri Mkuu pamoja na Taarifa za Kamati zilizo chini ya Wizara hii ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninaanza kumpongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia kwa kazi kubwa nzuri ambayo ameendelea kufanya. Kwa muda wote ambao sisi kama Wabunge tumetoka kwenye maeneo yetu, tumeona mchango mkubwa kwenye maeneo yote na nyanja zote namna alivyowagusa wananchi wanyonge hasa kwenye maeneo mbalimbali ambayo ndiyo kimbilio lao kwenye maeneo mbalimbali kulingana na taarifa zilizosomwa hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili niendelee kumshukuru sana, ninachukua nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa nzuri, namna alivyoanza katika utendaji wake. Ziara alizofanya kwenye maeneo mengi ya nchi yetu zimeacha alama kwa namna ambavyo amekuwa akitatua changamoto za wananchi hawa wanyonge ambao sasa wanaamini kimbilio peke limekuwa yeye pamoja na Wizara yote kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, ninachukua nafasi kuwapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri hasa Mawaziri wote walio chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu hususan Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Profesa Shemdoe, Naibu Mawaziri wawili pamoja na Makatibu Wakuu kwa kazi kubwa nzuri ambayo wameendelea kuifanya. Sisi kama Kamati tunajua mchango wao na namna walivyojitoa kuhudumia Wizara yetu hii ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna msemo unasema: “Mwenye macho haambiwa tazama,” tulio wengi tuna macho na tunaona kazi kubwa nzuri inayofanywa na Serikali yetu chini ya jemedari Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye leo ameweka hotuba na bajeti yake kwenye Bunge hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo mambo kadhaa kama Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI na leo nitajikita kwenye eneo moja tu la Wizara ya TAMISEMI kama sehemu ya kutoa ushauri na kuboresha taarifa yetu ambayo Mheshimiwa Mwenyekiti wetu ametoka kuiwasilisha vizuri, ameisoma hapo mbele. Nitachangia mambo kadhaa katika mazingira ya kushauri na muktadha wa kushauri Serikali ili kuweza kuyaboresha.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ni TARURA. Kwanza ninachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kama upande wa Serikali kuridhia fedha zote za Mfuko zilizokuwa zinakatwa kutoka kwenye tozo ya mafuta sasa kwenda moja kwa moja kwenye mifuko husika ili ziende zikatoe huduma TARURA. Hili ni jambo kubwa, ni jambo la kihistoria. Changamoto ya TARURA haikuwa fedha peke yake kuongezwa, pamoja na fedha kuongezwa, changamoto kubwa ya TARURA kutokufika kwenye maeneo mengi kutekeleza wajibu wao, ilikuwa ni pamoja na fedha kutokufika kwenye yale maeneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa na fedha ilikuwa haifiki kwa sababu fedha nyingi tulikuwa tukikata kwenye tozo zilikuwa haziendi moja kwa moja katika kuhudumia barabara zetu kwenye maeneo yetu. Kwa maamuzi haya ya Serikali kama itaamua sasa fedha hizi zinazokatwa kutoka kwenye mafuta, moja kwa moja ziende kuhudumia TARURA, tunaamini kabisa TARURA sasa watakuwa na uwezo wa kujipambanua na kusimamia kufanya kazi kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kiukweli kwenye hili tunaipongeza sana Serikali kwa kuliona hili na ndilo lilikuwa ni wazo na maoni ya Kamati kuona kwamba fedha hizi kwa muda mrefu TARURA wamekuwa wakilia, fedha ilikuwa inakwenda kidogo ukilinganisha na mahitaji waliyokuwa nayo. Tuipongeze sana Serikali kwa kuliona hili, lakini pia tunapongeza Serikali kwa kuridhia sasa kuongeza bajeti ya TARURA, walikuwa wanapokea shilingi 944,000,000, sasa wanakwenda kupata fedha zaidi ya shilingi bilioni 1.2 katika utekelezaji wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ongezeko hili likienda sambamba na fedha hizi zinazokatwa kutoka kwenye tozo, kwenye miradi ya mafuta, ikienda huko tunaamini changamoto za barabara kwenye maeneo mengi itakuwa ni historia. Hili sisi kama Kamati tunalipongeza sana na tunajua ni kazi kubwa nzuri ambayo inafanywa na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kutambua mchango mkubwa wa TARURA kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, liko jambo ambalo na sisi kama Kamati tumeliona. Pamoja na chanzo cha TARURA kuwa ni tozo, zipo halmashauri ambazo mwongozo wa TAMISEMI unasema, kama zinakusanya zaidi ya shilingi bilioni 10 na kuendelea, wanapaswa kupeleka 10% kuihudumia barabara zetu kwenye maeneo yetu. Sisi kama TAMISEMI, kama upande wa Kamati tumeona kwamba hili na lenyewe Wizara iisimamie Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha halmashauri na majiji yote yanayokusanya zaidi ya shilingi bilioni 10 na kuendelea wapeleke fedha hii 10% iende ikahudumie barabara za wananchi wetu kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ni upande wa matundu ya vyoo. Kwanza ninampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuliona hili na kutoa miezi sita kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kulitekeleza, lakini jambo hili ni kubwa kuliko vile tunavyolitazama. Wakati wa mapitio ya bajeti, sisi kama TAMISEMI kwenye mikoa husika, tumegundua changamoto na upungufu wa matundu ya vyoo ni zaidi ya 100,000 mpaka 150,000 kwenye maeneo yote waliyokuwa wanaleta ile tathmini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nini ushauri wetu sisi kama Kamati, tukiziachia Mamlaka ya Serikali za Mitaa peke yake waende wakatatue changamoto ile, itachukua zaidi ya miaka mitano mpaka miaka sita kutatua changamoto ya kero kwenye maeneo yetu. Nami nichukue nafasi kuwapongeza viongozi kwa kuliona hili kwa sababu si jambo jema kuendelea kuzungumza matundu ya vyoo hasa kwenye Bunge hili. Ninakupongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kuliona hili na kutoa maelekezo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nini maoni yetu sisi juu ya hili; la kwanza, Wizara ya TAMISEMI ifanye tathmini ya kupitia sera ili waje na ratio ambayo inahitajika kwa wanafunzi 20 wanatumia matundu mangapi ya choo. Sasa hivi sera inasema wanafunzi 20 wanatumia tundu moja. Wanafunzi 20 kutumia tundu moja ukiweka kwenye shule ya wanafunzi zaidi ya 1,000, au 1,200 utahitaji matundu 50 mpaka 60 kuzunguka lile eneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukaona sisi kama TAMISEMI kwamba vinginevyo kuna mahali itafika shule ukuta wake utazungukwa na matundu ya vyoo peke yake. Kwa hiyo tukasema, kwanza wapitie sera ile, waje na ratio ambayo inakwenda na dhana na uhalisia uliopo hivi sasa kwa sababu matundu haya wingi wa zaidi ya 100,000, 150,000 ni kwa sababu tunatumia ratio ambayo kimsingi inawezekana haiendi na uhalisia ulioko maeneo yale.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakifanya ile tathmini, wakapata uhalisia wa matundu mangapi yanatakiwa kwa mwanafunzi mmoja, then waje sasa Serikali itenge fedha na ninaamini watatekeleza kwa muda kwa namna ambayo litatakiwa lifanyike.
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, tulijadili juu ya NeST kwa maana ya bakaa. Hili jambo ni jambo mtambuka. Kwanza mimi binafsi ni miongoni mwa Wabaunge wachache ambao hawaamini kwamba NeST inatakiwa ifutwe turudi kule tulikotoka. Kama Waheshimiwa Wabunge wanakumbuka, wakati ule Afisa Manunuzi mmoja alikuwa anaamua nani ampe mradi na anatanguliza za kwake juu, anatoa, bila usimamizi wowote wa miradi.
Mheshimiwa Naibu Spika, NeST inazo changamoto zake ambazo zingine ziko ndani ya uwezo wa Serikali wanapaswa kuzitatua. La kwanza, lazima PPRA waendelee kutoa elimu namna ya kutumia Mfumo wa NeST kwenye maeneo yote, kwenye halmashauri zote. La pili, Serikali lazima ipeleke fedha za miradi ya maendeleo zinazopotakiwa kupelekwa kabla ya muda haujafika mwisho wa mwaka wa bajeti. Kwa mfano, leo tutanazungumza mwezi Aprili, fedha za miradi ya maendeleo kwenye halmashauri nyingine bado hazijaenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunawapelekea halmashauri fedha, mwezi wa sita tunafunga mwaka (tunakwenda kumaliza ule mwaka) na tunataka wazitumie kabla ya tarehe 31 Juni, wataitumiaje hii fedha? Kwa hiyo, utakuta kwamba tunamaliza mwaka wakati wanakwenda kutangaza kunakuwa na mrundikano wa maombi kwenye Mfumo wa NeST na kunapokuwa na mrundikano wa maombi kwenye Mfumo wa NeST, tunajikuta tunavuka na ile fedha kwenda kwenye mwaka mwingine wa bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kurundikana kwa fedha hizi mwishoni kwenye hatima yake tunagundua kwamba NeST, watu wengine wanaweza wakasema NeST haifanyi kazi. Ni kweli ninakiri kwamba wapo watu ambao wamejificha kwenye kivuli cha NeST, wanashindwa kusimamia majukumu yao, wanashindwa kutenda kazi. Sasa malengo yao ni kuhakikisha ule Mfumo unafutwa turudi tulikotoka kule nyuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wabunge lazima tuiombe Serikali iboreshe namna ya matumizi bora ya Mfumo wa NeST, lazima wasimamie fedha za miradi ya maendeleo ziende kwa muda ndani ya quarter ya tatu fedha ziwe zimekwenda. Kuanzia mwezi Desemba, hadi mwezi Januari, fedha za miradi ya maendeleo zianze kwenda, halmashauri zitangaze kazi ili tuwe na muda wa kufanya assessment ya kujiridhisha akina nani wanaomba na tuweze kuisimamia vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala lingine la migogoro ya ardhi ambalo kwenye hotuba yake Mheshimiwa Waziri Mkuu ameligusa. Lazima tukubaliane hapa, pamoja na kwamba hati ni zao la mwisho la umiliki wa ardhi kwa mwananchi yeyote, lazima kuna hatua kadhaa zinazopitiwa. La kwanza, lazima uwe na PP lazima eneo lile lipangwe matumizi bora ya ardhi. La pili, lazima eneo lile lipimwe. Ukipima ukipata survey plan ndiyo unakwenda hatua ya tatu ya umilikaji wa kupewa hati.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo mengi, lazima tu-plan na Waziri wa Ardhi alichukue hili. Mfumo wetu wa utoaji wa hati, mfumo wetu wa TEHAMA ambao unasimamia mlolongo mzima wa utoaji wa hati mpaka sasa una changamoto nyingi sana. Leo Mbunge ukienda pale unaenda kuomba hati Dodoma, utakaa zaidi ya siku moja, siku mbili, shida ni mfumo huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kabla ya kwenda kwenye hatima yetu ya mwisho, ninashauri sana Mheshimiwa Waziri afanye mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, apitie mfumo wenyewe, mfumo wa TEHAMA wa utoaji na usimamizi wa utoaji wa hati, wenyewe kwanza. Uwe na uwezo wa ku-generate Town Planning yenyewe, iwe na uwezo wa ku-generate TP yenyewe na uwe na uwezo wa kutoa hati bila kuingiliwa na mtu yeyote na utoe kwa uharaka ili angalau hizi changamoto zisiwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ni kuhakikisha kwamba ardhi maeneo yote inapangwa na kupimwa. Changamoto katika kijiji na kijiji kwa sababu maeneo mengi hakuna mipaka kati ya kijiji na kijiji, hazijapangwa na kupimwa. Ile collision ya wananchi kwamba kijiji kingine na kijiji kingine wakiingiliana wanazalisha mgomo kwenye maeneo yetu. Tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri alione hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa Serikali ni kuwekeza fedha kuhakikisha maeneo yote yanapangwa kwa matumizi sahihi ili kupunguza changamoto zilizoko kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, kwa harakaharaka nitakwenda kumalizia, ni 10% ya mikopo ya vijana. Hapa tumegundua changamoto kubwa sana sisi kama Kamati. Leo hii ukichukua halmashauri kwa maana ya manispaa zilizo Mkoa wa Dar es Salaam peke yake fedha ambazo wameweka benki 10%, waliyokata hapa ni mapato wanayokusanya, 10% wakaweka benki, siyo chini ya zaidi ya shilingi bilioni 60 kwenye Halmashauri za Dar es Salaam peke yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumefanya tathmini halmashauri zote nchini 186, zaidi ya shilingi bilioni 100 na kitu zipo benki zinasubiri vijana waende wakakope. Changamoto tuliyoiona ni kwamba, kwanza ni upungufu wa vijana; elimu haijatoka vizuri ya kuwahamasisha kwenda kukopa, hilo la kwanza, lakini Maafisa Maendeleo ya Jamii hawajajitoa kuona hii fursa pekee ya kutoa elimu, ili vijana waende wakakope.
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachofanyika ni fedha ile sasa imekaa benki, fedha nyingi ambayo imerundikana kule ndani, ninashauri, lazima Serikali itazame. Tunachoogopa ni fedha ile ikikaa zaidi ya miaka mitatu/minne anayefaidika ni benki hizi za kibiashara, sisi kama Serikali hakuna mtu atafaidika kwa sababu, wao wana-earn interest kutokana na ile fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati fedha ile inakwenda kukaa benki unakuta halmashauri hizo hawana chai, hawana madawati, hawana zahanati, lakini wamechukua mabilioni ya fedha yamewekwa, wanasubiri vijana wakope. Ninaishauri Wizara, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, wafanye-assessment ya kujiridhisha kama kuna uwezokano wa kufanya mabadiliko ya mwongozo na kanuni, ili fedha hizo wakati mwingine zikizidi ziende zikatumike kwenye mahitaji muhimu yanayowagusa wananchi wa maeneo yale badala ya kubaki kurundikana benki. Kimsingi, mwisho wake hatujui ni upi kwa sababu, fedha zimekaa kule na hatujajua mwongozo wake mwishoni unasema nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachukua nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi niwe mchangiaji wa kwanza jioni ya leo. Ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)