Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Kilumbe Shabani Ng'enda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. KILUMBE S. NG'ENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi niweze kutoa mchango wangu kwenye Bajeti Kuu hii na kwanza nianze kabisa kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutujalia afya na uzima na kuendelea kuwatumikia wananchi waliotuleta katika jumba hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kipenzi chetu, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiongoza nchi yetu vizuri akisimamia shughuli za maendeleo yanayokuja hatua kwa hatua tena kwa kasi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze sana Mawaziri wetu wawili; Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mheshimiwa Waziri wa Mipango pamoja na wasaidizi wao mahiri ambao wako hapa ambao wanafanya kazi kubwa sana ya kutuwekea sura halisi ya maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nianzie mahali ambapo kama mtu niliyelelewa na chama makini Chama Cha Mapinduzi nisiposema nitaona siitendei haki nafsi yangu. Ninataka niwakumbushe Watanzania na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba, baada ya uhuru wa nchi yetu mwaka 1961 na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar mwaka 1964 tuliendelea na kazi ya kujenga nchi mpaka leo na kazi hii ya kujenga nchi sisi hatutaimaliza. Sisi tutafanya kwa kiasi chetu na wengine watakuja watafanya na wengine watakuja watafanya. Hata katika Mataifa hayo yaliyoendelea bado wanaendelea na kazi za kujenga nchi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamaanisha nini? Tunapofika mahali tukasema hatumdai Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, hatumaanishi kwamba kazi ya kujenga nchi imekwisha. Hapana, ila tunamaanisha yale malengo yaliyowekwa na Ilani ya CCM ya Mwaka 2020 - 2025 amefanikiwa kuyakamilisha na mengine amepita kiwango cha kukamilisha. Kwa hiyo, hii tafsiri isije ikachukuliwa kwamba hatumdai. Hapana, ni kwamba tunasema hatumdai kwa sababu yale malengo yaliyowekwa kwenye Ilani kabisa kabisa ameyakamilisha na mengine amekwenda amevuka hata kiwango cha kukamilisha. Kazi ya kujenga nchi bado ipo na wananchi wangine wanaokuja hata sisi tukiondoka duniani wataendelea na kazi ya kujenga nchi kwa sababu kazi ya kujenga nchi ni kazi endelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaposema hapa kwamba tunampongeza Mheshimiwa Rais wetu, kwa sababu Rais anayejali watu anaonekana katika mambo ya msingi yanayohusu maisha ya watu. Ni chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais huyu tumeboresha elimu kwa kiasi kikubwa na kuondoa ada kutoka elimu ya msingi mpaka kidato cha tano na sita. Pia, tumeongeza mikopo katika elimu ya juu kupitia kwa Rais huyu.

Mheshimiwa Naibu Spika, chini ya Mheshimiwa Rais huyu pia tumeboresha huduma za afya. Leo hospitali za mikoa karibu zote zina CT scan machine. Hospitali za mikoa karibu zote watu wanafanyiwa dialysis. Ukiwa na matatizo ya figo sasa hulazimiki kuhama kwenye mkoa wao uende Dar es Salaam ukaishi. Utakaa mkoani kwako kwa sababu vifaa hivi Mheshimiwa Rais huyu kaleta katika hospitali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Rais anayejali watu ameongeza kiwango cha upatikanaji maji mijini na vijijini kiasi ambacho leo tatizo la maji kwa sehemu nyingine limekuwa ni hadithi. Rais anayejali watu ameongeza upatikanaji wa umeme. Leo Mkoa kama wa kwangu Kigoma ambao tangu Tanzania imekuwa Jamhuri ulikuwa haujaungwa na Gridi ya Taifa, mkoa mzima sasa umeungwa na Gridi ya Taifa. Kwa nini tusimpe maua yake Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Rais anayejali watu ameongeza na kusimamia suala la upatikanaji na utumiaji wa nishati safi ili kuwakinga akinamama na madhara yatokanayo na nishati chafu ya kupikia. Huyu ni Rais anayejali watu. Rais anayejali watu ameendelea kusimamia Mfuko wa TASAF ili kusaidia watu wenye familia ambazo ziko katika mazingira magumu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapofika kwenye haya na mengine mengi ambayo muda wa kuyataja haupo, ndiyo tunaposema Mheshimiwa Rais huyu ni Rais wa mfano na anastahili kupewa maua yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jimboni kwangu kuna mambo makubwa sana yamefanyika. Hili la umeme nimelisema, lakini sisi tulikuwa na tatizo kubwa la barabara inayotuunganisha sisi na Mkoa wa Kagera, yaani kutoka Kigoma kwenda Nyakanazi na barabara inayotuunganisha sisi na Mkoa wa Tabora yaani kutoka Kigoma kuingia Tabora. Leo ninavyozungumza kazi hizi zimefanyika. Barabara ya Tabora – Kigoma sasa hivi iko kwenye 98%, imebakia kama kilometa 17 tu wamalizie kuweka lami. Kwa hiyo, haya ni mafanikio makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninachokusudia kusema ni kwamba, hali ya jimboni kwangu na majimbo mengine nchini inatia matumaini kiasi ambacho kinatupeleka sisi Waheshimiwa Wabunge wa Bunge hili kifua mbele kwa wananchi kuomba ridhaa tena.

Mheshimiwa Naibu Spika, niruhusu nizungumze jambo moja kupitia bajeti iliyowasilishwa. Nalo ni suala la marekebisho ya Sheria ya Uingizaji Bidhaa Nchini, Sura ya 276. Nimemsikia hata mwenzangu Benaya ameligusia jambo hili nami ninaomba niligusie. Hapa ninatoa tahadhari kubwa kwa sababu sisi kama nchi moja ya watu ambao wanatuhangaisha kuhakikisha kwamba maisha yao yanaboreka ni wakulima na wafugaji wa nchi hii. Hawa ndiyo moja ya watu ambao tunahangaika nao kwa kiasi kikubwa na hawa wakulima tatizo lao siyo tu kulima, tatizo lao kubwa liko katika usafirishaji wa mazao yao kuyafikisha sokoni ili waweze kusafirisha mazao hayo ni lazima watumie barabara na lazima watumie magari.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wameweka kitu kinaitwa industrial development levy 10% na mnataka hii itozwe kwenye bidhaa zinazotoka nje ikiwa ni pamoja na magari ya transport kama vile ma-Scania, Leyland ndefu hizi, sijui mafuso. Sasa hii wataenda kuongeza gharama kubwa ya usafirishaji na kwa maana hiyo kufanya uwepo mzigo mkubwa sana kwa watumiaji na walaji. Kwa mfano, leo hii mzigo unaotoka Dar es Salaam kwenda Kigoma kwa kutumia usafiri wa magari unachajiwa kilo moja kati ya shilingi 250 hadi 260 lakini kwa kuongeza hii kodi, mzigo huu utakwenda utafika mahali hata shilingi 300 au 300 na kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukifanya hivi utatokea mfumuko mkubwa wa bei ambao sasa hivi tunao kile Kigoma, watatuongezea kutokana na kodi hii. Ninawaomba sana, ninawaamini Wizara ya Fedha na Wizara ya Mipango, wakae waangalie jambo hili. Jambo hili haliendi kumgusa tu yule aliyeagiza bidhaa lakini linakwenda kufika mahali linamgusa yule mwananchi ambaye ndiye anategemea kupata manufaa yatokanayo na usafirishaji wa bidhaa hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ninataka kulizungumza ni suala la liquidity kwenye benki zetu. Ndugu zangu lazima tuambiane na tuwaombe Wizara ya Fedha, wakae na Wizara ya Biashara na Wizara nyingine wazungumze. Sasa hivi lipo tatizo la wananchi wengi kutokupenda kupeleka fedha benki. Katika kila shilingi 10 ni shilingi tatu tu ndiyo inayoonekana katika mfumo ulio rasmi yaani kwenye mobile wallet, hizi M-Pesa na nyingine na kwenye benki.

Mheshimiwa Naibu Spika, pesa nyingi ziko mikononi na utaona tu hata yakipatikana majanga ya moyo au jengo limeanguka wananchi wanalia mara mbili. Unakuta mtu anasema nilikuwa na milioni 200 na bilioni 300. Tujiulize kwa nini watu hawataki kupeleka pesa benki? Watu hawataki kupeleka pesa benki kutokana na tozo na kodi. Hebu waangalie jambo hili ili liweze kutuweka mahali pazuri na benki zetu sasa zimefika mahali kwa kukosa liquidity zina-invite watu kuweka fixed deposit na wanatoa riba mpaka 15%.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama benki inatoa riba kwa mtu 15% kuweka fixed deposit, huyo anayekopeshwa na hiyo benki atatozwa asilimia ngapi? Hili ni tatizo. Ninaiomba sana Wizara ya Fedha ni watu ambao ninawaamini, kuna vichwa viko hapo; Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Naibu wake ni watu makini sana, wakae wa-harmonize hii hali. Pesa ziingie benki. Benki zipate liquidity ili ziweze kukopesha na hapo ndiyo tutakapopata maendeleo ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hilo tu, hata suala zima la kodi, kadri wanavyokuwa na pesa nyingi hata waichaji kidogo watapata fedha nyingi, lakini sasa hivi wanachaji tu kwenye ile shilingi tatu kwenye kila shilingi 10, lakini waki-harmonize zikaja pesa za kutosha maana yake watatoza kodi na watapata fedha nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache niliyoyasema ninaomba kuunga mkono hoja ya bajeti hii nzuri kwa manufaa ya wananchi. Ahsanteni sana. (Makofi)