Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. John Danielson Pallangyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arumeru-Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa nafasi hii ili niweze kuchangia kwenye bajeti hii ya mwaka wa fedha 2025/2026. Awali ya yote kwa ruhusa yako nitangulize shukrani zangu kwa Mwenyezi Mungu ambaye ametupa afya, uhai na leo tumeweza kukutana hapa; si ajabu itakuwa ni mchango wetu wa mwisho kwa Bunge hili la Kumi na Mbili tukitegemea kwamba Bunge lijalo tutakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu kwa kiwango kikubwa utakuwa ni ushuhuda wa mambo mazuri ambayo Serikali yetu ya Awamu ya Sita chini ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeyafanya jimboni kwangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kumpongeza Waziri wa Fedha na Naibu wake, Waziri wa Mipango, Naibu wake kwa hotuba nzuri ambazo kwa kweli zinaakisi kazi nzuri ambazo zinafanyika Wizarani; lakini pia zinatuonesha tulipotoka, tulipo na tunapokwenda. Niwapongeze kwa kazi nzuri sana timu nzima kuanzia Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba hii kama nilivyosema inaakisi kazi nzuri zinazifanywa na Serikali ya Awamu ya Sita na kwa hiyo moja kwa moja niseme kwamba ninaunga mkono hoja hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Awamu ya Sita ambaye kwa kweli kwa miaka miatano ambayo tumekuwa hapa kazi zilizofanyika jimboni ni kubwa mno. Nilisema nitatoa ushuhuda zaidi kwenye mchango wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na sekta ya elimu. Jimboni kwangu nimepata shule 11, kumi za sekondari, moja ya amali na moja ya primary, lakini ni shule ya mfano. Pia nimepata Chuo cha VETA ambacho kipo mbioni kumalizika, tunaamini kwamba siku si nyingi tutaanza kusajili wanafunzi na mambo yatakuwa mazuri jimboni kwangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiondoka sekta ya elimu bado nimepata madarasa mengi sana, madarasa 265; 188 ni ya sekondari. Kwenye sekta ya maji nimepata shilingi bilioni 3.2 kwa kata za Akheri na Nkoarisambu; lakini pia bilioni sita na milioni mia moja kwa Kata za Imbaseni, Maji ya Chai na Kikatiti hadi Maroroni; bilioni 4.1 kwa Kata ya Uwiro kule nyuma ya Mlima Meru. Pia na bilioni 8.2 kwa Kata za Makiba, Gubuni, Shambarai Burka na Kikwe. Hizi si fedha kidogo, ni fedha nyingi sana kwa sekta moja; ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye sekta ya afya pia tumefanyiwa mambo mazuri ndani ya miaka minne. Tumepata shilingi milioni 900 kwa ajili ya kuboresha hospitali ya wilaya. Tumejenga OPD mpya; lakini pia milioni 300 kwa ajili ya EMD, kituo cha matibabu ya dharura. Tumepata nyumba ya mtumishi milioni 90. Tumepata vituo vya afya vine; kuna Kituo cha Afya Usa River, kuna Kituo cha Afya Maroroni, kuna Kituo cha Afya Mareu kule King’ori na fedha shilingi milioni 250 zimeshakuja jimboni kwa ajili ya kituo kingine cha afya. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande wa barabara tulipata shilingi bilioni moja kwa ajili ya kufungua Barabara ya King’ori ambayo ni ahadi ya Rais kuiweka katika kiwango cha lami. Tuliifungua tukaijenga kwa kiwango cha changarawe na kwa sasa inapitika kwa mwaka mzima. Tunaendelea kukumbushia bwana mipango, Mheshimiwa Waziri wa Mipango tusikie vizuri, Barabara ya King’ori iliahidiwa kujengwa kwa kiwango cha lami; endelea kuifikiria uingize katika mipango. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Mbunguni ambayo inaunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Manyara, tulikumbusha hapa kwa hiyo barabara ni muhimu ikajengwa. Barabara hiyo imekwishafanyiwa usanifu na upembuzi yakinifu, lakini kwa bahati mbaya haijawekwa kwenye mpango. Ninaomba Mheshimiwa Waziri wa Mpango na Wizara ya Fedha waikumbuke barabara hiyo. Imekwishafanyiwa usanifu, ni ya kutafutiwa fedha ili iweze kujengwa katika kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru tumeendelea kupata fedha shilingi bilioni tatu na milioni mia sita kila mwaka kwa ajili ya barabara zetu zinazopanda milimani. Barabara ya Sagisi kwenda Akeri mpaka Ndobo imekwishajengwa kwa kiwango cha lami kilometa moja. Ninadhani Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI ameniona, aikumbuke ile barabara ili iendelee kupelekewa fedha ifike milimani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kilimo tumepata fedha nyingi, bilioni 10 kwa ajili ya kuweka miundombinu ya umwagiliaji katika Kata ya Makiba. Mradi huo unaendelea na tunaamini kwamba muda si mrefu wananchi watakuwa wanafanya kilimo chao bila kutegemea mvua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye umeme wa REA tumepata fedha nyingi. Sasa hivi kuna mkandarasi yupo jimboni anaendelea kufanya kazi ya kusambaza umeme kwa vitongoji 19. Mradi huo ulianza mwaka jana. Pia tuna ahadi ya vitongoji 29 mwaka huu. Tunaendelea kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakwenda kumaliza Bunge hili la Kumi na Mbili. Kipekee kabisa nishukuru wananchi wa Jimbo langu la Arumeru Mashariki kwa kuniamini na kuendelea kuniunga mkono tangu 2020 mpaka leo na kazi nzuri niliyowafanyia, kazi nzuri Serikali iliyowafanyia ninadhani watanipokea vizuri; mwezi Novemba tuonane tena hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kukutakia wewe heri, ninakutakia kila la heri. Tunakwenda kwenye kampeni siku si nyingi; wananchi wale kwa kazi ambayo unawafanyia wakurudishe hapa, pamoja na Mheshimiwa Spika mwenyewe, lakini pamoja na Wabunge wenzangu na Mawaziri wote kama tulivyo hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo machache. niseme ninakushukuru sana kwa muda huu na ninaunga mkono hoja. (Makofi)