Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arumeru-Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi pia ya kuchangia katika bajeti hii. Nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema yeye ambaye ametupa uzima kwa siku ya leo na tukaweza kuwepo katika Bunge hili, tangu tulipoanza 2020 hadi kufikia leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nisiache kumshukuru Mheshimiwa Rais wangu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anafanya ya kulihudumia Taifa hili na kutufanya sisi tuonekane ni Watanzania hasa katika masuala mengi ya maendeleo ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze pia Waziri wa Fedha pamoja na Naibu wake na Serikali yote nzima kwa ujumla kwa jinsi ambavyo wanaendelea kufanya kazi zao kwa uaminifu na uadilifu mkubwa na kufanya mafanikio haya ambayo tunayaona leo yakapata kuwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo ninasimama Bunge hili nikielezea mafanikio ambayo tumeyapata katika kipindi cha miaka hii mitano. Nikienda kwenye afya, nilipoingia kama Mbunge nilikuta katika Hospitali yetu ya Wilaya ya Oltument hakukuwepo kabisa na majengo kama haya; hayafanani hata na kituo cha afya, lakini pale tumeweza kupata kiasi cha shilingi milioni 900 na hospitali ile imebadilika kabisa; Hospital ya Wilaya ya Oltrument ya Wilaya imebadilika kabisa; imejengwa majengo manne na leo wananchi ni mashahidi na hata sasa kazi hiyo imekuwa ni njema na wananchi wanafurahia kazi hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya hospitali hiyo haikuwa nzuri, lakini leo barabara hiyo tumepata zaidi ya bilioni 1.5 ambayo imeweza kutengenezea lami ya kilometa moja na nusu kuelekea kwenye hospitali hiyo. Kwa kweli hongera sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hongera sana Serikali ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, haikuishia hapo, kulikuwepo na magofu ya zahanati ambayo ni majengo ambayo hayakumaliziwa ya miaka mingi; lakini kwa kweli imetengenezwa imekuwa nzuri, na wananchi wanafurahia huduma na zimefunguliwa. Kila zahanati imepata. Zahanati ya Leguruki milioni 50, zahanati ya kule Ilkerini wamepata 50, kule Laroi wamepata, kule Oljoro wamepata milioni 50; na maeneo mengi, takriban zahanati kama saba zimekarabatiwa na zimefikia mahali ambapo wananchi wanapata huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu vituo vya afya. Tumeweza kujengewa vituo vya afya takriban vine. Kituo cha Afya cha Oldonyo Sambu tumepata milioni 500 na kinafanya kazi kwa sasa, Kito cha Afya cha Engalaoni kimepandishwa; tumepata pale milioni takriban 870, imebadilika kabisa na ni pembezoni kabisa ambayo inahudumia wafugaji wetu, kule pembezoni wananchi wetu ambao walikuwa mbali sana na hospitali. Leo wanajivunia matunda ya Serikali yao chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Naibu Spika, kule Bwawani tumejenga kituo cha afya cha takriban milioni 603. Tumejenga kituo hicho chini ya Serikali yetu ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo kwa kweli ni mafanikio makubwa sana katika kipindi hiki. Pia tumeweza kujenga Kituo cha Afya kule Oloiye, kinafanya kazi na wananchi wanapata huduma. Hiki kimejengwa kwa mapato ya ndani. Ninamshukuru pia Mkurugenzi na timu yake nzima kwa kazi kubwa ambayo amefanya, ambapo tumeweza kutumia mapato ya ndani takriban milioni 450.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya yote yanatokana na ushirikiano uliopo baina yetu sisi viongozi wote wa ngazi zote kuanzia Mkuu wetu wa Mkoa Mheshimiwa Makonda, Mkuu wangu wa Wilaya, Mheshimiwa Mkalipa, wote hawa tumeshirikiana na Mkurugenzi na timu yake nzima ndiyo maana mafanikio haya ninayoyaeleza hapa yameweza kufanikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye elimu. Kwenye elimu tumepata mafanikio makubwa sana; kwa sababu ukiangalia tumeshaweza kupata shule tatu mpya. Shule ya Kihutu tumepata zaidi ya milioni 850, sasa hivi inaendelea vizuri watoto wapo ndani; Shule ya Sekondari Mweiga ni mpya tumepata milioni 584, watoto wapo ndani wanasoma. Tumejenga kule Kisongo milioni 584 watoto wapo ndani wanasoma. Haya mafanikio ni makubwa sana kwa kiasi ambacho kila mwenye macho na kila mwenye akili timamu lazima ayakubali na kuishukuru Serikali kwa sababu imefanya kazi kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi chote cha miaka mitano pia hakuna wananchi waliosumbuliwa kwa ajili ya kuchanga fedha kujenga madarasa kama wakati ule nyuma. Tumejengewa madarasa yenye thamani ya bilioni 14; fedha ambayo ni nyingi ambayo imeweza kuokoa wananchi kutokuteseka tena kwa ajili ya madarasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye upande wa barabara, ninaishukuru pia Serikali kwa sababu tunayo barabara ambayo inajengwa ya Mianzini – Sambaa – Shangalamtoni, ni barabara yenye thamani ya shilingi bilioni 22. Mpaka sasa wananchi wamefidiwa kiasi cha shilingi bilioni 3.5 na wote wamekwishapata fidia yao. Kwa kweli tunaishukuru Serikali kwa niaba ya wale wananchi, Serikali yetu imefanya kazi kubwa ya kutoa fidia. Hadi sasa mkandarasi yupo kazini, lakini amesimama kidogo kwa sababu hakupata fedha. Kwa hiyo hili ni ombi ambalo ninaliwasilisha kwa Serikali ili iweze kukumbuka barabara hiyo ili mkandarasi huyo aweze kuendelea na kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa maji miradi inaendelea vizuri. Ombi; tunaomba sasa ile miradi midogo midogo ya maji ambayo haikupata fedha basi Serikali ikakumbuke ili iweze kuhakikisha kwamba wananchi wale wanaweza kupata maji na waweze kufurahia matunda ambayo tayari wameshayaona wao wenyewe kwa macho.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo ninarudi jimboni nikiwa na mambo mengi ya kuyasema pale, kwa sababu mengi yamefanyika chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake. Sina wasiwasi kwamba nikisimama jukwaani sina la kusema. Nina mambo mengi ya kusema ambayo hata hapa Bungeni nikianza kuyaeleza kwa sababu ni mengi, mengi sana kiasi ambacho haiwezi kumalizika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukija kwa upande wa umeme, tumepata vitongoji 15. Nilipoingia kuwa Mbunge nilikuwa na vitongoji 258; na vitongoji vilivyokuwa na umeme ni kama 102. Hadi sasa tumeshafikisha vitongoji 200, vitongoji ambavyo bado ni 58 tu. Ni kwa kiwango kikubwa sana kwamba Serikali imefanya kazi kubwa ambayo inaamini katika mgao utakaokuja ule uliotangazwa jimbo langu pia litaendelea kupata na vitongoji hivi ambavyo bado vitaingizwa na tutapata umeme. Kwa hiyo kwa kweli tunaishukuru Serikali kwa kazi hii kubwa ambayo imefanyika (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti hii vile vile tunaipongeza Serikali kwa sababu kwa kitendo cha kupunguza usajili wa pikipiki kutoka 65,000 mpaka sifuri ni kazi kubwa na njema ya kuwafikiria vijana wetu wanaofanya kazi za bodaboda na kazi nyingine; guta kutoka 120,000 mpaka sifuri, lakini na service levy nayo imepungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa kweli bajeti hii ninaipongeza kwa sababu imefikiria na kugusa maeneo ya wananchi, ambayo inaleta matumaini makubwa kwa wananchi wetu. Pia ada ya leseni imepungua pia katika bajeti hii; kwa maana ya pikipiki na guta kutoa 70,000 mpaka 30,000. Hayo ni mafanikio makubwa pia kwa vijana wetu wa bodaboda na wengine wote ambao wanafanya kazi hii ya udereva katika bodaboda.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)