Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Benaya Liuka Kapinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbinga Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza ninaungana na wenzangu kuunga mkono kwa asilimia zote bajeti hii ambayo ni mwendelezo wa bajeti zilizopita. Inaenda kukamilisha mambo yote tuliyoyapanga katika Ilani ya Mwaka 2025. Kwa hiyo, ninaiunga mkono kwa asilimia mi moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ninaishukuru sana Serikali ya Awamu hii ya Sita chini ya Mama yetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ninaishukuru kwa mambo makubwa iliyofanya katika Jimbo la Mbinga Vijijini. Jimbo la Mbinga Vijijini katika kipindi hiki cha miaka mitano tunajivunia sana uwepo wa Mama huyu kwa sababu, tulikuwa hatuna hospitali ya wilaya, ndani ya kipindi hiki imejengwa, imekamilika na imeanza kutoa huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa hatuna vituo vya afya, sasa hivi vituo vya afya vitano vinafanya kazi. Vilevile, vituo vya afya viwili vimejengwa, upande vimeanza kufanya kazi. Vingine viwili vimepelekewa fedha na vinajengwa, kwa maana hiyo kwa kipindi hiki tutakuwa tumekamilisha vituo vya afya tisa. Kwa kweli, ni jambo la kumshukuru sana Mheshimiwa Rais na Serikali yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika kipindi hiki kifupi cha miaka hii minne/mitano zahanati 17 zimejengwa na kufunguliwa, lakini kupitia mapato ya ndani. Hivi ninavyoongea zahanati 16 zimepelekewa fedha, maana yake ni hizi 17 pamoja na 16, zote mpya, zitakuwa zimekamilika ndani ya kipindi hiki cha miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa shule za sekondari tumefungua sekondari 10 katika kipindi hiki, zote mpya zinafanya kazi kabisa, lakini na zile za nyuma zimepelekewa fedha; baadhi zinajengewa hosteli na baadhi zinakamilishwa maabara, zote hizi zimefanyika ndani ya kipindi hiki cha miaka mitano. Tumepata shule mpya mbili za msingi, Shule mpya ya Kilango na Shule mpya maalum pale Maguu, ndani ya kipindi hiki cha miaka mitano. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, tunaishukuru sana Serikali hii ya Awamu ya Sita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunaingia kipindi hiki, Jimbo langu lina vijiji 117, vijiji 96 vilikuwa havina umeme, leo hii vijiji vyote vimepelekewa umeme ndani ya muda huu wa miaka minne/mitano ya Serikali hii ya Awamu ya Sita. Maana yake ni kuna kazi kubwa imefanyika, kipindi hiki kifupi imefanyika kazi kubwa kwelikweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu hapa ni kwenye upande huu wa umeme, sisi Wanambinga tunatumia sana umeme na tunaoneana wivu wa maendeleo. Kwa hiyo, tukiona nyumba fulani imewekewa umeme na nyumba nyingine haina umeme tunaingia kwenye vita ya maendeleo. Kwa hiyo, kwa sababu vitongoji vyetu viko mbalimbali na tuko nyuma ukilinganisha na wenzetu, ninaomba sana, nimeona kwenye bajeti hii tumetengewa vitu vingi vizuri, kupeleka umeme kwenye vitongoji. Ninaomba sana utekelezaji wa mpango huu wa umeme vitongojini uanze, ili kila kitongoji kwenye Jimbo la Mbinga Vijijini kiweze kufikiwa na umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile upande wa Barabara. Tulikuwa na shida ya Barabara ya kutoka Mbinga hadi Mbambabay, ilikuwa ni historia, lakini kipindi hiki, mwaka jana Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alienda kuifungua Barabara ya kutoka Mbinga hadi Mbambabay, barabara hii sasa inaunganisha mpaka Mtwara. Pale Mbambabay tuna bandari mpya inajengwa na Mtwara kuna bandari kwa hiyo, inaendelea kuifungua Mbinga pamoja na kuufungua Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huko nyuma tulikuwa na malalamiko sana kwamba, sisi Wanambinga, sisi Wanaruvuma ni kama tumetengwa, lakini Awamu hii ya Sita imetufungua sisi Wanambinga kwa Barabara, pia imetufungua angani. Tuna uwanja mzuri wa ndege uko pale na ndege zinatua mara kwa mara. Kwa sababu abiria kule ni wengi sana, tunajazana kweli kweli kiasi kwamba, unaomba tiketi unakosa. Ninaomba watu wa Air Tanzania waongeze route, tuwe na route zaidi ya hizo tatu ambazo tunazo, watu ni wengi na wanasafiri kupitia ndege yetu ya Air Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tuna bandari yetu kule Ziwa Nyasa, kwa maana hiyo usafiri kwa maji kuja hadi Itungi, Kyela, nao unawezeshwa. Sasa hivi kuna mradi mkubwa kwelikweli wa bandari ya kisasa inayoenda kuunganisha Mtwara na Bandari ya Mbambabay ambayo itawezesha Mkoa wa Ruvuma kufanya biashara kati ya Nchi ya Tanzania na nchi jirani, zikiwemo Msumbiji na Malawi; ni bandari nzuri sana na kazi inaendelea. Ninaipongeza na ninaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye bajeti hii ya mwaka huu. Bajeti hii tunayoijadili leo ni nzuri kweli kweli. Kama nilivyosema pale mwanzo, kwamba ni mwendelezo wa bajeti zilizopita; ni kweli, kwa sababu tulikuwa tumezoea kule kupata mbolea za ruzuku kwa sababu sisi Wanambinga ni wakulima kweli kweli, bila mbolea hatuvuni, lakini bajeti hii imeweka tena ruzuku. Maana yake ni kwamba tutaneemeka kwa kutumia ruzuku ya awamu ya sita na sasa itaenda awamu nyingine inayofuata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye bajeti hii pia kumekuwa na punguzo; baadhi ya viuatilifu vimetolewa kodi. Kwa hiyo ni jambo zuri kwa sababu kwenye mikahawa kule na sisi tunatumia viuatilifu. Kwa hiyo kwa kupunguza kodi hii tunakwenda kunufaika sisi Wanambinga kwenye mazao yetu tunayolima. Vilevile pamoja na kodi hii ya ongezeko la thamani. Kwa hiyo kimsingi bajeti hii inakwenda kumtambua Mwanambinga, inakwenda kumtambua vizuri Mwanaruvuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe ushauri kwenye eneo fulani. Eneo la kwanza ni kwamba; bajeti hii tumeweka utaratibu wa kwenda kuweka tozo mpya ya maendeleo ya viwanda (Industrial Development Levy).

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo hili ni zuri kabisa kwa sababu linalenga kuvilinda viwanda vyetu vilivyopo hapa ndani; lakini twende mbele zaidi tujaribu kulipima kama litakwenda kuwanufaisha Watanzania ama linaweza kwenda kuwaingiza kwenye gharama kubwa. Lengo ni zuri, lakini ukienda kiundani kwenye ongezeko hili la kwenye tozo hii mpya hapa ndipo tunapokuwa na malori na ma-scania yanayotoka nje, ambayo kwa mazingira yetu ya Tanzania, kwa mazingira yetu tuliyoyazoea, malori haya ndiyo himilivu, ndiyo yanayotumika zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuweka hii tozo mpya inaweza kusababisha kuongezeka kwa gharama na kuongezeka bei za shughuli za usafirishaji, hali inayopelekea kukwamisha usafirishaji ndani ya nchi. Hivyo basi, ushauri wangu mimi ni kwamba Wizara husika ifanye tathmini kati ya faida tutakazozipata kwa ongezeko hili la tozo mpya na hasara tunayokwenda kuipata kama hii tozo inaendelea kubaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu, Serikali ingetathmini vizuri. Ushauri wangu hapo ni kwamba, ikiwezekana tozo hii ingeondoshwa, tubaki kama tulivyokuwa kwa sababu tumeona manufaa zaidi kuliko ongezeko tunaloenda kulipata hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi, ninaunga mkono hoja. (Makofi)