Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. BALOZI LIBERATA R. MULAMULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ninakushukuru sana kwa kunipatia fursa ya kuchangia kwenye hoja mbili zilizo mbele yetu, yaani Bajeti za Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026 na Mpango wa Taifa wa Maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaungana na walionitangulia kumpongeza sana Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa kuandaa na kutuletea bajeti inayoakisi uhalisia wa mahitaji ya wakati tuliopo, inayojielekeza kujibu changamoto za Taifa letu na iliyojaa umadhubuti kwa kukabili changamoto za hali ya uchumi wa dunia na kujenga ustahimilivu wa uchumi wetu (resilience).
Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa kuwasilisha bajeti za maeneo yao kwa umahiri mkubwa. Kipekee ninampongeza Waziri, Mheshimiwa Profesa Kitila Alexander Mkumbo, kwa kuwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, kwa kuwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali. Ninawapongeza Naibu Mawaziri wote wawili, Mheshimiwa Hamad Hassan Chande na Mheshimiwa Stanslaus Nyongo, ambao naona wamekaa kama mapacha hapo na timu za Wizara zote mbili kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama wasemavyo supu hunywewa ikiwa ya moto, hivyo nianze kwa kusema ninaunga mkono bajeti hii. Sababu za kuunga bajeti hii ni tatu. Kwanza kabisa, ni bajeti inayotujengea uhimilivu (resilience), pili, ni bajeti inayolenga kujenga uchumi shirikishi (inclusive economy) yaani kutomwacha mtu wala sekta yoyote nyuma (leaving no one behind) na tatu, ni bajeti inayothubutu kuongeza kasi ya kukuza uchumi wetu (disruptive growth). (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naanza na bajeti hii inatujengea uhimilivu kwa kuongeza nidhamu katika makusanyo na matumizi ya fedha za ndani. Bajeti hii inapunguza utegemezi wa misaada kutoka nje. Dhoruba tulizopitia hapo katika kipindi cha COVID au UVIKO-19, Vita vya Urusi na Ukraine iliyochochea kupanda kwa gharama za vyakula na bei ya mafuta na logistics, kuadimika kwa Sarafu ya Dola ya Marekani nchini na hatimaye kuondolewa kwa msaada kutoka Marekani na kupungua misaada kutoka Ulaya zimetufundisha kujihami na kujitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninafurahishwa kwamba, Serikali itatenga bajeti katika muda wa kati itakayolenga kuziba pengo la fedha zilizokuwa zinatarajiwa kupatikana kutoka kwa wabia wa maendeleo, hususani mataifa makubwa ambayo yamepunguza au kusitisha misaada iliyokuwa inatolewa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali zaidi katika eneo la afya. Hadi sasa Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 82 kuziba pengo litokanalo na mabadiliko hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nirudie tena kwamba, taasisi mojawapo iliyoathirika na kusitishwa kwa miradi hiyo ni Taasisi ya Benjamini Mkapa Foundation, ambayo ilikuwa inatekeleza mradi mkubwa wa afya endelevu kupitia msaada wa Shirika la Maendeleo la Marekani ambalo limefungwa na kusitisha misaada yote na kuathiri wafanyakazi na wataalam wapatao 1,296 ambao wanatoa huduma za afya katika hospitali na vituo vya afya vya umma vipatavyo 701 kwenye mikoa yote 22 ya Tanzania Bara na mikoa mitano ya Zanzibar ambao wote wamepoteza ajira. Ni matumaini yetu kwamba, bajeti itakayotengwa na Serikali itasaidia katika kuwarudisha kazini watumishi hao.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema pia, nimefurahishwa na maboresho ya mfumo wa kodi, mapendekezo ya kodi mpya na nafuu katika baadhi ya kodi zenye lengo la kuchochea uwekezaji wa ndani, wepesi wa kulipa na kuongeza matumizi ya kidigitali katika ukusanyaji wa mapato unaotuongezea uhimilifu kwa kuvutia uwekezaji wa ndani. Nimependa uamuzi wa kuongeza kodi kwenye michezo ya kubahatisha, betting na maeneo mengine, ili kupata fedha, kwa ajili ya kufikia pengo la msaada kwenye sekta ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninavutiwa zaidi na uamuzi wa kupunguza VAT kutoka 18% hadi 16% kwa malipo yatakayofanyika kwa njia ya mtandao. Ninafurahishwa na dhima ya kuimarisha ubora wa elimu anayopewa mtoto wa Kitanzania na siyo bora elimu, baada ya upatikanaji wa elimu. Hivyo hivyo kwamba, Serikali inakwenda kwenye modernization ya shughuli za uzalishaji kilimo bora, ufugaji na uvuvi wa kisasa pamoja na kuongeza thamani ya mazao ndani ya nchi na kuongeza ujenzi na upanuzi wa viwanda. This is the way to go. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa uchumi shirikishi, ripoti kadhaa huko nyuma zimeonesha kwamba, pamoja na uchumi wetu kukua, ukuaji huo ulikuwa haukui sana kwenye sekta zinazoajiri au kugusa watu walio wengi. Katika bajeti hii unaiona dhamira hiyo kwenye kupunguza kodi kwa pikipiki na bajaji ambazo ni ajira za mpito kwa vijana wetu na kuondolewa kodi kwa mbolea inayozalishwa nchini na kuweka kodi kwenye baadhi ya bidhaa kutoka Nchi Wanachama wa Afrika Mashariki, ili kulinda viwanda vyetu vya ndani. Kwa ujumla wake bajeti inatoa unafuu na mwanya mkubwa kwa biashara na huduma zinazozalishwa na wawekezaji wa ndani, ili kuwezesha sekta binafsi kushiriki zaidi, kupanuka zaidi na kuajiri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda pia, kusema katika uthubutu wa kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi, bajeti hii tunatarajia itupeleke kwenye ukuaji wa uchumi wa asilimia sita kutoka 5.5 kwa sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niongelee kwa kifupi, kutokana na ufinyu muda, utekelezaji wa diplomasia ya uchumi ambayo imegusiwa kwa kifupi kwenye Hotuba ya Bajeti ya Serikali. Pamoja na kutambua mafanikio ya diplomasia ya uchumi katika kuchangia kwenye kukuza maendeleo ya nchi yetu rai yangu ni kwamba, Serikali iwe na mkakati wa Kitaifa katika utekelezaji wake maana ni suala mtambuka, haliwezi kuachiwa tu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pekee yake. Ili kufanikisha sera hii, balozi zetu zinahitaji rasilimali fedha na watu kukidhi mahitaji ya kuhamasisha uwekezaji, utalii, masoko, biashara na kadhalika ambapo bajeti ya Wizara peke yake haikidhi mahitaji hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kabla muda wangu haujaisha niongelee kuhusu, I mean mwisho lakini siyo kwa umuhimu, inawezekana leo ni mara yangu ya mwisho kuzungumza katika Bunge hili la Kumi na Mbili nikiwa kama Mbunge wa Kuteuliwa. Utakumbuka kwamba, Rais wetu, Mheshimiwa Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliniteua Waziri na Mbunge, hivyo niliapa kama Mbunge mbele ya Bunge lako Tukufu tarehe 31 Machi, 2021. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo ninasimama kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kunipa fursa ya kuwa kwenye Bunge hili kujifunza na kutoa mchango wangu wa Chama changu Cha Mapinduzi na Serikali yetu nikiwa Mbunge back bencher, sasa nimetumikia utumishi wa umma kwa ngazi mbalimbali. Ninaamini nimekusanya uzoefu mkubwa kwenye medani ya siasa na utumishi wa umma ambao utanisaidia kusonga mbele na kuendelea kutoa mchango wangu kwa moyo wangu wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, napenda nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa dakika moja, kama mwanadiplomasia namba moja, kwa kuniwezesha kuteuliwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kuwa Mjumbe Maalum wa Masuala ya Wanawake kuhusu amani na usalama Barani Afrika. Ninapenda pia, kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wenzangu wote na Watanzania kwa ujumla kwa salamu zenu za pongezi, kunitakia kila la heri na mafanikio katika majukumu hayo mapya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hakika sitawaangusha. Ninawaombea wenzangu wote Mwenyezi Mungu awarudishe tena kwenye Bunge lijalo. Kazi na utu, tunasonga mbele, Oktoba tunatiki, Mheshimiwa Rais miaka mitano tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Sasa Mheshimiwa Balozi Mulamula, ndio umeishia hapo hapo? Nikafikiri labda unamalizia mengine? Unaendelea bado?
Basi unga mkono hoja. Nikafikiri ulikuwa na mengine unasema, maana haya mambo, anyway tuendelee.
MHE. BALOZI LIBERATA R. MULAMULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)