Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi na kuwa sehemu ya kuchangia katika hii Bajeti Kuu. Kwanza niipongeze Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo imeifanya kwa kipindi cha miaka mitano; hongera sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Tanzania wote wameona kazi kubwa ambayo imefanyika katika maeneo mbalimbali na tumeshuhudia utekelezaji wa miradi mikubwa ambayo ilikuwa inaendelea kutekelezwa katika nchi yetu kwenye Sekta ya Ujenzi, Sekta ya Mawasiliano, Sekta ya Maji na Sekta ya Umeme. Tumeona kila angle fedha wamepeleka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya mwaka jana tulipitisha hapa Bungeni bajeti ya shilingi trilioni 50.2 na Wizara leo imekuja kutuambia tumekusanya shilingi trilioni 45 kutoka mapato yote, maana yake tumekaribia kufikia lile lengo. Vilevile, fedha hizi nazo tulizopitisha mwaka jana tulikuwa Wabunge wote hapa, tulipitisha bajeti hii shilingi trilioni 50.2, maana yake Wabunge tulichambua, tukaridhia na tukaipitisha kwa maana kwamba Serikali iende ikafanye kazi. Pia, mwaka huu Serikali imekuja imeliomba Bunge tupitishe bajeti ya shilingi trilioni 56 na hapa tunaijadili na kuchambua. Maana yake tukimaliza tukapitisha, maana yake tumeiruhusu Serikali iende ikafanye kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipongeza kwa kazi kubwa ambayo imefanya. Inatokea unaweza kuona mtu mmoja miongoni mwetu Mbunge anatoka nje anasema Serikali inakopa sana hatuoni fedha inapoelekea. Sasa unabaki unashangaa tulikaa humu Bungeni, tukapitisha wote bajeti. Kwa mfano katika shilingi trilioni 50, uwezo wetu wa kukusanya mapato yetu ya ndani kupitia Serikali yetu tunakusanya shilingi trilioni 30, mwaka jana tumekusanya shilingi trilioni 30 na zilizobakia hizi 15 tumekopa ambazo hizo tumekopa ndani na nje ya nchi yetu na sisi tulipitisha na tumeruhusu.

Mheshimiwa Naibu Spika, uwezo wetu wa kukusanya mwaka 2020 tulikuwa tunakusanya bajeti yote kwa mapato ya ndani shilingi trilioni 20, lakini leo uwezo wetu wa kukusanya Serikalini umeongezeka, tunakusanya zaidi ya shilingi trilioni 30. Hongera sana Wizara kwa kazi nzuri na mikakati mbalimbali waliyoiweka. Kutoka shilingi trilioni 20 mpaka kufika shilingi trilioni 30 kukusanya kwenye mapato yetu ya ndani ni kazi kubwa imefanyika; hongera sana. Waongeze mianya ambayo tunaweza kupata fedha ili uwezo wa kujihudumia uongezeke. Ninapongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu anahoji uwezo wetu wa kukusanya shilingi trilioni 30. Kwa mfano kwa mwezi, mwaka 2020 tulikuwa tunakusanya shilingi trilioni 1.7, leo tunakusanya kwa mwezi shilingi trilioni 2.8. Maana yake ni kazi kubwa imefanyika, lakini fedha hizi tunazozikusanya katika hizi shilingi trilioni 2.8, trilioni moja peke yake inaenda kulipa mishahara ya wafanyakazi ambao hao wafanyakazi wanaoenda kulipwa mishahara tunawaajiri sisi na kila siku tunasema hapa tuongeze ajira kwa watu wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo anapokuja mtu anatokea anasema anashangaa; unashangaa vipi wakati tunapoajiri maana yake tunaongeza wigo mpana wa kulipa mishahara? Kama tunaongeza wigo mpana wa kulipa mishahara (shilingi trilioni moja inaenda kwenye mishahara), shilingi trilioni moja tunaenda kulipa deni, maana yake katika shilingi trilioni 2.8, shilingi trilioni mbili zimeshatumika tayari na shilingi milioni 800 zinabaki kuhudumia Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za miradi ya maendeleo ni fedha ambazo tunakopa tunatekeleza. Ninaiomba Serikali iendelee kwa sababu hizi fedha zinahitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ambalo ninaweza nikasema ni Wizara mwaka 2000 kwenye ile mahafali ya 43 ya Open University yaliyofanyika Kigoma ambapo mgeni rasmi alikuwa Mheshimiwa Rais akamtuma Mheshimiwa Waziri Mkuu. Katika hotuba ya Mkuu wa Chuo aliiomba Serikali yale madeni yaliyokuwa yamehakikiwa yalipwe, kwa mfano ya madaktari na maprofesa wa vyuo vikuu kwa sababu, imekuwa ni muda mrefu kabla ya Bunge hili halijakwisha. Tunaomba Wizara ya Fedha iwalipe fedha zao hawa madaktari na maprofesa wa vyuo vikuu kwa sababu, walihakiki, kilichobaki ni utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaiomba Wizara, bahati nzuri Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara amekuwa analisemea jambo hili mara zote kwa hiyo, ninampongeza kuwa mstari wa mbele. Ninaiomba Serikali iwalipe hawa madaktari pamoja na maprofesa wa vyuo vikuu, ili waendelee, wengine wamestaafu na wengine wamefariki, tunaomba haki zao waweze kupewa. Kwa hiyo, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha wahakikishe wanawapa hawa watu stahiki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine niweze kusema ninawapongeza sana, kazi kubwa imefanyika, Serikali imefanya na miradi mikubwa inaendelea. Tunaona leo kuna uzinduzi wa Daraja kubwa la Kigongo - Busisi kule Mwanza, fedha nyingi zimetumika, hawa ndiyo ambao wanakusanya na wanapeleka kwenye utekelezaji. Ninaomba hii miradi yote, kwa mfano treni ya umeme ambayo tayari imefika Kigoma na tunajua kuna wakandarasi wapo kutoka Kigoma, Dodoma kwenda Tabora, Tabora – Isaka, Isaka – Mwanza na Tabora kwenda Kigoma na Tabora kwenda Katavi, wawalipe wakandarasi ili kazi ifanyike na mwaka 2028 Watanzania watembee, wafurahie matunda ya nchi yao kwa kutumia treni ambayo itarahisisha kufanya kazi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua Serikali inafanya kazi na sisi Wabunge tunawaunga mkono, hasa kwa kupitisha hii bajeti kuu. Wachape kazi, sisi Wabunge tunawaunga mkono na tunasema kwamba, miradi yote inayotekelezwa na wanayoifanya Watanzania wanaiona katika maeneo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kwetu tunahitaji umeme vitongojini, tunaona wakandarasi wameanza kuingia kwenye maeneo yetu na kazi inafanyika. Tumepewa awamu hii vitongoji 86, lakini uhitaji ni zaidi ya vitongoji 86. Tunaiomba Serikali kwa sababu, tunapitisha bajeti hii fedha zinazotoka kwenda kwenye miradi ya umeme vijijini tuipate kwa wakati, wakandarasi waje kwenye site, wananchi waweze kupata huduma ya umeme kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye sekta ya maji, pia tumeona miradi mikubwa inafanyika nchi nzima maeneo mbalimbali. Sisi watu wa Manonga tumepata miradi mikubwa ya maji ya fedha za kutoka Benki ya Dunia, hizo ndiyo fedha za mikopo, lakini zinakuja kufanya kazi, kwa ajili ya wananchi wetu. Mtu anasema fedha hizi za mikopo hatuoni zinapoenda. Zinaenda kwenye miradi ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jimboni kwangu tumepata fedha hizi za Benki ya Dunia ambazo zinatekeleza Mradi mkubwa wa Maji wa Ziwa Victoria, kutoka Ziba kwenda Ndembezi, kutoka Ndembezi kwenda Nkinga, kutoka Nkinga kwenda Mizanza – Mwisi, kutoka Mwisi mpaka Simbo na bado tutaomba tena fedha nyingine zitengwe kutoka Simbo kwenda Igoweko, kwenda kule Tambalale na kwenda Uswaya kwa sababu, wananchi wanahitaji huduma. Kwa hiyo, ninaomba sana Serikali iendelee kufanyia kazi suala la mikopo, deni letu ni himilivu na tunaweza kulipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tumeweza kulipa mwaka huu trilioni 11 na sasa hivi hapa tunapitisha bajeti ya kwenda kulipa mwaka unaokuja shilingi trilioni 14 maana yake nchi yetu ni himilivu, inaweza kulipa deni, inakopesheka na inaaminika kwa sababu, tunakusanya tunalipa, tunakusanya tunalipa. Kwa hiyo, sisi kama Wabunge tunasema chapeni kazi, chukueni fedha tekelezeni miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wale ambao wanasema hawaoni inakotekelezwa miradi, hawaoni fedha zinakoenda, maana yake ni kwamba, hawafuatili hata bajeti zinazowasilishwa hapa Bungeni. Kama unafuatilia hauwezi kuhoji masuala ambayo yanatekelezwa kwenye maeneo yetu. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante.

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha na ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)