Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Tecla Mohamedi Ungele

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii. Awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunipatia afya njema lakini pia kwa kuniruzuku uhai. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninawashukuru jamii yangu ya Mkoa wa Lindi kwa kuniamini kuwawakilisha kwa muda huu wa miaka mitano. Ninawashukuru sana kupitia Chama Cha Mapinduzi na ninaamini kabisa tutaendelea kufanya kazi kwa kipindi kijacho kwa kadri Mwenyezi Mungu atakavyotupatia uhai. Mimi ndugu yao Tecla Mohamedi Ungele, ninaendelea kufanya kazi ya kuwawakilisha katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninawapongeza Wizara ya Mipango na Uwekezaji, lakini pia Wizara ya Fedha. Timu yote hiyo wamefanya kazi vizuri na wanaendelea kufanya kazi kubwa sana ya kuendeleza na kumsaidia Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, michango yangu ninaielekeza kwenye maeneo mbalimbali; eneo la kwanza kwenye Sekta ya Afya. Tunajua afya ni mtaji na hili Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliahidi na ametekeleza kwa kiasi kikubwa sana na kwa kiasi chote kule Mkoa wa Lindi. Tulikuwa na hospitali ya Mkoa (hospitali ya Rufaa), amejenga hospitali kubwa ya Rufaa kule maeneo ya Mitwero; tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Pia, amejenga hospitali ya Manispaa ya Lindi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hospitali nyingine pia maeneo mengine ya wilaya nyingine kulikuwa hakuna hospitali za wilaya, tumemsikia Mheshimiwa Kuchauka, Wilaya ya Liwale kulikuwa hakuna hospitali ya wilaya walikuwa kwenye kituo cha afya tu, lakini kuna hospitali ya wilaya tayari. Pia, hata Ruangwa kuna hospitali ya wilaya na Jimbo la Mtama kuna hospitali ya wilaya pia. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, amepeleka pia vifaa, vitendea kazi na vifaatiba kwenye maeneo hayo. Hata hivyo sisi wana Lindi tunamshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametuletea huduma za tiba za huduma za dharura kwenye Hospitali ya Ruangwa, Kinyonga pale Kilwa lakini pia na Liwale. Pia, tunashukuru ametuletea huduma ya ICU (kuhudumia wagonjwa mahututi) pale hospitali ya Wilaya ya Nachingwea. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ametuletea ambulance 13 vile vile katika kipindi chake cha miaka minne ambapo kila wilaya imepata ambulance mbili. Zilikuwepo zingine lakini kipindi chake Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameziongeza hizo 13 pamoja na hiyo moja ya hospitali ya Mkoa. Hatujawahi kuyaona haya huko miaka mingine iliyopita. Huyo ndiye Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunayemfahamu sisi Wanalindi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika uwakilishi wangu hapa Bungeni mimi nikiwa mtaalam wa afya pia nilipigania sana mafunzo haya ya community health workers yarudishwe tena. Kweli yamerejeshwa lakini Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, naye katika programu yake ya community health workers kwenye mikoa ile 10 tunaona Mkoa wa Lindi ni mmojawapo katika hiyo programu ya Community Health Workers. Sasa hivi Community Health Workers kwa Mkoa wa Lindi inatekelezwa Manispaa ya Lindi na Mtama pamoja na Ruangwa. Tumeona vijana wameajiriwa kule wanaendelea kufanya kazi ile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Community Health Workers ni muhimu, hao wanakuwa linkage kati ya jamii na idara ya afya. Wanafanya huduma ya kushauri, lakini kwa kiasi kikubwa kwenye kuzuia magonjwa yasiyoambukiza. Pia kushauri akinamama kwenda kliniki kuhudhuria chanjo na kadhalika. Kwa hiyo kwa kiasi kikubwa idara hii ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona sisi Mkoa wa Lindi pia tumetekeleza ile programu ya M-Mama ile ya kumuwakilisha mama kuhakikisha anapata rufaa ya kwenda kwenye huduma za afya (mama mjamzito na mtoto chini ya siku 28). Tunaona hii ndio iliyopunguza vifo vya akinamama wajawazito kutoka 550 kwa kila vizazi hai 100,000 mpaka kufikia 104 kwa kila vizazi hai 100,000 kwa mwaka huu 2025 kuanzia pale tulipotoka 2020. Sisi Wanalindi, tunashukuru sana (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Sekta ya Elimu pia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya mambo makubwa Mkoa wa Lindi. Amejenga Shule ya Sekondari ya Wasichana kubwa kule maeneo ya Kilangala iliyogharimu shilingi bilioni 4.5. Tunashukuru sana na miaka miwili iliyopita Mheshimiwa Rais, alipitia alienda kwenye ile sekondari na akaahidi, tukawa na kilio cha kuomba barabara ya lami. Ninakumbuka Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo Mama Salma Kikwete aliomba na kweli sasa hivi tunajengewa ile barabara ya lami kutoka hapa Kilangala barabarani kwenda kule kwenye sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, pia anajali watoto wa kiume. Kunajengwa sekondari kubwa ya wavulana ya Kanda ya Kusini (Mtwara, Lindi na Ruvuma) inajengwa pale Kiwalala katika Jimbo la Mtama inaenda kugharimu shilingi bilioni 4.5; huyo ndiye Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kilimo sisi Wanalindi na Mtwara hakutuacha, anatupatia pembejeo bure kwenye zao la korosho. Huu ni mwaka wa nne na ndiyo imeongeza hata mapato ya korosho. Hilo ni jambo kubwa sana na hata bei imekuwa nzuri, tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wanalindi vilevile tunafaidi maji. Maji yanatoka Mavuji kwenda Nangurukuru, itaenda Kivinje na mpaka Kilwa Masoko. Pia, maji yanatoka Ng’apa kwenda mpaka Mchinga. Wana Mchinga sasa hivi wanakunywa maji ya kwenye bomba, maji safi na salama, huyo ndiye Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile maji kutoka Nyangao kwenda Ruangwa na baadhi ya vijiji vya Nachingwea tuna mradi mkubwa pia kule. Hata hivyo kwenye hotuba ya Wizara ya Maji walionesha kwamba wamefanya utafiti maji ya Mkoa wa Lindi na Mtwara yana manganese, madini ya chuma pamoja na chumvi. Kwa hiyo, sisi wana Lindi tunaomba mradi ule mkubwa wa kutoa maji kutoka Rufiji kuja Lindi na Mtwara, hilo jambo litakuwa ukombozi mkubwa sana kwa sisi Wanalindi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wanalindi tunasema hivi, itakapofika Oktoba (tena tunaona inachelewa tu), sisi tunatia tiki kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mambo haya aliyotufanyia ni makubwa hayajapata kutokea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapongeza sana Wizara hii na katika maeneo yao Wizara hii ya Fedha na Wizara ya Uwekezaji wamefanya kazi kubwa sana walivyokuja kwenye kubuni mfumo huu wa kodi ya tozo kwa ajili ya kugharamia na kudhibiti maambukizi ya Virusi vya UKIMWI na kugharamia bima ya afya kwa wote... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante, kengele ya pili hiyo.

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)