Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hanang'
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ENG. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye Bajeti yetu Kuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ameniwezesha kulihudumia Jimbo langu la Hanang kwa miaka mitano na hii ni bajeti yangu ya tano ninachangia na ninaamini ni bajeti ya mwisho kwenye mpango wetu wa miaka mitano. Ninawashukuru sana wananchi wa Hanang kwa jinsi ambavyo wamekuwa wakishirikiana na mimi, mara zote wamekuwa wakiniunga mkono wakati ninafanya shughuli zangu za Ubunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru wewe pamoja na Spika, Wenyeviti wetu wa Bunge, kwani mara zote nikiwa na jambo la wananchi wa Hanang wamekuwa wakinipa nafasi niliseme hapa Bungeni na Wanahanang kwa njia hiyo wamesikika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mawaziri wote, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Watumishi wote wa Serikali, kwani mambo mengi ya Wanahanang ambayo nimepeleka Serikalini tumepata majibu.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru sana Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mheshimiwa Queen Cuthbert Sendiga, mara zote amukuwa akiiangalia Hanang kwa jicho la pekee, ninamshukuru sana Mkuu wa Wilaya ya Hanang Mheshimiwa Almishi Hazali, kwani amekuwa akiwahudumia wananchi wa Hanang na tumekuwa tukishirikiana naye. Ninamshukuru Mkurugenzi kwa kuwa miradi mingi ambayo inapelekwa Jimboni kwangu yeye amekuwa msimamizi mkuu na amekuwa akisimamia vizuri na watumishi wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang kwa ushirikiano ambao tumekuwa tukifanya kazi nao.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushirikiano huu ambao nimeupata kutoka Serikalini umewezesha kwenye sekta ya miundombinu ya barabara kufungua Barabara ya Waama – Mureru kupitia Diloda, Barabara ya Hirbadaw – Mwanga, Barabara ya Mogitu – Gendabi. Tumeweza kufungua Barabara ya Dawar kwenda Ziwa Chumvi, Barabara ya Mulbadaw Kibaoni kwenda Bassodesh, Barabara ya Gijetamohog kwenda Garawja, Barabara ya CMC kwenda Bassodesh, lakini tumefungua barabara za lami kwenye Mji wa Kateshi. Pia tumejenga Stendi kubwa ya Kisasa pale Kateshi, Stendi ya Dkt. Samia Suluhu Hassan na stendi ile sasa inatumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Sekta ya Maji, ushirikiano nilioupata Serikalini umewezesha Mji wa Katesh kuwa na maji; pale imewekwa zaidi ya shilingi bilioni 10. Tumetekeleza Mradi wa Maji ambao unaenda Kata ya Gehandu na maeneo ya jirani, mradi ambao kwa sasa umefikia 80%. Wananchi wa Gehandu wanapata maji, yamebaki maeneo machache ambayo yanatakiwa yapelekewe maji ikiwepo eneo la Gidabwanja, Marega, Mwanina na Milongori.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumetekeleza Mradi wa shilingi bilioni 16 wa Ziwa Bassotu ambao kwa sasa umefikia kwenye 48%. Pia, tumeanza kutekeleza Mradi wa Bwawa la Bassotughang pale ambapo maji yameanza kutumiwa na wananchi na mradi ule unaendelea. Baada ya mradi ule kukamilika utahudumia Kata ya Dirma, Wareta, Simbay na maeneo ya jirani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushirikiano huo pia umeondoa adha ya maji kwenye maeneo ambayo yalikuwa korofi kama eneo la Backchand ambayo ipo kata ya Masakta pamoja na eneo la Basodami ambalo lipo Kata ya Balangdalalu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye umeme tulikuwa tuna vijiji 46 havikuwa na umeme, lakini sasa vijiji vyote vina umeme. Pia, vitongoji 64 vimepelekewa umeme, njiani tunavitarajia kupata vitongoji 81.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye Sekta ya Afya tumejenga vituo vipya vya afya saba. Pia, tumeboresha hospitali yetu ya Wilaya ya Tumaini na tumejenga zahanati zaidi ya 20.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye elimu tumejenga shule mpya za sekondari karibu sita, lakini tumejenga madarasa na tumejenga maabara. Maana yake Sekta ya Elimu nayo imekuwa bora. Ukiacha kujenga na kuboresha elimu ya msingi na elimu ya sekondari, tumejengewa Chuo cha VETA pale Nangwa na shughuli inaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mazuri yote haya ambayo yamefanyika kwenye eneo letu, Wanahanang wamenituma nimwombe Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais msikivu ambaye mara zote amekuwa akisikia kwamba barabara zetu kwa sasa nyingi zimekuwa korofi. Kwa mfano, Barabara kuu inayotoka Babati kwenda Singida, eneo la Dareda kwenda mpaka Gehandu mashimo yamekuwa mengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ile sasa kwa sababu ya mazingira na ubovu wake imekuwa ikisababisha ajali nyingi kwa sababu watu wanakwepa mashimo wanaenda pembeni mwa barabara. Pia, wananchi wanaotembea kwa miguu wamekuwa wakipata adha. Tuna barabara nyingi ambazo kwa kweli kwa sababu tumepata mvua nyingi zina hali ambayo si nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni Rais mpenda watu, Rais mbunifu na alibuni ile bond ya miundombinu kwa kushirikiana na CRDB na kwa kuwa zilishakusanywa fedha za kutosha, zile fedha sasa zitoke. Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Naibu Waziri, tunaomba zile fedha sasa zitufikie kwenye majimbo yetu, zile fedha zikakarabati barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliomba shilingi milioni 831 kwa ajili ya Barabara ya Mogitu kwenda Balangdalalu ambayo kwa sasa kama imekuwa njia ya maji. Watusaidie kwa sababu hiki ni kipindi cha mavuno na wananchi wanataka wakavune mazao yao na kuyasafirisha. Barabara ya Endagaw - Gidahababieg nayo imekuwa na makorongo mengi na haipitiki vizuri kwa sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, tuna barabara zetu zile ambazo ziliathirika wakati wa maporomoko ya Mlima Hanang. Kuna Barabara ya Endasak – Dawar na barabara ya Jorodom - Nangwa – Gitting; barabara hizi zina hali mbaya. Pia, barabara za Mji wa Katesh na barabara za Ganana tunaomba tusaidiwe zile fedha zikitoka mapema barabara zile zikakarabatiwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo, uchumi wa wananchi utachangamka kwa sababu wananchi wa Hanang ni wakulima wazuri na kwa hakika miundombinu ya barabara ni sawa na mishipa ya damu kwenye mwili wa binadamu; popote pale ukipata changamoto ya mshipa hutapata usingizi. Uchumi wa Hanang kwa sasa haupati usingizi kwa sababu ya changamoto ya miundombinu ya barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo mengine yote mengi yamefanyika mazuri, lakini kwa kuhitimisha tunavyoenda kwenye Ilani mpya tunayoenda kuinadi, tunayo barabara yetu ambayo tumekuwa tukiisema mara nyingi (Barabara ya Haydom – Mogitu). Barabara hii imeshafanyiwa usanifu wa kina na upembuzi yakinifu. Tunaomba fedha zitoke kwa ajili ya kuwalipa fidia wale ambao wataathirika ili barabara ile ianze kujengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati barabara hiyo inajengwa, tuangalie namna ya kujenga barabara chache za Mji wa Bassotu kwa sababu ule ndiyo mji mkubwa kwa maana ya Wilaya ya Hanang ndio eneo ambalo lina watu wengi. Tuangalie namna pia ya kujenga barabara za lami kwenye Mji wa Endasak, tuone namna ya kuendelea kujenga na kuboresha barabara za lami katika Mji wa Katesh na tuendelee kupeleka huduma za maji kwenye maeneo ambayo bado hatujafikia kwa namna ya kuunganisha vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, maji mengi tunayapata kwenye visima virefu, inavyoharibika pump wananchi wanakosa maji. Tuone namna ambavyo tunaweza kuunganisha vyanzo mbalimbali ili angalau tuweze kuwa na changamoto upande mmoja, upande mwingine uweze kupata maji na wananchi waendelee kupata maji muda wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimewasikia Wabunge wenzangu wakisema tutengeneze gridi ya maji. Tutengeneze gridi ndogo ndogo za maji ili kwamba upande mmoja ukiwa na shida upande mwingine uendelee kupata huduma. Kwa namna hiyo tutadhibiti suala la wananchi kukosa maji chanzo kimoja kikiwa na changamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nihitimishe hotuba yangu leo kwa sababu ndiyo mara ya mwisho nikisimama hapa Bungeni na nikipata nafasi labda kwenye maswali ya nyongeza na nini, niwashukuru sana wananchi wa Hanang. Sisi tunasema Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametufaa kwa mengi. Tulipata changamoto ya maporomoko ya Mlima Hanang, wengi ni mashahidi Serikali yote ilihamia Hanang na ilihamia Hanang kwa sababu ya upendo wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliona shida yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunasema inapofika Oktoba tutalipa fadhila kwa mema ambayo ametutendea na Wabunge wenzangu wamekuwa wakisema sisi ikifika Oktoba hatuna mjadala, tunatiki kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe wananchi wenzangu wa Jimbo la Hanang, nimewatumikia kwa muda ambao unakaribia miaka mitano. Kijana wao bado nina nguvu, nipo na nitaendelea kuomba idhini ya kuwatumikia tena. Wakati utakapofika tutayasema ya kwetu, tufanye kazi ya kuletea maendeleo Jimbo letu la Hanang.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)