Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana nami kupewa nafasi ya kuchangia katika bajeti hii muhimu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na mimi leo kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuchangia bajeti hii. Ninampongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake, kwa kipindi cha miaka minne wamefanya kazi kubwa sana ya kuliongoza Taifa letu na kuwaletea Watanzania maendeleo, akisaidiwa na wasaidizi wake wote, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Naibu Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitofauti sana utulivu wa nchi yetu umechangiwa na uimara wa vyombo vya ulinzi, vikiongozwa na Amiri Jeshi yeye Mkuu, ninavipongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee sana nipongeze uongozi wa Bunge ukiongozwa na Spika mahiri sana, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Naibu Spika pamoja na Wenyeviti na Watumishi wote wa Bunge. Wamefanya kazi kubwa sana kuongoza Bunge hili kwa kipindi ambacho tumekaa humu ndani, wapokee pongezi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi ama Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea sana kutambua mchango mkubwa wa wafanyakazi katika Taifa hili katika ujenzi wa uchumi, uzalishaji na utoaji huduma kwa Watanzania, hii yote ni kutokana na uimara na maelekezo mazuri ndani ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi katika Ibara ya 128, 129, na 130 ambayo Serikali inatekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi imeielekeza Serikali kuendelea kutoa mazingira mazuri ya vyama vya wafanyakazi, wafanyakazi na waajiri ili kuwe na harmony kule mahali pa kazi ili mwisho wa siko maslahi ya wafanyakazi na haki zao ziendelee kuboreshwa kwa umoja huu ambao tunaita utatu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha miaka hii minne ambayo Mheshimiwa Rais amekaa madarakani, nikiwa kama mwakilishi wa wafanyakazi na Wabunge wenzangu wakinisaidia, wafanyakazi walikuwa wana changamoto nyingi sana, lakini tumeona jinsi ambavyo Serikali ya Mama Samia imefanya kazi kubwa sana na huo ndiyo moyo wa Mama Samia eneo la watumishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni mengi sana ambayo tulishawahi kuchangia na wenzangu humu ndani, lakini leo nitaje machache tu machache ambayo Mheshimiwa Rais na Serikali yake wamewafanyia wafanyakazi wa Tanzania. Mojawapo ni kuwa, Serikali toka ameingia madarakani Mama Samia ameweza kupandisha madaraja watumishi zaidi ya 470,000, ametumia zaidi shilingi bilioni 689. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, si hivyo tu, Mheshimiwa Rais ameweza kulipa malimbikizo ya mishahara ya wafanyakazi na wale wastaafu. Kilikuwa kilio kikubwa, hakumaliza yote lakini amefanya kazi. Amelipa wafanyakazi na wastaafu na waliokuwa madarakani malimbikizo ya mishahara wanaotimia 187,000 na imemgharimu Serikali shilingi bilioni 318. Ni kazi kubwa Mheshimiwa Rais ameifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, si hivyo tu, Mheshimiwa Rais alivyoingia madarakani tu kilio kikubwa sana cha watumishi wale wa kima cha chini, mwaka 2022 akapandisha mshahara, kutoka 300,000 mpaka 370,000. Hakuishia hapo, juzi tu Mei Mosi mama amepandihsa tena. Kima cha chini kutoka shilingi 370,000 hadi shilingi 500,000. Huyo ndiyo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wafanyakazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, si hivyo tu, ameweza pia kuboresha pensheni. Sasa hivi bajeti ijayo wale kima cha chini wastaafu pensheni yao itaongezeka kutoka shilingi 100,000 mpaka 200,000. Amewakumbuka wastaafu hawa, maana maisha yanabadilika. Hawawezi kubaki kwenye mshahara huo huo pensheni hiyo wakati maisha yakienda yakibadilika. Huo ndiyo moyo wa Mheshimiwa Rais na Serikali kwa wafanyakazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, si hivyo tu, ametoa ajira nyingi zaidi ya 400,000, kuajiri siyo mchezo, wage bill kubwa inatumika, lakini tumeona nia yake ya kuongeza ajira kwa Watanzania. Ameanzisha hili suala la BBT, hii yote anajaribu kutanua wigo kwa vijana nao wapate ajira. Huo ndiyo moyo wa Mheshimiwa Rais kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais ameweza kurudisha watumishi kwenye utumishi wa umma waliotolea kwenye utumishi wa umma, amewarudisha zaidi ya 2,000. Huo ndiyo moyo wa Mheshimiwa Rais kwa watumishi na watumishi wa Tanzania wanasema Oktoba wanatiki kwa Mheshimiwa Dkt. Samia kwa maslahi bora ya wafanyakazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, si hivyo tu, ameendelea kuongeza bajeti ya OSHA, ameongeza wafanyakazi. Hawa ni watu muhimu sana, wanakagua maeneo ya kazi ili watumishi wafanye kazi katika mazingira ambayo ni salama. Huo ndiyo moyo wa Mheshimiwa Rais kwa watumishi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, si hivyo tu, hata kuongeza au kuruhusu tena ile 10% ya mikopo kule kwenye halmashauri zetu, huo ni moyo wa Mheshimiwa Rais kukuza wale wajasiriamali wa kati na wa chini ili angalau wawe na ajira, wawe na kipato. Hiyo ni sehemu ya ajira kwa watu ambao wako kule kwenye biashara ndogo ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, si hivyo tu, kwa moyo wake wa dhati alishauri, alipendekeza iundwe bodi, bodi ambayo itasimamia kima cha chini cha mishahara, sekta binafsi na sekta ya umma. Umma imefanya vizuri na juzi kwenye Mei Mosi tumemsikia akitamka, akiwaasa na kuwataka wale ambao wanasimamia upandishwaji wa kima cha chini cha mishahara sekta binafsi wafanye kwa haraka ili nao wasione wametengwa, watu wa sekta binafsi. Huo ndiyo moyo wa Mheshimiwa Rais kwa wafanyakazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote aliyofanya hayo, bajeti hii ambayo imesomwa na Mheshimiwa Waziri, ninampongeza sana wanafanya kazi kubwa sana na Naibu Waziri, imeendelea katika vipaumbele vyake vya utekelezaji wa bajeti iliyopita. Moja ya kipaumbele kati ya vitano ilikuwa ni kuendeleza rasilimali watu ili kuhakikisha ufikiwaji wa malengo ya Dira ya 2025 unafikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa habari njema sasa, hata juzi nimeangalia, katika bajeti hii waliyoisoma wameendelea kutekeleza kipaumbele hicho ambacho ni kuimarisha rasilimali watu hususan katika sekta ya huduma za jamii. Sekta ya huduma za jamii ina maana na afya iko hapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitasema kidogo kwenye afya leo. Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza sana kwenye afya, sana sana. Elimu kwa wabobezi, vifaatiba, miundombinu na kadhalika na kadhalika. Inastahili pongezi kubwa na bajeti hii tumeona ya afya imepanda kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze sana TRA, imefanya marekebisho ya TEHAMA na kutoa elimu na hamasa kwa wale wote wanaokusanya kodi ili mwisho wa siku pato la ndani liwe juu. Ninaipongeza sana TRA chini ya Kamishna mpya wa sasa hivi, lakini lazima sasa tufikie mahala mindset ya Watanzania ibadilike kutoka kwenye utegemezi wa afua za mambo ya afya kutoka kwa wenzetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima tu-finance Wizara ya Afya, tui-finance kwa viwango vya juu, katika vipaumbele tunatoa vipaumbele mbalimbali. Ninashukuru kwamba kuna uwekezaji kwenye kilimo, mifugo na kadhalika, lakini hawa watu tunaowekeza huko kama watakuwa afya zao ni mgogoro au wanauguliwa magonjwa sugu, hakika ufanisi wao katika uwekezaji utakuwa ni wa chini. Kwa hiyo, moja kwa moja tunahitaji kuwekeza sana kwenye Wizara ya Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wahisani wengi sana wamejitoa kwenye mambo ya afya na utaona hizi vertical program nyingi zinaelekea ku-collapse, huo ndiyo ukweli. Kwa hivyo.....
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kidogo muda. Ni kwamba, tulikuwa tunategemea wahisani kwa mfano Marekani, sasa hivi Irani wanapigana, anawekeza nguvu kuwa-support washirika wake. Tumeona kwenye bajeti ya Ujerumani wametenga zaidi ya trilioni moja Euro wameweka Jeshini, atakukumbuka kukuletea vifaatiba huyu? Hawezi kukumbuka!
Mheshimiwa Naibu Spika, nini ninachozungumza? Tuwekeze kwa hawa watu wanaitwa wahudumu wa afya ya jamii ya msingi. Kwa hiyo, hawa watatoa elimu chini ambayo itasawasaidia Watanzania wasifikie complication, wawahi hospitalini. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Dkt. Kaijage.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)