Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Liwale
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nikushukuru kwa nafasi ya kuchangia Hotuba hii ya Bajeti Kuu. Hotuba yangu la leo itajikita zaidi kwenye kushukuru na kupongeza na hapa nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kudumu kwenye nyumba hii miaka 10 leo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee vilevile kumpongeza na kumshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna alivyoisimamia Ilani cha Chama Cha Mapinduzi na namna anavyowatendea mema, mambo ya msingi, anavyoendelea kuboresha maisha ya Watanzania. Mwenyezi Mungu ampe afya na umri mrefu aendelee kututumikia kwenye Taifa letu hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pongezi hizo hizo pia zinakwenda kwa Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango kwa namna anavyomsaidia Mheshimiwa Rais kufikia malengo yake, vilevile Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu, kwa namna alivyoshiriki kikamilifu kumsaidia Mheshimiwa Rais. Pia, ninakupongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba na Naibu Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Hamad Hassan Chande. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli bajeti hii ni bajeti kama ambavyo Wabunge wenzangu walisema, ni bajeti ya mwisho kwenye Bunge hili la Kumi na Mbili, lakini ni bajeti ya wananchi. Tunapozungumza kwamba hii bajeti ni ya wananchi ni kweli kabisa hii bajeti ni ya wananchi, inakwenda kujibu matakwa ya wananchi, inakwenda kuboresha maisha ya wananchi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na Watendaji wake tunawashukuru sana. Pia pongezi hizi kwa Katibu wa Wizara hii kwa namna wanavyochapa kazi kumsaidia Mheshimiwa Waziri ili kufikia hapa tulipofika leo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika pongezi siziwezi kuacha kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson. Mimi amenilea kwenye Bunge hili zaidi ya miaka 10 leo, tunakushukuru sana Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson. Pia ninakushukuru Naibu Spika kwa namna anavyoliongoza Bunge letu na kututendea haki sisi Wabunge, tunaweza kudumu hapa Bungeni. Nisiwasahau vilevile Wenyeviti wetu wa Bunge ambao wao nao wako bega kwa bega kutusaidia kumsaidia Mheshimiwa Dkt. Tulia ili kuendesha Bunge vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mbunge wa miaka 10 leo, sitaacha kuwapongeza watumishi wote wa Bunge hili kwa namna walivyotuhudumia tangu tumeingia kwenye Bunge hili na tunakwenda kuhitimisha Bunge la Kumi na Mbili. Vilevile na wahudumu wetu kule nje mwa benki, Benki za NMB, CRDB, NBC, na AZANIA, kwa namna wanavyotuhudumia, kwa ujumla ninasema ahsanteni sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mwenyezi Mungu akijaalia mwezi Novemba tutakutana tena hapa, kwani Wanaliwale bado hawajachoka. Wanaona Mbunge wao ninawatumikia vizuri na wataendelea kunipa imani hii, ninategemea hilo. Kwa hiyo, Ndugu zangu miaka 10 siyo haba, mimi kama Zuberi yapo niliyopatia na yapo niliyokosea, lakini yote haya ni ubinadamu. Tunawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nimetanguliza shukrani? Nimetanguliza shukrani kwa sababu ya utekelezaji ulio bora wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Mimi ndiyo niliyokabidhiwa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwenye Halmashauri au Wilaya ya Liwale kuomba kura kuitangaza hatua kwa hatua na hapa ninasema kwamba Ilani imetekelezwa zaidi ya 95%, kwa hiyo, hasa kwa upande wa kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa kilimo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan sasa hivi ni mwaka wa nne mfululizo sisi wananchi wa Liwale au kwa Mkoa wa Lindi kwa ujumla wetu tunapata pembejeo bure pembejeo za kilimo, ile ni dhahabu ya Kusini, tunashukuru sana. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuona umuhimu siyo tu kwa kutupatia pembejeo za kilimo bure, lakini na uboreshaji wa bei. Kwa kweli sasa hivi hali imekuwa ni nzuri kidogo, kwa hiyo jambo hili ni jambo la kushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu nyingine inayofanya ninaendelea kushukuru ni tangu nimeingia kwenye Bunge hili kilio changu kikubwa ilikuwa ni Barabara ya Nangurukuru – Liwale, Barabara ya Nachingwea – Liwale. Ninashukuru mwaka huu nimeiona, kwenye bajeti hii nimeiona na Barabara yangu ya Nachingwea – Liwale, Masasi – Liwale kilometa 175, mwaka huu nimeiona inakwenda kuanza kilometa 55, hili ni jambo la kushukuru sana. Ninamwomba Mwenyezi Mungu na iwe hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Nangurukuru – Liwale kilometa 230. Mwaka huu tumetengewa kilometa 72 na kwa kuanza kwa mwaka huu tunakwenda kuanza kilometa 10. Jambo hili ni jambo la kushukuru sana na niendelee kumshukuru Mheshimiwa Rais na ninaendelea kuishukuru Serikali sikivu ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa wafugaji sisi katika Mkoa wa Lindi ndiyo Wilaya ambayo tulikubali kupokea wafugaji kutoka kule Ihefu. Ninaomba hapa napo niendelee kuwashukuru sana mwenye Wizara hii kwa namna anavyotutendea haki. Hapa niendelee kusisitiza, shida kubwa ya kuhama Ihefu iliyowapeleka Liwale ni kufuata malisho, kwa maana ya majani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli malisho yapo ya kutosha lakini wafugaji wale bado wanahangaika na masuala ya maji. Ndiyo maana wanahangaika, utakuta barabarani kiangazi wanahama kutoka Liwale wanaenda Rufiji, masika wanarudi Liwale. Ninaomba Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana hapa tuanagalie namna ya kuwapatia maji wafugaji wale ili wapunguze kijiji kile ufugaji wa kuhamahama, wabaki kule Liwale kama malisho yanawatosha na kwa sababu sisi tayari kule tumeshatengeneza mpango kazi wa kupanga eneo la wafugaji na eneo la wakulima ili kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali migogoro ile sasa inaendelea kupungua, ingawa bado haijakwisha, lakini inaendelea kupungua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuwashukuru watu wa Maliasili. Watu wa Maliasili tulihangaika sana hapa na jamii ya tembo na kweli juhudi zinaonekana, Ndege Nyuki tunawaona na wale vijana wa VGS kweli kabisa kwenye vijiji vyetu vijana kadhaa wamechukuliwa wamekwenda huko VGS kwenda kujifunza namna ya kuishi na wale wanyama, lakini kikubwa zaidi, mwezi uliopita tumepokea kifuta machozi, ingawaje unajua siyo kwamba kimekidhi haja kwa watu wote walioathirika, lakini angalau inaonyesha juhudi kwamba Serikali inawajali watu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka huu wamelipwa watu zaidi ya 2,690, wote hawa wamepata kifuta machozi na ndiyo maana kwenye hotuba yangu nikatanguliza kushukuru, kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema, asipomshukuru mwanadamu mwenzie basi hata Mwenyezi Mungu hawezi kumshukuru. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani hizi nimezielekeza kwa namna ambavyo sisi Wilaya ya Liwale kwenye kipindi hiki cha miaka mitano tumeweza kujenga shule za sekondari mpya tano, vilevile tumejenga vituo vya afya vya kisasa kabisa vitano, pia tumejengewa hospitali ya Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hospitali peke yake au vituo vya afya peke yake, vipo vifaa vya hospitali ambavyo zamani sisi pale unaweza kwenda kuvikuta Muhimbili au uende Sokoine au uende hospitali ya rufaa, lakini leo vifaa hivi vipo kwenye hospitali ya Wilaya ya Liwale. Kwa hiyo, tunapoendelea kuisifia Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, tunaisifia tunamaanisha na kweli tofauti zinaonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa maneno haya ninashukuru sana na naiunga mkono bajeti hii na ninawatakia kila la heri. Wabunge wote walioko kwenye Bunge hili tumwombe Mwenyezi Mungu mwezi Novemba tukutane hapa wote tukiwa salama kama ambavyo mimi wananchi wa Liwale wamenihakikishia kwamba watanirudisha na ninawaombea Wabunge wote walioko humu ndani warudi salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, Mungu awabariki sana. (Makofi)