Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Abeid Ighondo Ramadhani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ilongero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipatia nami fursa, ili niweze kusema maneno machache ya muhimu ya ku-wind up hotuba zangu tano za bajeti hii, ya tano tangu mimi nikiwa Mbunge mwakilishi wa Jimbo la Ilongero tangu waliponipatia kura mwaka 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kukuombea wewe jirani yangu mtaani hapa. Ninakuombea afya na tarehe 28 uende ukachukue fomu na tarehe 2 Mwezi wa Nane ushinde kwa kishindo. Tuna imani na wewe pia ninawaombea na Waheshimiwa Wabunge wenzangu wote, niwaombee afya na kila la kheri katika michakato hii inayoanza ili na wao waende wakarudi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema hivyo kwa sababu ya kazi nzuri ambayo imefanywa na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan katika maeneo yetu. Pia unafahamu timu huwa ina first eleven; Mheshimiwa Rais ameshatengeneza timu yake first eleven analo Baraza lake la Mawaziri ni zuri, anao Wabunge wake hawa wazuri. Kwa hiyo, hakuna haja ya kufanya vurugu kuwaondoa hawa Wabunge, wote watarudi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende niseme kwamba nimesoma vizuri hotuba ya Mheshimiwa Waziri nimeipitia maeneo mengi. Ninampongeza Waziri kwa hotuba yake na Mheshimiwa Kitila pamoja na Naibu Mawaziri kwa kazi yao nzuri wanayoifanya, kimsingi wanatusikiliza. Hawa sisi tunaitana comrades huwa ni watu ambao ni wasikivu na wanyenyekevu, tunaongea nao. Hakuna tofauti unapoongea na Mheshimiwa Waziri au Naibu Waziri ni kama unaongea na Mbunge mwenzako. Kwa hiyo, ninawapongeza na waendelee na utu na utendaji huo wa unyenyekevu katika kulitumikia Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina michango yangu kwenye mambo machache ninataka nizungumzie kwa kulingana na Hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Nitakwenda kuzungumza kwenye eneo la production sectors (sekta za uzalishaji) pia miundombinu ya usafiri na usafirishaji na maeneo ya viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza na haya nizungumze kidogo kuhusu tathmini yangu ya hii bajeti; ni kwamba tunapokwenda kuhitimisha Bunge hili la mwisho tunapoelekea kwenye uchaguzi, mimi kwa upande wa Jimbo langu la Singida Kaskazini tunakwenda kusema ndiyo tarehe 24 kwenye hii bajeti kwa sabbu kubwa zifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, kwenye maeneo ya huduma za kijamiii, eneo la afya jimbo letu limepata vituo vya afya, hospitali ya wilaya na zahanati. Kwa hiyo, kwenye eneo la afya lazima tukaseme ndiyo ili hizi huduma ziendelee kuboreshwa. Hapa tunapozungumza tunayo milioni 250 haijaanza kutumika ipo kwenye akaunti pale Halmashauri ya Wilaya kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kinyagigi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, tunayo pia hapo hapo fedha zinaendelea, ujenzi unaendelea pale kwenye Kituo cha Afya Ngimu shilingi milioni 686. Sasa hivi nina sababu gani ya kuja kusema no kwenye hii bajeti? Sisi wana Singida Kaskazini tumeheshimishwa sana na Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, bado tunataka tuendelee kumuunga mkono na hizi fedha ziendelee kuja ili wananchi wetu waendele kupata huduma. Huko kwenye afya leo tuna madaktari. Leo Ilongero tuna Madaktari Bingwa Ilongero kule ninadhani Waziri anaifahamu Singida. Tuna Madaktari Bingwa kule Ilongero wanafanya na upasuaji kwenye hospitali zetu, vituo vya afya pamoja na wilaya. Sasa kwa nini asiseme ndiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazo pia shule nyingi ambazo zimeota za msingi na sekondari kwenye maeneo yetu; Kiomboi Sekondari, Sekoutoure, Msange Sekondari, Msimii Primary, Minyaa Primary na zinaota kama uyoga. Unaona unaanza msingi, shule inaenda moja kwa moja kwenye kukamilika. Sasa ni lazima tuseme ndiyo, ili wananchi wetu waendelee kupata huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikizungumza kwenye hizi sekta za uzalishaji ambazo nimeona hata Mheshimiwa Waziri amezizungumza kwenye hotuba. Nchi yetu inahitaji kwenda kwenye uchumi wa viwanda. Tunahitaji kwenda kwenye uchumi wa mtu mmoja mmoja. Tuimarishe uchumi wa mtu mmoja mmoja na 90% ya wananchi wetu wapo kwenye kilimo, ufugaji na uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, nimeona Mheshimiwa Waziri ametupatia hata takwimu kwamba sekta hizi zimechangia kwa 4.05% kwenye uchumi wa nchi yetu. Sasa ni lazima hizi sekta ziendelee kuimarishwa, ili tuweze kuzalisha ipasavyo, hizi ndiyo zitakazolisha viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuondoke kwenye kuagiza raw materials nje ya nchi kuja kuhudumia viwanda nchini. Sisi hapa tuagize raw materials kutoka nje zije zihudumie viwanda vyetu. Siyo sisi kuchukua mahindi kupeleka Kenya, kuchukua samaki kupeleka Ulaya, kuchukua pamba kupeka Ulaya. Inatakiwa sisi tuzalishe halafu viwanda vyetu humu vihudumie wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi zitaongeza ajira hata zile nyingine ukiacha zile za moja kwa moja kwenye kilimo, hata informal zile ambazo inaenda kutokana na production inayofanywa na wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapokuwa na miundombinu mizuri ya barabara, reli kama unavyoona sasa hivi SGR na ninaomba sana hii SGR ikamilike iende mpaka kule kwenye mpaka wa nchi yetu. Iende mpaka kule Isaka na Kigoma ili mazao yanayozalishwa kule yaje kwenye eneo lenye viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ninapozungumza eneo la miundombinu ninagusa pia kwenye eneo la jimbo langu. Tuna barabara za muhimu ambazo zinahitaji kuboreshwa zaidi, kwa sababu sisi kule tunalima na kufuga. Sasa ile mifugo tunayosema twende kwenye kuhakikisha kwamba tunakwenda kwenye viwanda au kwenye masoko, ni lazima tuwe na miundombinu mizuri ya barabara, ili ziweze kusafirishwa ipasavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana ninasema ile barabara yetu ya kutoka pale Igauli kwenda Ilongero kwenye Makao Makuu ya halmashauri kilometa 11.5, ikamilike kwa wakati Iende mpaka Haydom ikamilie kwa wakati, ili tuunganishe Mkoa wa Simiyu, Manyara na Sindiga waache kuzunguka kutumia ile barabara ya mbali inayotoka Mwanza, ili kuwarahisishia wananchi kuwapunguzia gharama pamoja na usumbufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo kwenye barabara pia tunayo madaraja makubwa. Leo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kipenzi chetu anazindua Daraja la muhimu sana la kilomita tatu lile la Kigongo – Busisi. Haya ni mageuzi makubwa sana ya uchumi wa nchi yetu na ndio ambayo tulikuwa tunasema lazima yafanyike.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ighondo malizia kwa mchango mzuri, malizia.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono hoja, pia ninasema Serikali yetu lazima tuhakikishe tunapeleka nguvu za kutosha, tunaweka vipaumbele kwenye sekta za uzalishaji, ili ziweze kulisha viwanda vyetu na sisi tuweze kuajiri jamiii yetu ambayo kwa kiwango kikubwa ipo huko chini kwenye maeneo ya kilimo, ufugaji na uvuvi. Pia, umeme uendelee kufika mpaka kwenye vitongoji kama alivyosema Mheshimiwa Rais wetu juzi akiwa Mwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na ninaomba kuwasilisha. (Makofi)