Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muleba kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipatia fursa hii. Nimshukuru Mwenyezi Mungu muweza wa yote aliyetuwezesha kipindi cha miaka mitano kuwatumikia wananchi na hususan Wananchi wa Jimbo la Muleba Kusini na Wilaya ya Muleba. Ninaishukuru familia yangu kwa kuniwezesha, kunilinda na kuniombea.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa kipindi cha miaka mitano au hii Awamu ya Sita. Kwetu Muleba tunasema tunaunga mkono bajeti hii na tunamuunga mkono Rais wetu kwa kazi kubwa alizozifanya kwa kipindi cha Awamu yake ya Sita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenye macho hawaambiwi angalia na mambo yote yaliyofanyika kwa kipindi cha miaka mitano hatuhitaji kuyatangaza, yanajitangaza.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunapoongea Muleba tunafanya sherehe kubwa. Kahawa walikuma walikuwa wanauza shilingi 5,000, jana nimepokea taarifa kahawa imeapanda kutoka shilingi 5,000 imekwenda 11,755 kwa bei ya Robusta, maganda wanauza kwa shilingi 5,500. Arabica inakwenda 11,500 kahawa safi na shilingi 5,500 kwa Arabica maganda. Hii ni kazi ambayo imefanywa na Serikali ya Awamu ya Sita. Ninawashukuru Waziri Mkuu alifanya kazi kubwa kuhakikisha kwamba, wakulima wanapata bei nzuri na ninamshukuru Rais wetu kwa sababu ndiye aliyemtuma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru Mawaziri kwa bajeti hii nzuri waliyotuwasilishia hapa Bungeni. Binafsi nimshukuru Mheshimiwa Chande kwa kazi kubwa anayoifanya, viongozi wote wa Wizara na Makatibu Wakuu. Kusema kweli kama Mbunge wa Jimbo la Muleba Kusini ninasema na juzi tumepita tumekubalina kwa Muleba tunakwenda kuwa namba moja kwa kura za Rais Oktoba. Wanaotaka kushindana waje wajifunze kwetu na tunayo sababu ya kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo ninamshukuru Rais anazindua Daraja la Busisi, lakini kwetu pale Muleba tuna Daraja la Mto Ngono na Daraja la Kamishango. Kusema kweli ni mfupa ulioshindikana miaka nenda rudi, lakini tunavyoongea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametupatia fedha shilingi 12,500,000,000 tunajenga lile daraja ambalo lilikuwa ni shida kubwa kwa Wafanyabiashara wa Wilaya ya Muleba kwa sababu maeneo yote ya Nshamba na Mgongo wafanyabiashara wanaoleta magari makubwa walikuwa wanalazimika kushusha mizigo kupakia kwenye magari madogo, ili wapite kwenye daraja lililokuwepo, lakini Mama Samia amesema hayo sasa basi, tunamshukuru kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, inakwenda kuchangamsha uchumi kwa sababu bidhaa zilikuwa zinauzwa kwa bei kubwa kwa sababu ya gharama kubwa ya usafirishaji. Vilevile, kana kwamba hilo halitoshi ninakushukuru nimesema Mheshimiwa Chande alitusaidia sasa Hospitali ya Wilaya ya Muleba Makandarasi wapo site. Majengo yanapanda kwa kasi na Wanamuleba wanasema ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wengi wamesema hapa sisi kwetu Muleba tumejenga shule mpya 16 ambazo zimepunguza umbali wa watoto wetu kwenda na kurudi shuleni. Shule zenyewe ni za vigae zile.
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilikuwa ninaongea na mama mmoja akaniambia alikuwa na biashara yke ya kuuza viatu vya wanafunzi akasema biashara yake imekufa kwa sababu Mama Samia amejenga shule karibu na wanafunzi, hawasafiri umbali mrefu. Kwa hiyo, viatu walivyokuwa wanatumia havichaniki kwa haraka kwa sababu wanasafiri umbali mfupi. Hii ni kuchangamsha uchumi. Yule mama nilimwambia pole, lakini hongera hiyo ndiyo kazi ya Chama Cha Mapinduzi na ndiyo kazi waliyotutuma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo kwa Wilaya ya Muleba hatuna jambo, hatuna neno lolote. Kazi yetu ni kwenda kujaza kura Oktoba wameshakubalina ni kwenda ku-tick tu hatuna jambo lingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa miundombinu; 2020 kuna maeneo ambayo yalikuwa hayafikiki. Kwangu pale kwenda Burigi ninadhani wananchi wa Burigi wananisikia. Wakati ninakwenda kuomba kura ilibidi nitumie pikipiki, lakini juzi nilienda pale nimeshangaa mpaka daladala zinafika na zinalala kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi iliyofanyika ni kubwa na ndio maana ninawaomba Wanamuleba tutoe turudishe shukrani yetu ifikapo Oktoba na kazi lazima iendelee na Muleba inakwenda kuwakawaka kama ambavyo wilaya nyingine zimefanya. Hayo yaliyofanyika Muleba yamefanyika wilaya zote na hii ni kazi ya Rais wa Awamu ya Sita.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana niwaombe Wanamuleba, Mbunge wanaye yupo anarudi hakuna propaganda na mbambamba, kazi tumeifanya na aliyetuwezesha ndiy huyo tunakwenda kumrudisha. Kwa hiyo, yaliyofanyika awamu hii ndiyo yale yatakayofanyika awamu ijayo. Tuendelee kumwomba Mungu atupatie uzima, ili tuendelee kutumikia wananchi wetu. Kazi imefanyika na itaendelea kufanyika na ndiyo hiyo falsafa ya Mama, kazi iendelee na kweli itaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo mengi yapo mbele ila kwenye hili nishauri mambo machache. Kwenye bajeti iliyowasilishwa Mheshimiwa Waziri ameongelea kwenye para 15 ya hotuba yake Sheria ya Msajili wa Hazina ameongelea kubadilisha vipengele viwili, kipengele cha 8A na 8F. Ninaomba hiyo sheria badala ya kubadilisha hicho kipengele pekee, tukaifanyie marejeo sheria nzima kwa sababu tunataka fedha na Msajili wa Hazina…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Dkt. Kikoyo, malizia.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga hoja mkono. (Makofi)