Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi asubuhi ya leo kutoa mchango wangu kwenye Hotuba ya Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2025/2026. Nami niungane na Wabunge wenzangu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa namna ambavyo ametuwezesha kulitumikia Bunge hili la Kumi na Mbili na hatimaye tunaelekea ukingoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi ninamshukuru sana kwa afya njema kwa viongozi wetu na kwa sisi sote, na leo michango ya Bajeti ya Serikali ambapo mimi nimechangia karibu kila mwaka, na leo ni mchango wangu wa mwisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru Mheshimiwa Spika, Dkt. Tulia Ackson, nikushukuru na wewe Naibu Spika kwa namna ambavyo mmetuwezesha sisi Kamati yetu ya Bajeti tangu mlipotuteua kwa miaka mitano mfululizo, tumefanya kazi hiyo kwa uadilifu, weledi na kujitoa. Hapa niipongeze sana Serikali yetu ya Awamu ya Sita kwa kipindi chote cha miaka mitano ya kutumikia hii Kamati ya Bajeti, kwa kweli wametoa ushirikiano wa kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni Serikali sikivu pale ambapo tulikuwa tunabishana ilikuwa ikitafakari, ikiona hoja ya msingi na ikikubali mapendekezo yetu, na kwa kweli tumeenda vizuri mpaka tutakapohitimisha tutapopitia hii Finance Bill. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombee dua viongozi wetu wote, Spika na wewe Naibu Spika katika mchakato mnaoendea na wao Mawaziri, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, Mheshimiwa Prof. Kitila na Manaibu wote kwa namna ambavyo wamefanya kazi, Mwenyezi Mungu awawezeshe kuwarejesha, pia na Wabunge wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina faraja kubwa ninapohitimisha kuchangia bajeti hii ya mwaka huu, kwa sababu kama nilivyosema, nimechangia bajeti zote, lakini faraja yangu ni kuona ninachangia kitu ambacho kinaleta manufaa kwa Taifa. Tunachangia bajeti ambazo wanafikia malengo, wanakusanya, na fedha zinafikia kwenye miradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninafurahi kwamba bajeti wakati tunaanza awamu hii ya sita kutoka makusanyo ya zaidi ya shilingi trilioni 25 mpaka sasa tunapohitimisha nyongeza ya makusanyo ya mwaka huu, matarajio ya kufika trilioni 30 na kuvuka malengo kwa mara ya kwanza kulingana na kiasi ambacho walikadiriwa kwenye mapato ya ndani, kwa hiyo, hicho ni kipimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipimo kingine kwa Serikali hii kufanya vizuri ni kwa matumizi ya maendeleo ya hasa kwenye mapato ya ndani, kutoka shilingi trilioni tisa mwaka 2021 mpaka shilingi trilioni 12 mwaka huu 2024/2025 unaoendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake, ukurasa wa 22 mpaka 23 ya kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupambana na maadui watatu: ujinga, umasikini na maradhi kupitia kazi mbalimbali alizozifanya katika kuingoza hii Serikali ya Awamu ya Sita. Kwa nini Mheshimiwa ninasema hivyo? Kwanza, sisi katika Mkoa wa Pwani tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwani kwa bajeti zote mpaka Machi, 2025 tumepokea kiasi cha shilingi trilioni 1.35 fedha za kwenye maendeleo, lakini pia kugharamia shughuli mbalimbali za Kiserikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye mapambano dhidi ya ujinga, tunamshukuru Mheshimiwa Rais pamoja na jitihada zote za Kitaifa, na jana tumeona akizindua shule ya amali kuwakilisha shule 103. Kwa Mkoa wa Pwani, tunamshukuru kwa kiasi cha shilingi bilioni 83 alizotuletea kwa ajili ya miundombinu ya elimu, lakini pia kwa ajili ya elimu bure ambayo amekuwa akiiendeleza mpaka kufikia kidato cha sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujenzi wa shule mpya, ujenzi wa shule ya wavulana, ujenzi wa shule ya wasichana, ujenzi wa shule nne za amali, na ujenzi wa vyuo zote, tumepata na tunaamini kwa kupitia miundombinu mipya na kwa mara ya kwanza tumepokea fedha nyingi kwenye sekta hii. Ni wazi ujinga katika mkoa wetu, Mheshimiwa Rais amepambana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kana kwamba haitoshi, katika mapambano ya umaskini ndani ya mkoa wa wetu, tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwanza kwa uboreshaji wa miundombinu ya barabara, na madaraja kiasi cha shilingi bilioni 92 kwa ajili ya barabara vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye ujenzi wa madaraja, hapa ninaomba niliseme, Daraja la Wami Mkoa wetu wa Pwani, Daraja la Mbuchi visiwani delta, Daraja la Mbwera, Daraja la Mbambe pamoja na Daraja la Muhoro yamesaidia sana kuwezesha wananchi kufanya shughuli zao, kuwezesha kufunga kwa mawasiliano na kuwezesha shughuli za kiuchumi kuchangamka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kana kwamba haitoshi, katika kupambana na umaskini, sekta ya nishati kukamilika kwa Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere wa shilingi trilioni sita, unajengwa ndani ya mkoa wetu wa Pwani, kukamilika kwa substation ya Chalinze, na kukamilika kwa njia ya kusafirisha umeme kutoka Rufiji mpaka Chalinze. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, kwenye sekta ya viwanda, ongezeko la viwanda 135 ndani ya mkoa wetu wa Pwani, ambao umezalisha ajira nyingi; pia, ongezeko la ruzuku ya mbolea kwa wakulima wetu wa korosho pamoja na bei nzuri ya korosho na mazao ya ufuta, ninaamini ni kupambana na umaskini. Amekuwa Rais ambaye amefanya hayo kwa kiwango zaidi kuliko wakati wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kwenye kupambana na maradhi, tunamshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa zaidi ya shilingi bilioni 28 alizopatia Mkoa wetu wa Pwani. Kipekee kwa Hospitali yetu ya Rufaa ya Tumbi kwa kuhakikisha hospitali ile kwa mara ya kwanza ina CT-Scan, wodi za ICU na emergency. Pia, kutujengea vitu vya afya zaidi ya 19, kutukarabatia hospitali za wilaya, na kutujengea zahanati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee utaratibu wa kusafirisha wajawazito M-Mama kwenye maeneo ya delta umewezesha kupunguza vifo vya akina mama, na ni wazi kwamba mkakati huu umepambana na maradhi ya ndani ya Mkoa wetu wa Pwani na kutuwezesha kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima hilo la nishati, ninapenda kutoa shukurani za dhati kwa namna ambavyo wametuwezesha eneo la visiwani. Ilikuwa haitarajiwi kupata umeme wa gridi ya Taifa, lakini leo ukienda Kibiti, Kata za Mbuchi, na Kihongoroni, huko kote kuna umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, niishukuru ilani inayoendelea sasa hivi na kwa kweli Mheshimiwa Rais hana deni kwa kuleta Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Bagamoyo. Hata hivyo, ahadi ya kulipa fidia ni kilio cha miaka mingi tangu 2015 wakazi wa Kata ya Zinga maeneo ya Mlingotini, Pande, wanaenda leo kupata ahueni ya kulipwa fidia na tarehe 26 Serikali itakuwa Wilayani Bagamoyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ambayo tulikuwa tunaitarajia muda mrefu pia utaongeza shughuli za uvuvi katika Wilaya yetu ya Bagamoyo. Kwa mara ya kwanza pia tumeshuhudia kilio cha kulipwa fidia cha Barabara ya Tanga – Pangani – Mkange inayoelekea Makurunge fidia imelipwa mwaka huu 2025. Ilikuwa kilio cha muda mrefu lakini Serikali imelipa fidia Barabara ya TAMCO kwenda Mapinga ambayo ilikuwa kilio cha muda mrefu. Hizo zote ni jitihada za kupunguza umaskini wa watu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimalizie kwa kweli Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hana deni amefanya kazi nzuri na inaoekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie pia kwa kuwashukuru UWT wa Mkoa wa Pwani kwa kunipatia fursa ya kuwa Mbunge wa vipindi vitatu kwa Chama Cha Mapinduzi kwa uongozi wa juu. Mwenyekiti wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan na Katibu Mkuu, Dkt. Emmanuel Nchimbi kwa kuteuliwa kuwa wagombea ndani ya Chama Cha Mapinduzi na kwa viongozi wangu ma-boss wangu wa UWT Taifa, Mama Mary Chatanda, Mama Zainab Shomari na Katibu Mkuu Mama Suzan Kunambi kwa kazi nzuri ya kutembelea miradi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaposimama hapa tumetoka kwenye ziara Mkoa wa Pwani, tumetembelea miradi zaidi ya 131 yenye thamani ya bilioni 359; tumefanya mikutano ya hadhara 77. Yote hayo ni mazingira yaliyowekwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kufanya Vyama vya Siasa vifanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli hakuna wa kulinganishwa naye. Tumefanya kazi ya kibunge kwa wepesi. Tunamshukuru kwa majiko ya gesi 200 aliyotupatia. Tunamshukuru kwa mashuka 100 kila Mbunge Mwanamke aliyepatiwa tumepeleka katika maeneo yetu. Hakuna wakati kazi ya kibunge imekuwa rahisi kama Bunge hili la Kumi na Mbili, unapata ziara unafanya, hakuna maeneo hukosi la kusema. Kwa hiyo, ninataka kusema Mkoa wa Pwani tumejipanga kumpatia kura za kishindo Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hana deni nchi nzima na hana deni ndani ya Mkoa wetu wa Pwani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipatia nafasi. Hongera kwa Wizara ya Fedha na taasisi zote waliofanya kazi hii nzuri. Hongera Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa kuanza kazi vizuri. Ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuunga mkono hoja hii. (Makofi)