Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtwara Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninakushukuru nami kwa kupata nafasi hii ya kuchangia Bajeti Kuu iliyokuwepo mbele yetu, lakini nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha siku ya leo na takribani miaka yote mitano tukiwa humu Bungeni tukitekeleza majukumu tuliyopewa na wananchi ya kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na wenzangu kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na ni Rais wa pekee Afrika. Kwa muda mfupi ameonesha uimara wake na uthubutu ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwahudumia Watanzania, kwa kutuletea maendeleo ambayo yametukuka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninawashukuru Mawaziri wote wawili ambao leo tunajadili bajeti zao. Kaka yangu, Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo niseme ninamshukuru sana, sana, sana kwa sababu amefika mahali ameonesha sasa alichomwagiza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kufungua Mtwara, amelipokea, na sisi tunamshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunamshukuru Rais kwa ujenzi wa bandari ya kisasa ambayo iligharimu zaidi ya shilingi bilioni 157 ambapo sasa meli ya aina yoyote ile inafunga pale na shughuli nyingine za kijamii zinaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiingia kwenye suala la afya, tunayo hospitali yetu ya kanda ambayo ilisimama kwa muda mrefu sana, lakini alivyoingia Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliweza kuiwezesha hospitali hii na sasa imekuwa ni hospitali ya mfano kwenye kanda ya kusini. Watu wa Msumbiji na maeneo mengine wanapata tiba pale. Tunamshukuru sana Rais na tunajivunia Wanamtwara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda mrefu wananchi wa Mtwara walikuwa wanatembea zaidi kilometa 400, 500 kwenda kutafuta huduma ambazo zinaweza kupatikana Muhimbili na maeneo mengine. Kwenye hili tunamshukuru sana Mheshimiwa Rasi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hilo tu, wakati tunaingia mwaka 2020 tulikuwa tuna shida ya maji Mtwara. Maji yetu yalikuwa yakitoka kwenye bomba, unaona ni maji ya njano kama jezi ya Young African, lakini Mheshimiwa Rais aliweza kutupatia fedha za kujenga chujio la kisasa zaidi ya shilingi bilioni 3.4.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wetu hakuishia hapo tu, akatuletea fedha tena shilingi bilioni 29 kwa ajili ya kutengeneza miundombinu na kuweka mabomba ya kisasa kwa sababu bomba zote ambazo zilikuwepo ni bomba ambazo ziliwekwa na mkoloni na bomba zile zilikuwa za chuma. Haya yote Rais ameona kwamba kuna haja ya kuwawezesha wananchi wa Jimbo la Mtwara wapate maji yaliyokuwa salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo mradi huo tu, ametujengea tenki kubwa pale airport la zaidi ya shilingi milioni 500, na tenki hilo limeanza kufanya kazi maeneo yote ya pembezoni zaidi ya kata kama nne, tayari maji yameshaanza kupelekwa, na wananchi wanakunywa maji hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, ninamshukuru tena Mheshimiwa Rais, tulikuwa tuna mgogoro mkubwa sana baina ya wananchi na tajiri mmoja ambaye sasa hivi ni marehemu. Eneo lile Mahakama iliamuru kwamba nyumba zile zote zivunjwe, lakini baada ya hapo tukarudi tena Mahakamani, tukatumia diplomasia, na Rais akaweza kutusaidia nyumba zile zimebaki, wananchi wale wamebaki, na sasa hivi wanaendelea kupewa hati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni Rais wa pekee kufika mahali akatambua kwamba kuna wananchi ambao wanapata shida na wanatakiwa kusaidiwa. Vilevile, katika eneo ninalozungumza la visima vyetu vya maji, Mtawanya, miaka hiyo wakati panatengenezwa visima hivi vya maji wananchi walitoa ardhi zao takribani miaka 30 iliyopita, lakini walikuwa hawajalipwa fidia. Nilipiga kelele Bungeni na Mheshimiwa Rais alisikia hilo, akatupatia fidia, pesa zaidi ya shilingi milioni 770. Nani kama Mama Samia? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema yale yanayosemwa kwamba sisi hatuna deni, yaani tunachelewa tuone lini tunakwenda kumpigia kura Rais huyu wa mfano ili Watanzania na maeneo mengine wajue kabisa kwamba wananchi wa Mtwara Mjini wameridhika na huduma za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna hospitali zetu mbili, tuna hospitali ile ya kanda, na tuna hospitali ya rufaa. Hospitali hizi zote zilikuwa hatuna vifaatiba, lakini ukienda hospitali za kanda ya kanda pale utakuta kuna ma-CT scan, na kuna MRI. Mashine zote ambazo ziko Muhimbili unazikuta pale Hospitali ya Kanda Mtwara. Pia ukija kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, huduma zote zinazopatikana kwenye hospitali ya kanda zinapatikana pale. Hongera sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tunakushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo letu la Mtwara Mjini tuna takribani kata zaidi ya 11, hazina shule za sekondari, lakini Rais, Dkt. Samia ametuwezesha ndani ya miaka hii mitano kutupatia shule za sekondari tatu za kisasa, za mfano ambazo zina maabara na mambo ya sayansi yameanza mle, na vijana wameshaanza kuji-tune kwa ajili ya kusomea sayansi.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hilo tu, tumepata shule za msingi mbili za kisasa. Tumepata pale Chihiko Kata ya Mtawanya lakini tumepata shule nyingine pale Ufukoni. Shule hizi ni nzuri na ni shule za mfano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa ambalo wananchi wa Mtwara wanamwombea Rais wao awe na maisha marefu ni kutukubalia kutujengea Daraja la Mozambique na Tanzania pale Mto wa Kilambo. Hili ninasema, katika kelele zote tulizokuwa tunazisema hapa Bungeni kuhusu ujengwaji wa daraja lile Mheshimiwa Rais amelipokea na tayari liko kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tunapozungumza, wananchi wa Mtwara wanamsubiri Rais wao sasa wampokee kwa shangwe na sherehe jinsi yeye anavyofika mahali akasema kwamba Mtwara ataifungua. Neno la Rais analosema ataifungua Mtwara limeanza kuonekana siyo kwenye daraja tu. Leo katika airport ile tunajengewa sasa jengo la abiria la kisasa na ameshaleta fedha zaidi ya shilingi bilioni 63 tunakwenda kujenga Mtwara International. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka kuzungumzia suala la mazao. Mtwara ni eneo ambalo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Malizia.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mtwara ni eneo ambalo kilimo chetu ni cha korosho, lakini hatujawahi kuuza korosho kilo shilingi 4,200.00 na kuendelea. Rais huyu wa sasa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ametuwezesha kupata mbolea za kisasa na wakulima wakapata mbolea, na sasa korosho imekuwa ni hitajio kubwa, lakini hata hivyo wananchi wa Mtwara wameanza kuwa matajiri kupitia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)