Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Edward Olelekaita Kisau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kiteto

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa nafasi. Kwanza tumshukuru Mwenyezi Mungu, ametulinda miaka mitano yote hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, tumpongeze Mheshimiwa Dkt. Samia kwa sababu Bajeti Kuu ya Serikali tunayoihitimisha ni hitimisho la awamu ya kwanza ya Meshimiwa Dkt. Samia. Ametekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa kishindo kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niwapongeze Waheshimiwa Mawaziri, Prof. Kitila Mkumbo, Dkt. Mwigulu Nchemba, Waheshimiwa Manaibu Mawaziri wote wawili wa Fedha, Mipango na Uwekezaji; rafiki yangu wa Kamati Kuu shikamoo; Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu, na wataalam kwa hotuba hizi mbili za hali ya uchumi na Bajeti Kuu ya Serikali. Tunaipongeza pia Kamati ya Bunge ya Bajeti kwa maoni yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunampongeza Mheshimiwa Dkt. Samia kwa miaka minne ya uongozi wake na utekelezaji wa Ilani wa Chama cha Mapinduzi 2025. Ilani hii imetekelezwa kwa viwango vya juu sana na kwa umahiri mkubwa sana. Kishindo cha Mheshimiwa Dkt. Samia kupitia miradi ya maendeleo kimesikika kwenye majimbo yote Tanzania na kila mahali.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi hii ya maendeleo imetujengea Waheshimiwa Wabunge heshima kubwa sana kwenye majimbo yetu. Imeleta kigugumizi kikubwa sana kwa wale wanaotamani majimbo haya kwa sababu wananchi wameona miradi ya maendeleo ikitekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Kiteto tuna miradi ya zaidi ya shilingi bilioni 160. Shule za sekondari, vituo vya afya, shule za msingi takribani 20, maji, miradi kila mahali. Kwa kweli hii imekijengea taswira na heshima kubwa Chama chetu cha Mapinduzi kwa wananchi wa Tanzania; na ninadhani ndani ya miaka mitano tumejenga uhalali wa kuliongoza Taifa hili kwa kipindi kingine tena.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunawashukuru sana wananchi wangu wa Kiteto kwa ushirikiano mkubwa sana walionipa na kwa ari yao ya kupenda maendeleo. Ninawashukuru na viongozi wa mkoa, Mheshimiwa RC, Mwenyekiti wa CCM na viongozi wote; DC na Mkurugenzi wa Wilaya ya Kiteto na Wataalam wote kwa ushirikiano walionipa kwa miaka mitano.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bajeti Kuu hii ya Serikali ina sifa takribani tatu kubwa. Kwanza, inahitimisha dira ya maendeleo ya Taifa ya miaka ya 2025. Tunahitimisha na Bajeti hii Kuu ya Serikali. Pili, inahitimisha Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2025; na ninadhani huu utekelezaji wa ilani unaoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia imetujengea heshima kubwa sana na inatupa fursa kubwa ya kuendelea kuomba ridhaa ya Watanzania kwa kipindi kingine kijacho.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukizungumza habari ya ajira, tumekwenda zaidi ya tulivyoahidi kwenye ilani. Tuliahidi ajira milioni nane, lakini Bajeti Kuu ya Serikali hapa ajira imekuwa zaidi ya milioni nane. Kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi tulisema tutapeleka umeme vijijini. Tumemaliza na tunakwenda kwenye vitongoji sasa. Hatukuwa na vitongoji kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunavyosema, hatumdai Mheshimiwa Dkt. Samia tunamaanisha. Ni utekelezaji wa ilani na mkataba tulioandika na Watanzania, amemaliza kwa kishindo kikubwa sana. Haimaanishi kwamba tumemaliza matatizo yote, hapana, ndiyo maana tumeandika ilani nyingine ya miaka mingine mitano ijayo. Maendeleo ni safari, lakini tulichoahidi kupitia ilani hii Mheshimiwa Dkt. Samia ametekeleza kwa viwango vya juu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii vilevile, inahitisha safari ya miaka mitano ya Bunge la Kumi na Mbili. Kwa hiyo, ni bajeti kuu ambayo ina sifa hizo. Bajeti Kuu ya 2025/2026, ili kuweza kupima uzuri wa utekelezaji wa bajeti ama mipango yenyewe ni lazima iwe na sifa zifuatazo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, lazima iseme ina kitu kinaitwa fiscal responsibility, ama nakisi inayoweza kudhibitika ambayo haileti deni ambalo litatikisa uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma hotuba hii utaona mipango, deni letu himilivu, lakini lingine ni lazima tuone ukuaji wa uchumi na uhimilivu (economic growth na stability) na zote ziko kwenye bajeti hii. Sifa ya bajeti tukipata misukosuko, je, tunaweza tukapambana nayo? Ndiyo sifa ya bajeti ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumepata majanga mengi hapa, kwa mfano, Hanang kule hakuna mtu aliyetegemea, lakini kama kuna jambo ambalo Serikali imefanya kwa viwango vya juu sana na kila wakati ninawaambia, ambayo inastahili kurekodiwa, namna bora ya kupambana na majanga ni namna Serikali ilivyopambana na janga la Hanang’ kule. Kwa hiyo, bajeti yetu lazima iweze kupambana na mabadiliko ya uchumi na sera za Kitaifa. Ukisoma bajeti hii, utakuta hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sifa ya bajeti ni lazima iwe na usawa wa kijamii (social security) je, inapambana na umaskini? Inapambana na ujinga na maradhi? Hospitali tunazojenga na vituo vya afya tunaendelea, tuko kwenye safari ya kupambana na maradhi. Ujinga: shule tunazojenga na vyuo na miradi iliyoko hapa, lakini tunakuza uchumi tunapambana na umaskini. Ukisoma bajeti hii, utakutana na vitu hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nyingine ni uwazi kwenye usimamizi wa matumizi ya Serikali. Ukisoma hotuba hii, utakutana na mipango. Kazi ya Bunge ni kuisimamia Serikali, kazi ya CAG kila wakati ni kufuatilia namna ya kuweka nidhamu na kuongeza transparency na accountability, na zote ziko hapa. Sifa nyingine ya bajeti inatoa vipaumbele kwa miradi ambayo inaleta pesa kwa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ukisoma vilevile bajeti hii utaona kila kitu. Vilevile, bajeti lazima ioneshe vyanzo vya mapato, na vyanzo vyetu ni kodi. Ni lazima tulipe kodi. Kwa hiyo, mapato mengi yanatoka TRA, mapato yasiyo ya kodi ndiyo vyanzo vingine, mapato kutoka Serikali za Mitaa, mikopo ya nje na ya ndani, pamoja na misaada. Kwa hiyo, hoja hapa siyo mikopo, kila mtu anakopa, hata sisi wenyewe tunakopana huko mtaani. Tatizo, tunatumiaje mikopo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunachukua leo hii mkopo kama ule wa UVIKO – 19 na kupeleka miradi katika majimbo yote Tanzania, nani ana-questions kuhusu mikopo? Kama tunachukua leo tunajenga Daraja la Busisi ama Bwawa la Mwalimu Nyerere ama SGR ambaye kila mtu anapanda na anafurahia huduma hiyo. Ama kufanya bandari yetu ambayo ndiyo inaleta asilimia kubwa, karibu 40% ya mapato ya TRA; kama tunafanya hivyo na tunaendeleza uchumi wetu, nani analeta hoja za kukopa hapa? Sisi ni nchi maskini, mikopo ni chanzo kikuu na ni muhimu sana. Tukiongeza mapato yetu, na siku tukaondokana na hilo, hakuna mtu atataka kukopa… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa advocate, malizia…

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa nafasi. Ninadhani bajeti yetu imekidhi viwango vyote vya Kimataifa na sifa kuu za bajeti. Kwa hiyo, niongee na Watanzania wenzangu kwamba mwaka huu wa uchaguzi tumchague Mheshimiwa Dkt. Samia kwa kishindo kikubwa sana. Zawadi pekee ni kushiriki kwenye uchaguzi huu mwaka huu na mimi ninawatakia na Wabunge kila la heri Mwenyezi Mungu awabariki. Ahsanteni sana, ninaunga mkono hoja. (Makofi)