Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. Jasson Samson Rweikiza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami nichangie kwenye Bajeti ya Serikali. Ninapenda kuanza kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa sana anayoifanya ya kuigwa mfano. Amevunja rekodi, kama nitakavyoonesha hapa kwenye maelezo yangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru na kumpongeza Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Uwekezaji, Mheshimiwa Kitila Mkumbo, Naibu Waziri na watumishi wote wa Wizara hizo mbili kwa kazi nzuri safi kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Kagera ninamshukuru Mheshimiwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wa Mkoa, Nazir Karamagi kwa kusimamia vizuri Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru Mheshimiwa Fatma Mwassa, Mkuu wa Mkoa kwa kusimamia vizuri utekelezaji wa ilani. Ninamshukuru Mheshimiwa Evarista Babyegeya, Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Bukoba Vijijini, Mheshimiwa Erasto Sima Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Proskovia Jaka Mwambi, Afisa Tawala wa Wilaya, na Fatina Laay, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Wilaya ya Bukoba Vijijini. Tunafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na tunasonga mbele pamoja kwa ushirikiano mzuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunawashukuru sana wananchi wa Bukoba Vijijini, tunafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa sana kwenye kazi zetu za kila siku za kuleta maendeleo Bukoba Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Bukoba Oktoba ikifika kura zote ni kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Kama nilivyosema, amevunja rekodi, rekodi ambayo haijawahi kuvunjwa. Ameweka rekodi mpya. Jana mlimsikia Mheshimiwa Byabato, Mbunge pacha wangu wa Bukoba Mjini; sisi tumeshakubaliana na wananchi wetu kwamba, kura zote ni kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze Bukoba pale kwa upande wa sekta ya maji. Mheshimiwa Samia ndani ya miaka minne ameweza kufanikisha kufunga miradi ya maji na yanatoka vizuri katika vijiji 47. Alipoingia alikuta vijiji 14 vina maji, yeye miaka minne ameweza kufunga miradi vijiji 47. 14 vinaendelea na ndani ya muda mfupi kabla mwaka huu haujaisha itakamilika. Kwa hiyo, atafikisha miradi 61 ya vijiji 61 vya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye umeme amefunga umeme vijiji vyote 94. Alipoingia alikuta vijiji 41 vina umeme, leo vyote, ameongeza 53 na hivyo vimetimia 94 vina umeme katika miaka minne tu. Ameweza kutusaidia hadi leo tuna vitongoji 281 bado 234 ambavyo havina umeme kati ya vitongoji 515. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye afya, amekamilisha hospitali ya wilaya. Ameiboresha, amejenga wodi, idara mbalimbali zimeboreshwa, mitambo ipo pale, kama MRI, CT-Scan na kadhalika ambayo haikuwepo. Ametujengea vituo vya afya vinne vipya ambavyo vimeanza kazi pale, kama Lukoma, Lubare, Maruku, Kanazi, vyote vinafanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile ametujengea zahanati saba ambazo nazo sasa hivi zinafanya kazi. Ametupatia ambulance nzuri, mpya, Land Cruiser inafanya kazi vizuri sana. Waganga wapo, wauguzi, vifaatiba, dawa zinapatikana bila shida yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye elimu, tumepata sekondari mpya 10, na ni nzuri sana, nyingine zina mpaka maabara tatu, maktaba, na majengo ya kompyuta katika muda huu wa miaka hii minne aliyomaliza. Shule za msingi nzuri mbili pale Kanazi B na nyingine zinaendelea kujengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumepata madarasa mengi sana katika Jimbo la Bukoba Vijijini katika muda wake wa miaka minne. Amekarabati shule nyingi na tumepata shule za kidato cha tano na sita (A-Level), jumla ya shule sita hazikuwepo. Nimeongea mara nyingi hapa, leo tayari tuna shule za form five na six sita zinafanya kazi pale Bukoba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ametujengea bandari pale Kemondo. Ilikuwepo bandari ndogo ya meli moja, lakini aliyoijenga leo, inaweza kuingiza meli nne, na anajenga sasa hivi SGR kuendelea mpaka Mwanza. Ikifika Mwanza, SGR tayari kuna meli imeshajengwa pale MV Mwanza, Hapa Kazi Tu. Ikishakamilika hiyo reli ya SGR kufika Mwanza, tutanunua cement Bukoba kama bei ya Dar es Salaam, ambayo ni shilingi 16,000.00. Leo ni shilingi 25,000.00 kwa sababu zinakwenda kwa lori, mifuko 400, gharama inakuwa ni kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukishapata treni ya SGR na ikafika Mwanza na meli iko tayari na bandari iko pale Kemondo tayari, tutanunua cement kama huku mikoa ya Dar es Salaam na majirani. Kwa hiyo, kwa kweli nikisema amevunja rekodi, sitanii, ninasema nikiwa nimedhamiria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu madaraja, pale tunajenga madaraja mawili makubwa sana; Daraja la Kalebe na Kyanyabasa. Nimeongea mara nyingi hapa nikipiga kelele kuhusu madaraja haya. Kyanyabasa lina mita 105 na linahudumia kata 18. Leo linajengwa, limefikia 40% au 50%. Ni jambo ambalo kwa kweli hatukutegemea, ni la ajabu, na huyo ndiye Samia Suluhu Hassan, anatupeleka vizuri sana sana. Kwa kweli nikisema amevunja rekodi, narudia si jambo dogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kutoka Kyetema – Kanazi – Ibwera – Katoro ujenzi umeanza kwa kuanza na Daraja la Kalebe ni jambo ambalo nimelisema sana hapa ndani, lakini leo tayari tunapiga hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia amesaidia kupandisha bei ya kahawa. Nimesema hapa kwenye swali, kutoka shilingi 900.00 kwa kilo, leo ni shilingi 5,100.00. Hii ni ajabu kubwa, na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Naibu Spika, VETA imekamilika pale Bukoba. Chuo kizuri sana cha VETA cha hadhi ya Kimataifa, chuo cha mkoa kipo pale Bukoba. Ametujengea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tawi la Bukoba. Ujenzi umeendelea, uko kwenye 50%. Haya ni mambo makubwa sana, sana, sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo Bukoba hayakuwa na mitandao ya simu, kama Igabiro na mengine, lakini leo wanaongea wakiwa nyumbani kwao. Mtu amelala kitandani anaongea na simu yake, anaongea na mwanaye Dar es Salaam, na ndugu yake na kadhalika, anatuma fedha na anapokea fedha bila shida.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Rais Samia anafungua Daraja la Busisi – Kigongo pale Mwanza. Sisi ni wanufaika wakubwa. Kutoka Mwanza mpaka Bukoba ilikuwa saa sita mpaka saba kwa gari, leo ni itakuwa saa nne au tatu kwa sababu siyo mbali, lakini tulikuwa tunakaa pale saa nyingi kusubiri kivuko ambacho ilikuwa ni shida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajengewa uwanja wa ndege wa Kimataifa pale Bukoba Kyabajwa, hayo ni mambo makubwa. Nikisema amevunja rekodi na ninyi, mwelewe kwamba kwa kweli amevunja rekodi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunapongeza, lakini sisi kazi yetu, mengine ni kushauri na kuiongoza Serikali. Nina ushauri mmoja. Nimesema ameboresha afya, amejenga hospitali, zahanati, na vituo vya afya. Sasa nina ushauri katika eneo hili. Unapokuwa na hospitali ni ya kutibu wagonjwa, lakini tukifungua kila hospitali iwe na kituo cha kupima tiba kinga, kwamba idara hii iwe maalum, chumba kimoja au viwili kwa ajili ya mtu akienda pale apimwe, kuna daktari au kuna wauguzi, anakupima, anajua kwamba huyu anakaribia kuugua ugonjwa huu, wanazuia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kumtibu leo mgonjwa aliyeugua kansa ya tezi dume au kansa ya njia ya kizazi ni shilingi milioni 50 mpaka milioni 60, lakini mkizuia huo ugonjwa ni shilingi 200,000.00 au shilingi 300,000.00 tu anakuwa amezuia, tunaokoa fedha za wagonjwa na fedha ya Serikali. Serikali ndiyo mwenye kutoa bima na ndiyo inalipa fedha ya bima. Kwa hiyo, tukipunguza magonjwa hayo kwa kuyazuia kwa kujua tunaokoa fedha ya Serikali na wagonjwa, pia tunaokoa afya za wagonjwa nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie pia kuhusiana na reli nzuri ya kisasa ya SGR ambayo sasa hivi inafanya kazi toka Dar es Salaam mpaka Dodoma. Pale Pugu paongezwe kama kituo cha Dar es Salaam. Inasimama ile treni ya kawaida, lakini express haisimami pale. Dar es Salaam ina vituo viwili vya express Dar es Salaam yenyewe pale Station, na Pugu hata kama ni express ile pale Pugu isimame.

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wote ambao wanatoka Dar es Salaam Kaskazini Mbezi Luis, Mbezi Beach, Kunduchi hata Mikocheni, Sinza, Tegeta watapata faida pale. Badala ya kwenda pale station ambako kunakuwa na foleni kubwa sana, pale Pugu iwe ni kituo cha pili cha Dar es Salaam hasa kwa treni ya express. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na shida kwenye suala la ajira ya vijana. Suala la ajira ya vijana nilikuwa nina tatizo kubwa, lakini nimesoma Ilani ya CCM ya mwaka huu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa malizia.

MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninamalizia, dakika moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma Ilani ya CCM ya Mwaka 2025, nimeridhika kwamba CCM imejipanga kwa ajili ya kutatua tatizo hili la vijana kupata ajira. Kwa hiyo, sina shida na hilo, shida imekwisha. Nina hakika kwamba tatizo hili litatatuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)