Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Iringa Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kusimama leo katika Bunge hili Tukufu. Kwa kweli, kusimama kuchangia bajeti hii kwa mara ya mwisho ni wakati wa kumshukuru pia Mwenyezi Mungu. Nachukua nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa fursa ya kuwa Mbunge katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi hiki cha miaka mitano.
Mheshimiwa Naibu Spika, naungana na mtume ambaye alisema, kupitia Kitabu cha Timotheo wa Pili, 4(7) kwamba, Paulo alipomaliza kazi yake akasema, nimepiga vita vizuri, mwendo nimeumaliza, imani nimeilinda. Nami ninasema hivi, nimepiga vita vizuri kwenye nafasi ya Ubunge, mwendo wa miaka mitano nimeumaliza, (siendi kufa, ingawa Paulo alimaanisha kufa), na hadhi ya Ubunge nimeilinda.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango na bajeti hii ya fedha tunayoijadili, kama ambavyo Waheshimiwa Mawaziri wamesema, ni mpango wa kimkakati ambao unatupeleka mwishoni kumaliza mpango wetu wa miaka 25 ambao tulikuwa tumeupanga. Tuko kwenye transition kuelekea mpango mpya unaofikia 2050, ambao utachukua miaka mingine tena 25.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaweza kusimama kifua mbele kabisa kuipongeza na kuishukuru sana Serikali yetu kwa kazi kubwa ambayo imeifanya. Kwa namna ambavyo wametekeleza mpango wa miaka mitano, wame-lay foundation nzuri sana ambayo tukakwenda vizuri katika mpango unaofuata wa miaka 25 ijayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema hivyo kwa sababu ya miundombinu mikubwa ambayo imekamilika katika Taifa letu, ikiwepo ujenzi wa reli (SGR) na umalizaji wa Bwawa lile la Mwalimu Nyerere. Hiyo inatuhakikishia kwamba, tutaendelea kuwa na nishati ya kutosha katika Taifa letu kwa muda mrefu. Hivyo, mipango mingine yote tunayopanga ya uzalishaji itawezekana kwa sababu, tuna nguvu kubwa ya umeme ambao utaendesha sekta zetu zote za uzalishaji na utoaji wa huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, miundombinu ya usafirishaji imeimarishwa ikiwemo reli, lakini tunaona katika kila ziwa kuna ujenzi wa meli kubwa ambao unaendelea katika nchi yetu kuonesha kwamba, usafirishaji utaimarika. Tumeona ununuzi wa ndege zile sita ambazo tumeongeza na utanuzi wa bandari ambao unatuhakikishia kwamba, shughuli za usafirishaji tukizalisha kwenye kilimo na sehemu yoyote zitawezekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaipongeza sana Serikali kwa foundation hiyo ambayo mmeiweka na sasa tunaamini kweli, mpango huu wa miaka 25 utawezekana kwa sababu, tayari foundation kubwa imejengwa, na mimi sitakuwa nyuma. Kama Mbunge, nilikuwa na wajibu wa aina mbili; kwanza, ni kuwatetea wananchi wangu, mabosi wangu wazito sana, wananchi wa Jimbo la Iringa Mjini na bila kuwasahau wajumbe wazito walionichagua kwa kura ya maoni, wajumbe wanaotokana na Chama cha Mapinduzi. Hilo lilikuwa ni jukumu langu la kwanza, yale ambayo chama kimenituma kupitia Ilani ya CCM kuyatekeleza katika Bunge hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, ninapokuwa hapa, ni Bunge la Kitaifa kuangalia mambo yote yanayohusu Taifa letu. Kwenye habari ya Ubunge, wananchi wangu wa Iringa wao ni mashahidi, nimepita kila kata nimewaeleza kwa kufafanua kila kilichofanyika kata kwa kata, lakini yapo mambo makubwa yaliyofanyika ambayo sisi kama Iringa, hatujaachwa. Sisi pia, tumeunganishwa na Taifa hili kwa kutanuliwa uwanja wa ndege, mkubwa. Sasa hivi Iringa ndege zinatua mara tatu kwa wiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, ATCL wana ndege nyingine kubwa, wananchi wa Iringa wana-enjoy. Tulikuwa tunaenda Dar es Salaam kwa shilingi milioni moja, sasa tunaenda kwa shilingi 199,000.00 tu baada ya kutanua Uwanja wetu wa Nduli kwa zaidi ya shilingi bilioni 60.
Mheshimiwa Naibu Spika, Iringa imeunganishwa kwa miundombinu ya barabara. Sisi, kama watu wa Iringa, tunashukuru sana. Ipo Barabara yetu ya Ruaha National Park kilometa 104, ambayo inaenda kujengwa kwa zaidi ya shilingi bilioni 140. Barabara ile inaanzia Iringa Mjini mpaka geti la Ruaha, kule Ruaha National Park.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru sana tumeletewa Iringa Bypass itakayojengwa kwa kilometa 40 na ujenzi wake umeanza. Tunaishukuru sana Serikali kwa kutuunganisha Iringa na kufanya Iringa kuwa kituo cha utalii kwa maana ya kutuwekea miundombinu ya usafirishaji wa anga, barabara, na pia, kutujengea kituo cha utalii Kusini, pale Kesakilolo. Ni kutuunganisa Iringa na Tanzania, na dunia, na pia, kuongeza kuchechemua uchumi wa wananchi wetu wa Iringa. Tunawapongeza sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, yamefanyika mengi kwenye elimu. Tumejenga zaidi ya shule tano, tumekarabati shule zetu kongwe za Iringa Girls na Lugalo kwa zaidi ya shilingi 1,400,000,000.00. Tumejengewa shule za shilingi milioni 630, karibu tano na tumeimarishiwa Chuo chetu cha Mkwawa, Chuo kikuu, ambapo tumejengewa lami kwa kilometa 3.5 na tumeletewa zaidi ya shilingi bilioni 14, kwa ajili ya mabweni na kujenga lecture rooms pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu katika Chuo chetu cha Roman Catholic (RUCU). Tunashukuru mikopo ya elimu ya juu kwa ajili ya chuo chetu cha KKKT ambacho kinaitwa Tumaini University, lakini ni University of Iringa. Tunashukuru sana, tumefanyiwa mambo mengi kwenye elimu ya msingi kwa kuletewa shule mpya zaidi ya tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, maji Iringa ni 97.8% na umeme Iringa ni zaidi ya 95%. Mamlaka ya Maji Iringa ndiyo mamlaka bora ya pili Afrika kwa kufanya kazi vizuri. Tunawashukuru sana, tumeletewa mbolea kiasi cha kutosha yenye ruzuku, na wananchi wa Iringa wanaendelea kulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu yangu ya pili nilikuwa kama Mbunge wa kuliwakilisha Taifa langu. Ninasema vita nimeipiga vizuri, wanaume wa nchi hii nimewatetea, nimesimama nimewasemea umuhimu wa kujenga usawa na kuangalia jinsia zote mbili. Vita nimeipiga vizuri, masuala ya afya ya akili nimeongelea hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuendelea kustawisha ubora wa Taifa letu lazima tuendelee kuangalia masuala ya afya ya akili na ninashukuru kwa ahadi ya Serikali, ninaamini kabla hatujamaliza Bunge hili, Baraza la Afya ya Akili nchini litakuwa limeanzishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepambana kuhakikisha kwamba tunasema masuala yale yaliyo kinyume na mila na desturi zetu ikiwemo masuala ya ushoga, ndoa za jinsia moja kupambana nazo na ukatili wa kijinsia. Haya yote tumeyaongea mahali hapa. Zaidi sana tumepata fursa ya kutoa mchango wetu kwa Serikali yetu ambayo ni sikivu na imetusikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema hivi, Serikali yetu tunaendelea kuwaombea. Hatukusita kuongelea vyombo vyetu vya ulinzi na usalama na kuvitia moyo mahali ilipohitajika. Tuliwatia moyo kwamba hatuko tayari kuona nchi yetu inaathiriwa kwa namna yoyote ile kuhakikisha kwamba tunavuruga amani na utulivu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulipambana na Mataifa mengine ambayo yalitaka kuleta vurug,u na tuko tayari kuendelea kupambana. Hatutakaa kimya, kuhakikisha kwamba Tanzania inaendelea kuwa kisiwa cha amani, na Rais wetu anaendelea kuheshimiwa na anaendelea kupata comfort ya kulitumikia Taifa letu akishirikiana na Serikali yake. Hayo tutaendelea kuyafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninaiomba Serikali kuhusu mifugo. Moja ya mikakati ya Serikali ya Awamu ya Tano ilikuwa ni kujenga machinjio za kisasa kwenye nchi hii ili mifugo, kama alivyosema Mheshimiwa Waziri wa Mipango ukurasa wa 21 ile bullet 26, kwamba idara atakazoziangalia ni mifugo na uvuvi ili ziendelee kuzalisha zaidi na kuongeza vipaumbele katika uzalishaji wa Serikali. Ninaomba sana, Iringa tulitakiwa kujengewa kiwanda cha nyama. Sasa pale kile kiwanda kimegeuka kimekuwa tena machinjio kwa sababu hakijamaliziwa. Tunaomba kimaliziwe ili kiwe kiwanda na ki-save nyanda za juu kusini kwa ajili ya kufanya packaging za nyama, kama ilivyokusudiwa kwenye andiko lake, kwamba nyama zitumwe nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Utalii Kihesa – Kilolo nacho kikamilike ili connection iwe nzuri. Ndege zipo, barabara inajengwa, lakini kituo cha utalii Kihesa – Kilolo bado hakijakamilika. Watalii wanashuka pale na ndege, hawajui wapi wapate information za utalii Nyanda za Juu Kusini. Tunaomba kile kituo kikamilike ili connection iwe vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii sekta ya utalii kwa kuwa pia inaongeza sana kwenye pato la Taifa, hasa kwenye fedha za kigeni. Nyanda za Juu Kusini tuwe ni sehemu ya kuchangia utalii wa Taifa hili na kuingizia Taifa letu fedha za kigeni za kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu ,baada ya kusema maneno haya ninawashukuru sana na ninaunga mkono hoja. Ninawaomba wananchi wangu wa Iringa, ninaamini wameniona na hawataniacha. Ninawaomba sana Wajumbe waendelee kunikumbuka. Bado nipo, na mambo mengine bado yapo, ninaamini kabisa Mwenyezi Mungu atakusudia, nina kasi zaidi ya nilivyokuwa mwanzo. Ahsante sana. (Makofi)