Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Abdallah Jafari Chaurembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbagala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kutoa mchango wangu katika mjadala unaoendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, namshukuru sana Mwenyezi Mungu, ambaye kwa kipindi hiki cha miaka mitano tunachomaliza, ameendelea kunitunza, kunipa afya njema na kunipa weledi mkubwa wa kuweza kujadili mambo mbalimbali ambayo yamekuwa yakiwasilishwa hapa Bungeni na hasa katika suala zima la kuwasilisha changamoto na kero zinazowakabili wananchi wangu wa Jimbo la Mbagala.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nakishukuru Chama changu cha Mapinduzi, CCM, kwa kipindi chote cha miaka mitano, kimenipa ushirikiano mkubwa sana. Kimenikumbusha mambo mengi ambayo yalikuwa yameahidiwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nawashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Mbagala, wameweza kunipa nafasi kubwa ya kuchangia. Sikuweza kupata usumbufu wowote katika wakati wangu wa uongozi wa kipindi cha miaka mitano; wamenipa ushirikiano mkubwa na wamenipa hoja za msingi za kuweza kuzungumza hapa Bungeni. Ninawashukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, naishukru sana Serikali. Hoja zangu zote nilizoziwasilisha hapa Bungeni, zikiwepo kero za wananchi wangu wa Jimbo la Mbagala, Serikali yetu sikivu pamoja na Mawaziri wake wote wamenitekelezea kwa asilimia kubwa. Ninawashukuru sana, inshallah, Mwenyezi Mungu atawalipa na Mheshimiwa Rais pia, atamlipa kila lililo la heri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kutoa shukrani zangu kwa Serikali kwa miradi mikubwa ambayo imefanyika katika jimbo langu. Katika sekta ya elimu, msingi peke yake katika kipindi hiki, haijawahi kutokea, shule tisa mpya zimejengwa katika Jimbo langu la Mbagala, na pia, shule za sekondari nane mpya zimejengwa. Jimbo langu la Mbagala lilikuwa halina high school, sasa hivi zimejengwa mpya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana viongozi wote wa Serikali kwa kuniletea Shule ya Mchepuo wa Kiingereza katika Jimbo langu la Mbagala. Ninaamini katika suala la elimu, Jimbo la Mbagala sasa hivi tunatembea kifua mbele, lakini pia, niendelee kushukuru, vituo vya afya vitano vipya, vimejengwa katika Jimbo langu la Mbagala pamoja na hospitali kubwa mbili za wilaya zimejengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kuishukuru sana Serikali katika suala zima la barabara. Fidia ya shilingi bilioni 16.8 ambayo ilikuwa kero kwa muda wote imetekelezwa, na watu wamelipwa. Kikubwa zaidi, naishukuru sana Serikali chini ya Rais wetu, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa suala zima ambalo lilikuwa kero; suala la X zilizowekwa kutoka Rangitatu - Mbande mpaka Mongola. X zile baada ya kuleta hoja zangu hapa Bungeni, zilifutwa na wananchi sasa wanaendelea na taratibu zao, hawana bugudha. Huko tunakokwenda tumeanza kuomba upanuzi wa barabara ile na hatimaye ikikubalika barabara ile kupanuliwa, wananchi wale watalipwa fidia zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ilani ya Uchaguzi imetekelezeka kwa asilimia kubwa. Ukisoma kuanzia ukurasa wa kwanza mpaka wa mwisho mambo yaliyokuwa yameahidiwa katika Jimbo la Mbagala yametekelezwa. Kwa hiyo, ninaendelea kuishukru sana Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, vitabu vya bajeti vyote tulivyokuwa navyo, yale yote ambayo yameandikwa katika jimbo langu yametekelezeka. Nimeyataja baadhi, na kwa sababu ya muda, siwezi kuyataja yote. Tunayo Ilani Mpya ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, vile vitu ambavyo vimebaki, vidogo vidogo, vyote vimewekwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2025.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaendelea kukishukuru sana Chama cha Mapinduzi, kwa maana yale yote tuliyokuwa tukiyawasilisha na wao wameendelea kuyafanyia kazi. Kikubwa zaidi, ukichukua kitabu cha bajeti ambayo ndiyo tunaijadili na kuipitisha hii leo, yale mambo yote ya msingi yaliyobaki, zikiwepo barabara za Mtaa wa Dovya, Mwapemba, Kwa Mfindi, Vigoa, Kwa Kashikashi, Kwa Mwarabu, kwa Mzungu na Kilamba hadi Mashine ya maji zimeandikwa katika kitabu hiki. Ndiyo maana sina sababu ya kutokuiunga mkono bajeti hii kwa maana sisi watu wa Jimbo la Mbagala tunashukuru sana, yale yote tuliyoyaomba yameweza kutekelezwa na mengine yapo katika kitabu cha bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kumshukuru Rais, Mama yetu Samia Suluhu Hassan, wakati akitoka Dar es Salaam kuelekea Rufiji alisimama pale Mbagala. Baada ya kusimama Mbagala, pamoja na michakato mbalimbali tuliyokuwa tukiifanya katika halmashauri ya kuomba Jimbo letu la Mgagala likatwe, tuliomba tena Mheshimiwa Rais baada ya kumweleza tuliyoyafanya na michakato mbalimbali. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais, jambo letu la Jimbo la Mbagala kukatwa, limekatwa na sasa tumepata Jimbo jipya la Chamazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hapa Watu wa Mbagala na Chamazi yapo mambo ambayo tunatakiwa tujiulize. Kama jimbo lilipokuwa na Mbunge mmoja maendeleo yamepatikana kwa kiasi hiki, je, sasa hivi yamepatikana majimbo mawili? Ninaamini maendeleo yatakuwa makubwa zaidi ya haya yaliyopatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, natumia nafasi hii sasa kuwaambia Wanambagala, mimi kama Mbunge wao, kwa kuwa makazi yangu yapo katika Jimbo Jipya la Chamazi, kwa hiyo, ninawaambia nitagombea katika Jimbo la Chamazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nawatoa hofu wale wote waliokuwepo katika Jimbo la Mbagala, Bunge hili ni la Kitaifa. Tunajadili mambo ya nchi nzima. Kwa hiyo, zile changamoto zilizokuwepo katika Jimbo la Mbagala ambalo ninaenda kuliachia, nitaendelea kushirikiana na Mbunge anayekuja kuhakikisha tunaendelea kutatua changamoto hizo. Wale marafiki zangu nawatoa hofu, tutaendelea kushirikiana nao.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kengele ya kwanza hiyo, lakini nina mambo mawili machache ya mchango katika bajeti hii. Jambo la kwanza, tumeendelea kuipongeza Serikali, lakini kiukweli Serikali inatumia fedha nyingi sana kwa ajili ya kutibu magonjwa yasiyoambukiza.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni jukumu letu Wabunge tuipunguzie mzigo Serikali kuwatibu wagonjwa wa magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza kwa kutoa elimu na ushauri kwa wananchi wetu kubadilisha life style tunazokwendanazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia magonjwa ya moyo, shinikizo la damu, kisukari na kansa, haya siyo magonjwa ya kuambukiza, lakini yanatokana na life style zetu tunazoishi. Ninaomba nichukue nafasi hii kuwaomba Wabunge wenzangu, inshallah Mwenyezi Mungu ataturudisha hapa Bungeni, muda wetu mwingi tukiwa majimboni, mwakani tuwaelimishe wananchi wetu ili waweze kuepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ambayo yatailetea faida kubwa nchi yetu kwa kutokutumia fedha nyingi, kwa ajili ya kuwatibu wagonjwa hao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kusafisha damu. Wabunge wengi hapa tuliomba gharama za kusafisha damu zishushwe, lakini tumeshindwa kuona ni namna gani ambayo tunaweza tukawashauri wananchi wetu wakaepukana na matatizo yanayotokana na magonjwa ya kuambukiza.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiwahamasisha wananchi wetu kuepukana na magonjwa ya kuambukiza, tafsiri yake, ni hatutakuwa na sababu ya kuona sasa namna gani ya kuiomba Serikali ipunguze gharama.

Mheshimiwa Naibu Spika, gharama ya kusafisha damu kwa mgonjwa mara ya kwanza anapofika hospitali ni shilingi laki saba, lakini kila wiki anatakiwa atumie zaidi ya shilingi laki tatu, mara mbili au tatu kwa wiki, ni gharama kubwa. Tutakapoendelea kuwashawishi wananchi, maana yake ni kwanza wao maisha yao yataendelea kuboreka, kwa maana watakuwa hawatumii fedha nyingi kwa ajili ya matibabu, lakini la pili, tutaipunguzia mzigo Serikali yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwa wale ambao wanapata misamaha, katika zile shilingi 300,000.00 Serikali inachangia shilingi 120,000.00; hebu tuangalie mzigo mzito ambao tunaikabidhi Serikali. Kwa hiyo, nawaomba Wabunge wenzangu, tuwashauri na tuwaelekeze wananchi wetu kufanya mazoezi pamoja na kubadilisha maisha yetu, ili tuepukane na magonjwa haya yasiyo ya kuambukiza.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ni suala la ardhi. Ninashukuru, tunaenda vizuri, lakini zipo changamoto kwenye ardhi, changamoto ambazo zinasababisha Serikali kutumia gharama kubwa wakati wa fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika miaka mitano, hapa tumekuwa tukizungumzia suala la fidia, fidia, fidia, lakini kama tungepima maeneo yetu vizuri, leo hii tungekuwa hatuzungumzii suala la fidia, kwa sababu, maeneo yote yangekuwa yamepimwa. Maeneo ambayo tunataka kujenga barabara yangekuwa hayana tena changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na nikutakie kila la heri na wewe kwenye Jimbo lako la Ilala. Nimtakie kila la heri Mheshimiwa Spika kwenye jimbo lake jipya na niwatakie kila la heri Wabunge wote tuliopo hapa kwa kazi kubwa tulizozifanya. Ninaamini watakaobaki ni wale wenye roho mbaya kwa sababu, roho mbaya haina dawa.

NAIBU SPIKA: Ahsante.

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninaomba kuunga mkono hoja.