Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Biharamulo Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hotuba hii ya Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2025/2026 ambayo in fact, tuseme ndiyo hotuba yangu ya mwisho katika Bunge hili la Kumi na Mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kipekee niwashukuru sana wananchi wa Biharamulo walionipa ridhaa ya kuwa mwakilishi wao katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miaka hii mitano ambayo tunaimalizia. Kwa niaba yao, nimshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kama Kiongozi Mkuu wa Serikali na Kiongozi wa nchi kwa miradi mingi ya heshima ambayo ametupatia watu wa Biharamulo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri hii juzi Jumatatu nilikuwa jimboni nikafanya nao mkutano wa kueleza ni mambo gani yamefanyika. Kwa hiyo, yote wanayo, wanayajua. Tuzidi kuishukuru Serikali na tukitarajia katika bajeti hii ambayo tunaipitisha sasa, lakini na Ilani ya CCM ambayo tayari imeshazinduliwa, waliokabidhiwa wagombea wetu kwenye mkutano uliopita tunaamini tutapata ushindi wa kishindo kwa haya tuliyoyatekeleza na tutatekeleza yale ambayo tumeahidi katika ilani mpya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru sana Serikali kwa sababu bajeti hii kwangu mimi nimesema kwamba ni bajeti ambayo imegusa maisha ya wanyonge na watu wa chini kabisa ambao kiasili walisahaulika kwa muda mrefu. Jambo la kwanza, ninamshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais na Serikali yake ya Awamu ya Sita kwa ongezeko la mishahara ya kima cha chini cha wafanyakazi wa nchi hii kwa 35.1%. Hili ni ongezeko kubwa na la kihistoria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaamini tunaposema mambo mazuri haya yanafanyika, hata wale waliokuwa wanyonge wakilipwa kidogo, wamelipata ongezeko na wameliona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tutakuwa mashahidi, tumemsikia Waziri wa Fedha na kitabu chake cha bajeti hapa kimesema, hata wastaafu wanaolipwa kutokea hazina pensheni zao waliokuwa wanapokea shilingi 100,125.9 kwa mwezi na sasa imeongezeka, imeenda shilingi 250,125.9. Hili ni ongezeko kubwa sana kwa wastaafu, hivyo tuzidi kuishukuru Serikali kwa kuwaona. Tunaamini hakitoshi, lakini kitasaidia kusukuma maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ukisoma katika Sheria ya Kodi ambayo kwenye kitabu chetu cha bajeti ni sura ya 332, Serikali imetangaza unafuu wa kodi ya mapato kwa bajaji na pikipiki. Pikipiki zikitoka shilingi 65,000.00 mpaka kuwa zero, lakini bajaji na baiskeli zote za miguu mitatu zikitoka shilingi 120,000.00 na kuwa sifuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huu ni unafuu mkubwa sana, ndiyo maana nikasema hii ni bajeti ambayo imegusa maisha ya watu wa chini kabisa. Wote tunajua maisha yetu na hasa familia zetu za kimaskini na za Kitanzania, tumekuwa tunabebwa na watu wa bodaboda na ndiyo ajira kubwa iliyoko kwenye familia zetu na maeneo yetu. Kwa hiyo, tunapoona Serikali inawagusa na kuwakumbuka kwamba hata wao wapatiwe unafuu wa maisha hasa katika kodi, ni jambo zuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ninaipongeza Serikali, kwani wakati Waziri wa Fedha anawasilisha hotuba yake hapa alisema dhahiri kabisa kwamba katika bajeti hii wanaelekeza biashara za watu zisifungwe, bali kuwe na dialogue kati ya taasisi zinazo-control biashara na wafanyabiashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini hili jambo limesikika kwa muda mrefu, nadhani watu walikuwa wanasema halijawahi kutolewa maelekezo na Serikali. Sasa kwa sababu Serikali imetoa maelekezo vividly ndani ya hili Bunge, tunaamini hiki kitu kitatekelezwa na sasa itasimamiwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwangu mimi unaposema mfanyabiashara, dereva wa bajaji ni mfanyabiashara; na dereva wa bodaboda au pikipiki ni mfanyabiashara, maana ndicho kinachompa kipato na ndiyo maana alikuwa considered hata katika habari ya mapato. Sasa tuombe kupitia Bunge hili, na hasa Serikali inapoenda kumalizia majibu, tupate majibu ya uhakika kwa sababu tunachokipitisha hapa ni kwamba Serikali imeelekeza wafanyabiashara wasisumbuliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, unajua dereva wa bajaji au bodaboda maisha yake na biashara yake ni pikipiki. Pale anapokosea ukamnyang’anya leseni, maana yake umemfungia biashara kwa sababu hawezi tena kufanya biashara; na hawa watu wanalea familia na ndiyo hao wanaotunza familia zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuombe kuwe na dialogue kuanzia kwa watu hawa wa chini wa bodaboda, na watu wa bajaji. Hata anapokosea, suala la kumnyang’nya leseni na kumfungia leseni, Serikali imeeleza, tuwe na dialogue, atafutiwe adhabu, lakini asikatishwe cashflow ya familia yake kwa sababu huyu mtu anatunza familia, anasomesha, na vitu vingine. Unapomtoa barabarani, kama alikuwa anaendesha bodaboda ya mtu, na yule mtu akamnyang’anya, inamharibia kila kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa ninasoma katika kitabu chetu cha bajeti ukurasa wa 108, Sheria ya Kudhibiti Uingizaji wa Bidhaa Ndani ya Nchi Sura Na. 276. Ninaishukuru sana Serikali, nimekuwa Mjumbe wa Kamati ya Viwanda na Biashara kwa miaka hii mitano, na katika kitu ambacho tulikuwa tunaomba sana, Serikali ikifanyie consideration, ni protection ya wazalishaji wa ndani katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua kwamba kunakuwa na tariffs za HS Code na nini huwezi kuongeza import duty au kufanya mpaka mkubaliane, lakini introduction au kuviweka hivi vitu vingi ambavyo vimeenda kwa kuweka kwenye kitengo kinachoitwa tozo ya maendeleo ya viwanda, imetusaidia mno. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeongea kwa habari ya mabati ALAF, sasa hivi wamefungua kiwanda kikubwa, na Kamati yetu ilitembelea pale. Kwa hiyo, introduction ya tozo kwenye HS code hizi kwa 15% itasaidia sana uingizaji wa mabati yanayotoka nje, tulinde viwanda vyetu vya ndani. Pia, tumeona hata viwanda vya nondo, Kamati yetu ilitembelea kiwanda cha Ruvia, nilisema tunatengeneza mpaka BS500 zinazalishwa hapa. Zamani tulikuwa tuna-import hizi nondo, lakini leo zimezalishwa hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nondo nyingi zilizotumika kwenye mradi wa SGR zimezalishwa hapa nchini. Kwa hiyo, kitendo cha kufanya protection kama hii, itasababisha uwekezaji mkubwa ndani ya nchi. Licha ya uwekezaji, itasababisha ajira ndani na mapato ya watu wetu yataongezeka rather than pale ilipokuwa inazalishiwa kule nje, tunakuwa tu soko la kupokea bidhaa ambazo zimeshazalishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaipongeza Serikali kwenye haya yote, maana nilikuwa napitia ukurasa wa 108 mpaka ukurasa karibu wa 110, mambo mengi ambayo tuliyaomba yamekuwa considered. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Sheria hii ya Kodi ukurasa wa 108(2) inasema, “kutoza tozo ya maendeleo ya viwanda kwa kiwango cha 10% kwenye vichwa vya trailer vinavyoingizwa nchini vinavyotambulika kwa HS code zimetajwa hapo.” Hii ndiyo case ambayo nilitaka niongee kidogo, na ninadhani Waziri wa Fedha angenisikiliza vizuri hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi katika hii nchi, vichwa vya trailer tunafanya importation. sasa tunapoongeza hii kodi ya maendeleo ya viwanda why? Sisi hatuzalishi vichwa vya trailer, what are we bring in the market now?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba, hii itasababisha usafirishaji uwe mgumu kwa sababu, unapoongeza 10% na wenzako hawajaongeza 10% kwa kuwa hivi vichwa tunavi-import. sisi sio watengenezaji wa Volvo, Howo na vitu vingine. Tunachotengeneza ni trailers, lakini vichwa vinakuwa imported, vichwa tayari vina-import duty, vina VAT na vitu vingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba, pamoja na kwamba tuna nia nzuri ya kuongeza mapato, hili jambo tuliangalie, litaumiza Watanzania wengi kwa sababu, wasafirishaji wataongeza hizi gharama na anaenda kuzibeba mtu wa mwisho. Sisi tunaotoka bara huko, mbali kutoka Dar es Salaam kwenye bandari, kilometa zaidi ya 1,400 unafika Kagera, hii itatuumiza. Maisha yatapanda sana kwa sababu ya usafirishaji. Kwa hiyo, tuombe hili liangaliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua tunahitaji kodi, lakini tusiumizumize hawa watu. Kama sehemu nyingine tumetengeneza unafuu, Mtanzania wa mwisho tunayemtengenezea unafuu ndiye huyu aliyeko huko mikoani kwa sababu, tuna ujenzi wa madarasa na tuna ujenzi wa vitu vingi; tutahitaji mizigo isafirishwe kutoka kwenye viwanda vingi ambavyo viko Dar es Salaam kufika bara kwetu huku. Hii bajeti ya ujenzi ambayo imepangwa na vitu vingine, bei zitapanda kwa sababu ya usafirishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, bei zitakapopanda, maana yake ni hata bajeti itakuwa distorted. Kwa hiyo, tuombe hili tujaribu kuangalia, kama mnaweza mkapata chanzo kingine, hii 10% ya maendeleo mnayoongeza kwenye vichwa vya trailer vinavyokuwa imported kwa sababu, what are we protecting?
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna mtu anayezalisha vichwa vya trailer hapa kwamba, tungekuwa tuna alternative humu ndani. Kama kuna mtu angekuwa anazalisha, una alternative, is well, unam-protect mtu wa ndani ili anayeingiza aweze kupata shida, lakini sasa tunaenda kupandisha kila kitu. Aliye na ma-trailer ya zamani kwa sababu wafanyabiashara ndio wale wale, anayeingiza mapya atapandisha tu bei automatically.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaingiza soko kwenye distortion kubwa na wananchi wanaenda kuumia, especially tunapopokea bidhaa huko nje. Kwa hiyo, tuombe hili mlione, kama mnaweza mkafanya consideration ya adjustment ya kutafuta hela kwenye vipengele vingine, bado tuna nafasi. Ndiyo maana tunajadili muswada huu. Hili tuliona tuwapunguzie wananchi mzigo ili tuweze kupunguza hii gharama.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema haya, kwa mara nyingine tena nashukuru. Nakushukuru wewe mwenyewe binafsi na ninamshukuru sana Spika wetu wa Bunge, Wenyeviti wa Kamati ambao wamekuwepo hapa pamoja na viongozi wengine kwa ushirikiano mlionipa kwa miaka hii mitano. Ninaamini kilikuwa ni kipindi changu cha kwanza cha kujifunza. Mungu akisaidia tutakaporejea, tutarejea na nguvu mpya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mungu atusaidie wengi tuliomo humu, kwa kazi kubwa ambayo imefanywa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunayo ya kujivunia majimboni na tunayo ya kwenda kusema. Tusiwe waoga, tunyanyuke kishujaa, turudi majimboni, tukawaambie wananchi, tumefanya nini kwa kushirikiana na Mheshimiwa Rais? Ninaamini wananchi ni wasikivu, Watanzania wameona yaliyofanyika, watatupa ridhaa nyingine tena. Ahsanteni sana kwa kunisikiliza Mungu awabariki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono hoja. (Makofi)