Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Joseph Anania Tadayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana kupata nafasi hii ya kuwa mchangiaji wa kwanza kwa asubuhi hii ya leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa jinsi ambavyo ameniongoza katika kipindi chote hiki cha Bunge la Kumi na Mbili ambalo sasa linaelekea mwisho kwa salama na amani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ninakishukuru chama changu, Chama cha Mapinduzi kwa kupeleka jina langu kwa wananchi mwaka 2020 ili nipeperushe bendera ya Chama Cha Mapinduzi kwa nafasi hii ya Ubunge. Ninaamini kabisa nimekitendea haki chama changu katika dhamana ambayo walinipa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru zaidi wananchi wote wa Jimbo la Mwanga kwa kunipokea nilipoletwa na Chama Cha Mapinduzi na kuniamini na kunipa dhamana ya kuwawakilisha kwa nafasi hii ya Ubunge. Ninaamini kazi hii imefanyika vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwataarifu tu kabisa kwamba tunaelekea mwisho wa kuchukua fomu, na mimi niko njiani ninakwenda kuchukua fomu na ninaamini kabisa kwa kazi ambayo Mungu ametuwezesha kufanya, basi watakuwa tena na imani ya kuweza kunirudisha siyo mimi tu, hata wewe kule Jimboni Ilala, pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote ambao tumekaa vizuri sana humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa uongozi wake makini. Kwa kweli wananchi wa Mwanga wameona kazi ya Mheshimiwa Rais, Tanzania imeona na hata dunia imeona na ndiyo maana hata Mheshimiwa Rais amepewa tuzo awards nyingi sana katika kipindi hiki, kwa sababu dunia imeona kazi ambayo amewafanyia Watanzania na ameifanyia dunia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazi kabisa kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiye mtu sahihi wa kupeperusha bendera ya CCM na kuendelea kuliongoza Taifa hili kwa kipindi hiki kinachokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nisiwe mchoyo wa fadhila, ninamshukuru sana Mheshimiwa Spika pamoja na wewe na viongozi wetu wote wa Bunge kwa jinsi ambavyo mmetulea hasa sisi Wabunge wa Awamu ya Kwanza, mkatuongoza tukaweza kufanya kazi zetu kwa viwango hivi ambavyo tumefanya. Tunawashukuru mmetujengea uwezo mkubwa sana wa kuweza kutupa confidence ya kurudi kwa wananchi kusema tupeni tena kipindi kingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti iliyopita ilitekelezwa vizuri sana. Tumeona kwenye taarifa kwa viwango vikubwa vya zaidi ya 90%. Hii inadhihirisha kwamba viongozi wetu waliotuongoza katika eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na Naibu wake pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Mipango na Naibu wake ni viongozi sahihi kwa sekta hii. Kwa hiyo, tunaweza kuwaamini kabisa na kuiamini pia bajeti ambayo wameileta kwamba itatuvusha. Bajeti hii iko vizuri, na mimi niseme mwanzoni kabisa kwamba ninaiunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kifupi ninaitazama bajeti hii kama bajeti ambayo imelenga kuondoa utegemezi kiuchumi kwa kuchochea zile sekta muhimu za uzalishaji na kupanua wigo wa kodi na kuweka pia mifumo rafiki kwa ajili ya kukusanya kodi. Kwa hiyo, ni bajeti ambayo imeanzia pazuri, kwa vile ile iliyopita ilitekelezwa vizuri kiasi ambacho tumeona kwamba uwiano wa deni na pato la Taifa ni 20% wakati ukomo ni 40%. Hilo ni jambo zuri na hata mashirika yenye hadhi kubwa Kimataifa kama MOODY’S yalipokuwa yanatufanyia tathmini, yametutathmini kwamba bado tuko vizuri, na hivyo kufanya hata deni letu liwe himilivu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuendelee mbele kwa ujasiri bila hofu na bila kusikiliza maneno mengi. Tufanye kazi kwa moyo na kwa kujiamini kwa sababu kweli tunasonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona mapunguzo ya kodi katika maeneo mbalimbali ambayo ni nyeti kama vile maeneo ya kilimo, utalii, madini pamoja na uendelezaji wa rasilimaliwatu. Kwa upande wa kilimo ninapongeza kuondoa kodi ya ongezeko la thamani katika viuatilifu. Hii itasaidia wakulima kuweza kulima vizuri zaidi na kuondoa VAT kwenye nguo zinazotengenezwa na pamba yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hilo litachochea sana wakulima wa pamba kuendelea kufanya vizuri na kupata kipato na hiyo sekta kukua kwa kasi pamoja na maeneo kama ya mbolea, mafuta ya kula yanayotengezwa kwa mbegu zinazolimwa hapa nchini, matairi ya trekta pamoja na vipuri mbalimbali. Hizo ni hatua nzuri za kusaidia kukuza zile sekta za muhimu ambazo tunaziangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona pia kwenye madini na gesi, bajeti haikuwasahau wale watu wadogo wadogo wa bodaboda ambayo ni ajira kubwa, kwani nimeona pia kuna unafuu wa kodi kwenye badoboda, yaani katika maana ya pikipiki, bajaji, pamoja na guta.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupunguzwa kwa Hotel Levy pamoja na bima ya wageni, pia ni jambo la muhimu sana ambalo litachochea sekta hii ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona pia upunguzaji wa kodi kwenye magazeti yanayotengenezwa humu ndani. Hii pia ni hatua nzuri katika kuwafanya watu waendelee kupata taarifa na pia kuweza ku-exercise demokrasia kwa sababu demokrasia pia inahitaji haki ile ya kupata taarifa na kutoa taarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapendekeza na kusisitiza sana kwamba tasnia nzima ya habari pamoja na sanaa iweze kupatiwa nafuu mbalimbali. Pia, urahisishwaji wa masharti yao ya usajili na kulinda kazi zao kwa sababu sanaa na habari ni ajira kubwa, lakini pia ni kiungo muhimu sana katika kutimiza haki ya kidemokrasia ya kutoa na kupata taarifa, jambo ambalo ni muhimu katika uchumi wa nchi inayokua kama hii ya kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimefurahishwa pia na suala la kudhibiti uholela wa wageni kufanya kazi ambazo zinapaswa kufanywa na wenyeji. Kwa kweli ni aibu tunapoona wageni wanafanya kazi za screen printing, ku-print t-shirt kule Kariakoo, na kuuza vitu barabarani. Hii kwa kweli imekuwa aibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwamba sasa tumeamua aibu hii tuachane nayo. Sisi wenyewe tukienda huko nje tunafuata masharti ya kufanya kazi; siyo kwamba mtu aje hapa na ukiangalia vyeti vyake labda amekuja kama mhandisi, lakini anauza tiles barabarani. Hii siyo sawa sawa. Suala hili ni muhimu sana, Serikali ikatae watu wa namna hii ili tuweze kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia lipo jambo moja ambalo aligusia rafiki yangu Mheshimiwa Byabato jana kuhusu hili sharti kwamba lazima mwekezaji akifungua kampuni kuwe na hisa fulani ambazo zinashikiliwa na wazawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa pamekuwa na mtindo kwamba ikishaandikwa pale kwenye Memorandum and Articles ukienda anakuonyesha hii hapa, utakuta labda ni mhudumu wake wa ndani au dereva wake au messenger pale ofisini amempa zile shares.

Mheshimiwa Naibu Spika, inatakiwa kwa kweli twende hatua mbele zaidi kwa sababu shares zinazoandikwa kwenye mtaji ambao kampuni inaruhusiwa kufanya biashara (Memorandum and Articles ile ni authorized share capital). (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka twende chini zaidi tuone he should share capital, kwamba ni share ngapi zimekuwa issued kwenye ile kampuni na paid share capital? Tuone yule ana-share certificate, amelipia kodi na baadaye tumwone kwenye minutes akiingia kwenye vikao na akishiriki kwenye maamuzi na kupata dividend mwisho wa mwaka, na kodi ilipwe, ndiyo tutakubali kweli huyu ni mwanahisa; lakini hii habari ya kuchomekachomeka watu tu pale siyo sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikirudi tu jimboni kwangu Mwanga, kwa kweli niseme wazi kwamba katika Awamu hii ya Sita, jimbo la Mwanga limetendewa haki. Miradi yote ile ya kimkakati ambayo ilikuwa kwenye ilani na ambayo tuliomba baada ya ilani, imetekelzwa. Kuna iliyokamilika kabisa, lakini kuna iliyo kwenye hatua nzuri za utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sisi kama Mwanga, tunasema ilani imetekelezwa, Serikali imetutendea haki, na Mheshimiwa Rais ametufanyia haki. Kwa hiyo, hatuna mashaka na tunachokisema kwamba yeye ndio mtu sahihi wa kuendeleza kupeperusha bendera ya CCM. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi nzima inafahamu kwamba kulikuwa na mradi mkubwa sana wa maji wa Same – Mwanga – Korogwe. Mradi umekamilika sasa mwaka wa 19 huu toka umeanza, lakini Mheshimiwa Rais ameufungua, tunakunywa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekamilisha masterplan ya Mji wa Mwanga ambayo ilikuwa na package ya miradi; Hospitali ya Wilaya, VETA, barabara ya kimkakati ambayo tumeita CD Msuya Bypass, jengo la utawala la halmashauri pamoja na stendi. Hivyo, kuna ambavyo vimekamilika na vingine viko kwenye hatua nzuri za kiutekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa siwezi kumaliza mambo yote, lakini ukienda tu kwenye elimu, tumejenga madarasa 139, tumejenga shule mpya tano za sekondari na za msingi kadhaa, tumejenga mabweni 19, tumepandisha hadhi Chuo cha Ustawi wa Jamii kuwa Chuo Kikuu Kishiriki, tumejenga lango la utalii sasa, tunafaidi matunda ya hifadhi ya Mkomazi na tumepata miradi mikubwa ya umwagiliaji, wa mwisho ukiwa ni mradi wa shilingi bilioni 16.894 na ni mradi mkubwa sana ambao utatupunguzia sana kero ya suala la ajira, kipato na chakula.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, siyo huo peke yake; kuna mwingine wa shilingi bilioni 4.8 na mwingine wa shilingi bilioni 1.064. Si jambo la mchezo, kwa kipindi kifupi ambacho Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekaa madarakani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kimsingi, sisi mambo yako vizuri, lakini yako mambo tu matatu ambayo ni ya kukumbusha. Ninasema ni ya kukumbusha kwa sababu yameshaanza utekelezaji na mengine Mheshimiwa Rais alishayatolea maelekezo. Kwa mfano, stendi ya kisasa katika Mji wa Mwanga, bajeti ilishapita na tumeshaandaa uwanja. Kwa hiyo, ni suala tu tunaomba fedha zile ambazo ziliahidiwa zije pamoja na kituo cha afya cha kimkakati. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa.

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, mradi wa kuondoa magugumaji ya Ziwa Jipe ambazo pia bajeti ilishatengwa. Tunaomba Wizara ya Fedha sasa; hili hatumwambii tena Mheshimiwa Rais, tunaiambia Wizara ya Fedha, tunaomba tukamilishe hiyo miradi. (Makofi)