Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Francis Isack Mtinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii adimu sana ya mwisho ya kuchangia kwenye Wizara hii muhimu sana ambayo inaangalia afya za Watanzania na Taifa lenye afya ndiyo linaendelea kuwa Taifa bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze watendaji wa Wizara hususan Naibu, kwa sababu amekuwa hapo muda mrefu na kwa kweli ukimwangalia hata wakati anajibu tu maswali unajua kwamba pale Serikali imeweka chombo cha maana na ni msikivu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana wananchi wa Mkalama wajue tunapongea vituo vya afya ni kwenye TAMISEMI na zahanati zao ni kwenye TAMISEMI. Kwa hiyo, tunapoongelea kwenye Wizara hii tukiongelea mambo ya Kitaifa wasiseme Mheshimiwa Mbunge wetu anasimama anaongelea mambo ya Kitaifa wakati bado hatuna zahanati, hatuna vituo vya afya, huko ni TAMISEMI. Hata tunaongelea suala zima la nchi kwa maana ya afya ya Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wanahitaji matibabu. Watanzania wa hali ya chini ambao ndio wengi wanahitaji afya, na afya ni lazima wapate matibabu na matibabu ni ghali. Popote duniani matibabu ni ghali kwa sababu ya vifaa vyenyewe na kwa sababu ya dawa zinatengenezwa kwa gharama kubwa. Kwa hiyo, ndiyo maana tunakuja na suala zima la bima ili watu wazima wengi wachange fedha wawachangie wagonjwa wachache ili na wao waweze kuwa na afya bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Watanzania wajue kwamba tunapoongelea bima hatuongelei wagonjwa kuchangiana, tunaongelea Watanzania wenye afya njema wengi wachange fedha ili wagonjwa wachache katika nchi yetu waweze kutibiwa. Ndiyo maana chanzo cha fedha kinakuwa ni kitu muhimu sana kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wingi wetu Watanzania si laana. Wingi wetu ni baraka na wingi wetu ni mtaji wetu, kwa sababu siku zote mtaji wa watu, watu wakiwa wengi umoja wao ndiyo mtaji wao. Kwa hiyo, ninataka niwaambie Watanzania wanielewe vizuri, Serikali na Bunge hili linielewe kwamba tunapaswa kutumia wingi wetu ili tuweze kupata afya bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyanzo ni vingi vimetumika, mafuta sijui nini na nini, lakini chanzo cha wingi wetu bado hatujakitumia vizuri. Nitakwenda kwenye wingi wetu kwenye suala zima la matumizi ya simu za mkononi. Ni jambo jema sana kwamba Watanzania wamechukua vizuri teknolojia ya simu za mkononi, mpaka wazee vikongwe wana simu, mpaka watoto wa shule wana simu na wanazitumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa takwimu za TCRA za mwezi Machi, line za simu zilizo hai, siyo mfu hai ni milioni 90.4; katika line hizi hai watumiaji wa internet ni milioni 49. Maana yake hawa wanatumia MB kweli kweli. Wanaotumia dakika tu viswaswadu vile na nini bila internet kwa ujumla wao, dakika zinazotumika ni takribani bilioni 40.6, dakika bilioni. Katika hizi, kutoka nje ya nchi zinakuja karibu dakika milioni 36. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii maana yake nini? Ninapenda tukitumie chanzo hiki Watanzania wanielewe. Hii wasije wakachanganya, wasije wakachanganyana yaliyotokea huko nyuma kwenye suala la kutuma fedha unakatwa na yule anayepokea sijui na nini, hapana! Hapa tunataka tuongelee mchango wa Mtanzania kidogo ambaye ni mzima amchangie Mtanzania mwenzake ili Watanzania wote wapate bima ya Taifa, bima kwa ajili ya matibabu kwa Watanzania wote, tena bima isiyo na ngazi, bima ambayo ni flat rate. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa idadi hii ya Watanzania, ya line zilizo hai milioni 90.4, ninataka niende na hesabu ndogo sana. Tuchukulie kila Mtanzania anaponunua voucher, awe anaitumia kwa MB kwa ajili ya internet, awe anaitumia kwa dakika, ili mradi lazima atoe hela kidogo apate uwezo wa kuitumia simu yake. Ninataka nimwombe Mtanzania anielewe sana. Mtanzania maskini wa hali ya sana mwenye uwezo wa kununua voucher ya shilingi 1,000 kwa siku, nimwombe Mtanzania huyu anayenunua voucher ya 1,000 kwa siku atuchangie 10% ya shilingi 1,000 ambayo ni shilingi 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi 100 hii ukizidisha kwa line zilizo hai milioni 90.4 nitapata kwa siku bilioni 9.4 per day, lakini hela hii nikiipeleka kwa mwezi kwa siku 30, nikachukua bilioni tisa hizi nikazizidisha mara 30 nitapata bilioni 271.2. Bilioni! Lakini nikizipeleka kwa mwaka kwa sababu bajeti zetu zinakwenda kwa mwaka, nikazidisha hizi fedha bilioni 271.2 mara 12 nitapata trilioni 3.2. Sasa, kwa sababu hizi ni hesabu za karatasi, basi nifanye tu kwamba nimekosea sana niende half way ya hizi hesabu, nusu yake. Maana yake tutapata trilioni 1.5 ambayo itaingia kwenye Mfuko wa Bima kwa ajili ya Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtanzania ambaye amechangia shilingi 100 kwenye 1,000 yake anaponunua vouche, na kampuni za simu kazi yao ni kutukusanyia tu hawatakiwi kuweka charge nyingine yoyote. Kwa hiyo, ninaomba Watanzania, ukitoa hiyo ambayo hutaona maumivu yake, kwa sababu wewe ukitoa 1,000 unawekewa MB za shilingi 900. Wala hu-feel lakini ujue kabisa umemsaidia Mtanzania akatibiwa kwenye MRI, anaweza akatibiwa kwenye cancer vipimo mbalimbali, kwa hiyo shilingi 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona mifano hai kwenye Kodi ya Pango. Watanzania walikuwa wanalalamika sana kwenye Kodi ya Pango, lakini tulipoipeleka kwenye LUKU wala hawa-feel. Wananunua umeme wao wameshalipa pango, wa kijijini analipa. Tumeona kwenye ile kodi ya barabarani ile ya magari ambayo ilikuwa inasumbua sana tunakamatwa na trafiki njiani, lakini tulipoipeleka kwenye mafuta hata Mtanzania anayemwagilia nyanya tu shambani akiwasha ile pump yake ya petroli ameshachangia ile levy ya barabarani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa mtindo huu niombe sana hizi data zichukuliwe na kama kwa kufanya uchunguzi zaidi wakaunda hata tume wakafuatilia vizuri, hii ni pesa nyingi ambayo Mtanzania wala ha-feel. Wako watoto wadogo tu, wanasema baba niwekee MB anacheza game tu, baba niwekee MB anaangalia tu picha, lakini ukishamwekea zile MB za 1,000 tayari yule mtoto ameshachangia shilingi 100 kwa ajili ya matibabu ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki ni chanzo cha uhakika ambacho hakina maumivu, hakina kelele, lakini kinaleta trilioni tatu kwa mwaka katika bajeti ya Bima ya Afya. (Makofi)

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana Serikali ...

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Gekul.

TAARIFA

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nimpongeze Mheshimiwa Francis kwa mchango mzuri. Nimpe tu taarifa, kwenye Kodi ya Majengo wanaolipa siyo wale wenye LUKU tu saa hizi. Majengo yote yaliyojengwa kwa tofali pia wanalipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwenye 1,800 kwa mwaka ikatumika tu shilingi 50 itasaidia wale wananchi ambao wanahangaika na moyo, cancer, dialysis, itatusaidia sana. Serikali ichukue mawazo mazuri ya Mheshimiwa Francis. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Francis unapokea mchango wa Mheshimiwa Gekul?

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapokea kwa mikono miwili. Niiombe Serikali, hivi ni vyanzo vya uhakika ambavyo Watanzania wote watatibiwa tena bima iliyo sawa, hamna acha kusema hii kubwa hii Serengeti hii sijui hii Ngorongoro. Itakuwa ni bima ambayo inaenda popote kwa sababu watakuwa wamechangia fedha za uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani ikianza tu leo kesho unasikia mabilioni yameingia Mheshimiwa Waziri. Yaani ikianza kesho, kesho unasikia matrilioni, haina ujanja, sisi wenyewe ndiyo tunanunua. Nina line nne, zote ziko hai na kila siku lazima niziwekee voucher. Kwa hiyo, kila nikiweka tu line ujue tayari nimechangia. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali ichukue jambo hili, ni la muhimu ambalo litasaidia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tu nimalizie kwa kusema mchango ambao ulisemwa pia na mwenzangu pale muda mfupi. Suala zima la madaktari kufanya consultation kwa wagonjwa; niombe, badala ya kuangalia kituo sasa tuangalie taaluma ya yule anayetoa consultation. Awe ameitoa kwenye kituo cha afya, awe ameitoa kwenye zahanati, kwa sababu daktari anaweza kuwa ni specialist yulo kijijini kwao likizo. Ameenda kusaidia wananchi kwenye kizahanati cha pale kijijini, akatoa huduma pale akasikiliza wagonjwa; lakini sasa eti yule atachajiwa kwa sababu ya kile kituo ni kizahanati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini asichajiwe ile hela yake kwenye bima kwa sababu yule ni specialist na atakuwa amesaidia jamii pale? Hii itasababisha hata madaktari wengi ambao hawana ajira watakwenda kujitolea kwenye hizi zahanati zetu, kwa sababu anajua akitoa huduma atachajiwa kwa sababu atalipwa na bima, kwa sababu ya elimu yake, siyo kwa sababu ya kituo alikotolea huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itasaidia. Kama kuna kuogopa kwamba itatumika vibaya, Chama cha Madaktari chenyewe ndicho kidhibiti leseni zao. Kwamba kuna daktari fulani alikuwa kijijini kule Mkalama akatoa consultation, akaandika dawa ame-over. Pengine ameandika hovyo labda kwa rushwa, Chama cha Madaktari ndicho kitadhibiti kimnyang’anye leseni. Kwa hiyo, niombe huduma za consultation ya madaktari bingwa zitolewe na hao madaktari kwa elimu zao, siyo kwa kituo anakotolea huduma ili Watanzania watumie hii huduma ya madaktari wengi walioko mtaani ili waweze kupata afya njema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa nafasi hii, ninaomba mchango wangu uchukuliwe kwa uzito mkubwa sana. Ahsante na ninaunga mkono hoja. (Makofi)