Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Eng. Stella Martin Manyanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nyasa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ENG. STELLA N. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu na vilevile nikushukuru wewe kwa kazi kubwa anayoifanya na ninaamini kule Njombe hawatamsumbua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo kawaida nitaanzia kwa kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu pamoja na wote wanaomsaidia katika kuhakikisha kwamba afya za Watanzania zinazidi kuimarika. Pia, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri mdogo wangu Jenista Mhagama pamoja na Naibu wake. Ninaamini leo kule Songea yule mwanaye Ibrahim kwa jina maarufu tall leo atakuwa ana furaha sana, kwa sababu kila wakati tall akimwandika kwenye mtandao hajawahi kubadilika kumsifu kwa kazi zake nzuri. Kwa hiyo, ninamuunga mkono leo na ninasema watu wenye roho nzuri kama hao, leo Ibrahim nimeona aingie kwenye Hansard za Bunge, ni mtu mwema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hayo yaliyozungumzwa nianzie na pale alipoishia Mheshimiwa Gekul kwa sababu muda ulimwishia. Kwa kweli hali ya hivyo vifurushi vilivyopangwa haioneshi sisi Watanzania kuthamini utu na utu uzima. Kwa sababu huyu mzee mara nyingi ndiye aliyestaafu. Amestaafu kutoka kwenye aidha ajira rasmi au hata kama alikuwa kwenye ajira zake binafsi za kilimo na kadhalika. Ametumika miaka yote ya umri wake katika kuisaidia nchi hii halafu mwishoni anaambiwa sasa wewe kwa sababu umeshakaa sana tunakuwekea hiki kifurushi kikubwa kikusaidie. Hivi maana yake ni nini ndugu zangu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninadhani waliopanga walikuwa hawajajua hali halisi. Huyu mzee anahitaji kusaidiwa, hana kitu halafu ndipo kifurushi chake kinakuwa cha milioni. kwanza hata kula yake ni tatizo, sasa hizo milioni kadhaa zinatoka wapi? Simply kwa sababu tunamhofia atakuwa anaumwaumwa kila wakati, ana magonjwa yale mazito mazito. Ndiyo gari bovu limeshatumika, kwa hiyo inabidi wote wenye nguvu tumsaidie na hiyo ni heshima na hekima kubwa mbele za Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, ninamwamini, pamoja na Naibu wake na timu yao yote wayasikie haya maneno yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii si mara ya kwanza tunazungumzia juu ya umuhimu wa kuwa na utaratibu wa kuchangia hizi bima kiurahisi zaidi kuliko kung’ang’ania kuweka fedha nyingi kwa mtu mmoja. Jamani sisi tunaotoka vijijini tunashuhudia watu wanakufa kwa kushindwa kupata huduma na tena hizo huduma zinapatikana mbali, inabidi asafiri. Kwanza nauli ni nyingi halafu akifika hapo anatakiwa tena kutoa hizo gharama nyingine. Tafadhali, kwa namna ya kipekee ninaomba tuliangalie hilo suala upya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwanza pongezi kwa Mheshimiwa Waziri kwa jitihada kubwa walizozifanya. Wilaya yangu ya Nyasa sasa hivi ina sehemu nyingi za kutolea huduma za afya ikiwemo zahanati; tunazo sasa 40, vituo vya afya tulikuwa navyo vitano, sasa hivi tunaenda kwenye saba. Pia, hospitali ukijumlisha na zile za Makanisa tutakuwa nazo sasa tatu; na ambulance wametuletea. Hata hivyo kuna changamoto ya wataalam. Tunaomba sasa tusiangalie tena vijijini kama wakati ule. Watu wameelimika, wanahitaji kupata zile huduma mbalimbali zinazojitosheleza, ikiwemo huduma za kibingwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi leo huduma za kibingwa katika mwongozo walionao, wanasema kwamba kwenye wilaya hakuna huduma za kibingwa; kwa hali hiyo mtu mwenye bima ya afya akienda kutibiwa na bingwa katika eneo lile, anaambiwa huyu daktari bingwa huyu kama yupo kwenye hospitali ya wilaya ni sawasawa na ameenda pale kwa bahati mbaya. Kwa hiyo, hawezi kumwandikia mgonjwa wake dawa zile zinazoandikwa na daktari bingwa simply kwa sababu yupo katika hospitali ya wilaya. Hiyo inakatisha tamaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa tumeifanya na Serikali yetu imefanya kazi kubwa. Sasa, ipunguze gharama za watu kuendelea kuhangaika kwenda mpaka mijini mbali huko wakati tayari wangeweza kupata huduma hizo kwenye maeneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hao mabingwa uzuri wake hata wakienda kwenye maeneo haya ya wilayani wanapenda kabisa kwa sababu sasa hivi wilaya zote ni nzuri. Wilaya kama ile ya Nyasa wewe mwenyewe unaona Maasha Allah, wilaya nzuri. Mtu atapenda tu kukaa kule siyo? Sasa vitu vidogovidogo vinakwamisha. Yeye akimtibu mgonjwa eti kwa sababu yupo wilayani alipwe 7,000, huyu aliyeko mkoani au maeneo mengine alipwe 25,000 (yaani inalipwa kutoka kwenye hospitali). Sasa, hiyo inakatisha tamaa na hata zile hospitali za wilayani zinashindwa kukusanya mapato stahiki kwa sababu wale madaktari wao kama bingwa wanachukuliwa kama daktari wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kuuliza swali hili humu Bungeni, kwa hiyo ninaomba lifanyiwe kazi mapema ili hospitali zote za wilaya ambazo zina uwezo wa kupata madaktari bingwa zipate madaktari bingwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo changamoto kubwa imebakia kwenye uzazi. Kwa sasa hivi tumeshapunguza sana vifo vya mama na mtoto na sasa tunataka kupata maisha bora zaidi. Kwa hiyo, tunataka hao Gynaecologists waende huko kwenye wilaya sasa. Mabingwa waende kwenye wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna huu usafiri wa pikipiki ambao upo kwenye kila eneo na tunautumia sana, lakini hivyo hivyo watu wanavunjika miguu, mikono, meno. Sasa unakuta kwenye maeneo ya wilaya kwanza wataalam wa X-Ray wapo wachache, kuna maeneo hawapo kwa mfano kwenye vituo vya afya hawapo, lakini vilevile, hao wa meno hawapo wa kutosha. Kwa hiyo, tunachoomba tuwekeze kwenye kupata hawa wataalam. Washuke sasa huku chini ili tuendelee kufaidi kazi nzuri aliyoifanya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha kwaba wananchi wake wa Tanzania wanakuwa na afya bora, wanakuwa na maisha bora. Kwa kweli saa hizi hata ukimwona mtu wa kijijini hana tofauti na mtu wa mjini. Hakuna tofauti kabisa, kwa sababu wote wanafurahia maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo niseme tu kwamba ninazidi kuomba. Ningetamani katika upangaji wa bajeti zinazoendelea, pale Tingi ambapo ni makao makuu ya Tarafa ya Mpepo wapate kituo cha afya ambacho kitakaribiana na hadhi ya hospitali kwa sababu idadi ya watu katika ukanda ule ni kubwa. Kwa hiyo, ni mambo ya kumalizia tu katika kazi nzuri ambazo zimefanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizidi kuwashukuru na kuwapongeza sana wananchi wa Wilaya ya Nyasa. Kwanza kwa heshima kubwa ambayo wamenipa mimi kuwa Mbunge wao kwa vipindi viwili. Mbunge mwanamke, ninaamini sijawaangusha na ninaamini wao wananipenda na ninaamini hawatatishwa na kitu chochote kile (kiwe pesa, au maneno) bado wataendelea kumuenzi Mbunge wao mpendwa aka Kagauni Engineer Stella Manyanya, kwa sababu tumefanya kazi kubwa kwa kushirikiana na wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, pia niseme tu kwamba maisha yetu yanahitaji utulivu. Maisha yetu yanahitaji upendo, maisha yetu yanahitaji kusaidiana. Kwa misingi hiyo, sisi Wabunge ambao tunamaliza muda wetu tulijitahidi kwa uwezo wetu wote kuhakikisha tunatimiza wajibu wetu. Saa hizi wao na wenyewe watapimwa kwa kutimiza wajibu wao kuwatendea haki waliofanya vizuri kwenye maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo itakuwa ni motisha hata kwa Wabunge wengine wanaokuja, kwamba, kumbe nikifanya vizuri nitachaguliwa tena. Kumbe nikazane nifanye inavyotakiwa ili nichaguliwe tena, lakini kama watathamini visenti vinavyomwagwamwagwa kama upupu huko wakasahau yote mazuri yaliyofanyika, hakika watakuwa wanatunziwa vifedha kwenye bahasha halafu hakuna watakachokiona kinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana wananchi wangu wamenizoea nikisema hayo kila wakati, lakini nimeona iwe kwa faida ya Watanzania wote. Hali kadhalika, hicho ndicho kitakachompa sana Mheshimiwa Rais wetu kura za kutosha kwa kazi kubwa aliyoifanya. Tunawashukuru sana wote, tunamshukuru Makamu wa Rais kwa kumsaidia sana Mheshimiwa Rais, tunamshukuru Waziri Mkuu, Naibu Waziri Mkuu, Mawaziri wote na kwa kweli kila mmoja kwa nafasi yake bila kuwasahau wataalam wa afya. Wamekaa huko saa hizi wananisikiliza, tunawashukuru sana kwa wema weo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kumsahau DMO wangu, ananisaidia sana katika Jimbo langu la Nyasa. Ninasema ahsanteni sana, Mwenyezi Mungu awabariki. (Makofi)