Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Babati Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa nafasi. Jioni ya leo nichangie Wizara ya Afya Vote 52 katika bajeti yao hii muhimu ambayo inagusa maisha ya Watanzania. Nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutupatia nafasi kuendelea kutimiza wajibu wetu kama Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni shukrani. Nimshukuru sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo ametuheshimisha na kutukimbilia Wanababati kwa sekta hii ya afya. Sisi Wanamkoa wa Manyara tunamshukuru na tuna deni la kulipa kwa Mheshimiwa Rais wetu kwa mambo ambayo yamefanyika na ambayo muda wote yalikuwa hayajawahi kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Hospitali yetu ya Mkoa ni juzi tu ametupatia vipimo vya dialysis (mashine za dialysis), pia kwa mfumo mzima wa chakula ili wananchi waweze kupata matibabu hayo na maendeleo yanaonekana katika Hospitali yetu ya Mkoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wetu Jenista atufikishie salamu zetu za dhati kwa Mheshimiwa Rais, kwamba Wanamanyara tunamshukuru kwa hospitali ile. Matibabu yanatolewa na majengo yanaendelea. Niombe tu hizo bilioni mbili ambazo zimepangwa katika bajeti hii katika miradi 55, ambapo miradi 31 ikiwemo Hospitali ya Mkoa wa Manyara hazijapata, tunaomba ikiwapendeza katika hizi siku 20 zilizobaki basi watupatie hizo fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hospitali ya wilaya tumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kweli kwa miaka hii ya Mheshimiwa Dkt. Samia tumepata hospitali ya wilaya pale majengo yenye thamani ya zaidi ya 1.4 billion, wametupatia. Mpaka wametupatia Kangaroo room kwa ajili ya wale watoto njiti, wamekuwa sasa wanahudumiwa pale. Pia, tumejengewa wodi ya wanawake kwenda kujifungua zaidi ya shilingi milioni 500. Tumepatiwa emergence ward yenye thamani ya milioni 300; na sasa 1.4 billion inaendelea pale, majengo yetu yameboreka sana. Tusipokuwa na shukrani kwa kweli hata Mwenyezi Mungu hawezi kutubariki. Mheshimiwa Waziri atufikishie shukrani hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vituo vyetu vya afya. Mimi nina kata nane, katika kata hizo ni kata mbili tu zimebaki. Kata ya Nagala pamoja na Kata ya Singe vituo vya afya ambako hizo hela Mheshimiwa Waziri niliongea naye pia kwamba, tupatiwe ili vile vituo viwili viweze kukamilika. Kwa kweli kwa jimbo letu tuna moyo wa shukrani kwa Mheshimiwa Rais wetu, Serikali yetu pamoja na Mawaziri wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri yeye na msaidizi wake, wamekuwa wasikivu, wanafikika na tunapokuwa na shida yoyote tukiwapigia simu kwa kweli wamekuwa wakitusaidia; hasa wagonjwa wale ambao wameshindwa kutibiwa, wamekuwa wakitusaidia sana. Hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri. Kwa uzoefu alionao ninaamini atasaidia hii Wizara ya Afya; akisaidiana na Dkt. Mollel. Tunawashukuru sana kwa jinsi ambavyo wamekuwa wakituhudumia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la pili, kuhusu hizi fedha za MSD, ambapo wanaomba wapatiwe deni hili la bilioni 434, na NHIF bilioni 210. Kwa kuwa sekta hii bado wahitaji ni wengi tunaomba basi fedha hizi zitolewe na Wizara ya Fedha ili taasisi zetu hizi ziweze kufanya kazi kwa ufanisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni kuhusiana na suala la Sera ya Afya Bure kwa wajawazito, watoto chini ya miaka mitano pamoja na wazee. Juzi niliuliza swali; kwamba ni nini hasa ambacho ni bure? Kwa sababu tumekuwa tukipata sana simu za akinamama wajawazito wanaojifungua. Nimshukuru sana Dkt. wetu wa Hospitali ya Mrara pale Babati, amekuwa akitusaidia sana Madiwani pamoja na Mbunge. Mama anakwenda kufanyiwa operation; operation ni bure, lakini akitoka tu kule theatre vifaatiba, sindano dawa, kila kitu anachajiwa (to be charged).
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Waziri amesisitiza kwamba sera hii bado ipo pale pale na ndiyo tunayoisimamia. Basi ninamwomba ikimpendeza dada yetu wakati wa ufafanuzi atuambie tu, kwamba ni bure kweli au kuna vifaa vinakuwa charged? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri alisema kuwa 60% ndiyo ambayo Serikali inachangia, 40%; kwenye swali la nyongeza nililoliuliza ndiyo yule mama anayochangia. Basi atuweke wazi ili iepushe usumbufu tunaowapatia madaktari wetu na kuwaambia tibuni bure, sera ni bure, kwa nini wanawa-charge? Tukiweka hili huru litatuweka huru. Tunaomba siku ya leo wawatangazie Watanzania kwamba kuna mtu mwenye uwezo anakuwa charged, kuna mtu asiyekuwa na uwezo anakuwa charged hata kama yupo kwenye hiyo package. Itatusaidia sana na itabariki kazi njema tunayoifanya katika Serikali yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana pia atupatie ufafanuzi, kwamba, baada ya kuleta hivi vifurushi vya bima ya afya; je, bado tunasimamia hii sera yetu ya afya bure kwa wale au kuna change sasa; kwamba tunahama sasa wote ni lazima twende kwenye bima ya afya? Sasa, wakati tukisema sera yetu inasema tunawatibu bure wakati huu tume-introduce vifurushi vya bima ya afya kwa wote na sheria tumepitisha, hapa atatusaidia ufafanuzi. Tunaenda na lipi, wote twende kwenye bima au bado hii timu inatibiwa bure?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye hivi vifurushi; Mheshimiwa Waziri ana vifurushi vya Tarangire, Ngorongoro, Mikumi, Serengeti na Tanzanite. Ni jambo jema kabisa. Tulipopitisha Sheria hii ya Bima ya Afya kwa Wote Mwaka 2023 tuliomba Serikali yetu na Mheshimiwa Waziri watuletee hivi vifurushi kupitia kanuni. Ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri, Kamati yetu ya Bunge ya Huduma za Jamii pamoja na Kamati ya Sheria Ndogo wapitie hivi vifurushi waone affordability ya hivi vifurushi kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye vifurushi hivi; mfano, mzee mwenye miaka 60 plus ukimlipia kifurushi cha Tarangire shilingi 240,000 anapata huduma zifuatazo; anamwona daktari bingwa, lakini huyu mzee mwenye 60 plus anakosa huduma ya dialysis. Mheshimiwa Waziri anafahamu kuwa wazee wengi wa 60 plus wana matatizo ya sukari, pressure, magonjwa ya moyo na wanahitaji mazoezi tiba; lakini wanakosa vipimo vya MRI, CT-Scan, mazoezi tiba, saratani na cha dialysis. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki kifurushi cha tarangire ndicho ambacho wananchi wetu wengi wa hali ya kawaida wakisaidiwa na vijana wao kuwalipia labda, maana ni mzee tunataka awe na bima, hiki ndicho kifurushi ambacho ni affordable kwa vijana na familia wanaweza wakamlipia huyu mzee ambaye ni 60 plus.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama huyu mzee ambaye yupo kwenye 60 plus yupo kwenye ndoa; hawa wawili kwenye kifurushi cha tarangire analipa 472,800/-; lakini akienda kwenye kifurushi ambacho kinamsaidia kupata tiba za dialysis, saratani, mazoezi, tiba ya MRI, CT-Scan na kadhalika analipa milioni 13,214,760/-. Hayo ndiyo mahitaji ya wananchi tunaowawakilisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wazee ambao wapo kwenye ndoa, Mungu kawajaalia, wanalipa milioni 13. Maana yake ni kwamba watoto wao wanapaswa watafute, per month, isipungue milioni moja, ili waweze kupata hizi milioni 13 kwa mwaka. Bado tunaona hivi vifurushi ni ghali sana. Niombe na niishauri Serikali yetu, kwamba, kwa kuwa hivi vifurushi siyo affordable kwa wananchi, tuone sasa tuangalie jinsi gani tunaweza tukachangia matibabu, sisi Watanzania kwa wote. Hii ni kwa sababu lengo la bima ni kuchangiana, kusaidiana. Yule ambaye hajiwezi tumsaidie au asaidiwe na wale ambao wanajiweza. Huyo asiyejiweza ukimpeleka milioni 13 maana yake hawezi kwenda hospitali akatibiwa, akapata hayo matibabu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Mheshimiwa Waziri wasi-hesitate kuleta vyanzo ambavyo Watanzania wote tutavichangia. Kama kwenye barabara tulikatwa shilingi 100 ikatusaidia katika kujenga barabara zetu why not kwenye line za simu milioni 90 tulizonazo tukahitaji hata shilingi 500, ili hiyo isaidie mtu mwenye moyo, saratani, sukari ambapo hayo magonjwa yanaendelea kwa kasi kubwa sana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri kwenye bajeti ya Mheshimiwa amesema hivi, kwamba amesamehe wagonjwa zaidi ya 3,000, zaidi ya bilioni tatu; maana yake Mheshimiwa Waziri amezitafuta na kuzilipa, wale ambao tunamwambia hawajiwezi. Sasa, ili taasisi zisiendelee kulipa hizi fedha kwa machungu makubwa kwamba mtu amefariki, imeletwa milioni sita, wanajamii hawana, tunawashukuru tunawapigia wanatusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri tusi-hesitate, twendeni tuka-identify chanzo ambacho Watanznaia watachangia wote. Tunaweza tukaenda kwenye crop cess. Kwa sababu watumishi wa Serikali…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MWENYEKITI: Kengele ya pili.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja na ahsante. (Makofi)