Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuchangia katika hii Wizara muhimu. Moja kwa moja ninaanza kwa kumpongeza sana dada yetu, Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama, Mlezi wa Mkoa wetu wa Kilimanjaro, Kiserikali kwa hiyo, Waziri ndiyo mlezi wangu kule Kilimanjaro. Pongezi sana kwako dada Mheshimiwa Mhagama kwa kazi nzuri anayoifanya Wizarani na mkoani kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza kwa namna ya pekee, kidiplomasia yuko vizuri, anaona mambo, nilimwona alivyokuwa anapambana Marehemu Dkt. Ndugulile apate ule u-director, Profesa Janabi na hata mama sasa amepewa Award ya Bill Gates, ambayo tunaita ni Goalkeepers Award. Inaonesha kwamba, kwenye diplomasia uko vizuri. Ninampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeze pia rafiki yangu, Mbunge mwenzangu wa Mkoa wa Kilmanjaro, Mheshimiwa Dkt. Molel, watu wa Siha wajue wana jembe. Nina siri kubwa sana na Mheshimiwa Mollel, mwaka 2009 aliokoa maisha yangu, hatakumbuka, lakini mimi ninajua; nilivyorudi kumletea suti akawa ameshahama, nikiwa ninafundisha South Africa. Kwa hiyo, tuna jembe, tena zuri sana, hongera sana. Pia, ninampongeza Katibu Mkuu – Dkt Shekalaghe, Makamu wake, Naibu wake pamoja na watu wengine wote wa Wizarani kwa kazi nzuri wanazofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza sana Serikali, imewekeza vizuri pale kwenye Hospitali yetu ya KCMC, kama alivyosema Mbunge mwenzangu, Mheshimiwa Priscus Tarimo wa Moshi Mjini. Pale tunaona Serikali imewekeza shilingi bilioni nne kwenye lile Jengo la Mionzi na wamewekeza kwenye jengo moja, bado kuna majengo manne yako tu kwa hiyo, tuwaombe, hakuna hasara hata kidogo kuwekeza KCMC kuna wabobezi wa hali ya juu ambao wanatoa tiba ya kubadilisha nyonga; ukishazeeka, nyonga ikikataa, nenda pale utapata tiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanafanya upasuaji kwenye mfumo wa chakula, tezi dume wanafanya oparesheni, wanatibu ugumba, wanapandikiza cornea na wanatengeneza viungo bandia. Kwa hiyo, ni hospitali ambayo hutashangaa kwenda pale, kusema ukweli, wanatoa huduma nzuri kwa hiyo, ninaiomba Serikali tuendelee kuwa-support.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Profesa Masenga. Kupitia msamaria mwema wametoa, wame-waive, msamaha kwa wagonjwa wengi sana, kama 4,002, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 2.1 wamesamehe bure. Kwa hiyo, tuna Profesa, Mungu ambariki kuendelea kusaidia watu wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kabla sijaanza mchango, ninaomba mambo ya kwenye jimbo langu kwanza. Mheshimiwa Waziri nilimwomba anisaidie Digital X-Ray, kwa ajili ya Hospitali ya Kibosho, ambayo ni Referral Hospital ya Wilaya ya Moshi, ilikuwa ni Bajeti ya 2023/2024. Alivyokuja Mabogini nilimwomba, yaani ni kama nimeonekana mtu wa ajabu ni kwamba, hawa watu hawajapata kile kifaa na wananilaumu sana. Ninaomba jamani, aandike mahali tu, wasije wakawasahau tena hawa jamaa zangu, ni hospitali muhimu sana inasaidia Watanzania (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba vifaatiba, ninajua mengine ataongea na pacha mwenzake. Vifaatiba katika Vituo vya Afya vya Uru Kusini, Uru Shimbwe, Uru Kyaseni na Kibosho Umbwe; Kituo cha Afya cha Kibosho Ubwe ni cha zamani kinahitaji vifaatiba na pia, kwenye ile Hospitali ya Wilaya ya Mabogini bado vifaa tiba havijafika pale. Tunaomba watusaidie ikiwa ni pamoja na magari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu kiujumla utahusu changamoto za tiba hapa nchini. Ninaanza kwa kusema kwamba, huduma ya afya ni haki ya binadamu. Hata kwenye Biblia kuna mistari 108 inayoongelea kuhusu afya ya mwili na tujikumbushe hapa, hata Yesu Kristo alivyokuja duniani hapa alitibu watu kwa kutumia nguvu zake za Kimungu, alijua nini maana ya afya na alitoa tiba ya magonjwa mbalimbali, sote tunafahamu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Mungu mwenyewe alituhurumia sisi wanadamu akatutibu, ninaiomba Serikali, ambayo ni mamlaka iliyowekwa na Mungu yuleyule, tujitahidi kabisa tuwasaidie wananchi wetu wapate tiba, ili tupate baraka za Mungu, Serikali yetu ipate baraka za Mungu. Ninamshukuru Rais anajitahidi kusema ukweli, wamefanya vitu vingi vizuri sana, tuweke nguvu kwenye hizi changamoto nitakazozisema, ili tusaidie wananchi wapate tiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya kwanza hapa nchini ni gharama kubwa ya matibabu kwa baadhi ya magonjwa. Mtu akiugua ugonjwa kama figo, wenzangu wameshasema, cancer, moyo, kubadilisha damu na ugonjwa wa selimundu, wewe ujue unakwenda, kama usipokuwa na pesa unakwenda kufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu kidogo niongelee ugonjwa wa selimundu ambao wachangiaji wenzangu hawajausema. Katika ripoti ya Mheshimiwa Waziri amesema kwamba, 15% ya Watanzania wana vinasaba vya selimundu kwa hiyo, huko mbele ya safari nina hakika tutakuwa na wagonjwa wengi sana wa selimundu kwa sababu, tutakuwa tunaoana kati ya mtu mwenye selimundu vinasaba na mwingine mwenye selimundu, tutakuwa na wagonjwa wengi. Sasa hivi wame-identify watu 34,220 wenye selimundu na 60% wanaowatibu kwa kutumia hydroxyurea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, safi kabisa, lakini ni watu 11 tu katika hao watu 34,000 ambao wameishawafanyiwa upandikizaji wa uroto, ambayo ni sawa na asilimia 0.03 ya watu wote ambao wamekutwa na ugonjwa huu. Ninaiomba Serikali, haya magonjwa ni makubwa, magonjwa aliyoyataja Waziri ikiwepo selimundu, wataalam tunao, vifaa tunavyo; ninaipongeza sana Hospitali ya Benjamini Mkapa, wanafanya kazi nzuri, tusitibu watu 11 tu, tutoe ruzuku ya kutibu hawa watu, ili nao wapate maisha na wafurahie kuwa Watanzania. Ninaiomba sana Serikali itoe ruzuku, kwa ajili ya haya magonjwa makubwa niliyoyataja ukiwepo huu wa selimundu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine, ya pili, ni ukosefu wa vifaatiba, ukosefu wa dawa na chanjo kwenye baadhi ya maeneo ambayo yako vijijini. Tukiondoa yale maeneo, ambayo ni hospitali mpya, tumezijenga au vituo vya afya vipya tumevijenga, vile vya zamani vingi vina uhaba wa vifaa tiba. Kwa mfano, vitanda vya kulaza wagonjwa kusema ukweli, ni shida katika baadhi ya maeneo; majokofu ya kutunza dawa, kutunza maiti, magari, dawa, hata chanjo, ninaiomba Serikali, hebu tujiongeze, tuwekeze kwenye haya maeneo tusaidie vile vituo vya vijijini ambako ndiko wanakoishi watu wengi. Tukishasaidia kule vijijini idadi ya watu watakaokuja Mjini kupata tiba itapungua na tutakuwa tumewasaidia sana Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine kubwa ambayo iliyopo kule vijijini au kwa Watanzania kwa ujumla ni uwepo wa wanachama wachache waliojiandikisha kwenye Mfuko wetu wa Bima ya Afya. Watu wengi hawajajiunga na mfuko huu kutokana na gharama kubwa ambazo zimeainishwa. Ninaomba nitoe mifano, japokuwa wenzangu wamekwishasema, ninataka tu tuangalie umuhimu wa hiki kitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Ngorongoro Afya na kuna Serengeti Afya. Sasa kwa watoto wadogo kati ya umri wa 0 – 17 years akichukua kifurushi cha Ngorongoro ni shilingi 240,000, akichukua cha Serengeti ni Shilingi 660,000. Kwa miaka 18 – 35 hapa kwenye hii age ndipo tuna idadi kubwa ya Watanzania. Akichukua cha Ngorongoro ni 432,000 na Serengeti ni 792,000. Akiwa na mke vyote vinapanda zaidi, kama alivyoongelea mchangiaji mmoja aliyepita. Miaka 36 – 59 Ngorongoro ni 540,000 na Serengeti 1,620,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wale watu wazima kama mimi. Ukishakuwa mtu mzima kama mimi Ngorongoro ni shilingi 708,000 na Serengeti ni shilingi 3,336,000. Ukiwa na mwenzako Ngorongoro ni 1,345,000/- na Serengeti ni 6,338,400. Hizi data nimezipata kutoka kwenye website ya NHIF. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, tuwe wakweli; watu wengi kule vijijini uwezo wao wa kununua hivi vifurushi ni mdogo sana, huo ndio ukweli wa Mungu. Kwa hiyo, niiombe Serikali hebu chondechonde, ninajua kuna gharama zinatakiwa mtu alipe ili atibiwe, lakini Watanzania ni hawa hawa uwezo wao ndiyo huo. Sasa tusipofanya kitu kurekebisha mambo watakuwa wanafia kule nyumbani kwa sababu hawawezi kukata hivi vifurushi. Watakuwa wanafia nyumbani badala ya kwenda hospitali kwa sababu kama mtu hana bima ya afya na hana fedha ya kwenda kujitibu itakuwa ni ngumu sana. Niiombe Serikali kwanza itafute namna ya kusaidia hawa watu ili waweze kumudu hivi vifurushi, virekebishwe if possible; wafanye marekebisho fulani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuhamaishe; tufanye uhamasishaji wa hali ya juu kwa sababu inaonekana watu wengi hawajaingia kwenye bima ya afya. Tuhamasishe watu watu wajiunge na hii mifuko, ili mtu atakapougua kama ana bima ya afya akienda kupata tiba hospitali hatapata shida, hatarudishwa, atatibiwa na ataishi kama ambavyo Mungu amempangia awe na maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo ni mengi, ninaomba niseme tu mengine nitachangia kwa maandishi. Baada ya kusema hayo nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake na watendaji wake wote. Sisi tunawatakia kila la kheri; lakini ninaomba yale niliyomwomba kwenye jimbo langu na yale ambayo nimependekeza ayachukulie seriously ili Watanzania wanufaike na kazi nzuri wanayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)