Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa nafasi hii ya kuchangia Hotuba ya Wizara ya Afya, nianze tu kwanza kwa shukurani. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu, sisi Moshi Mjini kwa kipindi hiki tulikuwa hatuna Hospitali ya Wilaya; tunajengewa, tena ya ghorofa na kazi inaendelea. Mheshimiwa Waziri alikuja pale aliiona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tuna vituo vya afya viwili, lakini tumepata vingine viwili na cha tatu, nimeambiwa muda wowote hela itakuja, kwa ajili ya Kituo cha Afya cha kule Kata ya Kiboroloni. Zimefanyika kazi nyingi sana kwenye Hospitali yetu ya Mawenzi na pia, zimefanyika kazi nyingi sana, hata nikizitaja sitaweza kumalizia, katika Hospitali yetu ya Kanda ya KCMC.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri wetu pamoja na Naibu Waziri kwa kweli, wanafanya kazi nzuri sana. Ni watu wasikivu, wanafikika muda wote na wanatusaidia sana. Ninampongeza sana Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu, bahati nzuri Katibu Mkuu alishakuwa RAC pale Mkoa wa Kilimanjaro, kila ninapomgusia jambo, Dkt. Shekalaghe, anakuwa analijua kichwani kwake na kwa kweli, wamekuwa msaada mkubwa sana pamoja na watendaji wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaenda moja kwa moja kwenye Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCMC. Nimesema hapo awali kwamba, kazi nzuri kubwa sana imefanyika pale na haya ambayo ninakwenda kusema ni ya kuboresha tu; kabla sijayasema nampongeza Profesa Gileard Masenga, ambaye ni Mkurugenzi wa hospitali pamoja na timu yake yote. Kwa kweli, wanafanya kazi nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili moja ni ombi; lile eneo la uzazi pamoja na chanjo kwa watoto ni finyu sana na ile sehemu ya kusubiria haina paa, sasa unajua mimi bado ni mzazi, ambaye nina watoto wadogo. Kutokana na Sera ile ya Serikali ya kwamba, mwanaume akienda kwenye kupeleka mtoto chanjo hapangi foleni, basi ninaenda pale. Sasa nikienda nimekuwa nikipata hizo changamoto, wananiambia lile eneo liboreshwe, liongezwe ukubwa na kupauliwa, hasa lile eneo la kusubiria, ile sehemu wanayosubiria wale akinamama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo ambalo tumeliombea muda mrefu, najua Waziri analijua, Naibu Waziri, najua hata Wizarani limekwenda kupitia kwa Katibu Mkuu, wote wanalijua. Ni suala la wage bill; ninajua siyo suala rahisi kwa sababu, bado kuna hospitali nyingine za kanda nazo zinahitaji, lakini ninaomba waiangalie changamoto ya KCMC, Moshi Mjini na Mkoa wa Kilimanjaro kipekee, kwa sababu ya ukaribu wake na Arusha. Arusha population ni kubwa na purchasing power ni kubwa kwa sababu, uchumi wake ni mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hawa madaktari wetu bingwa pale KCMC hawatulii, maana baada ya muda wa kazi wanawahi Arusha kufanya tena kliniki nyingine, ili waweze kupata fedha za ziada. Sasa hiki kitu kwa kweli, kinafanya ubora wa kazi pale unapata changamoto, hebu waiangalie kiupekee, zipo nyingine ninajua, lazima tuanze Kibong’oto, twende Kanda nyingine, Mbeya, wapi!
Mheshimiwa Spika, lakini sisi ukaribu wetu na Arusha unatuletea shida. Hebu watuangalie kwa jicho la kipekee tuweze kuboresha yale mazingira, vinginevyo tunasubiri tu kwa hamu uzinduzi wa lile banka na matibabu ya cancer kwa mionzi pale KCMC, tunawasubiri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Mawenzi, ambayo iko Moshi Mjini. Kwa kweli na yenyewe imewekezwa sana, tunayo changamoto kidogo ya man power, hebu tuangalieni, vifaa vimewekwa, kumekuwa na maboresho mazuri, manpower kidogo ni tatizo. Ninampongeza sana Mkurugenzi pale, Dkt. Edna Joy Munisi, anafanya kazi kubwa sana, anafikika, anajaribu kupambana, lakini bila manpower sasa liko kwenu, naomba muangalie namna ya kumsaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni kuendelea kurekebisha ile master plan. Ile hospitali ni ya Mwaka 1922, yale majengo pale ni ya zamani, tunaendelea, kuna master plan ambayo walishaichora, wanajenga majengo ya ghorofa pale, ili tuendelee kuboresha ile huduma. Sasa ni lazima Wizara walete hela kuendana na ile plan ilivyo, vinginevyo vile vijengo vya zamani tukiendelea kuvikarabati tutachukua muda mrefu. Kwa hiyo, ninaomba sana tulizingatie hilo kwenye Hospitali yetu ya Mawenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaenda kwenye Bima ya Afya kwa Wote. Ninajua kuna watu wameongelea vifurushi kwa ujumla wake na mimi siko mbali na yale wanayosema. Ninampongeza sana Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Irene Kisaka, anajitahidi kwa kweli, kwenda na kasi inayotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo ya harakaharaka, moja ni TEHAMA. Ukienda KCMC, Idara ya Macho, kabla hujapata huduma kule unaambiwa urudi mile kadhaa tena, ili kadi iangaliwe halafu sijui wa-verify, paper work nyingi jamani! Hatuko kwenye karne hiyo tena! Ni vizuri wa-integrate mifumo yao idara zote za hospitali hiyo, ukifika kwenye idara husika hulazimiki tena kutoka. Inabidi sasa kila mgonjwa akienda awe na mtu wa kumpa kampani, kwa ajili ya kwenda kupeleka hizo hela kwenye bima ku-verify, kurudi huku na nini! Hebu waangalie namna ya kuboresha matumizi ya TEHAMA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kwenye vifurushi. Sasa kwenye vifurushi mimi niko tofauti kidogo na yale yaliyosemwa na wenzangu, siyapingi, nafikiri ni hisia za jumla na zinatakiwa ziangaliwe. Kuna mahali ninaona kuna shida kidogo, hapa kwenye watu wazima wa miaka ya 60 kwenda juu, kifurushi cha mtu mmoja na cha mwanandoa hakuna tofauti! Sasa sijui tuna encourage watu wakifika miaka 60 waachane au iweje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa tu mfano, kifurushi cha Serengeti kwa mtu mmoja wa miaka 60 and above ni shilingi 3,336,000 lakini wanandoa ni shilingi milioni 6,338,000; yaani kuna discount ya shilingi 300,000 tu, sasa sioni kama kuna pointi hapo na ni vizuri wajue haya. Kuna wakati kada fulani za Watumishi wa Umma kwenye mikoa fulani, sitaitaja, hasa walimu walikuwa wanaolewa; pamoja na mambo mengine na uzuri na nini, ni kama lile la afya. Mtu anajua nikiolewa au nikioa Mwalimu, pamoja na mambo mengine, mambo yetu ya afya yatakuwa yamekaa vizuri kwa sababu ya kile kifurushi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hiki cha wanandoa wastaafu, miaka 60 kwa mfano, hiki cha Serengeti, Tanzanite, mwanandoa mmoja 60 years and above ni shilingi milioni 6,708,000 wakiwa wawili ni shilingi milioni 13,400,000 hakuna discount yoyote! Sasa sijajua kina maana gani, kama siyo ku-discourage ndoa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, basi watuambie ni vizuri discount ya wawili ionekane kubwa, ili ku-encourage watu waweze kuingia kwa wingi zaidi, lakini hapa hamna tofauti kati ya kuingia mmoja na kuingia wanandoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaenda kwa MSD. Ninampongeza sana Tukai Mavere, kaka yangu, kwa kweli, anafanya kazi nzuri. Zipo changamoto, ninakumbuka kwenye hotuba zilizopita tulishafikiria kuifanya MSD ifanye kazi kibiashara hasa kwa kuangalia maeneo ya SADC na ninadhani mpaka mkataba ulishasainiwa. Sasa haya matatizo tunayayaona hapa ya bajeti, ingekuwa imewezeshwa kufanya kazi kule SADC, faida inayopatikana kule, ingetupunguzia mzigo huku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa lile suala la ku-supply kwenye nchi za SADC, na ni lazima niseme ninampongeza sana Mheshimiwa Rais, na wao wenyewe hapa asubuhi wamesema, wamekuwepo Watanzania wengi ambao wameweza kufanya kazi kwenye kada za afya Kimataifa maana kidiplomasia tuko vizuri, tulimalizie. Tumalizie hiyo effort ya kufanya biashara kule SADC, ili ikipata faida huko, basi huku nyumbani tuendelee kupata unafuu, lakini zaidi nisisitize kuangalia namna ya kulipa lile deni lake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaenda Ocean Road. Napo kwa kweli, ni eneo tegemeo ninaipongeza sana Serikali. Ninamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutuletea kile kipimo cha PET Scan na kwa kweli, Dkt. Diwani Msemo anafanya kazi nzuri pale, ninampongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ninaloenda kusema nimeshamfikishia Dkt. Molel in personal, kile kipimo cha PET scan ambacho ni cha bei kubwa sana. Serikali imewekeza, kimesaidia na kimepunguza hata referral kwa zaidi ya 67%. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna nyongeza kidogo kwa baadhi ya magonjwa. Kwa mfano Hodgkin lymphoma hauwezi kupima pale kwa sababu, kuna nyongeza kidogo inatakiwa u-upgrade. Hebu, tafadhali, kwa sasa Hodgkin nayo imekuwa ni tishio, watu wengi sana wanaumwa ugonjwa huo. Hebu tuangalie namna ya kuboresha tuweze kupima mpaka cancer pale, ili tuweze kuhudumia wananchi wengi zaidi na ku-save fedha za kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ni la ujumla, la manpower, ninaipongeza sana Serikali. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais, ninakupongeza Waziri pamoja na timu yenu yote, wamepunguza lile gap kutoka 64% ya uhitaji mpaka 55%, ni kazi nzuri sana. Sasa ninawaomba tuendelee kuongeza nguvu. Kwa mfano, sisi kwenye Kamati yetu ya LAAC tuliwahi kutoa ushauri kwamba, baadhi ya mapungufu yanaonekana, kwa mfano, kwenye Serikali kwa ujumla linaloleta shida kwenye wage bill.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakwenda kumalizia, watu ambao wanapandishwa cheo. Kwa mfano, Mkurugenzi wa Halmashauri alikuwa ni mwalimu, anapandishwa anakuwa Mkurugenzi; anapoondolewa kwenye ile nafasi, tena kwa sababu ya uzembe, ule mshahara unabaki pale, amezuia wage bill za watu wengine hapo chini, wengi sana. Tuangalie namna, akipandishwa, akishushwa, basi ashuke kwenye ule mshahara ule wa chini kwa sababu, hapa tunataka tuangalie kazi iweze kuwahudumia Watanzania wengi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)