Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hanang'
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Bajeti ya Wizara yetu ya Afya. Awali ya yote kwanza, nitoe shukrani za Wanahanang kwa Mheshimiwa Waziri wa Afya kwani wakati tunapata changamoto ya maporomoko ya mlima yeye ndio alikuwa Ofisi ya Waziri Mkuu na tulikuwa naye. Ninafikiri zaidi ya siku karibu 40, tumekesha naye na tumepambana wote. Mheshimiwa Waziri, Wanahanang wanasema ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe wenzangu wa Wizara ya Afya ambao tumefanya nao kazi zaidi ya miaka 12 kwamba ni mtu sahihi na mchapakazi; wampokee na pia wamuunge mkono. Nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri Dkt. Mollel, tunashirikiana mambo mbalimbali ambayo nimemletea ya Wanahanang amekuwa akiyashughulikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Katibu Mkuu Dkt. Shekalaghe, siku ambayo tuko tunapambana na maporomoko ya Hanang, yeye ndiye alikuwa anaratibu hilo zoezi la wananchi kwa sababu wakati ule alikuwa upande wa masuala ya jamii. Kwa hiyo, alifanya kazi nzuri sana na niseme tu ahsanteni sana kwa Wizara ya Afya kwa kazi kubwa ambayo wametufanyia sisi watu wa Hanang. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza mchango wangu kwa maana ya suala ambalo tunalo hapa mezani; Mheshimiwa Waziri tumekuwa na utaratibu wa kujenga kituo cha afya kila kata, baadaye tukasema tuanze na vituo vya afya ambavyo vipo kwenye maeneo ambayo yana watu wengi hasa makao makuu ya tarafa. Pia, tuna maeneo ambayo tayari yana zahanati na yana watu wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu tu kwenye eneo hili badala ya kufikiria kutafuta milioni 500 yote iliyokamilika, tuangalie namna ya kuboresha zahanati ambazo ziko kwenye makao makuu ya kata, tuboreshe hasa eneo la huduma ya mama na mtoto ili tuweze kuboresha huduma za afya za msingi kwenye ngazi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo langu la Hanang kwa mfano, ukienda pale Dirma tuna zahanati; tuboreshe angalau tuweke huduma ya afya ya mama na mtoto pamoja na maeneo ya Ishponga, Laghanga, Getanuwas na Lalaji yenye mahitaji yanayofanana ili wakati tunaelekea kila kata kuwa na kituo cha afya tuwe tumeanza na zile huduma za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ninataka kuongelea ni suala la mapambano dhidi ya malaria. Nipongeze juhudi kubwa ambayo imefanyika kwamba, tumepeleka dawa za mseto 4,567,020 na tumepeleka dawa zile za chupa zaidi ya karibu 900,000 hivi. Tumepeleka vile vipimo vya MRDT zaidi ya 10,000,000 na upatikanaji wake ni zaidi ya 95%. Niwapongeze sana kwa mafanikio hayo kwa sababu inawezesha watu wetu ambao wameugua wanapata matibabu kwa wakati na matibabu ya uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwenye eneo hilo ninaomba tujielekeze kwenye uelekeo wa kuangamiza vile vijidudu vinavyosababisha malaria. Twende sambamba; nilipata bahati ya kutembelea kile kiwanda chetu pale Kibaha; changamoto wanayolalamika ni kupata masoko. Tujielekeze kwenye hatua ya kuhakikisha kwamba, mbu wote wanaoambukiza malaria wanaangamizwa ili tusihangaike na dawa, tusihangaike na vipimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, nilipata bahati ya kuhudumu Kamati iliyokuwa ya Huduma na Maendeleo ya Jamii karibu miaka miwili na nusu hivi na mara zote nimekuwa nikisemea Hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara. Yamefanyika mambo mengi, hospitali ile kwa sasa ukiitazama pale ninafikiri imeboreka sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wameanzisha huduma ya dialysis karibuni na imeanza kufanya kazi Mkuu wa Mkoa amezindua. Wametuletea vifaa vya kisasa, wametupa digital x-ray ya kisasa. Vipimo vya kuangalia mfumo wa chakula wametuletea. Pia, suala la sickle cell na kuchambua mazao ya damu yamefanyika mengi. Kwenye eneo lile bado tunayo changamoto ya jengo la emergency. Tuna changamoto ya jengo la ICU, jengo la radiology kwa maana ya mionzi na wodi bado hazijajengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Mkoa wa Manyara ina changamoto ya eneo. Mji wa Babati unakua kwa kasi sana, tukichelewa kutafuta eneo la ziada baada ya muda itakuwa ngumu kupata eneo. Ninaomba lile eneo lipanuliwe ili mahitaji ya baadaye ya ile hospitali yaweze kukidhiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti ya 2024/2025 tumetengewa shilingi bilioni mbili, lakini mpaka sasa hata senti moja haijaenda. Ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri iangalie ile hospitali kwa sababu ndio inayotegemewa. Ina huduma nzuri, kwa sasa Wanamanyara wameanza kuamini kama ndio hospitali ya rufaa na watu wote ambao wananiuliza mimi ni sehemu gani ambako tunaweza kupata huduma fulani Fulani, mimi nina wa-refer pale na kwa kweli huduma ni nzuri sana; tuwaboreshee mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, madaktari wa mkoa, wale madaktari bingwa ambao Waziri ametuletea wamezunguka wilaya zote za Mkoa wa Manyara. Wametoa huduma kwa Wanamanyara na Wanamanyara wamefurahia ile huduma; ile huduma iendelee. Ninachoomba tu ni kwamba, haya mapungufu ambayo nimeyasema Mheshimiwa Waziri utusaidie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni eneo la vifaa na vifaatiba. Kila mtu amekuwa akiongea kwamba huduma za afya ni ghali. Tumepeleka vifaa kwenye ngazi ya wilaya, mikoa, hospitali zetu za rufaa na hospitali za kanda. Ombi langu kwenye eneo hili tunao wataalam wetu wa vifaa na vifaatiba, tuendelee kuwajengea uwezo na tuwape elimu ya kutosha. Waziri amekuwa akishirikiana nao ninazo taarifa kwa sababu ni wenzangu nimefanya nao kazi. Aendelea kushirikiana nao, awape elimu ya kutosha. Changamoto zinazokuja hapa nchini ni teknolojia mpya; waendelee kufundishwa wawe wabobevu zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu akipiga x-ray Katesh hiyo iaminike mpaka Hospitali ya Rufaa Muhimbili ili kusiwe na gharama za kujirudia. Nimepiga x-ray Katesh, nikienda Muhimbili iwe ni hiyo hiyo kusiwe na gharama za kujirudia. Watanzania tulionao ni watu maskini, hivyo fedha zinazotumika zitumike kwa umakini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuhakikishe kwamba hili linafanyika, boresha eneo la Telemedicine (waboreshe wataalam). Mtu yeyote ambaye amepiga labda Bunda x-ray akifika Muhimbili aweze kuaminika. Akipiga x-ray Singida iaminike kokote nchini na hizi taarifa ziende kusiwe na gharama za kujirudia. Tukiboresha kwenye eneo hili tutapunguza gharama za matibabu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ninataka kuongea kwenye hilo hilo la vifaa tiba; tunayo Taasisi yetu ya Mamlaka ya Dawa, Vifaa Tiba na Vitendanishi (TMDA). Kwa sababu vifaa tunavyoviagiza hapa nchini 90% mpaka 95% vinatoka nje. Dawa tunazoagiza hapa nchini sehemu kubwa inatoka nje na vitendanishi vivyo hivyo. Hawa tuendelee kuwajengea uwezo waendelee kufanya ukaguzi wa viwanda wa vifaa na vitendanishi vinavyokuja hapa nchini ili tuwe na uhakika na ubora wake, usalama wake na ufanisi wake kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa sababu sehemu kubwa; nimemsikia mwenzangu akichangia suala la kuangalia kuhakikisha kwamba tunakuwa na namna ya kuhakikisha dawa tunazozitumia zinasimamiwa vizuri. Hata hivyo, tukisimamia eneo la uchunguzi vizuri ambako tunategemea vifaa na vitendanishi, yawezekana tukapunguza matumizi ya dawa kwa sehemu kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ambayo ninataka niisemee ni suala la bima ya afya kwa wote. Wakati nikiwa kwenye Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ambayo baadaye imegawanyika ikapata Kamati tatu, hili eneo tulilijadili kwa kina na Watanzania sehemu kubwa ndio tumaini lao. Mheshimiwa Waziri tunachoomba aiharakishe ili hatimaye kila Mtanzania aweze kuwa na bima ya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ngumu sana kwa mazingira tuliyonayo mtu kuwa na fedha mfukoni muda wote utakapoumwa ujitibu. Bima iwe ndiyo daktari, bima iwe ndiyo njia ya kujichunguza kwa maana ya ukitakiwa x-ray ndiyo bima yako inakusaidia; ukitakiwa MRI bima ndiyo inakusaidia; na CT-Scan pia bima ndiyo iwe inakusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipata changamoto ya kansa unaenda kwenye PET-Scan, bima ndio iwe inaweza kumsaidia Mtanzania ambaye ni maskini. Kwa mazingira tuliyonayo tunapoteza Watanzania wengi kwa sababu ya kushindwa kulipia matibabu. Ninachomwomba Mheshimiwa Waziri hii aharakishe. Akiifanya, yeyote yule hapa ataniambia Mheshimiwa Mbunge ambaye amefanya ziara kwake jambo la kwanza ambalo ataulizwa ni matibabu kwa wazee; eneo hilo lina changamoto kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa na bima ya afya kila Mtanzania akiwa yuko covered, itatusaidia kuwapunguzia Watanzania gharama. Ninaamini baada ya Watanzania kuwa na uhakika wa matibabu na wakapata matibabu kwa wakati, uchumi wa kila mmoja utaboreka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninakushukuru sana ninaunga mkono hoja. (Makofi)