Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Afya. Kwanza, ninaomba nimtangulize Mwenyezi Mungu katika mchango wangu. Moja kwa moja nianze pongezi kwa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri sana ambayo ameifanya katika Wizara hii ya Afya, pia kwa tuzo nyingi sana ambazo amezipata ikiwemo tuzo ya kupunguza vifo vya akinamama na watoto nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Watanzania wote waliompongeza Profesa Janabi kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika, kwa kweli ametuheshimisha Watanzania kwa mara nyingine tena, hongera sana. Pia, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Afya Mheshimiwa Jenista Mhagama, ambaye kwa kweli amekuwa Waziri wa muda mrefu, amefanya kazi kwenye Wizara nyingi na tunamshukuru tena anaendelea kupambana kwenye hii Wizara kuhakikisha kwamba tunaendelea pia pamoja na kupunguza vifo vya akinamama na watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Naibu Waziri Mheshimiwa Dkt. Mollel ambaye kwanza majibu ya kila siku hapa Bungeni, amekuwa akitujibu pia amekuwa na utayari wakati wote tukimpigia simu hata akiwa nyumbani. Tunakumbuka kuna mtoto mmoja wa Kilolo aliumwa na nyuki alilazwa pale Muhimbili alikuwa hatarini kufa kwa sababu ya kusafishwa damu. Tulipompigia Dkt. Mollel hatutamsahau, alipiga simu saa hiyo hiyo wakaenda kumsafisha damu na huyo mtoto nitamleta Bungeni kwa sababu alitaka kufa. Tunamshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumshukuru pia Katibu Mkuu wa Wizara hii ya Afya, Naibu Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara hii ya Afya kwa kazi nzuri ambayo imesababisha hata Serikali ya Awamu ya Sita kufanya vizuri sana. Nitakuwa sijatenda haki kama nisipompongeza Daktari wetu wa Mkoa, Dkt. Mwakalebela. Kwa kweli huyu Daktari amekuwa akitusaidia sana wananchi wa Iringa, ni Daktari ambaye amekuwa akitusikiliza na akitusaidia sana katika mkoa wetu, tunamshukuru. Tunatamani hata miaka irudi nyuma asiweze kustaafu ili aendelee kuhudumia katika mkoa wetu na pengine hata akistaafu basi endeleeni kumpa mikataba kwa sababu uwezo anao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na Serikali yetu, lakini ziko baadhi ya changamoto ambazo na mimi ningetamani niziseme. Katika Mkoa wetu wa Iringa kwanza, kuna ufinyu mkubwa sana wa eneo kwenye Hospitali ile ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa. Hii inatokana na mwingiliano ambao kila siku wanauzungumzia kati ya Gereza la Mkoa na Hospitali yetu ya Rufaa. Kwa hiyo, tunaona majengo mengi hayajengwi kwa sababu ya ule mwingiliano; eneo ni finyu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukikuta wafungwa wanatoka na ambulance zinakuja unaweza ukajisikia vibaya sana. Ninashukuru nilipoongelea kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani niliwaomba kwamba, gereza lile sasa lihame na ninashukuru pia niliongea siku ile na Mkuu wa Magereza akanihakikishia kwamba sasa hivi watapata bajeti na gereza litahama. Tunaomba kwa kweli kazi hiyo ifanyike ili majengo mengi yajengwe ikiwa ni pamoja na nyumba za madaktari wetu wakae jirani na hospitali waweze kusaidia wagonjwa waliopo katika Mkoa wetu wa Iringa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine pale Iringa tuna ukosefu wa jengo la kisasa la mama na mtoto. Hii ni kutokana na ongezeko kubwa sana la mama wanaojifungua na kwa kweli Iringa tunajitahidi tunajifungua sana. Kwa hiyo, tunaomba wodi ile watuletee pesa ili tuweze kuongeza kwa sababu halitoshi kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia kuhusu gharama za huduma za kusafisha figo (dialysis). Kwa kweli wananchi wengi, uwezo wao ni mdogo sana kiasi kwamba, watu wengine wanashindwa kwenda kufanya hiyo huduma kwa sababu hawana uwezo wa pesa na hawana bima ya afya. Kwa hiyo, inakuwa ni shida mno, wananchi wengi wanapoteza maisha na wananchi wengi hawajui wafanye nini wanaotoka vijijini na wengine hawajui wafanyeje. Kwa hiyo niombe hebu iangaliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hospitali inashindwa kujiendesha kwa sababu wananchi wanashindwa kwenda kupata hiyo huduma. Kwa hiyo pesa inakuwa haipo ya kujiendesha kwenye hiyo huduma. Ninaomba Serikali iangalie upya huduma za usafishaji wa figo ikiwepo Mkoa wetu wa Iringa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu upungufu wa watumishi katika Wizara ya Afya katika Mkoa wetu wa Iringa ambao ni karibu 50%. Kwa hiyo, niombe waangalie kwa sababu ni muhimu sana kupata hao watumishi kwenye Sekta ya Afya na hasa madaktari kwenye vituo vya afya na zahanati wawepo ili waweze kusaidia huduma katika hospitali zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoa mfano; kwa kweli tunashukuru kwani kwenye Hospitali ya Rufaa kuna ambulance sita, kuna magari manne, lakini kuna dereva mmoja tu ambaye ameajiriwa. Kwa hiyo hii inasababisha hata saa nyingine kukimbiza mgonjwa kuleta huku Benjamini Mkapa inakuwa shida. Niombe hata madereva pale wapatikane wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu majengo yaliyojengwa na wadau. Katika Mkoa wetu wa Iringa sisi kwanza, tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu. Tunaye mdau ambaye ni Mkurugenzi wa ASAS ambaye ni m-NEC na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais juzi alimteua kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu na Wajumbe wa Halmashauri Kuu wakamchagua kwa kura nyingi. Kwa kweli hii tunampongeza amekuwa akifanya kazi kubwa sana katika Serikali hii na katika Mkoa wetu wa Iringa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikikupa tu mfano maana yake watu wasije wakafikiri labda ninasemaje; amejenga jengo la benki ya damu salama ya mkoa; amejenga jengo la watoto wachanga; ametujengea jengo maalum la wagonjwa mahututi (ICU); amejenga jengo la viungo bandia na vifaa saidizi; ametujengea jengo la wagonjwa maalum. Majengo haya yote ni mazuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru pia Mheshimiwa Waziri mara nyingi tumekuwa tukiongea na yeye kuhusiana na hili jambo. Ningeomba hebu kitu kifanyike pale Iringa ili tuendelee na wadau wengine wajitokeze kwamba wanapoisaida Serikali mambo makubwa kama haya kuponyesha maisha ya watu basi angalau tuzo maalum na itambulike ili wengine waendelee kusaidia katika Wizara hii ya Afya ambayo ni muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tunaomba madaktari wa magonjwa ya physiotherapy hasa kwa wazee, watoto na watu wenye ulemavu. Kwa kweli hili ni jambo ambalo linahitajika. Unaona tuna jengo zuri sana, lakini naona vifaa pamoja na wataalam wanakuwa wanakosekana na sasa hivi watu wengi wanaugua ugonjwa wa kupooza, lakini wanaona kwamba wakienda hospitali wanakuwa hawawezi kufanyiwa mazoezi. Kwa hiyo, inawachukua muda mrefu sana wa kupona BP. Vilevile tuna watoto wamezaliwa na ulemavu, tukipata wataalam wakawasaidia inasaidia pengine wengine wanakuwa wananyooshwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa na mimi nizungumzie vifurushi vya bima ya afya, hebu viangaliwe upya. Mbunge aliyepita amezungumza sana. Kuna vifurushi vingine unakuta kweli umenunua, lakini hupati vile vipimo, hupati zile dawa, inabidi viangaliwe sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)