Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia. Kwanza kabisa ninapenda nimpongeze Waziri wa afya Mheshimiwa Jenista Mhagama kwa kazi nzuri sana anayofanya katika Wizara hii. Kwa kweli sishangai kwa sababu kwenye Wizara zote alikopelekwa amefanya vizuri sana, kwa kweli yeye ni jembe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri Dkt. Mollel, yeye akiwa kama daktari ana mchango mkubwa katika mambo mazuri ambayo tunaona kwamba na mafanikio yametokea katika Wizara hii hongera sana. Ninampongeza Katibu Mkuu, Mganga Mkuu wa Serikali, Wakurugenzi wa taasisi mbalimbali ndani ya Wizara hii na watendaji wote kwa mafanikio mkubwa sana katika hii sekta ya afya. Hongera sana kwa Mheshimiwa Mohamed Yakub Janabi kwa ushindi na vilevile kwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika kwa kweli ametuheshimisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake na mapinduzi makubwa ndani ya sekta ya afya, kwa hiyo tunasema mama ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mjumbe wa Kamati ya Afya, tumesikia kilio kikubwa cha Bohari Kuu ya Dawa MSD unajua kwamba ina majukumu makubwa ya uzalishaji, ununuzi, utunzaji, na usambazaji wa vifaa tiba ikiwemo madawa. Hata hivyo, hawa wamepungukiwa mtaji na kila mwaka wamekuwa wakiomba lakini mwaka juzi 2023/2024 wakapewa bilioni moja na mkaona mambo makubwa ambayo walianza kufanya, nina uhakika kwamba wakiongezewa mtaji watafanya vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kukosekana kwa mtaji sasa kunafanya hii bohari kuu ifanye kazi kama si kama bohari kuu ni kama duka la kawaida la dawa. Sasa hivi mnaona tendency ya wafadhili wanaanza kujitoa, Tanzania 90% ya afua za UKIMWI na TB zilikuwa zilikuwa zinafadhiliwa na Mfuko wa Rais wa Marekani na wanaona jamaa Mheshimiwa anaanza kujitoa kama anavyojitoa sasa itakuwaje kama sisi hatutakuwa tumeiwezesha taasisi yetu ya MSD ikawa na madawa ya kila wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama mwanakamati tunaleta ombi kwa Serikali kwamba kwa kuwa wanadaiwa na MSD bilioni 434.2, tunaomba hizo zikalipwe. Lakini vilevile hii MSD ipewe mtaji wa kutosha kusudi hata hawa wafadhili wakija kujitoa hawa wagonjwa wetu karibu milioni1.5 ambao ni wagonjwa wa UKIMWI wanaendelea kutumia ARVs na wagonjwa wa TB wanaopata matibabu ya muda mrefu tuwahakikishie kwamba madawa yatakuwepo wakati wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuna Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa maana ya NHIF na yenyewe inaidai Serikali bilioni 210.29. Ni ukweli usiopingika kwamba Serikali imeboresha huduma za afya, tumejenga zahanati kila kona, kuna vituo vya afya, hospitali za wilaya, hospitali za mkoa, hospitali za Taifa, hospitali za kanda zote zimeboreshwa ili kusudi Watanzania waweze kupata huduma iliyo bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona vifaa tiba vimenunuliwa ma-CT-scan na digital x-rays, pet-scan, dialysis machines karibu kila mkoa MRI na kadhalika, lakini matibabu bado ni ghali ndiyo maana Serikali mkaja na Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ili kusudi Mtanzania asife kwa kukosa matibabu kila Mtanzania aweze kutibiwa kwa kupitia bima ya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili bima ya afya iwezekane, inabidi Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya uwe na ukwasi ambao unatosha. Hivyo, tunaiomba Serikali ilipe deni hilo la Bima ya Afya shilingi bilioni 210 ili kusudi tuweze kuongeza ukwasi katika hii mifuko; itaongeza uhimilivu na uhai wa Mifuko na hivyo waweze kutoa huduma zilizo bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania sekta ya afya imeendelea sana kwa sababu sasa hivi tunapandikiza uroto, tunapandikiza figo na tunaelekea kwenda kupandikiza ini na moyo, Serikali tunaomba haraka sana ilete sheria ya kuwawezesha hawa wataalam wetu waweze kupandikiza hivyo viungo pamoja na chembechembe hai kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kagera umepakana na nchi nyingi ikiwepo Uganda, Kenya, Burundi, Rwanda na kadhalika, kwa sababu ya mwingiliano mipakani unakuta kwamba magonjwa ya mlipuko na hasa yakiwa kwenye nchi hizo jirani kama Marburg, Mpox, Ebola na kadhalika yanaweza yakaingia Tanzania kwa kupitia mipaka ambayo iko katika Mkoa wa Kagera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka mingi Wabunge wa Mkoa wa Kagera tumekuwa tukiomba tujengewe isolation centres, lakini vilevile tujengewe na hospitali kubwa ya kuweza kutibu haya magonjwa ya mlipuko. Kwa niaba ya wananchi wa Kagera tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mama Samia Suluhu Hassan kwa kutujengea isolation centre pale Mutukura, ambao ni mpaka uliopo kati ya Uganda na Tanzania kule Misenyi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaomba isolation centres nyingine ziendelee kujengwa kwenye mipaka ambayo ni rasmi kwa mfano kwenye mpaka wa kati ya Tanzania na Uganda ulioko kule Kyerwa, mpaka uliopo kati ya Tanzania na Rwanda uliopo pale Rusumo - Ngara na mpaka uliopo kati ya Tanzania na Burundi uliopo kule Kabanga tujengewe isolation centres ili kusudi wale wasafiri wakifika pale mpakani wakihisiwa kwamba wana haya magonjwa ya mlipuko waweze kutengwa kwenye hizo isolation centres kabla hawajaja Tanzania kuchanganyikana na Watanzania na kuambukiza hayo magonjwa.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tumekuona Mheshimiwa Waziri wa Afya, Mheshimiwa Jenista Mhagama ukiwa unatia saini mkataba wa kutujengea hospitali kubwa ya kisasa ya magonjwa yasiyoambukiza Mkoani Kagera, tunasema ahsante sana Mheshimiwa Waziri na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutujali wananchi wa Kagera. Sisi tunachoweza kumuahidi ni kwamba itakapofika mwezi Oktoba tunaenda kumlipa, tutampigia kura nyingi, kura za kishindo, kura za ushindi ili kusudi ashinde aendelee kuwa Rais na aendelee kutuletea maendeleo katika Mkoa wetu wa Kagera. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Elibariki Immanuel Kingu ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Afya na Masuala ya UKIMWI, kwa kweli umetuongoza vizuri sana. Ninawashukuru na ninawapongeza na Wajumbe wote wa Kamati, Sekretarieti yetu kwa kutuongoza vizuri pamoja na ushirikiano tuliokuwa nao ambao ndiyo mambo yaliyotuwezesha kuyafanikisha yale yote ambayo tumeyafanikisha kama Kamati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ninaunga mkono hoja. (Makofi)