Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Jacquline Andrew Kainja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. Nami nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu na nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri wa Afya mama yangu Jenista Mhagama pamoja na Naibu Waziri wake, lakini vilevile watendaji wote wa Wizara ya Afya wakiongozwa na Katibu wetu Mkuu wa Wizara ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anazofanya hususani sisi wananchi wa Mkoa wa Tabora tunampongeza na tunamshukuru kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kupitia sekta hii ya afya kwa maana ya kwamba Mkoa wetu wa Tabora tumepokea bilioni 33.2 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali tano za wilaya katika wilaya saba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ukarabati wa hospitali kongwe mbili za wilaya ikiwemo Hospitali ya Urambo pamoja na ya Igunga. Vilevile tumekuwa na vituo vipya vya kutolea huduma za afya, vituo vya afya na zahanati kwa maana kwamba 2021, 2023, 2024 kutoka vituo 348 mpaka vituo 428 kwa kweli sisi wananchi wa Mkoa wa Tabora tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa jitihada hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea pia pesa za bajeti ya ruzuku za dawa na vifaa tiba kutoka bilioni nne kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 hadi 2023/2024 bilioni 9.8. Hayo kwetu ni maendeleo makubwa na hii inatusaidia sisi wananchi wa Mkoa wa Tabora kupata hali nzuri ya upatikanaji wa dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tumepata huduma nyingi ambazo sitaweza kusema zote, tuna CT-scan tulitumia bilioni 1.8, inaweza kuwasaidia wananchi wetu wa Mkoa wa Tabora, lakini tumeweza kupokea ambulance 23 katika Mkoa wetu wa Tabora, hayo sisi ni mafanikio makubwa na tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais na tunamwambia aendelee kuchapa kazi mitano tena tutamhakikishia na atashinda kwa kishindo kwa kura za kutosha kutoka Mkoa wa Tabora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mazuri yote hayo ambayo yanafanywa na Serikali yetu ya Awamu ya Sita, lakini vilevile niweze kujielekeza katika kushauri Serikali katika taarifa ya Kamati ambayo imesomwa na Mwenyekiti wa Kamati, nimeona ukurasa wa 16 imejielekeza kwa miaka miwili mfululizo nyuma Kamati imekuwa ikishauri Serikali kuweza kuisaidia mkopo MSD bilioni 561 ambazo zilikuwa zinahitajika ili wao waweze kujisimamia kwa ajili ya mtaji mkubwa wa kuendesha huduma zao na tumeipa MSD kazi kubwa ya uzalishaji, uhifadhi, usambazaji na ununuaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kuiwezesha MSD Mheshimiwa Waziri hapa tutakuwa bado hatujafanya kazi vizuri na tukategemea matokeo mazuri kutoka MSD.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kamati ikiwa inasisitiza Wizara na Serikali kutoa pesa hizo Wizara walikuwa wasikivu na Serikali ilikuwa sikivu ikatenga bilioni 100 kwa ajili ya kuisadia MSD. Kwa hapa kwa kweli niwapongeze sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue pia nafasi hii kupongeza taasisi hii ya MSD chini ya Mkurugenzi Mavere Tukai, pamoja na timu nzima ya MSD wao walifanikisha kupata milioni 162.4 kwa ajili ya kuendelea kupambana na changamoto mbalimbali zilizopo ndani ya MSD.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona vilevile namna ambavyo MSD hii ikiwezeshwa inaweza ikajisimamia. Ukurasa wa 17 taarifa ya kamati inaonyesha kwamba MSD inadai Serikali; mbali na kwamba MSD inahitaji mtaji, lakini vilevile tunaweza tukajikita kwenye kulipa madeni ambayo MSD inadai ya bilioni 434.2 hivyo tukiwapatia wanaweza wakajiendesha kwa sababu waliomba 561 ikatoka bilioni 100, lakini bado bilioni 300 basi Serikali tuangalie tulipe madeni ya MSD wanayodai yote ili tuweze kuona ikifanya kazi yake vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali iweze kuwekeza pesa kwa ajili ya kiwanda chetu kile cha TPI ili kiweze kufanya kazi na tuweze kuzalisha ARVs ili tuweze kuondokana na kutegemea wafadhili na kama tunavyoona sera za kinchi, sera za nchi za Marekani ambazo zinabadilika zisije zikatuingiza kwenye changamoto kubwa. Kama tuna uwezo huo ni vema basi tukajielekeza pia kuhakikisha kiwanda hiki kinaweza kusimama vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nihamie kwenye suala lingine kwa sababu ya muda. Suala hili niliwahi kuliongea mwaka jana 2024 wakati Waziri wa Afya akiwa ni Ummy Mwalimu na alilipokea na akasema atalifanyia kazi. Hata hivyo, leo hii ninaomba kwa sababu Waziri wetu wa Afya mama yetu Jenista Mhagama yuko hapa na mama yangu ni mfuatiliaji na ni msikivu ninamwomba kwa unyenyekevu mkubwa sana alibebe hili alipeleke Wizarani na wakakae walifanyie kazi. Suala hilo si lingine ni Kurugenzi ya Pharmacy.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaongelea Kurugenzi ya Pharmacy kwa maana katika utendaji wa muundo mzima wa Wizara yetu ya Afya na hasa kwenye hospitali zetu huwa kuna kurugenzi katika idara zote, lakini kuna baadhi ya idara hazijawekewa kurugenzi kwa maana ya wale wasimamizi kuingia kwenye vikao vya maamuzi kama Bodi au Menejimenti ya Hospitali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kabisa tuna Mfamasia Mkuu wa Serikali, ambaye yeye amekuwa Mkurugenzi Msaidizi lakini yule anaishia kule Wizarani huku chini kwenye watendaji na wananchi wote tunaishia kwenye hospitali kuhakikisha tunaenda kutibiwa bado kurugenzi hiyo haijafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa nini ninaomba kurugenzi ya pharmacy? Ni kwa sababu 50% ya bajeti za dawa zinaenda kwenye idara ya pharmacy na msimamizi mkuu ni Mfamasia, lakini Mfamasia huyu kwa Hospitali ya Muhimbili au hospitali zozote zile za kanda hana uwezo wa kuingia kwenye vikao vya bodi vya ndani, badala yake anawakilishwa na kurugenzi ya tiba chini ya daktari ambaye hana utaalam wa pharmacy. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaangalia 95% ya wagonjwa wanaoenda hospitali wanahitaji kutumia dawa na vifaa tiba na tukisema vifaa vya tiba vyote viko chini ya pharmacy msimamizi ni Mfamasia, lakini kwa nini inashindikana? Mfamasia huyu kuingia kwenye Bodi ya Hospitali au Menejimenti ya Hospitali ili kuweza kupeleka mawazo yake moja kwa moja ya idara ambayo idara hii ya pharmacy 40% ya mapato ya hospitali yanatoka katika idara ya pharmacy. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nini kinachoshindikana? Nimwombe Mheshimiwa Waziri, jambo hili dogo sana, hatutaweza kupata tija kubwa ya matokeo chanya kama asilimia kubwa tunategemea upande wa pharmacy lakini mfamasia huyu hapewi dhamana ya kuingia kwenye vikao vya maamuzi makuu ndani ya hospitali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimwombe, hizo kurugenzi ni Hospitali ya Muhimbili na Hospitali zote za Kanda na Benjamini zinatakiwa zitengenezwe Mfamasia Mkuu wa Serikali mmempa nafasi ya Mkurugenzi Msaidizi kwa ngazi ya Wizara je, huku ambako kuna watendaji hawa kada ya pharmacy tunawashirikishaje? Ikiwa kama tuna wafamasia wameweza kujiendeleza sana? Tunao wengi wa kutosha kwa nini tusiwatumie kupata mawazo yao moja kwa moja badala ya kuwakilishwa na daktari ambaye yeye pia hana taaluma ya pharmacy? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja na ahsante kwa nafasi. (Makofi)