Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Neema Gerald Mwandabila

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kupata nafasi jioni hii ili niweze kuchangia katika Wizara yetu hii muhimu kwa Watanzania, Wizara ya Afya. Awali ya yote pia niweze kutumia nafasi hii kuendelea kumpongeza Mheshimiwa Jenista na timu yake kwa kuendelea kufanya kazi nzuri. Tunajua kusimamia Wizara hii siyo kazi nyepesi kwa sababu ni Wizara sensitive yenye mahitaji muhimu kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee pia kumpongeza Mheshimiwa Rais, kazi iliyofanyika katika kuboresha utoaji wa huduma ni nzito. Tumeona hospitali zinaendelea kujengwa pale kwetu Mbeya tuna jengo kubwa la kisasa kabisa limejengwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Meta upande wa wazazi. Kwa hiyo, ukienda upande wa majengo mengine, huduma zingine ukiacha hii ya wazazi majengo pia yameongezeka mengi ya kisasa. Ninajua siyo kwa Mkoa wa Mbeya tu ambao unahudumia sisi watu wa Nyanda za Juu Kusini, lakini na maeneo ya kanda zingine pia yameendelea kufanyiwa uboreshaji mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo sina mengi ya kusema ila kuna vitu ambavyo vichache ninataka kufanya kama angalizo, nilikuwa ninasoma taarifa hii nilikuwa ninatafuta kuona ni wapi Wizara hii na TAMISEMI kuna connection. Sijaona eneo ambalo lina-clarify ni kwa namna gani Wizara ya Afya inaisimamia TAMISEMI kwenye utoaji wa huduma zake. Mfano, kule TAMISEMI tuna vituo vya afya ambavyo vimechakaa sana, lakini tuna zahanati ambazo zimechakaa sana sasa kama hakuna hawa watunga sera ambao ni wasimamizi wa mambo ya afya na kule watekelezaji nikaona kama hapajakaa sawa. Kwa hiyo, kupitia bajeti hii tulitakiwa tuone hata ni sehemu gani inaonesha ushirika wake na wapi na TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii pia kuendelea kumwomba Mheshimiwa Waziri aende akahakikishe vituo vya afya vyote chakavu zahanati na hata kama kuna hospitali nyingine ambazo ni za level za wilaya zina uchakavu uliokithiri, basi zikafanyiwe maboresho. Hili tunamwomba aende kulisimamia. Nina mfano wa vituo vya afya kwetu kule Songwe, mfano pale Mbozi kuna kituo kinaitwa Masangula ukikiona kabisa unaona kabisa hiki kituo kwa kweli majengo yake yamechakaa kitu ambacho tungependa kuona yanaboreshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitamani pia kuongelea kwenye kipengele cha magojwa ya mlipuko. Unapoongelea magonjwa ya mlipuko ni magonjwa ambayo kiukweli ni rahisi kuenea hata kwa watu wengine inakuwaje kituo cha isolation kinawekwa katikati ya mji? Mimi nina mfano mzuri pale Kata ya Makambini sisi kama wananchi tuliomba kituo cha afya, lakini ajabu na kweli tumewekewa isolation centre. Hivi ni nani ambaye aliwahi kumwomba baba yake mkate akapewa jiwe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, maombi ya Wanamakambini, Wanatunduma tuliomba kituo cha afya. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri atusaidie ile isolation walipoiweka pale si sehemu sahihi, watafute sehemu ya kuiweka ambapo kutakuwa hakuna watu wengi. Watupe kituo cha afya Makambini ndilo lilikuwa ombi letu. Kwa hiyo, katika hilo suala la connection ya Wizara hii na kule TAMISEMI watusaidie wakaondoe ile isolation watupe kituo cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najaribu kupitia ripoti sehemu ya ubora wa huduma. Kumekuwa na changamoto ya wananchi kutokuwa na imani na hospitali zetu na hii naiongea kwa moyo mkunjufu kabisa kwamba wananchi wale ukiwaambia nenda hospitali za Serikali unakuta wanabisha. Utashangaa kwa sisi watu wa Nyanda za Juu Kusini wanasema bora niende Ikonda au niende private hospital nyingine, lakini ukimwambia nenda kwenye hospitali za Serikali wanakataa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nimeiona kwa watu wanaokuwa wamepata ajali za mifupa, lakini hata tu kwa wale wagonjwa, unakuta anaumwa unamwambi nenda hospitali hizi za Serikali wanakuwa ni wabishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mfano hai, juzi nilikuwa na mgonjwa wangu wa karibu kabisa ambaye yeye alikuwa analalamika kizunguzungu na maumivu ya mifupa na nyama (muscles) amefika hospitali ambayo ni ya kuaminika siwezi kuitaja hapa kwa ajili ya heshima yake. Anaenda kupewa dawa za kutuliza maumivu na kuambiwa kwamba mifupa imekaza. Hivi mifupa inakaza bila sababu? Badala ya kwamba aende akapimwe ijulikane ni kwa nini hiyo mifupa imekaza, hakuna. Akaenda private sekta akapimwa anaonekana ana uric acid. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uric acid tu hospitali za rufaa zingine wanashindwa ku-identify. Kwa hiyo, hilo Mheshimiwa Waziri niseme tu kwamba ubora wa hospitali zetu tunaomba uwe unafuatiliwa kwa ukaribu. Wamesema wamefanya monitoring ya ubora wa huduma kwenye hospitali 28 ambapo waliangalia katika huduma za mama na mtoto, lakini wakaangalia kwenye kitengo cha dharura. Kwenye huduma ya mama na mtoto score ilikuwa ni 67%, lakini kwenye huduma ya kidharura score ilikuwa ni 64%. Sasa ninajiuliza hapo hii huduma haifanyiki mara kwa mara maana watalaam walioonyesha wamewasomesha ni wachache ina maana hii huduma haifanyiki mara kwa mara kufuatilia ubora wa huduma zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wanatuhakikishia vipi wananchi tuendelee kuwa na imani na hizi hospitali? Kama vitengo tu ambavyo hata havina shughuli nzito sana sana kama huduma ya mama na mtoto ina-score 67%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, kwenye magonjwa mengine magumu huduma zinaendaje? Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri kwamba tusaidie kitengo cha ubora wa huduma kiboreshwe, kiongezwe wataalam, watu wapatiwe training za kutosha ili waweze kusimamia hospitali zetu ili ninapokwenda kama ni hospitali ya mkoa ninapata huduma ileile, ya wilaya ninapata huduma ileile na kituo cha afya ninapata huduma ileile. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri hili aliangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye kipengele kimoja cha Hospitali ya Muhimbili. Hospitali ya muhimbili kwa kweli ni hospitali ambayo inafanya kazi kubwa sababu inapokea wagonjwa wengi wengi unakuta watumishi wa pale wako busy muda mwingi. Hata hivyo, kuna hiki kitengo ambacho kimeanzishwa kinaitwa kitengo cha IVF, kitengo cha upandikizaji wa mimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipata nafasi ya kuwasiliana na daktari mmoja wa eneo lile akaniambia kwamba ni kweli huduma imeanza na tunatoa na hapa inaonyesha wamehudumia wagonjwa nane, lakini wana changamoto zao. Huduma imeanza, lakini dawa na vitendea kazi ambavyo vinatumika kwa ajili ya utoaji wa huduma hizi haviko-registered MSD.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekanaje huduma ianze halafu hizo dawa na vitendea kazi wanasema lab media na hizo dawa zake mpaka waagize Ujerumani ndiyo wazipate halafu tena ndiyo zinatakiwa zisafirishwe kwa mnyororo baridi. Sasa unaweza uka-imagine mnyororo baridi kutoka Ujerumani hiyo dawa mpaka ije ifike huku ubora wake unakuja unafika ukiwa una ngapi, lakini gharama yake inaongezeka inakuwa kubwa zaidi. Ni wananchi wangapi wanaweza ku-afford hiyo dawa au hiyo huduma? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe, Madaktari walisema wanaomba dawa hizi yaani vifaa tiba na dawa zake ambazo zinatumika katika zoezi zima la upandikizaji wa mimba ziwe registered, MSD waweze kuziagiza wanunue ili wawe na urahisi wa kuzipata ili tuweze kuwasaidia wanawake wengi au wanaume wengi ambao hawana watoto. Tunajua kabisa kukosa mtoto ni mojawapo ya vitu vinavyoweza vikampelekea mtu kuwa na msongo wa mawazo. Kwa hiyo, hilo pia tunaomba wawasaidie wafanye kazi nzuri wahudumie watu wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niendelee kusisitiza kwamba Kituo chetu cha Afya cha Tunduma kinaendelea kuelemewa pamoja na kwamba wametujengea hospitali tunawashukuru inasaidia, lakini pamoja na kwamba wamejenga vituo vingine vya afya tunawashukuru, bado wananchi wengi wanaendelea kuamini Kituo cha Afya cha Tunduma kwa sababu huku bado wengine madaktari siyo wa kutosha na majengo bado hayajakamilika, yaani vifaa vya utoaji huduma na watalaam bado hawajapelekwa kwenye vituo vingine vya afya. Kwa hiyo, tunaomba Wizara waweze kutusaidia kwa sababu tunajua kuna vifaa vingine vinatoka direct kutoka kwao kwenda TAMISEMI. Kwa hiyo, waendelee kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuchangia hayo, niseme ninashukuru sana. (Makofi)