Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Eng. Mwanaisha Ng'anzi Ulenge

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi ya kuchangia. Awali ya yote nimshukuru Mungu mwenye enzi na utukufu kwa kuniwezesha kusimama mahali hapa muda na wakati kama huu. Pia, nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Mheshimiwa Naibu wake kwa kazi kubwa wanayofanya katika Wizara hii ya Afya, hakika mimi sina mashaka na uzoefu wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo imefanyika kwa kushirikiana na watendaji wote wa Wizara ya Afya katika Mkoa wetu wa Tanga, hakika wananchi wa Mkoa wa Tanga tumejawa na shukrani nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeletewa zaidi ya shilingi bilioni 158 kwa ajili ya miundombinu ya afya pamoja na vifaatiba. Tumeweza kujenga zahanati 72, lakini na kuweza kukarabati hospitali za wilaya sita pamoja na hospitali nyingine tatu. Vilevile, tumeweza kutengenezewa vituo vya afya 23 ndani ya Mkoa wetu wa Tanga hakika mioyo yetu imejawa na shukrani na hatuna namna nzuri ya kumzungumzia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, zaidi ya tunu ya Taifa hili ambalo tutailinda na kuitetea kwa nguvu zetu zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba vilevile niseme kwamba, licha ya mambo mazuri ambayo wametufanyia bado wananchi wa Mkoa wa Tanga especially Wilaya ya Korogwe pale Hospitali ya Magunga, tunaomba sana Wizara hii ya Afya iendelee ku-influence hospitali ile kongwe ya muda mrefu sana ambayo mara zote imetengewa fedha na fedha zile haziendi kwa hiyo matengenezo hayajaweza kufanyika Hospitali ya Wilaya ya Magunga – Korogwe. Tunaomba sana hospitali ile na yenyewe ipewe kipaumbele ili kuendelea kuzienzi fikra za viongozi watangulizi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiiangalia hospitali ile ipo kwenye highway ya kutoka Tanga kwenda Kilimanjaro ambapo ajali nyingi zinatokea. Wametuwezesha tumepata idara ya dharura tunashukuru sana, lakini bado jengo lile kwa maana ya main building ya hospitali ile. Tunaomba msaada ili tuweze kuishi kwa kupata huduma nzuri za afya kama ambavyo zimetamalaki sehemu zote nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakumbuka niliwahi kuuliza swali hapa na Mheshimiwa Dkt. Mollel alilijibu vizuri kuhusiana na Benki ya Kijerumani ambayo inaitwa KfW – Germany ambayo imekuwa ikitoa huduma za bima za afya kwa mama na mtoto. Benki ile ilikuwa inafanya kazi kwa muda mrefu Mkoani Tanga na wanawake na watoto waliweza kunufaika, lakini baadaye walisitisha huduma ile na kwenda kwenye mikoa mingine. Niliomba kujua ni kwa nini huduma ile imesitishwa Tanga na Mheshimiwa Dkt. mollel alijibu vizuri kwamba tutaweza kufanya mazungumzo na benki ile ili huduma ile irejee Mkoani Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadaye katika kufuatilia hospitalini nilipata taarifa kwamba wameshakubaliana na Benki ile ya KfW – Germany kurudisha huduma ile Mkoani Tanga, lakini mpaka sasa ni kimya sijapata mrejesho wowote, nitaomba sana Mheshimiwa Waziri atakaposimama hapa ku-wind up hoja yake nisikie neno kuhusiana na jambo hili kwa manufaa na mustakabali mpana wa wanawake wa Mkoa wa Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba vilevile kuchangia kipengele cha 41 cha Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mheshimiwa Jenista Muhagama. Amezungumza vizuri kwamba kama Taifa tumeimarika katika huduma za ubingwa bobezi na amezitaja huduma za ubingwa bobezi ambazo tumeimarika nazo ni pamoja na upandikizwaji wa vifaa vya usikivu. Niipongeze Serikali hakika tume-save fedha nyingi kwa suala hili la upandikizaji wa vifaa vya usikivu. Watu walikuwa wanapelekwa India na surgery ile ya cochlea implant surgery ni milioni 35 USD ninakumbuka, 35 thousand USD ni gharama ya cochlea implant surgery moja. Kwa hiyo, ninaipongeza Serikali imefanya jitihada kubwa kutatua changamoto hii, lakini niseme kwamba Serikali bado haijakwenda kwenye chanzo cha tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, chanzo cha tatizo si kwa watoto wetu kufanyiwa cochlea implant surgery; chanzo cha tatizo ni kujua ni kwa nini watoto wetu wanachelewa kujulikana kama wana usikivu hafifu wakati wanapozaliwa. Ninaiomba Serikali kama ambavyo wameweza kuanzia ABR test pale Muhimbili kwa maana ya Auditory Brainstem Response test Muhimbili, tunaomba kwenye wilaya zetu vifaa vile vya kupima usikivu watoto mara tu watoto wanapozaliwa viende kwenye wilaya zetu yote hili jambo linawezekana. Serikali inatumia fedha nyingi kwa wenye ububu na uziwi wanajenga shule lakini not only that tumeona jinsi ambavyo ububu unaongezeka. Niliwahi kutoa records hapa, hela Serikali inayotumia ilitoka kutoka bilioni tatu mwaka 2022 imefika mpaka bilioni sita imeji-double.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake idadi ya bubu na viziwi nchini inaongezeka, maana yake ni nini? Tunakwenda kuathiri human resource ya nchi hii na tunakwenda kuwapa ugumu uzito wazazi wanahangaika na watoto wa namna hii. Niiombe Serikali iseme kitu itakapokuja ku-wind up ni nini mpango wake katika jambo hili? Wanafanya katika level ya juu sana, lakini mtoto mara anapozaliwa iwe ni compulsory kupimwa usikivu na kupimwa usikivu katika nchi za wenzetu siyo hata expensive ni kama shilingi 15,000 ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewahi kuzungumza na Dkt. Edwin, Dkt. Edwin ambaye ni bingwa wa ENT amewahi kusema kile kifaa cha kupima usikivu mtoto anapozaliwa ukiacha hii ABR Test haizidi milioni 15. Ninaomba Serikali katika vifaatiba ambavyo watavipa kipaumbele kwenye wilaya zetu. Ninaomba na vifaa hivi vya usikivu ili kukuza Taifa la watoto wenye weledi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niwaambie, ninazungumza kitu ninachokijua vizuri mimi na mume wangu kama tungekuwa ni wazazi ambao hatuna uelewa wa kutosha, mtoto wangu wa kwanza mimi angekuwa bubu au kiziwi kama siyo kuhangaika kufika mpaka India na hali kadhalika, mpaka leo tunapata challenge ya kumfundisha...

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa wapi? Mheshimiwa Esther Taarifa.



TAARIFA

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Kwanza ninampongeza kwa mchango anaotoa Mheshimiwa Engineer Ulenge, lakini ninataka tu nimpe taarifa tunavyo-address wenzetu ni vyema kusema watu wenye ulemavu wa kusikia either kuona na kuongea kuliko kusema ububu, na; uziwi watu wenye ulemavu wa kusikia, watu wenye ulemavu wa kuongea na watu wenye ulemavu wa kuona. Ahsante!

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Injinia Ulenge unaipokea taarifa hiyo?

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, niipokee tu kwa maana ya tafsiri kila mtu anaweza akaizungumza anavyoweza yeye, ninashukuru kwa hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninachoweza kusisitiza ni kwamba vifaa vile vya kupima usikivu mara mtoto anapozaliwa siyo ghali kiasi ambacho Taifa letu kushindwa kuvinunua. Ninaomba msisitizo huu, vifaa hivi viweze kupatikana katika hospitali za wilaya jitihada walizozifanya ni kubwa sana katika level ya hospitali ya Taifa, ninaomba hili jambo nilisikie likisemwa katika vipaumbele vya Wizara wakati watakapo-wind up hoja hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile, ninaamini kabisa Mheshimiwa Waziri, dada yangu...

MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ikupa, Taarifa.

TAARIFA

MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niweke record sawa kwa sababu Mheshimiwa Ulenge amepokea taarifa, lakini jinsi ya tunavyoyatumia maneno haya zamani tulikuwa tunasema wasiosikia, lakini sasa hivi tunaita viziwi. Kwa hiyo, hatuiti tena wasiosikia, tunaita viziwi na wale wenzetu ambao wana ulemavu wa macho tunaita wasioona na kwa sisi walemavu wa viungo (waliokuwa wanaitwa viwete) sasa hivi tunaitwa walemavu wa viungo. Kwa hiyo, terminologies zipo hivyo sasa hivi. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Engineer Ulenge unaipokea?

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa tafsiri hizo nzuri, ninaomba ulinde muda wangu tafadhali. Ninataka kusema kwamba hili la vifaatiba hivi vya usikivu kwa maana vipimo vile vya awali mara mtoto anapozaliwa nina hakika dada yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama analimudu. Kama ambavyo alisimamia hoja yangu ya muda mrefu ya ufuatiliaji na tathmini na ulipokuwa kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu na leo Serikalini kumekuwa na vitengo vya monitoring and evaluation kwenye kila taasisi ya umma nina hakika kabisa dada yangu na hili analiweza, ninaomba akalisimamie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya mwisho, ninaomba kusema kwamba ninampongeza sana Daktari Janabi kwa nafasi aliyoipata na tunamtakia kheri kubwa sana katika hatua hizo anazoziendea na hakika Tanzania tunaona fahari sana kwa hatua hizi ambazo tunazipiga kwa madaktari wengi na Dkt. Regasha hali kadhalika tunamkumbuka sana ametutibu sana H.pylori. Tunashukuru sana waendelee, wakapambane na wakalitangaze Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niseme tu kwamba sisemi kwa dhamira yoyote ya kwamba nina wasiwasi na yaliyofanyika, lakini tu ni katika curiosity ya kawaida, ninaomba hawa watu sensitive kwenye Taifa letu sasa waangaliwe with a specific attention suala la kwamba mtu ameshakuwa Mkurugenzi wa WHO hata kama ni daktari, hata kama mke wake ni daktari anakwenda India peke yake bila kuwa na escort ya daktari yoyote huku nchini wakati tunaamini hii nafasi ni nafasi sensitive kwa Taifa letu. Ninaomba Serikali waiangalie kwa aina yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakumbuka zamani mtu alikuwa akienda hospitali India yule mtu ambaye ni sensitive kama kina Mafuru walikuwa wanapata ma-escort ya madaktari wetu na maamuzi yanayofanyika yanaendana na mashauriano ya madaktari wetu wa Tanzania; lakini watu wanainuka wanakwenda wenyewe India, mwisho wa siku tunapoteza watu. Sisemi kwamba kuna uzembe uliofanyika, lakini ninaomba tuiangalie hii kwa namna ya aina yake ili twende kulinda vichwa hivi vya Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, neno la mwisho ambalo ninaweza kulizungumza ni Hospitali ya Taifa Muhimbili…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Muda wako umekwisha, malizia tu hiyo hoja haraka haraka.

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalizie kwamba suala la Hospitali ya Taifa Muhimbili kulipiwa parking kwa muda wote mgonjwa anapokwenda hospitalini pale, ninaomba liangaliwe kwa namna yake. Mtu anapokwenda Muhimbili haendi kama anakwenda Milimani City haendi kwa relaxation wala haendi aki-determine time atakayoitumia pale, yeye anakwenda lakini atakaa muda gani inategemea na daktari ambaye anampa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwekwa parking pale, I do appreciate kuona kwamba ma-chief executive wanatafuta namna ya kuongeza fedha kwenye taasisi zao, lakini hiki siyo chanzo genuine cha fedha, tunawaumiza Watanzania ambao wanakwenda Muhimbili kwa shida, hawaendi ku-relax, hawaendi kutembea. Ninaomba mtafute chanzo mbadala kuliko kuwadai wananchi waliokwenda Muhimbili kwa matibabu parking muda wote watakaoishi Muhimbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)