Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi kuwa sehemu ya wachangiaji katika bajeti hii ya Wizara ya Afya. Ni kwamba, Wizara ya Afya imebeba dhamana kubwa sana katika nchi yetu; lakini ni Wizara ambayo hivi tunavyozungumza yako mambo mengi sana ambayo Wizara ya Afya, bado Serikali yetu haijaweka kipaumbele kikubwa sana katika Wizara hiyo. Tunaipongeza Wizara ya Afya, pamoja na kuwa na watumishi wachache, lakini wameweza kufanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha kuwa Watanzania wanakuwa salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mbadala katika afya, binadamu anatibiwa, lakini binadamu hana spare kwamba unaweza ukaweka spare mpya akarudi kuwa mpya, linakuwa ni jambo kubwa sana. Ikifikia mtu kuumwa, akaugua mtu au wazazi au nani, kwa hiyo ni jambo ambalo familia yote inakosa amani; na hasa wakiugua watoto wadogo na wakiugua akinamama. Halikadhalika sisi ambao labda ndiyo nguvu kazi ya familia, ukaugua baba, ukawa uko kitandani. Kwa nini ninayasema haya, ni kwamba Serikali imejitahidi sana kuboresha miundombinu ya afya nchini, hakuna mahali katika nchi hii ambako Serikali haijaweka mkono wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Sita imefanya kazi kubwa sana katika miundombinu. Kwa mfano, mimi tu nimeingia katika Jimbo la Sengerema, tumejenga hospitali ya wilaya mpya kabisa. Katika hiyo hospitali ya wilaya bado pamoja na kujengwa kwake ina mambo mengi sana ambayo bado yamepungua, lakini ina vifaa vingi sana vipya vimepelekwa pale katika ile hospitali ya wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri, tumekwenda naye katika hospitali ya wilaya, tumekwenda naye DDH ameona, lakini tumekwenda naye katika hospitali ya wilaya iliyojengwa kwa ajili ya halmashauri yetu. Tumepewa mitambo mingi, vifaa viko vingi, lakini tumejengewa vituo vya afya, tumejenga vituo vya afya zaidi ya sita. Wizara ya Ujenzi ilitupatia majengo kwa ajili ya kituo cha afya sehemu inayoitwa Busisi, pia pale tulikwenda na Mheshimiwa Naibu Waziri alikwenda kuangalia wakati wanapokea majengo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa nini ninasema hivyo; sisi tuna zahanati kama 31, tuna zahanati mpya tena zimepata fedha, zimejengwa kama zahanati 13. Katika vijiji tulivyonavyo, vijiji 71 pia navyo vina ujenzi wa maboma unaendelea. Tuna zaidi ya maboma 30 ya zahanati hizo mpya, tuna vituo vya afya na vyenyewe vimeshapata vifaa vyake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri zaidi tunaishukuru Wizara ya Afya, wametuletea majokofu kwa ajili ya mochwari mpya. Tumepata majokofu katika Vituo vya Afya vya Kagunga pamoja na Katunguru; na hivi tunategemea Mungu akijaalia tunapata katika Kituo cha Afya cha Ngoma; Butimba; na Kituo cha Afya Kijuka; Kituo cha Afya Kanyerere; na Sima. Hii inaonyesha kwamba Serikali imefanya jitihada za kuwekeza miundombinu kwa sehemu kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wizara hii madaktari imekuwa shida kubwa. Pamoja kuajiri wahudumu wa afya na madaktari, lakini huwezi kuwa na vituo vya afya saba, ukiweka na vituo vilivyokuwepo vitatu na vituo vya afya 10, hospitali ya wilaya lakini hakuna daktari bingwa katika wilaya. Sisi katika Sera ya Afya tulikuwa tumekubaliana kwamba kila wilaya itapata angalau surgeon mmoja na itapata physician mmoja. Sasa imekuwaje kwa hili jambo kukosekana? Kwa sababu kuna magonjwa ambayo yangeweza kutibika huko huko katika wilaya zetu, lakini sasa tunalazimika kwenda katika hospitali za rufaa, hali inakuwa ni mbanano mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunaonekana tumebanana kifedha, kwamba bajeti yetu si nzuri, hizi hospitali za wilaya katika nchi, kwa nini hawa madaktari bingwa wasiwe wanakwenda kwenye hizi wilaya? Kwa mfano, siku ya Jumatano labda, tunajua leo daktari bingwa atakuwepo siku ya Jumatano, madaktari bingwa wawili kila mwezi wanakwenda angalau wanakuwepo pale mpaka hapo tutakapokuja kupata madaktari bingwa. Inakuwaje mifumo haisomani kati ya TAMISEMI pamoja na Wizara ya Afya? Hili jambo Serikali ni moja, baba mmoja, mama mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili jambo tunaomba sana Bunge lako lielekeze kwamba hao madaktari bingwa sasa wawe na siku maalum, tujue kama ni surgeon anakuja wa mifupa anapatikana Jumamosi ya kila wiki, wananchi wenye matatizo badala ya wote kurundikana Muhimbili; kurundikana Benjamin Mkapa; kurundikana Mbeya Hospital; kurundikana labda Mount Meru sasa hivi vitu vya namna hii tunaona kama vile tunajikwamisha sisi wenyewe wakati tumetekeleza mambo makubwa sana katika Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ninataka nilizungumze katika hili suala ni kwamba, sisi Sengerema pale tuna hospitali yetu DDH. Hii hospitali imeanza kutoka huduma tangu mwaka 1953, mwaka 1953 mpaka leo ni zaidi ya miaka 72; leo ndiyo tunakuja kupata mwaka huu sisi hospitali yetu ya wilaya. Kwa hiyo hawa wenzetu Roman Catholic wamefanya kazi ya kuihudumia jamii katika Kanda ya Ziwa kwa muda mrefu, miaka 70.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wameomba tu nafasi kwamba, wao wawe hospitali ya rufaa, wasajiliwe kuwa hospitali ya rufaa kwa sababu wana kila kitu. Mheshimiwa Naibu Waziri, amekuja Sengerema na ameona wana theatre za kisasa; wana umeme wao megawatt kama tano ambazo wanaweza wakahudumia ile hospitali; wana mifumo ya maji; wana kila kitu tools za macho, yaani kila kinachoweza kufanywa katika hospitali ya rufaa wale DDH Sengerema wanayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukanda huo sasa mpaka uje uvuke kuja kuingia Mwanza tunamshukuru Mungu tumepata daraja lakini hata kama hawa wanaoletwa kutoka Kigoma, kutoka Ngara wapi lazima wavuke Sengerema. Kwa nini wasiifanye Sengerema ikawa hospitali ya rufaa? Hatukatai, tunakubali wameweka Ukerewe lakini na sisi Sengerema tupo ng’ambo kuna wilaya zinazoweza kuhudumiwa na ile DDH.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri hili jambo ukija kwenye majumuisho yake tuone kwa sababu wamejitahidi wameshapeleka kusomesha madaktari wanne kuwa specialist, wao wenyewe kwa pesa zao. Kwa nini Serikali isije ikawapa wale ma-specialist watatu tu tuka-qualify ili iweze kusajiliwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ambayo tumeyaomba hapa sisi tuweze kuhudumiwa kama Hospitali ya Rufaa DDH Sengerema. Ina vitanda zaidi ya 400 ina kila kitu ile hospitali. Mheshimiwa Waziri kama atakubali hiki kipindi ambacho tunakimalizia hiki cha muda wa mwisho, aje Sengerema yeye mwenyewe aje ajionee. Katibu Mkuu anajua hii hospitali, yeye anajua, Mheshimiwa Naibu Waziri anajua hilo jambo, tunawaomba sana kwamba wangekuja Sengerema tukaja tukaona na sisi wakatupa nafuu, tuna visiwa, tuna nini. Kwa hiyo moja ya tatizo letu kubwa ni hilo ambalo limebaki lakini kwa shughuli zingine zote sisi tunaipongeza sana Wizara ya Afya kwa kazi kubwa wanayoifanya, lakini tunaiomba Serikali iongeze bajeti hii bajeti iliyotajwa kwa Wizara ya Afya sisi tunaona kama haitoshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imesikia hapa kila Mbunge anayesimama hapa anaona kama bado tuna matatizo makubwa hasa katika magonjwa haya haya makubwa kama magonjwa ya figo. Tulizungumza mwaka jana wakasema watalifanyia kazi, sasa tunaomba mwaka huu Serikali iliangalie sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ninataka kuzungumzia ni suala la tiba asili. Ndugu zangu bila kufichana mwaka jana na mwaka juzi CORONA ilitutesa sana hapa Tanzania, lakini tiba asili ilifanya kazi. Tulichemsha chai za rangi hapa, chai dawa tukaweka vitunguu swaumu, tukaweka tangawizi, limao, ndimu, na majani ya ndimu tukajifusha sisi wenyewe. Watu wa tiba asili wamefanya kazi kubwa sana lakini hatujajua je, hawajagundua tu kwamba tiba asili imesaidia kiasi gani? Mbona wakija hapa wanatoa maelezo, nimesoma hotuba yako Mheshimiwa Waziri hakulizungumza kabisa suala la tiba asili hawa watu anawasaidia namna gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona tu wametambulishwa hapa watu wa tiba asili, lakini yapo magonjwa kama kifafa hayatibiki hospitalini hawa wanatibu. Sasa hivi wanatibu mpaka kisukari, wanatibu magonjwa mengi sugu, mpaka ini wanatibu watu wa tiba asili. Hebu sasa tuwatambue vizuri na leseni zao huko vijijini zimekuwa shida sana kupatikana, kwa hiyo unakuta mganga...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante! Mheshimiwa Tabasamu.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika moja nimalizie.

MWENYEKITI: Ninaomba malizia hiyo.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamalizia tu; ni kwamba hebu wapunguze hizi leseni na huu urasimu wa kupata leseni watu wa tiba asili wauondoe. Kwanza leseni za tiba asili zingekuwa bure tu hawa watu wanatusaidia sana maeneo ambapo hakuna hospitali wametulinda kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)