Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. Paulina Daniel Nahato

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi mchana huu au jioni hii kuchangia katika Wizara hii muhimu sana ya Afya. Awali ya yote ninapenda sana kumshukuru Mungu kwa kunipa uwezo wa kusimama mbele. Ninapenda sana kumshukuru sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano kwa pongezi nyingi alizozifanya katika sekta ya afya na sekta nyingine zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda pia kuwashukuru sana, kuwapongeza sana Mawaziri. Waziri Jenista Mhagama ambaye ni dada mchapakazi. Mwanafunzi mwenzake kipindi cha nyuma aliwahi kusema, Jenista aliwahi kusema; “I am born a Leader and I’ll die a Leader.” Leo katika umri huu ninamwona akiwa a Leader, mengine ya mbele sisemi. Ninapenda kumpongeza Naibu Waziri Dkt. Mollel, kwa jinsi anavyopangua maswali kisomi kwelikweli. Anaitendea haki taaluma yake, anakitendea haki Chuo chake cha Muhimbili na mimi nikiwa sehemu ya chuo hicho. Hongera sana kwake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ninaomba nijikite mchango wangu katika Wizara hii. Baada ya pongezi zote zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa Rais kwa jitihada zake za kuboresha sekta ya afya, mimi leo ninaomba nijikite katika mwendelezo wa kazi katika Wizara hii ya Afya. Nitajikita katika jambo moja la kuzuia, au kinga. Katika afya kuna kutibu na kukinga, hivi vyote vinakwenda sawa, lakini moja inatakiwa iwe juu zaidi ya nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wangu, au kwa tafiti nyingi zinaonyesha kwamba kinga ni bora kuliko tiba. Kama tutaweza kuwekeza zaidi katika kinga tutaokoa fedha nyingi sana katika tiba. Sasa basi, nianze kwa kusema kwamba, Wizara ya Afya, hebu tujikite zaidi katika suala la visababishi vya magonjwa. Magonjwa mengi au takriban yote yana visababishi; na hii siyo kwa Wizara ya Afya tu, ni kwa wizara zote, kwamba zinachangia katika usababishi wa magonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ni kisababishi vya magonjwa, waterborne diseases; barabara ni visababishi vya magonjwa, ajali nyingi za bodaboda; ukienda kwenye Wizara zote za viwanda ni visababishi; ukienda kwenye shughuli zote za kibinadamu, wanyama, mifugo ni visababishi vya magonjwa, Rift Valley Fever. Tukiwekeza zaidi katika visababishi tutaokoa fedha nyingi na wagonjwa watapungua hospitali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitoe mfano mmoja, mtu unapokwenda kuchota maji kwenye bomba lenye koki, ukifika pale unafungua koki, maji yanajaa kwenye ndoo. Ukiondoka na ile ndoo ukaacha koki na maji yanaendelea kutiririka na ukaenda kuyatumia maji na huku koki hujafunga maji yale yatatiririka bila sababu, halafu unarudi tena unakuta maji yanaendelea yamepungua. Kwa hiyo cha msingi katika mfano huo, ni kufunga koki pale unapojaza ndoo yako ya maji; ukayatumie, halafu ukirudi ufungue tena koki utumie. Ninamaanisha nini, wagonjwa walioko hospitali waendelee kupata tiba na wale walioko nje wasiendelee kupata magonjwa ili kwenda kujazana hospitali. Tuwekeze katika visababishi vinajulikana. Magonjwa yote yanajulikana, iwe malaria iwe cancer; iwe figo; iwe pressure; iwe moyo, vyote vina visababishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Profesa Janabi. Profesa Janabi popote alipo ninampongeza sana asisahau kutuhimiza, kutuelezea visababishi vya magonjwa ili tusirundikane hospitali. Ninasisitiza kwamba tuendelee kuwekeza katika afya ya jamii, afya ya jamii itatusaidia kupunguza wagonjwa hospitalini. Mgonjwa mmoja anapokuwa hospitalini anakuwa na wategemezi wa kumhudumia, anakuwa na wategemezi wa kumpelekea chakula na kwenda kumwona, muda ule mwingi wa watu kurundikana hospitali unapunguza nguvu kazi. Kwa hiyo tukipunguza kuwa na wagonjwa wengi watu muda mwingi watautumia kufanya kazi badala ya kuwa hospitalini tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Muhimbili katika Kitengo cha Mifupa, walioko pale wamejazana ni wagonjwa wa ajali za bodaboda. Ajali za bodaboda zinazuilika; kwa nini hawa watumia bodaboda wasichukue tahadhari? Kwa nini wasivae helmet? kwa nini wabebane mishkaki? Balance ya pikipiki inakosekana. Mtu ameweka mtoto mgongoni, amebeba mzigo, mama yeye, wakianguka ni watu wanne hapo wameumia, Serikali inabeba mzigo mzito. Hebu Wizara zote ziingie katika vita ya kupunguza visababishi vya magonjwa ili Wizara hii fedha inazopewa iweze kutumika ipasavyo na kusiwe na manunguniko katika vituo vya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, madaktari hawatoshi kwa sababu wagonjwa wanaongezeka; lakini visababishi vikipungua tukiwekeza zaidi katika kinga madaktari watafika mahali hata wao watakuwa wanawasikiliza Wabunge, watakuwa wanasoma magazeti, watakuwa wanachangia vitu vya maana. Kwa sasa madaktari wako busy, wahudumu wako busy, kwa sababu kila dakika hawa wanaingia, hawa wanatoka, hawa wanaingia hawa wanatoka. Ifike mahali mahali watu wabaki wafanye kazi za uzalishaji mali na hawa walioko hospitalini, kwa sababu hatuwezi kuzuia kabisa, waendelee kupata tiba vizuri, tutakuwa tumeokoa pesa nyingi za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine katika vyuo vikuu; kama mwakilishi wa vyuo vyote kuanzia vya chini mpaka vyuo vikuu, hebu tuongeze udahili wa wanafunzi watakaoenda kusomea masuala ya kinga, waongezeke. Ili hawa wafanye kazi ya kurudi katika vijiji mpaka sehemu zozote kutoa elimu juu ya visababishi vya magonjwa mbalimbali. Public health (afya ya jamii) nayo ipate kipaumbele katika vyuo vyetu vyote vinavyotoa wauguzi na madaktari. Hawa watakaporudi kule watasaidia kuchagiza elimu ya afya ya kujikinga na maradhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi niseme tu kwamba, hivi visababishi vikidhibitiwa na siyo kwa Wizara ya Afya tu; Wizara ya Mambo ya Ndani ikidhibiti; Wizara ya Maji, ikidhibiti; Wizara ya Mifugo, ikidhibiti, Wizara zote haya ya Elimu ikidhibiti, ninamwona Waziri wangu wa Elimu pale; vyote vikidhibiti tutakuwa tumepunguza visababishi vya magonjwa, wagonjwa wale ambao walikuwa wanaumwa kwa sababu kuumwa mtu huwezi kuchagua, nitaumwa tu, lakini tutapunguza msongamano wa magonjwa na tutapunguza gharama ya matibabu, tutaipunguzia Serikali mzigo wa fedha nyingi ambazo zinatumika isivyo lazima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii watu wengi hawajui, mtu akiumwa kitu fulani anakimbilia “ooh! leo ninaumwa, ninaumwa shingo, Mheshimiwa nitumie hela, ninataka nikapime CT scan, ninataka nianze chemo, hata hajui chemo ni nini, hata hajui hiyo shingo ni nini, kwa sababu hatujui visababishi vya magonjwa, mtu anakuja kujua visababishi ameshachelewa; kwa hiyo anaanza matibabu kwa gharama kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi watu wameongea kuhusu mambo ya figo ambayo yanazuilika. Figo zinajulikana visababishi vyake ni nini, Kisukari inajulikana, lishe duni, hebu tuwaelimishe watu kuhusu lishe, hii imesemwa sana Bungeni. Lishe ni moja ya visababishi vya magonjwa mengi. Watu wanafikiri kwa kula vizuri, kwa kula hivi basi hapo wamefika, visinia mtu anafakamia tu kila aina ya msosi mwenye umri mkubwa kama mimi, kumbe anajiingiza katika matatizo ambayo tiba yake ni gharama kubwa. Ninawaomba Mawaziri hebu tuzingatie suala la lishe ili watu wajue, kwamba katika umri fulani wanatakiwa kula nini. Pawe kabisa na vijarida vinavyoonyesha mtu anakula nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia ninakushukuru kwa kunipatia nafasi. Ninawapa hongera sana Mawaziri, wachape kazi, tuko nyuma yao. Mungu awabariki sana pamoja na Mawaziri wengine. (Makofi)