Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kuniona kunipa nafasi hii ili nichangie, niungane na Wabunge wenzangu. Kwanza nianze sana kwa kumshukuru Mungu. Pili, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwaletea Watanzania maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa tumeona wakati Waziri anawakilisha kwamba kuna 1,600,000,000,000 na ushehe. Hii yote inaonyesha Rais ana dhamira nzuri na Watanzania kuhakikisha anawaletea maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wako watu wanasema kila kitu tunasema ameleta Rais Samia. Unajua hapa leo tunapitisha bajeti hii ya 1,600,000,000,000. Sisi tunapitisha, nani sasa mwenye kuidhinisha hela ziende? Watu wasijizime data. Mwenye kupitisha hela ziende kwa wananchi ni Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa hiyo, niombe sana waone kwamba Rais anafanya kazi kubwa nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wako watu wanamchora kama kamdoli fulani hivi. Niiombe Wizara hii ya Mawasiliano washughulike nao. Rais huyu ni tunu ya Watanzania, washughulike nao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama pamoja na Naibu Waziri wake, pamoja na Katibu Mkuu. Kwa kweli tumeona tangu ameingia kwenye Wizara hii tumeona mageuzi makubwa sana. Tunampongeza sana Mheshimiwa Jenista na timu yake, anafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi letu sisi kama Wabunge wenzako, tunamwombea sana kwa wananchi wa Peramiho kwa sababu yeye ni Waziri anafanya kazi katika Tanzania. Tunamwombea wananchi wa Peramiho, tunawaomba wananchi wa Peramiho waone kwamba iko haja urudi uweze kuwatumikia Watanzania wakiwepo na wa Peramiho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo wamesema wenzangu hapa, niseme mambo machache. Kwenye Wizara ya Afya kama tulivyosema wanafanya kazi nzuri, tuna tatizo sasa la ugonjwa wa watu, magonjwa ya figo. Sasa yamekuwa ni makubwa sana, tatizo hili limekuwa ni kubwa katika nchi yetu. Tuiombe Wizara ione kwa sababu tatizo hili sasa linahudumiwa na Mkapa, linahudumiwa na Kanda kule Mbeya na Muhimbili.

Mheshimiwa Spika, tuombe sasa waone iko haja sasa ya kupeleka huduma hii kila mkoa kwa sababu hospitali za mkoa zipo nyingi, zimejengwa kila mkoa hospitali nzuri. Kwa hiyo, tuombe kila mkoa suala hili la wagonjwa wetu wa figo lishughulikiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine nizungumzie sasa kwenye Jimbo la Makambako ambalo wananchi wake ninawapenda sana na wao wananipenda sana; lazima niwe mkweli. Kwa kazi nzuri iliyofanyika niliyosema ya afya, Makambako tuna vituo vipya vitano vya afya. Tuna zahanati zaidi ya 17. Kwa hiyo tunaipongeza sana Wizara pamoja na TAMISEMI kuhakikisha kwamba sisi Makambako tuna vituo vya afya na zahanati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa Wizara, tuna Kituo cha Afya pale Ikelu ambacho Mheshimiwa Waziri alikuja yeye mwenyewe tuliungana na mimi kwenda wakati ule kwenda kuona ujenzi ambao unaendelea. Tunaomba washirikiane na Wizara ya TAMISEMI kuhakikisha tunapata fedha ili kituo hiki kiweze kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna kituo cha afya vilevile kule Usetule Kata ya Mahongole, kinaendelea. Tunaomba tupate fedha ili kituo hiki pia kiweze kukamilika. Pia, tuna kituo kingine ambacho kilianzwa kimesimama kule Kitandililo. Tunaomba washirikiane na TAMISEMI kuona kituo hiki kinaweza kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, Ukanda huu wa Kusini Makambako pale tuna kiwanda cha dawa. Kiwanda hiki tunaomba waendelee kuhakikisha kinapata fedha kuhakikisha lile kusudio waliloanza kinaweza kukamilika, hasa kutengeneza dawa za vidonge pamoja na syrup kwa sababu kiwanda kipo. Watu wa Makambako na ukanda huu tunategemea sana kuona kwamba kiwanda hiki kitakamilika ili kiweze kutoa ajira za ndani na nje ya Mji wa Makambako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni Bima ya Afya. Suala la Bima ya Afya baadhi ya watumishi wetu unakuta wanapokwenda watu wenye bima hawahudumiwi kama ambavyo sawa na mtu anayetoa fedha taslimu. Jambo hili Wizara waliangalie wakishirikiana na TAMISEMI, kuhakikisha kwamba Bima ya Afya ni bima ambayo mtu amelipia, ni sawa na fedha taslimu. Kwa hiyo, isimamiwe kuona watu hawa wenye bima wanahudumiwa kama sawa na mtu ambaye amepeleka fedha pale dirishani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niungane na wenzangu; Serikali sasa imejenga vituo vingi, hospitali nyingi na zahanati nyingi. Tuhakikishe tunapeleka watumishi wa kutosha ili waweze kuwahudumia Watanzania katika vituo hivi ambavyo vimejengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho, hili haliko kwenye Wizara yako lakini kwa sababu Serikali iko hapa. Mheshimiwa Waziri, pale Makambako tuna madai ya fidia ya muda mrefu. Tunadai la fidia la umeme wa upepo ambalo wananchi wake sasa takribani zaidi ya miaka 10 na kitu wamezuiliwa hawawezi kufanya jambo lolote na nimekuwa nikifuatilia juu ya kulipa fidia wananchi hawa ili shughuli zao ziendelee, waweze kupata fedha waweze kufanya majukumu mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile tuna fidia ya soko la Kimataifa ambalo Serikali ilishalipa fidia. Kuna wananchi walibaki 18 ambao uhakiki wao ulikuwa bado. Kwa hiyo, kwa sababu Serikali iko hapa Mheshimiwa Waziri, shirikiana na wenzako kuhakikisha wananchi hawa wanapata fidia, stahiki zao za watu 18 hela zilizobaki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna fidia nyingine ambayo ilikuwa kwa ajili ya kujenga ...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa. (Makofi)

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, dakika moja ni summary. Fidia ya mwisho ni Idofi, kwa kujenga One Stop Centre kwa ajili ya kuondoa yale makaburi zaidi ya shilingi milioni 100 na kitu watu wa TANROADS.

Mheshimiwa Spika, vinginevyo nikupongeze wewe binafsi sana kwa kazi kubwa unayofanya. Kwa kweli lazima tuwe wakweli. Tunapata heshima sisi wenzako hata tukitembea. Juzi nilikuwa nchi moja huko, nilikuwa nchi za nje, wanasema unatoka kule anakotoka Spika Tulia? Nikasema ndiyo. Kwa hiyo, umetupa heshima kubwa sana kwa kuwa Mbunge wa Bunge la Dunia. Sisi wenzako tunakupongeza sana. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunampongeza vilevile, Rais wetu kwa kazi kubwa anazofanya za kuletea Tanzania maendeleo. Tunamwombea kule Mbeya, kule Mbeya, wasikie kule Mbeya. Kwa kweli kwamba wewe ni tunu yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunakushukuru sana. Ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Ahsante.

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, Uyole, Uyole! Wananchi wa Uyole tunawaomba sana waone kwamba umuhimu wa kukupatia wewe. Ninakushukuru sana, ahsante. (Makofi)