Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buchosa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, ninaomba nichukue nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi kuzungumza ndani ya Bunge hili Tukufu. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa uwezo wake wa kipekee, pia ninawashukuru sana wananchi wa Buchosa kwa heshima waliyonipa ya kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninavyoongea leo, ninaweza nisipate tena nafasi ya kuongea hapo mbele; ninaomba nianze kwa kusema, nilipokuja Bungeni hapa, nilikuja na ajenda tano. Ajenda ya kwanza ni ajenda ya ku-empower wazawa wa nchi hii. Ninamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pia ninawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, tumefanikiwa kubadilisha Sheria ya Manunuzi na kwamba tumekubaliana bilioni 50 ni wazawa watakaofanya kazi hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilikuja na ajenda ya RPL pamoja na kubadilisha curriculum zetu. Ninashukuru sana Serikali, kupitia Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba tumefanikiwa kurejesha RPL na sasa curriculum zimebadilika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nyingine ilikuwa ni kuhusu National Innovation Fund. Ninashukuru sana Serikali tumeanzisha Samia Innovation Fund kuwasaidia vijana wetu wabunifu wa nchi hii.
Mheshimiwa Spika, nyingine ilikuwa ni utumiaji wa rasilimali za nchi yetu kwa maendeleo. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya jambo hili kwa umakini mkubwa, sasa tunaona utalii unachangia mapato makubwa kwa nchi yetu. Nina uhakika kabisa tunapokwenda ni kuzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ajenda nyingine ilikuwa NHIF; nilipata nafasi ya kuzungumza na dada yangu Mheshimiwa Jesnista hasa ilikuwa ni juu ya mifumo kusomana. Mifumo kusomana ilikuwa ni changamoro kubwa. Nikienda Hospitali ya Kairuki kutibiwa, nikienda Muhimbili ninahitaji kurudia vipimo, matokeo yake ilikuwa inatokea duplication of care na NHIF ikawa inaingia kwenye matatizo makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ajenda yangu ya tano ambayo inafanya nizungumze leo ilikuwa ni juu ya ugonjwa wa Homa ya Ini. Mtakumbuka kabisa zungumzo langu la kwanza Bungeni lilikuwa ni kuhusiana na Homa ya Ini. Nilipata nafasi ya kusoma data moja mtandaoni mwaka 2014 iliyonionesha kwamba prevalence rate ya Homa ya Ini ilikuwa kubwa sana, na Tanzania ilikuwa ni asilimia sita. Jambo hilo lilinifanya mimi na wenzangu tuamue kufanya kampeni nchi nzima kuwaelimisha watu kuhusu ugonjwa huu.
Mheshimiwa Spika, wakati ninafanya jambo hilo, dada yangu Grace Magembe alikuwa ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alikuwa Meck Sadick, na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Ilala alikuwa Meshack Shimwela. Tulifanya kampeni ile, lakini baadaye tuliambiwa tulikuwa tunasababisha taharuki kubwa, tukaamua kuacha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo ninapozungumza prevalence rate ya Hepatitis katika Taifa letu bado ipo juu. Ninavyozungumza, prevalence rate ya Homa ya Ini ni sita mpaka nane. Hii inaonesha kwamba tatizo hili ni kubwa na Shirika la Afya Duniani limetamka kwamba, kufikia mwaka 2030 ugonjwa huu uwe eliminated. Imebaki miaka mitano tu, na ninavyotazama mimi ninaona kama haitakuwa rahisi kwetu ku-eliminate ugonjwa huu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa kwa nini nimesimama kuzungumza? Nimesimama kuzungumza kuikumbusha Serikali yangu na nchi yangu juu ya umuhimu wa kutoa chanjo ya Homa ya Ini kwa watu wetu. Nimeshazungumza huko nyuma na ninazungumza tena leo. Ninaomba sana tuwachanje watu wetu, kwani ugonjwa huu upo na unazidi kuenea na watu wanapoteza uhai. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kumtibu mgonjwa wa cancer ya ini iliyosababishwa na Homa ya Ini inagharimu dola 50,000 kwa nchi kama Marekani, kwa India ni dola 20,000, kwa Tanzania hapa inagharimu siyo chini ya milioni 30 kumtibu mgonjwa mwenye cancer ya ini na inawezekana asipone, lakini kumzuia mtu asiugue cancer ya ini inagharimu siyo zaidi ya shilingi 4,000 peke yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa, nilishazungumza huko nyuma na ninaomba nizungumze tena leo. Ninakwenda kugombea Ubunge, nitarudi mwezi wa 11, nitaendelea na ajenda hii mpaka mwachanje watu wetu dhidi ya ugonjwa huu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, utakumbuka kabisa; ninaomba nitoe historia fupi tu kidogo hapa ili niweze kueleweka. Chanjo ya Homa ya Ini mwaka 2002 Hayati Benjamin Mkapa aliamua kuwachanja watoto wote kwenye Taifa hili, kila mtoto anayezaliwa anachanjwa. Kuanzia mwaka 2002 mpaka leo 2025 ina maana ya kwamba watoto wote, vijana wote wenye umri wa miaka 25 ambao ni 70% ya watu wetu wamekwishachanjwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa, ninachokizungumza hapo ni nini? Ninaomba nisikilizwe vizuri hapo. Ili uweze kuwachanja watu wako wote unahitaji kuchanja 90% tu ya watu. Hiyo inaitwa Herd Immunity. Herd Immunity usichanje watu wote 100%, chanja 90% peke yake.
Mheshimiwa Spika, sasa, kwa data tulizonazo hapa sisi ni kwamba, ukichanja 90% ya watu milioni 60 Watanzania unatakiwa kuchanja watu milioni 54 peke yake. Milioni 54 ukiwachanja, katika milioni 54 hiyo ukiondoa watu ambao ni vijana wa miaka 25, unatakiwa kuchanja watu 37,800,000 ambao ni 70%. Ukitoa 54 ukatoa 37 unabaki na watu 16,200,000 peke yake, ambao ukiwachanja hao utakuwa umechanja 90% ya Watanzania wote. Maana yake ni kwamba, utakuwa umesababisha Herd Immunity kwenye nchi yako, utakuwa ume-eliminate kabisa ugonjwa wa Hepatitis katika nchi yetu. Sasa, kwa nini hatuchanji? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninataka niongee jambo moja, linaweza likawasikitisha watu wengi. Ni kwamba, ukinunua chanjo India leo ya Hepatitis kutoka Kiwanda cha Serum India utanunua kwa nusu ya dola, ambayo ni sawa sawa na shilingi 1,400 approximately (chanjo moja kuinunua). Mtu anahitaji chanjo tatu ili aweze kuwa fully recovered. Kwa hiyo, tafsiri yake ni nini? Shilingi 1,400 mara tatu, ni kama shilingi 4,200. Mtu anachanjwa na anakuwa fully protected, lakini kwa nini hapa Tanzania tunashindwa kuchanja watu wetu wote? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna mtu mmoja ana monopoly ya chanjo ya Hepatitis (kampuni moja tu). Ukienda kununua chanjo India leo kwenye Kiwanda cha Serum watakwambia hapana; chanjo hii kule Tanzania anashughulika nayo Bilakwate. Kwa hiyo, maana yake ni kwamba huwezi kununua mpaka uje kwa Bilakwate. Huyu mtu mwenye monopoly hapa Tanzania anauza chanjo yake kwa bei kubwa, shilingi 10,000 kwa chanjo moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninachokiomba nisaidiwe, MSD waende moja kwa moja kiwandani wakanunue moja kwa moja kiwandani hii chanjo. Nimejipanga na nimejiandaa. Huyu mtu mwenye monopoly tunataka tumpeleke kwenye Fair Competition Tribunal, ili aweze kuondolewa hiyo kinga ya kununua peke yake. Tusipofanya hivyo watu wetu watazidi kuumia. Ninaomba sana Mheshimiwa Waziri anisikilize. Tumeongea jana kirefu sana mimi na yeye. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lengo langu hapo ni kuwa-protect watu wetu. Katiba yetu inatamka wazi kwamba, kazi ya kwanza ya Serikali itakuwa ni uhai, ni kushughulika na ustawi wa watu wake. Tukiokoa maisha ya mtu mmoja ni faida kubwa sana kwa Taifa letu. Sasa, hatuwezi kuwa nchi ambayo mtu mmoja ana monopoly ya kuuza chanjo ya Hepatitis katika nchi yetu, halafu ameachwa aendelee kufanya hivyo. Ninamwomba Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati, yeye ni mzalendo katika nchi yetu. Tusaidiane kwenye jambo hili, MSD wakanunue wenyewe chanjo kiwandani ili chanjo hii iwe ya bei rahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivi sasa mtu mmoja, watu wetu wanashindwa kuimudu hii chanjo, wanashindwa kuimudu. Chanjo moja shilingi 10,000, chanjo tatu shilingi 30,000. Wangapi wataweza kumudu? Kama hilo haliwezekani, kama watashindwa kumnyang’anya huyu mtu monopoly, basi NHIF wachukue dhamana ili chanjo iweze kutolewa na NHIF moja kwa moja kwa watu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba nimalizie kwa kusema, ninafurahi ninazungumza mbele ya Profesa Janabi na Dkt. Shekalaghe wananisikiliza. Ninawaombeni sana tukafanye kazi ya kuwalinda na kuokoa maisha ya watu wetu. Tusipofanya hivyo watu wataendelea kupoteza uhai na sisi tupo tunaangalia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba niunge mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)