Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa kupata fursa ya kuanza kuchangia bajeti ya Wizara ya Afya. Ukweli ni kwamba, mengi yamefanyika, Wizara inafanya vizuri na Wabunge wenzangu ninadhani hii ni Wizara ya kuwapatia tu ushauri, lakini wanaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze na Jimbo langu la Musoma Vijijini. Ninasema inaenda vizuri na uthibitisho ni huu. Huduma za afya toka niwe Mbunge wa Musoma Vijijini ni kwa miaka hii minne, mitano mambo yamebadilika kweli kweli. Musoma Vijijini tuna Hospitali ya Halmashauri yenye hadhi ya Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Spika, tunavyo vituo vya afya sita, tumepata tena fedha tunajenga kituo cha afya cha saba. Zahanati zinazotoa huduma ni 28, zahanati 24 ni za Serikali na zahanati tatu ni za binafsi. Sasa kwa mtindo wetu wa Musoma Vijijini huwa tunaanza kujenga sisi, halafu baadaye tunaomba Serikali itusaidie. Sasa hivi tunajenga zahanati mpya 18, lakini malengo yetu ni kujenga zahanati kila kijiji. Kwa hiyo, Musoma Vijijini tunajenga Shule ya Sekondari kila Kijiji na Zahanati kila Kijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, magari ya wagonjwa tunayo saba; mawili mapya ya Serikali, matano Mbunge na rafiki zake waliyanunua. Kwa hiyo, kwa yote haya ninatoa shukrani kubwa sana kwa Mheshimiwa Rais amewekeza na Wizara inafanya kweli kweli. Kwa hiyo, acha niende kwenye maombi mepesi ambayo ninajua na Wabunge wengine wataomba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wafanyakazi waongezwe na madawa yaongezwe. Sasa, kitu cha muhimu sana ni kutoa ushauri. Ushauri wa kwanza ni hivi, kwa mazuri tunayoyafanya, tunapasa kujipima na tutumie hata vigezo ambavyo sisi tulishiriki kuvitengeneza.

Mheshimiwa Spika, kigezo cha kwanza kabisa, na Wizara hii tulishiriki vizuri sana mwaka 2015 UN zile Sustainable Development Goals, sasa ya afya ni namba tatu SDG No. 3 ambayo ni good health and wellbeing. Hii ni kubwa mno, ninaomba Wizara kila tunavyokwenda mbele, rudini kweye hii SDG No. 3 mwangalie kama tunaenda vizuri. Ikifika 2030, tutafanya kupitia mafanikio, lakini katika nchi za Kiafrika na labda duniani Tanzania itaonekana inafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipimo cha pili, sisi ni wanachama wa WHO, tena Mheshimiwa Profesa rafiki yangu, hongera sana. Sasa huko WHO lazima nako tuongalie wanatoa mapendekezo gani? Kwa mfano, uwiano wa daktari na wananchi wanaopaswa kutibiwa. WHO inapendekeza daktari mmoja kwa watu 1,000. Wengine wanasema, daktari mmoja kwa watu 4,000.

Mheshimiwa Spika, ninapenda hii ya daktari mmoja, watu 1,000. Maana ya daktari hapa ni yule mwenye shahada kutoka kwenye Chuo Kikuu kinachotambulika, ndiyo maana yake hiyo. Kwa hiyo, tukichukua mapendekezo hayo, sasa hivi Tanzania tupo watu takribani milioni 70, kwa hiyo, daktari mmoja kwa watu 1,000 Mheshimiwa Waziri anapaswa kuwa na Madaktari 70,000. Sasa, mimi sikutaka kwenda kwenye database yao, siwezi kulumbana nao, afadhali niongee haya mimi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka 2050 kwenye dira yetu ya maendeleo, tukifika mwaka 2050 kama tunazaliana sana na itategemea na speed yetu ya kuzaliana, lakini tuchukulie tutakuwa watu milioni 140. Kama ni watu milioni 140 ifikapo mwaka 2050 tunapaswa nchini kuwa na madaktari 140,000 kulingana na mapendekezo ya WHO.

Mheshimiwa Spika, kingine ambacho ni lazima tujipime nacho ni uwiano wa ma-nurse kwa wagonjwa. WHO inapendekeza nurse mmoja kwa wagonjwa wanane, tunafanya vizuri lakini tunapaswa kujipima na kwenye maeneo kama ya emergency; na Psychiatric Hospital kama Milembe hapa wanataka nurse mmoja kwa wagonjwa wanne. Kwa hiyo, ndugu zangu, Waheshimiwa Wabunge, ukweli ni kwamba tunayo safari ndefu tumeanza kutembea, tusikate tamaa.

Mheshimiwa Spika, pendekezo langu la pili ni kwenye vifaa. Vifaa lazima tujipongeze, tumefanikiwa sana. Tukiviongea kwa lugha nyepesi nyepesi, mtu ataviona ni vyepesi vyepesi. Nimeshukuru kumsikia Mheshimiwa Waziri anasema tuna CT-Scans 45. Sasa ninaona niyaseme kwa kirefu ndiyo utaona umuhimu wake. CT-Scanner hiyo ni Computed Tomography ndiyo kule huwa ninawaeleza mambo ya science. Tunazo MRI, Mheshimiwa Waziri ametuambia tunazo 13 sasa hivi. Sikiliza, hii MRI ni Magnetic Resonance Image. Watu wa Sayansi tupo hapa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, tuna mambo ya X-Rays ambazo hata kule kwangu zipo. Mheshimiwa Waziri ameenda mbali, tumechukua ambazo ni digital za kisasa kweli kweli ambazo nyingine ni fixed na nyingine ni mobile za kumfuata mgonjwa alipo. Halafu kifaa cha nne kikubwa ni ultrasound machines. Mheshimiwa Waziri ametuambia tunazo 970.

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, sasa kwa mchango wangu mimi hapa, hivi vifaa vyote vinne vikubwa wanasayansi watajua ni mambo ya rays, lakini imaging techniques ni techniques za imaging, kuona mwili kwa undani wake.

Mheshimiwa Spika, hapa pendekezo langu ambalo ni muhimu na lilifanya niombe kuchangia ni wataalam, ambapo tunao wachache sana. Specifically, hili eneo litatusaidia hawa lazima tusomeshe vijana kwenye eneo la radiology. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mapendekezo yangu yatakuwa kama yale ambayo wakati sisi tulipoingia Chuo Kikuu tukiwa hatuna wataalam wa madini, Serikali ikasema tusomeshwe kwa haraka sana, na tukasomeshwa kwa speed kweli kweli. Sasa, pendekezo langu, hii radiology ninapendekeza tuwe na vijana wanaosoma hii Shahada GACC in Radiology angalau 100 kila mwaka na tuwapeleke kwenye vyuo ambavyo ni vizuri sana.

Mheshimiwa Spika, kwa nini? Kwa sababu hivi vitatu vyote CT-Scan, MRI, X-Rays and Ultrasound tunavyo, tatizo huwa ni tafsiri sasa. Wameshapiga picha, wanakupatia wewe utafsiri, uweze kupendekeza matibabu. Hapo ndiyo penye kazi hapo, kuhusu tafsiri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ni sawasawa kama kwenye sekta mafuta unaweza ukafanya exploration, ukaenda kutafsiri ukasema hakuna mafuta, mwingine akarudi hapo hapo akatafsiri akasema kuna mafuta. Sasa ndiyo kama hii ya radiology, anaweza akatafsiri asione kuna ugonjwa, mwingine akatafsiri hicho hicho akasema kuna ugonjwa. Kwa hiyo, hapa tunahitaji wataalam, na ndiyo ninasema kwa lugha nyingine, tuwe na marshal plan, watu wasomeshwe kwa kasi kubwa sana kwenye shahada ya kwanza 100, kwa miaka mitano tutakuwa na watalaam 500. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa nimalizie dakika moja. Hospitali zetu hizi mbili lazima tuzifanyie kazi. Kuna Teaching Hospital na General Hospital. Ni lazima tuwekeze sana kwenye Teaching Hospital kwa sababu inatoa kazi mbili, inatibu na kutoa elimu, na hapo ndiyo ninapendekeza na Hospitali ya jina la Mwalimu Nyerere, ile ya Mkoa wa Mara, Memorial Regional Hospital, tunaomba iwe ni Teaching Hospital, iwe ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Mwalimu cha Kilimo na Teknolojia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana na ninaunga mkono. (Makofi)