Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia hii Wizara. Cha kwanza ni kuwapongeza tu watendaji wa Wizara, Mheshimiwa Bashe, Naibu wake Mheshimiwa Silinde, Katibu Mkuu Gerald na watendaji wengine wote wa Wizara ya Kilimo. Pia nimpongeze Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba, huyu mzee anafanya kazi sana, Mheshimiwa Bashe wewe usiangalie umri angalia kichwa chake kinafanya kazi kiasi gani tuendelee kuwa naye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunampongeza Rais kwa kazi nzuri aliyofanya kwa kupandisha bajeti ya kilimo kuwa kiasi hicho. Mheshimiwa Bashe unajua kuna watu wanalitazama jambo hili kama la kawaida, wapo watu duniani waliwahi kuuliza tofauti kati ya akili na elimu; mmoja wa watu hao alikuwa ni Albert Einstein, aliuliza elimu ni nini na akili ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wako watu hawajui mambo hayo, wanasema Albert alisema ni bora uwe na akili kuliko kuwa na elimu na akasema wako waliotengeneza hii dunia, akamtaja Isaac Newton, akamtaja Galileo Galilei, akamtaja Archimedes akasema hao ndiyo wanasayansi, icon ya dunia ambao hawakuwa na cheti na diploma na degree na PhD na profesa, lakini leo ndiyo watu wanaiga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri wewe Mheshimiwa Bashe Mungu alikupa vyote, una akili na elimu, hongera sana na ndiyo maana watu wengine wanakuona tofauti tofauti wakati ukifanya mambo, ukikasirika asiyekujua anasema huyu bwana hawezi kusogea hapa, ukifurahi wanasema wewe ni mtu laini, lakini Mungu alikupa akili zote, alikupa elimu, akakupa na akili, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika maelezo yangu hayo huwa najiuliza umetumia elimu kupandisha bei ya korosho, bei ya kahawa, bei ya ufuta na tumbaku imeongezeka. Hiyo elimu na akili ambayo Mungu anakupa tatizo linakupata wapi kupandisha bei ya pamba? Wapi linakupata hilo tatizo? Yaani maeneo mengine yote unaweza, kwa nini sisi wakulima wa pamba tunalima pamba kwa kutumia milioni mbili, halafu ukiuza unapata milioni moja? Tatizo ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba, akili hizo alizotumia kwa mazao mengine kwa Kanda ya Ziwa aende. Huwa najiuliza hivi Mheshimiwa Bashe akiongea na viwanda vikubwa vya Marekani, vya Canada kule wanakonunua pamba, akawaambia jamani eeh mimi mwaka huu nina pamba, niwauzie bei gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakakwambia bwana pamba kipindi hiki tutakupa kilo shilingi 2,500 ukaja ukamwambia mkulima anayelima eka kumi, bei yake itaanzia shilingi 2,500. Sasa kwa nini mnatuacha sisi tunalima, tunatumia ng’ombe, tunatumia trekta, tunatumia nini, halafu unalima kwa shilingi bilioni 200, unalima kwa shilingi milioni 15, unalima kwa shilingi milioni 20, unapata shilingi milioni 10? Hiyo akili ya maeneo mengine, Bukoba, wapi huko, Songea, hii imeenda wapi huku kwetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana, mwaka huu unaokuja wa 2026 utafute hiyo akili uliyonayo utuwezeshe sisi tupate pamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, nimpongeze Mheshimiwa Rais. Skimu ya Maliwanda na Kisangwa ni skimu bora sana kwa Mkoa wa Mara na Skimu ya Kisangwa wakulima wa Jimbo la Bunda wanachukua 60% na wa Bunda Mjini 40%, Skimu ya Maliwanda tuna 100% kwa 100%. Umetangaza mkandarasi wa kuikarabati skimu iwe bora kuliko skimu zote Tanzania, lakini mkandarasi hajaja. Tunakuomba huyu mkandarasi, yale matangazo uliyofanya yaje mapema, lakini tunamuomba Mheshimiwa Rais, kama matangazo yatafika, muda wa uchaguzi umefika, akurudishe tena kwenye Wizara hii ili utengeneze skimu hizo. Tunakushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo mimi ninaliona ni namna pembejeo zinavyowafikia wakulima. Kwa nini pembejeo haiji kwa wakati? nikuombe sasa pembejeo ije kwa wakati, ili watu waweze kulima.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, vinginevyo Wizara yako hii ya Kilimo sasa hivi ina rindima. Watu wanajua kwamba Wizara ya Kilimo ina mtu ana akili, mtu ana elimu.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Getere, muda wako umeisha.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, hongera sana na naunga mkono hoja. (Makofi)