Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Korogwe Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Nina mambo machache, kama matano hivi ya kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniweka salama na kunipa afya, leo ninawasemea wananchi wa Korogwe na Watanzania kwa ujumla. Namba mbili ninaomba nitumie fursa hii kumshukuru na kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutekeleza miradi mikubwa kwenye nchi hii, lakini pamoja haiachi sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepiga mahesabu kwa miaka michache iliyopita, sekta ya kilimo bajeti yake imeongezeka kwa zaidi ya 100%, kutoka kwenye dola 290 mpaka 1.2 billion. Ni hatua kubwa sana kwa nchi yetu, hivyo nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, lakini pia niwapongeze viongozi wa Wizara hii, Mheshimiwa Bashe, kaka yetu Mheshimiwa Silinde, Katibu Mkuu Gerald na Naibu Katibu Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu Mheshimiwa Waziri naomba unisikilize vizuri, watu wa Korogwe wanatamani kusikia hapa vizuri, Mheshimiwa Waziri tangu naingia Bungeni nimekuwa nikifuatilia mabonde yangu mawili ya Korogwe Mji, moja ni Bonde la Mahenge na namba mbili ni Bonde la Kwamsisi. Mheshimiwa Waziri ulilitangaza Bonde la Mahenge, ukapeleka mkandarasi, wananchi wakawa na matumaini makubwa sana, lakini baada ya miezi sita/saba hakuna kilichofanyika, ukasema tunamtoa mkandarasi Tume ya Umwagiliaji itafanya yenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya mwaka hakuna kilichofanyika, ukasema tunatangaza kupata mkandarasi mwingine. Mheshimiwa Waziri hadi sasa hivi tunavyoongea hakuna kitu kinachoendelea kwenye Bonde lile la Mahenge, Kata ya Kwamndolwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi wananchi wa Kwamndolwa na Mahenge wanahisi sifuatilii juu ya jambo hili na wewe mwenyewe unafahamu namna ninavyohangaika, ninavyokufuata, ninavyokusumbua juu ya jambo hili. Mheshimiwa Waziri ninakuomba, ukiwa unahitimisha, u-note kabisa hapo, usemee Bonde la Mahenge. Otherwise nakuomba ukipata muda twende ukaseme mwenyewe mbele ya wananchi wa Korogwe, ili wadhihirishe kwamba mimi nimetimiza wajibu wangu, iliyobaki ni upande wenu. Mheshimiwa Waziri naomba hilo niishie hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo nina Bonde langu la Kwamsisi. Mheshimiwa Waziri mwaka 2024 kwenye bajeti ilionekana kama linaenda kutangazwa na ukaenda kuwaambia wananchi wa Kwamsisi shilingi bilioni tisa. Mama, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alivyokuja Korogwe nikaongelea Bonde la Kwamsisi kutangazwa na kuanza utekelezaji wake, akatoa maelekezo kwamba litangazwe, mkandarasi apatikane. Mheshimiwa Waziri hadi sasa hivi sijui kinaendelea kitu gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri na hili naomba ukiwa unahitimisha ugusie au hiyo safari yetu ya Korogwe uende na mimi Kwamsisi ili uweze kuwaeleza wananchi. Hayo ni ya kwangu mawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ninalotaka kutoa ushauri Mheshimiwa Waziri ninaona una malengo mazuri na makubwa juu ya kilimo cha nchi hii. Kimsingi tunazalisha zaidi ya mahitaji yetu na tunaweza kuuza, Mheshimiwa Waziri, nina ushauri mmoja, sijui kama unafahamu wapo wananchi wa nchi hii ambao wanatamani kulima, lakini hawana uwezo wa kununua mbegu. Wapo wanaonunua mbegu ambazo hazina ubora, kutokana na gharama kubwa ya mbegu, lakini pia wapo wananchi wanaoweza kuona mazao yao ya shamba yakiteketea na wadudu, lakini hawana uwezo wa kununua dawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, ninajua inaweza isiwezekane leo, lakini weka kwenye strategic plans zako, natamani siku moja kwenye nchi hii wananchi wote wakulima wawe wanagawiwa mbegu bure ili kusiwe ni option ya mtu kulima au kutolima, kwa sababu ya kukosa mbegu. Unaweza ukaanzisha utaratibu, wakati wa kulima watu wanapewa mbegu bure, baadaye wanapewa dawa bure, wanapewa mbolea bure na wakati wa kuvuna wanarudisha zile gharama Serikalini na zinatumika kwa kipindi kijacho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii tutaweza kumkomboa mkulima kwa sababu wananchi wa nchi hii wengi ni maskini. Kweli kuna ruzuku, lakini mbolea unaweza ukaishusha ruzuku mpaka 70,000, lakini yuko mtu ambaye analala na njaa, anaamua aidha anunue chakula kwa kuwalisha familia au siku hiyo wakanunue mbolea, ana-opt kununua chakula. Kwa hiyo, wananchi wa nchi hii wanatamani sana kuchangia kwenye sekta ya kilimo, lakini maisha magumu yanawarudisha nyuma. Hilo ni ombi langu tuliweke kwenye mpango siku moja nchi hii iweze kutoa mbolea na mbegu bure.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Huo ndiyo ulikuwa mchango wangu na ninaunga mkono hoja. (Makofi)