Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Yahya Ally Mhata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata nafasi hii jioni ya leo kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii ya Kilimo.

Kwanza nami nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema ambaye ameniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kutoa mchango wangu kwenye bajeti hii.

Pili, kama ilivyo ada, nami nimshukuru sana Waziri mwenye dhamana, ndugu yangu Mheshimiwa Hussein Mohamed Bashe na Naibu wake Mheshimiwa Silinde, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu Bwana Hussein na Bwana Stephen kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuendelea kumshauri Waziri wetu ili aweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nitoe mchango wangu katika maeneo yafuatayo; kwanza ni kwenye ushirika. Naishukuru sana Wizara kwa bajeti hii iliyowasilishwa asubuhi, imezungumzia kuhusu uanzishaji wa Benki ya Ushirika katika mikoa minne na moja ya mkoa ni Mkoa wa Mtwara ambako mimi natoka katika mkoa huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Mkoa wa Mtwara unahitaji sana benki ambayo ita-deal na wakulima moja kwa moja. Ni matarajio yangu Mheshimiwa Bashe benki hii ya ushirika itatatua changamoto za wakulima wetu. Wakulima wetu, hasa wa zao la korosho, naomba hapa ieleweke benki hii ije Mtwara kutatua changamoto za wakulima wa korosho, siyo wafanyabiashara wa korosho. Wakulima wa zao la korosho wanahitaji sana fedha, ili waweze kuinua mashamba yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Bashe unatoa pembejeo na viuatilifu bure kwa wakulima, lakini hivi peke yake havitoshi kwa sababu ili mkulima wa korosho aweze kufanya vizuri anahitaji fedha, kwa ajili ya palizi, maandalizi ya shamba. Mtu mwenye ekari kumi, mwenye ekari 15, yeye na mke wake hawataweza kulima bila kuwa na msaada wa mkopo. Kwa hiyo, tunategemea benki hii iwajali zaidi wakulima. Mtu mwenye ekari 10 au 15 hataweza kupulizia hivi viuatilifu unavyovitoa bure, kama hatakuwa na usaidizi wa watu wa kumsaidia, naye anahitaji fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kuokota korosho, Mheshimiwa Bashe umeshazungumza hapa, tunahitaji fedha ile, ndoo moja ya plastic ni shilingi 2,000. Kwa hiyo, mtu peke yake hutaweza kufanya bila kuwa na msaada wa wasaidizi. Kwa hiyo, benki hii ije kutatua changamoto zinazowakabili wakulima wetu, vinginevyo tutakuwa tunafanya kazi bure. Kwa hiyo, mimi nakushukuru sana Mheshimiwa Bashe kwa kuliangalia hili jambo kwa makini zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeangalia kwenye ushirika, huku ambapo ndiyo tunaenda kutia nguvu vyama vyetu vya ushirika, AMCOS. Kule chini au SACCOS zetu zinao watendaji ambao kwa kweli, hatuwatendei haki au hawatendewi haki, wanalipwa malipo madogo sana, Mheshimiwa Bashe. Hebu Wizara ikae iangalie hawa makatibu ambao ndiyo watendaji wakuu wa hizi AMCOS, uwezo wao wa malipo unafanana na kazi wanayofanya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Bashe watu hawa wanafanya kazi mwaka mzima, lakini unaweza ukashangaa, mtumishi wa AMCOS analipwa shilingi 100,000 kwa mwezi na kazi anayoifanya ni kubwa sana. Kwa hiyo, mimi ningeomba sana Mheshimiwa Bashe, hebu tukaangalie jinsi gani ya kuboresha mishahara ya hawa watendaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, hebu twendeni tukaiangalie sheria ya hivi vyama vyetu sasa hivi tubadilishe muda. Muda wao wa uongozi, kukaa madarakani, ni miaka mitatu. Mheshimiwa Bashe miaka mitatu kwa chama kufanya shughuli zake kikamilifu mimi naona hautoshi, anachaguliwa mwaka wa kwanza, akifika mwaka wa pili anawaza uchaguzi mwaka wa tatu. Kwa hiyo, kunakuwa na changamoto sana kwa hivi vyama kufanya shughuli za kimaendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hebu tufikie hatua, tufikirie jinsi ya kubadilisha muda, badala ya miaka mitatu twende miaka mitano, kama ilivyo katika hivi vyama vyetu vya kisiasa. Kwa kufanya hivi tutawezesha watendaji wetu wa ushirika kuweza kufanya kazi kwa uadilifu na kwa maangalizo makubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine Mheshimiwa Bashe kwenye kilimo mimi nakupongeza sana, umeeleza kwenye bajeti yako kwamba kilimo kimeweka ajira kwa maana ya chakula asilimia 100. Tunajitosheleza kwa chakula, ni jambo la kujivunia sana na siyo kwa Tanzania tu, hata Afrika Mashariki wanatutegemea sisi kwa chakula. Mimi nakupa hongera sana kwa hili, linachangia pato kubwa sana la Taifa, 26.3%; umezungumza kwenye bajeti yako kwamba kilimo kinachangia Pato la Taifa, karibu 26.3%, hili jambo ni la kheri, lakini 61.3% ya wananchi wake wanategemea kilimo. Nini matarajio yetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, matarajio yetu ni kwamba sasa nguvu kubwa uliyoielekeza sehemu nyingine, hebu nayo ilete upande wa Kusini. Mheshimiwa Bashe kule jimboni kwangu mimi sina mradi hata mmoja wa umwagiliaji. Ninalo Bonde kubwa la Mto Ruvuma, mwaka 2024 ulinipangia bajeti kule kwa ajili ya umwagiliaji, lakini hakijafanyika kitu. Nakuomba sana katika bajeti hii ya mwaka huu 2025 hebu tia macho kidogo utusaidie wananchi wa jimbo langu, ili waweze kupata mradi wa umwagiliaji, ila nakushukuru sana, umeleta miradi miwili ya umwagiliaji, kwa maana ya vyakula vya bustani, kule katika Kata ya Likokona na Kata ya Nangomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkandarasi yuko kazini; jambo hili ni la kheri na wananchi, naamini kabisa kuanzia mwakani wataona manufaa kwa kazi nzuri.

Mwisho kabisa, Mheshimiwa Bashe, mimi nakutakia kheri wewe, Naibu Waziri na watendaji wote kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuboresha zao letu la korosho na uchumi wa nchi yetu, ahsanteni sana. (Makofi)