Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Francis Isack Mtinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii ya kuchangia kwenye Wizara ya Kilimo, Wizara ambayo ndiyo tegemeo la nchi yetu kwa maana ya ajira, chakula, usalama na kila kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kutengeneza timu nzuri sana kwenye Wizara hii muhimu kwa kumuweka Mheshimiwa Bashe kuwa kinara wa Wizara hii. Mheshimiwa Bashe mimi ninamfahamu vizuri, ndiyo maana hata nilipokuwa Katibu Mkuu wa Vijana nilimuunga mkono awe Makamu Mwenyekiti wa Vijana Taifa, lakini bahati mbaya timu iliyokuwa inaongozwa na Mheshimiwa Ridhiwani wakatuzidi fitina wakatushinda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimpongeze pia Mheshimiwa Rais kwa kumpa timu Mheshimiwa Bashe ya watu wenye akili zinazofanana na Mheshimiwa Bashe. Naibu Waziri na Katibu Mkuu wanasababisha Wizara hii iende kwa kasi ambayo leo ushuhuda unaonesha kwa jinsi Wabunge wote ambavyo wanampongeza Bwana Bashe kwa kazi inayoonekana kwa macho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninataka tu niseme kwenye suala la umwagiliaji. Miradi ya umwagiliaji ni miradi ambayo inataka full package ikamilike ndipo uone matunda yake. Huwezi kuona matunda ya mradi wa umwagiliaji hata uwe na pesa nyingi kiasi gani kama uko nusu ama uko robo tatu ama uko robo. Kama ni maji kufika kwenye skimu lazima yafike, kama ni mifereji kwenda kwenye mashamba lazima iwepo ndipo uweze kuona matokeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zinazotakiwa kwenye umwagiliaji ni takribani kama shilingi trilioni 1.5; umwagiliaji peke yake. Hii ni zaidi hata ya bajeti nzima. Ninajua kwamba haiwezekani hivyo vitu vikafanyika kwa mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niiombe Serikali, kupitia Waziri wa Fedha, basi kile kinachopangwa kwenye mradi wa umwagiliaji kwenye bajeti husika kiende chote kwa sababu zile phase ambazo zimepangwa kwenye miradi hii, kama zitakuwa zinaenda kwa utimilifu baada ya miaka kadhaa tutaona matokeo makubwa sana ya miradi hii ya umwagiliaji. Haya yanayoonekana kwa sasa bado ni cheche tu, kama miradi yote ya umwagiliaji itakwenda kama ilivyopangwa nina hakika kwamba nchi yetu itailisha dunia.

Kwa hiyo, mimi ninaomba sana Wizara ya Fedha katika kutoa zile fedha kwenye Wizara mbalimbali, pesa zinazohusu umwagiliaji ziende zote ili matokeo yaonekane kwa sababu kilimo hiki kwanza kinaongeza mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukichukulia tu mazao ya horticulture yameongeza pesa nyingi sana za kigeni. Mwaka 2020 tuliuza kama dola za Kimarekani milioni 290, lakini mwaka 2024 zimekwenda mpaka karibu dola za Kimarekani 590, kwenye mazao tu ya horticulture. Sasa kama miradi ya umwagiliaji yote itaenda vizuri maana yake ni mazao haya yataongeza fedha kiasi gani. Kwa hiyo, mimi ninataka tu nisisitize na kuiomba Serikali, fedha zote za umwagiliaji zinazopangwa kwenye bajeti ya kila mwaka ziende zote ili haya matokeo ambayo tunategemea yatakuwa ya ajabu sana yaweze kufanyika haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikushukuru sana Mheshimiwa Bashe kwa jinsi ambavyo umelitendea jimbo langu. Kuna mabonde zaidi ya 900 ambayo yanatakiwa yapate umwagiliaji, lakini kwa upaendeleo maalum umenipatia shilingi bilioni 34 kwenye jimbo langu mradi wa msingi unaendelea vizuri, mifereji karibu yote ya urefu wa kilometa sita tayari na midogo inaendelea, lakini bwawa umeliongeza kutoka maji ya ujazo wa lita bilioni tano sasa linakwenda lita bilioni 12.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo la pekee, vijiji karibu vinne; Kijiji cha Kibi, Kijiji cha Msingi, Kijiji cha Nduhumo, Kijiji cha Inshinsi, wananchi takribani 12,000 wanakwenda kunufuaika na mradi huu. Nilikuja ofisini kwako nikakuomba uniongeze miradi miwili mikubwa, Bonde la Tatazi na Bonde la Mwangeza, umekubali na leo hii kuna consultant wa continental anafanya upembuzi yakinifu katika Jimbo la Mkalama. Ubarikiwe sana rafiki yangu, wewe unataka niendelee kuwa Bungeni na wananchi wa Mkalama watanirudisha kwa sababu wanajua unaendelea kunipa miradi ambayo inawanufaisha na kuwaondoa katika umasikini. Wananchi wa Mkalama huko mliko mjue kabisa Mheshimiwa Bashe ananilinda na miradi analeta, ninyi nirudisheni Bungeni ili mbadilishe maisha yenu. Ubarikiwe sana ndugu yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana, jambo la bajeti, kama nilivyosema kwenye horticulture msiliache, lakini Mheshimiwa Bashe mazao ya horticulture naomba utupie macho kwenye suala la embe. Kama parachichi na mazao mengine yameongeza kiwango cha pesa mpaka kufikia dola milioni 500 ninahakika ukitupia jicho la pekee kwenye embe, tena embe ina upendeleo maalum kwa sababu jimbo lako na mkoa wako wa Tabora watu wanalima embe. Wapo watu wengi sana wameitikia mwito wa kulima embe, naomba uliangalie kwa jicho la pekee zao hili, hakika kwa nguvu ambayo unaipeleka kwenye mazao mengine, ukipeleka robo tu, kidogo, kwenye zao la embe pesa nyingi sana za kigeni zitaongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuombe sana katika mipango yako, Mheshimiwa Bashe zao la embe na mazao ya horticulture kwa ujumla ni high values ambayo ina thamani kubwa sana. Zao dogo tu, lakini kiasi kidogo tu kinaleta fedha nyingi sana za kigeni kwa hiyo, nikuombe sana hili ulishughulikie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilitaka niseme tu kuhusu hili la bajeti na nikupongeze kwa kazi kubwa na nimpongeze Rais wangu kwa kukupanga. Ninaamini utarudi na kama atapenda atakuacha kwenye Wizara hii kwa sababu ndiyo Wizara yenye roho ya nchi na utaendelea kufanya mambo na Watanzania wataendelea kunufaika. Mungu akupe maisha kijana, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)