Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Innocent Sebba Bilakwate

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyerwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu. Awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia kuweza kufika wakati huu na kuchangia Wizara hii muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa mapinduzi makubwa ambayo ameyafanya kwenye kilimo. Kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Bashe pamoja na timu yake kwa kazi kubwa, nzuri na ya kipekee ambayo wanaifanya kwenye nchi yetu kupitia kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine tunapopongeza hapa watu wanasema sijui wengine ni chawa, sijui ni nini lakini tunasema vitu ambavyo vimefanyika. Mimi nianze kusema, Mheshimiwa Bashe wewe ni kijana wa pekee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakumbuka mwaka 2022 nimezungumzia sana suala la kahawa. Ninakumbuka Mheshimiwa Bashe ulisema sasa tunaamua kupambania kahawa. Mheshimiwa Bashe mimi ninakosa maneno mazuri ya kusema zaidi ya kusema Mungu akubariki pamoja na timu yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kahawa ya Kyerwa na Mkoa wa Kagera, wakulima walikuwa wanapangiwa bei; anayeamua kupanga shilingi 800, anayeamua kupanga shilingi 1,100, lakini tulipoongea Wabunge, Mheshimiwa Bashe ukasikia na ukasikiliza maelekezo ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kahawa ikakusanywa kwenye ushirika, kahawa ikaanza kuuzwa kwenye mnada. Mheshimiwa Bashe kwa kweli mimi niseme haya ni maajabu. Kahawa imetoka shilingi 800 mpaka 1,100 tulizokuwa tunapangiwa leo hii kahawa mwaka jana imefika shilingi 6,500; haya ni maajabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima hawa ambao walikuwa wananyonywa, ambao walikuwa wanafanyiwa vitu vya hovyo lakini kupitia kwako na kwa Mheshimiwa Rais leo hii imewezekana. Mheshimiwa Bashe tunakuombea, tunakutakia kila la kheri na haya uliyoyafanya umeyafanya kwa wakulima ambao walikuwa maskini. Mimi nikuhakikishie unapotenda mema hakika Mungu hatakuacha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajua ilikuwa ni vita kubwa sana. Wakati tunapambana kuhakikisha kahawa inauzwa kwenye minada ilikuwa ni vita, walikushawishi, walileta maneno ya kila namna kuhakikisha unakata tamaa, lakini Mheshimiwa Bashe hukukata tamaa, ulisonga mbele na sisi Wabunge tukaendelea kukuunga mkono, leo hii tunayaona mafanikio makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kahawa kwa Mkoa wa Kagera ndiyo siasa, ndiyo kila kitu. Unapogusa kahawa unagusa maendeleo, unagusa uhai wa Wana-Kagera na vita hii usifikiri imeisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii mimi niwaambie baada ya mimi kupambana kuhakikisha kahawa inauzwa kwenye mnada na Serikali ya Mama Samia ikasikia, vita inayoendelea Kyerwa siyo ya kawaida. Ninapowaambia leo, siku ya leo, hao waliokuwa wanawapangia bei wakulima wamezunguka kwenye kata zote kuhakikisha wanakutana na mabalozi na wajumbe wao, viongozi wote kuhakikisha wanawahonga pesa huyu Mbunge ambaye amepambania kahawa asirudi Bungeni. Hata hivyo, mimi ninaye Mungu anayenipigania na ninajua kama Mungu aishivyo ninarudi hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vita hii sitasahau kumpongeza Mkuu wa Wilaya pamoja na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama, wamefanya kazi kubwa. Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa Mheshimiwa Fatma Mwasa, mama huyu ni mpambanaji, amehakikisha kahawa ya Wana-Kagera inaendelea kunufaisha na kuleta tija kwenye Taifa letu. Kwa kweli tunampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kahawa kwenda kwenye minada, sasa kuna mbinu nyingine wamekuja nayo. Bado biashara ya butura inaendelea. Wanachofanya hao wanunuzi wakubwa wanapeleka pesa kwa mawakala wao na wameanza kununua kahawa kupitia hii na hili nithibitishe sitataja, lakini itafika wakati nitasema. Kuna kiongozi mmoja aliyeaminiwa, mwaka jana kahawa imekamatwa magari zaidi ya sita, kahawa ambayo haioneshi imepitia kwenye AMCOS yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo wamekuja nalo, wanasema hao wakulima ambao wako karibu na mipakani tupeleke hela cash ili wasipeleke kahawa Uganda. Sasa wanachokifanya, mimi nilikwenda kwenye Kata ya Murongo mwaka jana nikakuta wakulima hawa wanapewa cash shilingi 3,200 lakini kwenye mnada ilikuwa ni shilingi 4,500. Niliposema nikampigia Mrajisi. Mrajisi akasema tunalifuatilia na nikamwambia kiongozi mmojawapo ambaye huyo ndiye kinara wa kufanya hiyo biashara. Sitamtaja tu, wakati ukifika nitasema tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima ya chama changu na nidhamu sitamtaja, lakini kilipotokea mimi nikasema lazima wananchi wapewe bei ambayo iko kwenye mnada. Baada ya kusema, kiongozi huyo anasema Mbunge anafuatilia biashara yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimechaguliwa na wananchi kuhakikisha ninawatetea wananchi wangu, kuhakikisha ninaipambania Serikali yangu kahawa isiende Uganda na wananchi hawa wapate bei nzuri, hiyo ndiyo kazi niliyotumwa. Nitahakikisha ninaifanya, sitaogopa wala sitayumbishwa na siko tayari mimi kama Mbunge kuwekwa kwenye mfuko wa mtu mmoja kuona wananchi wangu wanateseka, wananchi wangu wanapewa bei ya hovyo. Kwa hiyo, hili nitapambana nalo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sana Mheshimiwa Bashe, amefanya mambo makubwa kwenye kahawa. Sasa kahawa yetu, mimi bado ninamini tunaweza kupata bei nzuri zaidi ya hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kahawa tunayoipeleka nje tunapeleka ghafi. Sasa Mheshimiwa Bashe nimeona unasema kuanzisha viwanda vya aina gani, lakini sasa tuombe, tafuta wawekezaji wakubwa wawekeze kwenye viwanda vikubwa vya kahawa. Kahawa yetu ichakatwe hapa ili na sisi twende kuuza nje kahawa ambayo imechakatwa hapa ambapo itakuwa imeongeza bei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Mheshimiwa Bashe, kahawa yetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, muda wako umeisha, tafadhali.

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)