Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Venant Daud Protas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igalula

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuwa mmoja wa wachangiaji leo katika bajeti ya Wizara ya Kilimo ambayo bajeti hii inawagusa wananchi wetu moja kwa moja hasa sisi tunaotoka maeneo ya vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze na mimi kuungana na Wabunge wengine wote walioanza kuchangia tangu asubuhi kumpongeza Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili niipongeze Wizara ya Kilimo ikiongozwa na ndugu yetu Mheshimiwa Hussein Mohamed Bashe, Mbunge wa Nzega Mjini, Mheshimiwa David Silinde, Katibu Mkuu na timu yote ya Wizara. Kwa kweli mwaka 2020 tulikuwa tunaingia hapa sisi Wabunge wapya, miongoni mwa Wizara ambayo ulikuwa ukiingalia iko hoi, ukimuangalia Waziri yuko hoi, watumishi hoi ni Wizara ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unamkuta Waziri hoi, Wizara hoi, wakulima hoi, ndiyo hii Wizara ilikuwa inaonekana hivyo mwaka 2020, lakini kwa sasa hivi unaweza kwenda hata shamba umevaa suti. Hii Wizara ndiyo imetupa mfano kuona mkulima namba moja anakwenda kukagua wakulima ana uniform ndiyo maajabu hayo, ndiyo mabadiliko hayo yameanza kwa kasi. Kwa hiyo, nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa na umeleta reform nzuri ambazo wananchi wanaziona moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na bajeti ya shilingi bilioni 200 mwaka 2020, leo tumefika shilingi trilioni 1.2. Hayo ni mapinduzi ya kijani na hapa maana yake ni nini? Mheshimiwa Rais ameona mbali sana, amesema tukiwekeza kwenye kilimo, kwa sababu wanasema kula ni lazima kuoga ni hiyari, ndiyo hii kwa sababu kuoga unaweza ukachagua siku gani nioge au nisioge, lakini kula lazima utakula hakuna siku ambayo utachagua leo nisile. Hata wale ndugu zangu wanaofunga wanakula daku ndiyo wanafunga asubuhi. Kwa hiyo, hii ni Wizara ambayo inakwenda sana kuwagusa wananchi kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais aliona mbali kwa sababu tukizalisha chakula kingi, tutajilisha wenyewe na tutalisha mataifa mengine. Yale mataifa ambayo ni wavivu kulima wenyewe kila siku wanashinda kwenye TikTok, sasa watakuwa wana njaa. Wakati sisi tunalima wenyewe wako kwenye TikTok, kwa hiyo wakati wanataka kula sisi tutakuwa na chakula tutakwenda kuwauzia na Serikali yetu na nchi yetu tutapata fedha za kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi ninawashukuru na hii bajeti ninaiunga mkono kwa 100% na Mheshimiwa Waziri ukimaliza tu anza kutekeleza majukumu yako bila kusubiri kelele za watu wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuipongeza Wizara kama nilivyosema, lakini niseme jambo moja ambalo ninataka nishauri. Jambo la kwanza Mheshimiwa Waziri, hebu simamia vizuri, umesimamia kote, hizi mbegu kwa nini zinakuwa kila siku bei haieleweki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuja hapa na swali la msingi, Mheshimiwa Silinde akanijibu majibu ambayo ukienda kwenye uhalisia hayaendani kabisa, akaniambia bei elekezi ya mbegu gani haizidi hata shilingi 14,000 lakini ukienda mtaani inafika mpaka shilingi 30,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima kule wanalalamika na sisi tumewaambia mbegu bora ili tupate mazao ya uhakika tulime mbegu za kisasa. Sasa mbegu za kisasa tumewaletea umaskini, unanunua mbegu shilingi 30,000 unaenda kupata gunia 20 sawa, lakini unakuja kumuumiza wakati anaenda kununua mbegu hana fedha yule mkulima. Mimi niombe kwenye Wizara hii, mwaka huu tunakupitishia bajeti, nenda kadhibiti mfumuko wa bei holela kwenye mbegu. Hilo ndilo jambo la msingi, nenda ukalianzie moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Taasisi ya ASA; nilikuwa leo na DG pale nimemwambia mzee kama una tatizo sema wakubwa ndio hawa. Sasa mimi niwaambie wekezeni pale huyu mzee apate fedha tuzalishe mbegu za kisasa. Tuna watu wa utafiti kule, TARI na nani wapeni fedha tumalize mambo yetu, achaneni na mbegu za kutoka nje anaangalia mwaka huu Tanzania tuwapelekee kwa shilingi ngapi, anakadiria akiwa huko amekaa kwenye computer. Hilo ninaomba mkalisimamie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la mbolea ya ruzuku mmefanya kazi nzuri, mwaka huu mmeleta kwenye vijiji. Ninaomba ongeza kasi, peleka mbolea kwenye vijiji na vitongoji ili wananchi waweze kupata vizuri mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake ya bajeti amesema vizuri sana, mwaka huu ana mpango angalau kwenye halmashauri tuwe na mashamba ya pamoja (BBT). Kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Uyui tulitenga hekari zaidi ya 17,000 tangu mwaka 2021 tunataka tulime korosho. Baraza la Madiwani limepitisha, wewe ukaja ziara ukiwa Naibu Waziri ukatuahidi trekta halijaja mpaka leo. Sasa mimi nikuombe ule mradi umekwisha changamka, mimi nikuombe kwenye bajeti hii usitusahau Mradi wa Kalangasi kuhusu korosho ambao tuliupitisha katika halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kuna mradi wa bwawa ambalo mimi nikushukuru sana. Hili bwawa mimi nimeanza kulisikia tangu niko darasa la nne na sasa nimekuwa Mbunge nimekwenda kulikwamua Bwawa la Goweko na wewe ulinipa heshima ulikuja.

Mimi nikuombe kwenye taarifa leo umeniambia lile bwawa liko 50%, ukienda physical kule wanasema 98%, wote mnachanganya taarifa. Mimi nikuombe, mkandarasi amepatikana advance payment inahitajika, mzee wa umwagiliaji anasubiri tu fedha umuingizie aende akasimamie kule kwa sababu na yeye mwenyewe ni mtu wa mjini anaweza kwenda kumsimamia mkandarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, Mheshimiwa Waziri, mimi nikuombe; Serikali ina mpango mzuri wa kuwasaidia wakulima wake katika kilimo cha miwa. Kwenye jimbo langu umeniletea kilimo cha miwa ambacho nilikwenda kuongea na wananchi wa Kata za Loya, Miswaki na kwingineko huko ambako ulipeleka wataalam wako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule wananchi wamekwisha niambia wenyewe hawahitaji kilimo cha miwa, wanahitaji kilimo cha mpunga kiimarishwe. Sasa mimi niombe wale wataalam ambao wanakwenda kila siku kuweka beacon kule, hebu toa maelekezo kwanza. Wale wananchi kama tunahitaji mradi twende tukashirikiane na wananchi tuwaeleweshe kwa utaratibu kuliko sasa hivi inavyokwenda kule nani hajui, wananchi hawajui, Mbunge hajui, Diwani hajui.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali…

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niombe kwenye kilimo cha miwa kule kwenye maeneo yetu ya Bonde la Loya, wananchi wamenituma na mimi ndiye mwakilishi wa wananchi, wamesema kwa sasa wanahitaji kulima mpunga na siyo miwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Waziri, kwenye hili ninaomba uniunge mkono ili wananchi wasipate taharuki kwa yanayoendelea katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)