Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi jioni hii ili nami niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisiwe mchoyo wa fadhila nami niungane na wenzangu ambao wamekuwa wakiendelea kutoa pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Bashe, Mheshimiwa Silinde pamoja na Katibu Mkuu na timu nzima ya Wizara ya Kilimo. Kikubwa kinachonifurahisha kwenye Wizara hii ni namna ninavyowaona Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na Katibu wanavyokuwa na ushirikiano mzuri na mafanikio yoyote panapokuwa na ushirikiano lazima muweze kufanikiwa kwa hiyo kwa hilo nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina yangu jioni hii, ninafahamu muda nilionao ni mchache, lakini kuna vitu ambavyo ninatamani kuongelea. Kwanza ningependa kuanzia kwenye zao la parachichi, niseme tu kwamba tunapongeza Wizara kwa hatua ambayo imeendelea kuchukua ya kuzalisha miche ya parachichi, lakini pia kuwezesha sekta binafsi kuanzisha uchakataji wa rejects yale maparachichi ambayo yalikuwa yanaonekana reject, kwetu tuna mwekezaji ambaye ni Lima anatusaidia sana kupunguza hiyo burden ya maparachichi ambayo yanakuwa hayajafikia viwango vya ubora wa kusafirisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati nilifanikiwa kumtembelea na alinipa uhitaji wake akaniomba niwasilishe kwa Wizara, nilijaribu kufikisha ujumbe, lakini kupitia forum hii ningependa pia kuomba kwamba Mheshimiwa Bashe na timu yako nzima tazameni namna ya kumsaidia Lima katika kutumia ile fursa vizuri kwa sababu kuna production ya mafuta sawa, lakini kuna bidhaa zingine ambazo zingeweza kuzalishwa ikiwemo mbolea baada ya ule mchakato wa kutoa mafuta kwa ile takataka inayokuwa imebaki. Kwa hiyo hilo pia naomba alinituma niwaombe, kwa hiyo, nawasilisha ombi lake kama lilivyo naomba mlipokee Mheshimiwa Bashe na timu yako nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nilikuwa na wazo dogo kwenye eneo la ufuta kwa maana ya kwamba tukiwekeza kwenye private sector kama ambavyo tumefanya kwenye kuwanusuru wakulima na hizo rejects za parachichi tufanye processing ya ufuta, tumekuwa tunaisafirisha kama ilivyo, tunafahamu kama ingefanyiwa mchakato wa uchakataji nchini ufuta ungeweza kuongeza ajira kwa watu wetu kwa eneo kubwa. Kwa hiyo, tujaribu ku-shift kutoka kwenye eneo la kusafirisha malighafi hii ya ufuta kama ilivyo, tui-process iwe angalau kwenye final product or semi final product ili iweze kwenda ikiwa imewasaidia wananchi wetu. Pia tunafahamu hata zile pumba tu zinazokuwa zinabaki zinaweza zikawa tija kwa uzalishaji kwenye eneo la mifugo, kwa hiyo hilo pia nilitamani niwasilishe hilo ombi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuwapongeza tena kwenye eneo la BBT. Kitendo tu cha kuwa na maono ya uanzishaji wa BBT mimi kwangu niseme tunafarijika kuona kwamba kweli Wizara ina dhamira ya kuwakomboa vijana, wanawake na watu wengine ambao wanakuwa na uhitaji. Ninataka tu niseme kwamba nilifanikiwa kupitia taarifa vizuri, nikasikitika tu eneo dogo kuona Mkoa wa Songwe na ukubwa wake hakuna shamba hata moja la kwenye Mradi wa BBT, kwa hiyo hili pia ninaiomba Wizara, ninamuomba Mheshimiwa Waziri na timu yake hebu angalieni namna ya kuanzisha shamba hata moja kwenye Mkoa wa Songwe la BBT, kwa sababu tunayo maeneo makubwa na sisi ni wakulima wakubwa na kwa kufanya hivyo utakuwa umewanusuru vijana na wanawake wa Mkoa wa Songwe, kwa namna moja au nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli kwa kufanya hivi utakuwa umewanusuru vijana na wanawake wa Mkoa wa Songwe kwa namna moja au nyingine. Hili ni ombi langu sasa mimi kama Mbunge, nikuombe Waziri na timu yako mtusaidie hata kuwa na mashamba. Mkiweka hata moja moja kila wilaya au hata moja tu kwenye Mkoa wetu, utakuwa umetusaidia sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuwasilisha ombi hilo nirejee kwenye Mfuko wa Pembejeo. Nilipata nafasi ya kutembelea katika Mfuko wa Pembejeo katika dhamira ya kuona kwamba wananchi wa Mkoa wangu wa Songwe wananufaikaje na Mfuko wa Pembejeo (AGITF) kwamba kuona ni namna gani wananchi wangu watanufaika. Nikaenda at least kuomba watufanyie mafunzo, niwaite kwenye mkoa wangu wafanye mafunzo. Changamoto tuliyokutana nayo ilionekana hawana bajeti kwa ajili ya utoaji wa mafunzo kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmewapa pesa nyingi ambapo mmeweza kutoa kwa bajeti ya mwaka 2024 mmetoa shilingi bilioni 5.7 out of ten billion lakini kwenye takwimu hizo hizo ilionesha kwamba ni wananchi 49 tu ndiyo waliopata mkopo ambao nao una thamani ya shilingi milioni 503.
Sasa Mheshimiwa Waziri kwa sababu wewe ni mtu wa matokeo na ungependa kuona mambo yanakuwa na tija, mmeweka pesa nyingi ambayo haijaenda kwa wananchi. Mnafanya nini kuhakikisha fedha hizi ziende kwa wananchi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu; kama vile tunavyowekeana malengo kwenye maeneo mengine kwamba tunakuomba mwalimu uhakikishe umefikia lengo hili basi na wewe weka malengo kwenye taasisi hii ionekane kwamba kila mkoa at least waweze kukopesha hata watu 50. Kwetu sisi kama wananchi tunaona kwamba itakuwa na faida, lakini Mheshimiwa Bashe huwezi ukaniambia nchi hii kwa mwaka mzima wakopeshwe watu 49 tu. Mimi sioni kama tunakuwa na dhamira kweli ya dhati ya kuwakomboa wananchi. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Bashe kwenye hili utusaidie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi tuna shida na hizi fedha, mashamba tunayo, dhamana tunazo na tuna uwezo wa kuonesha tija kwenye maeneo haya. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, ninaomba kwenye eneo la mfuko wa pembejeo muwekeane malengo, kila mkoa ulete watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kibaya zaidi hata maafisa kilimo tukiwauliza kwenye maeneo yetu hawajui kwa habari ya Mfuko wa Pembejeo, wanakuwa wanakushangaa tu unapokuwa unaongelea suala hili.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru. Nilikuwa na mengi ya kuongea lakini niseme tu tuna imani na Wizara hii na tuna imani na waliopewa kusimamia Wizara hii na tunaendelea kuwaombea Mungu aendelee kuwatunza ili wafanye kazi nzuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)