Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipatia nafasi na mimi kuchangia katika hoja ya bajeti ya Wizara ya Kilimo, kilimo ni uti wa mgongo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetujalia kupata afya njema na kuwepo hapa na sisi ni wawakilishi wa wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa hekima, utulivu na amani aliyoijenga katika nchi hii na kuleta kuheshimiana ndiyo tumefika hapa, nchi ambayo haina utulivu hata kilimo hakiwezi kufanya kazi, lakini kwa hekima yake ameifanya hii nchi imekuwa na hekima na kuwachagua vijana hawa, mimi nilikuwa nao Kamati ya Bajeti nawajua vizuri sana, namjua Mheshimiwa Bashe, namjua Mheshimiwa Silinde tulikuwa wote Kamati ya Bajeti, kwa kweli walikuwa wanafanya kazi kubwa sana na mimi napongeza sana, kazi zenu zinaonyesha sasa hivi kwamba ninyi ni vijana mnakwenda na 4G, ni vijana wa digitali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Katibu Mkuu Ndugu Gerald Mweli na watendaji wenzake wengine. Mimi kwa heshima ya Mkoa wangu wa Lindi na Mtwara na Ruvuma ambao ni wakulima wa korosho tunasema ahsanteni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli korosho ilichezewa kwa muda mrefu, kwetu korosho ilikuwa ni vita ya kiuchumi, watu walikuwa wanahakikisha wananunua korosho kwa bei ya kutupa, kilo moja shilingi 600 wakapandisha mpaka shilingi 2,000, lakini hata hiyo unapata kwa bei nusu nusu hauipati yote. Sisi ndiyo wa kwanza kuanza na stakabadhi ghalani, lakini tuseme kweli ya Mwenyezi Mungu leo korosho tumefikia zaidi ya shilingi 4,050 kutoka shilingi 1,200 zao ambalo lilikuwa linachezewa mpaka kufikia hapo tunasema ahsanteni, wakulima wanaheshimika huko nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili tumepewa ruzuku ya pembejeo za viuatilifu bure, tuseme nini sisi wakulima zaidi ya kuongeza kilimo tu. Zao la ufuta lilishakufa, leo kila mtu/watu wanahama huko Sikonge, wanahama Tabora, Mwanza wapi watu wote wanakimbilia Lindi kwenda kulima ufuta, kwa vile kule kwanza tunapata ufuta ambao ni bora, hii yote ni kwa ajili ya kuwa kuna utulivu, kuna amani, kuna kuheshimiana na hata hivyo mazingira bora yamewafanya watu waweze kulima kule Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona katika hii bajeti mahindi yameongezeka, mchele umeongezeka, korosho imeongezeka, kahawa imeongezeka, miwa imeongezeka, tunataka nini zaidi ya kumuomba Mwenyezi Mungu na kumshukuru! Usiposhukuru kwa kidogo basi hata kwa kikubwa huwezi kukishukuru, maana yake leo wale wakulima, mimi ni mtoto wa mkulima, lakini mimi mwenyewe ni mkulima, ninalima alizeti na ninalima mahindi, nasema Mwenyezi Mungu haya tunayoyaona yazidi kuongezeka, tuna nafasi kubwa ya kuongeza ili kilimo hiki tutakachofikia 4.1% kiweze kuongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la matrekta; nimeangalia matrekta yamegawiwa gawia Tanzania nzima Mkoa wa Lindi na Mtwara haipo. Hakuna haja ya kugawa sungura nusu nusu, kama ni maendeleo yasiwe ya kibaguzi baguzi, Mkoa wa Lindi pia tunataka matrekta. Nimeongea na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wenzangu, Kilwa walishaomba BBT lakini hawakupewa trekta hata moja, sasa tunataka vijana wa Kusini ambao walikuwa ni wazururaji wa hovyo hovyo nao wafikiriwe kupelekewa matrekta ili na wao waweze kuendeleza suala la kilimo kwa ubora wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia heshima kubwa anayotupa Mheshimiwa Rais ni kubwa lazima tuseme ahsante Watanzania. Leo unaona vurugu za kiuchumi hizi, economic crisis ambazo tunaziona economic interference, business interference, colonialisation interference hizi zote ni kwa ajili ya uchumi tu. Sasa hivi tunasema tumepata vijana mahiri ambao wameweza kusimama na ma-tycoon, ma-tycoon hawa wametajirika sana na nchi yetu lakini hawajatujengea hata shule, hawajatujengea hata hospitali, hawajatupatia hata ile hela wanayoipata wakawa matajiri kusema watatunufaisha Watanzania, wao ni kuchuma na kwenda mbele hatukubali!

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tumefikia mahali ambapo tunampa mzigo mzito huyu kijana kuwa wale kwanza hawatakubali kumuona mtu anakuwa strong kama vile. Kijana yeyote wa Kiafrika, Kitanzania akiwa strong lazima akutane na crisis! Nawaombeeni Mwenyezi Mungu atawapa ulinzi na wale wanaojifanya nchi hii wanaichezea wanavyotaka tumefika mahali tunasema enough is enough. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wajiulize wanafanya biashara kubwa kwa kutumia uchumi wa Tanzania tumenufaika nini na wao zaidi ya wao kututaka wanunua vitu kwa bei ya chini na kwenda kunufaika huko nje? Leo tunataka ulimwengu wa viwanda vya korosho viwepo Mtwara. Mheshimiwa Bashe ukae na Mheshimiwa Waziri wako wa Viwanda una uwezo wa kufufua viwanda vyetu. Lindi hakuna kiwanda hata kimoja, lakini viwanda vile ni ajira tosha kwa watu wa Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaizungumzia Nachingwea; wakati wa ukoloni walipima lile eneo wakakuta ardhi ya Nachingwea ni kwa ajili ya kilimo cha soya, ardhi ya Nachingwea ilikuwa ni ardhi mojawapo fertile mpaka ilitolewa treni kutoka Mtwara mpaka Nachingwea, maana yake nini? Ni kuhakikisha Nachingwea yenye maendeleo ya kilimo, inawezekana mkakae chini mjiulize tunafanya nini kuisaidia Nachingwea kuna farm one mpaka farm 17 ambayo waliacha wakoloni, yako pale mpaka sasa hivi. Tunaomba yale mashamba sawa suala la zao la soya ndiyo linastawi sana Nachingwea. Soya, karanga, mahindi ni matumaini yangu haya mazao ambayo tunayazungumzia sasa hivi tutazidi kuboresha na kuweza kuwapa kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu biashara ya soko, Mheshimiwa Bashe wewe ni mwanangu, ni marafiki zangu, naomba tutengeneze ujirani mwema kati ya Tanzania na Comoro. Comoro ni nchi ya jirani, tukitegemea masoko ya nje yakitukatalia sisi tutakuwa tumekwama na mazao yetu. Comoro ni watu ambao wana asili ya Kusini, chakula chetu ni kimoja, mazao yetu yanafanana, kaa chini na Mabalozi, Balozi Yakubu na nchi ya Comoro tuone tunafanya nini ujirani mwema kwa kuwapelekea chakula, maana yake Comoro yote unayoiona wanategemea chakula kutoka Tanzania Bara, hivyo tukifanya mradi ule wa Mtwara na Lindi kupeleka bidhaa zetu Comoro utatujengea uchumi bora katika Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia katika miradi ya umwagiliaji nimesoma toka mwanzo mpaka mwisho kwa muda mfupi bado tunahitaji umwagiliaji Kusini. Kuanzia Mto Rufiji, Mto Mwenkuru, Mto Matandu, Mto Ruvuma ni maeneo yenye mito tunahitaji umwagiliaji wa kutosha.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Mbunge.

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana Mwenyezi Mungu awabariki, naunga mkono hoja. (Makofi)