Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa jioni hii ya leo. Kwanza kabisa nichukue fursa hii adhimu kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maono yake na kiu yake katika kuhakikisha kilimo cha Watanzania kinakua na wakulima wa Tanzania wanapata tija katika mazao yao na kuinua uchumi wa nchi kupitia sekta hii ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza viongozi wa Wizara hii nikianza na Waziri wa Kilimo, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Makatibu wote pamoja na watendaji wote wa Wizara hii katika kuhakikisha wanalisaidia Taifa na wanawasaidia wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo mdogo wangu Mheshimiwa Bashe ni zawadi kwa wakulima wadogo wa nchi hii, nasema hivyo kwa sababu anajitoa maisha yake na usalama wa maisha yake kukabiliana na kuwasaidia wakulima hawa wadogo wanaodhulumiwa kwenye viuatilifu, kwenye kununua mbegu fake na mambo mengine yanayohusu sekta ya kilimo ambao anapambana na wahalifu hao, Mwenyezi Mungu ndiye atayekupa ulinzi.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea napenda pia kuwapongeza eneo ninaloliwakilisha, Taasisi Zisizo za Kiserikari kwa juhudi kubwa anayofanya kushirikiana na Serikali katika kuinua sekta ya kilimo, kuwasaidia wakulima kwenye elimu, kwenye mafunzo pia kuwajengea uwezo na kusimamia kilimo na hasa kilimo ikolojia, mbegu za asili, viuatilifu vya asili na mambo mengine yanayohusu kilimo pamoja na kuwatafutia masoko, wanafanya kazi kubwa sana kushirikiana na Serikali, wana haki ya kupongezwa na wao kwa mchango wao mkubwa kwa wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea na mchango wangu kuhusu huduma za ugani Serikali imejitahidi sana kuwawezesha, kuwajengea uwezo, kuwapa vifaa watu wetu hawa, wafanyakazi wetu hawa Maafisa Ugani, naomba tuendelee kuwajengea uwezo kuwapa elimu na mafunzo mbalimbali ili kukabiliana na changamoto mpya zinazojitokeza kila siku kwenye sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa ujenzi wa viwanda vya mbolea, lakini pia naendelea kushauri tuendelee kuwekeza zaidi kwenye viwanda vya mbolea tuwajengee uwezo wananchi wetu wa ndani ya nchi waweze kuwekeza kwenye viwanda vya mbolea pamoja na mbolea hizi za asili viwanda vidogo vidogo huko vijijini kwenye mashamba yetu sekta hii ipewe kipaumbele, kwa sababu kuimarisha sekta ya mbolea, kuimarisha sekta ya mbegu, kuimarisha sekta hii ya viuatilifu ni usalama wa chakula, lakini pia ni usalama wa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mbegu za asili naomba sera, sheria zitambue urithi huu wa mbegu za asili na kuwe na benki maalum ya mbegu za asili pamoja na mabenki hayo ya mbegu za asili, tuone na mpango kazi wa muda mrefu wa kuwa na mabenki haya kwenye maeneo, kwenye Wilaya hata kufikia kwenye eneo la kata. Kuwe na utafiti, uongezwe utafiti kwenye mbegu hizi za asili kuona virutubisho vyake na viini lishe vyake ili mtakapopata sasa uhakika mbegu hizi ziendelee kuzalishwa kwa wingi, zisambazwe kwa wananchi na zipewe ithibati kwa muda muafaka ili ziweze kutumika badala ya kufanyiwa utafiti zikabaki tu kwenye store na kwenye maghala, zipewe ithibati, wakulima weweze kutumia pamoja na kutoa mafunzo zaidi kwenye kilimo ikolojia kwa maana kilimo hai na kilimo hifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upotevu wa mazao; Serikali imejitahidi sana kujenga maghala na vihenge kwa ajili ya kuhifadhi mazao, naipongeza Serikali, lakini pia nashauri Serikali kwa wale wakulima wadogo wadogo wanaoweza kuhifadhi magunia 10 mpaka 100, kuna mifuko hii ambayo inaitwa hermetic haitumii kemikali, inahifadhi kwa kutumia viuatilifu vya asili hakuna kemikali kwenye hii mifuko, lakini bei yake ni kubwa sana ni shilingi 5,000. Tuone sasa namna ya kufanya kupunguza kodi ili mifuko hii iwe na bei nafuu wakulima waweze kuitumia na kuhifadhi mazao yao na kuepukana na ile adha ya kuharibu mazao yao bila ya muda muafaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nampongeza Mheshimiwa Makamu wa Rais nampongeza na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa maana hawa ni wasaidizi wakuu wa Mheshimiwa Rais, wanavyomtia moyo na wanavyompa support katika kuhakikisha kilimo cha nchi hii kinafanikiwa. Tunapoomba kwamba Wizara hii iongezewe bajeti, tunaipongeza Serikali kwa kuwa kila mwaka sasa hivi tunaongeza bajeti kwenye sekta hii ya kilimo na tuna kila sababu ya kuendelea kuiombea bajeti Wizara hii iongezeke ili kufikia mafanikio tunayoyatarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema baadhi tu ya mafanikio ambayo tunapoomba bajeti yanafanyiwa kazi, kwa maana sasa kuna ongezeko kubwa la ujenzi wa mabwawa ya umwagiliaji na uchimbaji wa visima, ongezeko kubwa la ruzuku ya mbolea, mbegu na viuatilifu, ongezeko kubwa la maghala na vihenge, ongezeko kubwa la bei ya mazao ya wakulima, ongezeko kubwa ya matumizi ya dhana bora za kilimo, ongezeko kubwa la kuwapatia vitendea kazi maafisa ugani wetu, kuanzisha kilimo cha hanga, kuongeza ajira kwa wanawake na vijana, kuanzishwa kwa Benki ya Ushirika ili kuwasaidia wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache tu niliyoyasema kuna haja ya kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuhakikisha mwezi Oktoba tunampitisha kwa kura nyingi za kishindo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)