Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza kabisa ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipatia uhai na afya niweze kuongea kwenye Bunge hili. (Makofi)
Pili, ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuipa kipaumbele sekta na Wizara ya Kilimo na tatu, ninampa hongera na pongezi nyingi Waziri Mheshimiwa Hussein Bashe, kweli amefanya kazi kubwa, tumekuwa wote pamoja kwa muda mrefu, lakini amefaya kazi kubwa kwenye Wizara hii ya Kilimo akisaidiwa pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Silinde; pamoja na Katibu Mkuu Ndugu Gerald Mweli, kwa kweli na Wizara nzima, wafanyakazi wote, sekta ya kilimo sasa hivi imekuwa juu inapaa. Tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu amekipa kipaumbele kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti; ninashukuru sana kuona bajeti ya utafiti imeongezeka, sasa hivi watafiti wanafanya utafiti wao kwa kufurahi kwa sababu angalau wanaona kitu walicho nacho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisema utafiti ninaungnisha hiyo hiyo inasema TARI ambayo wanatafiti mbegu na vitu vingine, ASA ambao wenyewe wanazalisha mbegu na TOSCI ambao wenyewe wanaona ubora wa mbegu, hivi vyote ukiviweka kwa pamoja unapata mbegu bora ambayo inakwenda kwa mkulima. Kwa hiyo, tunashukuru sana kwa jitihada kubwa ambazo mmeongezea bajeti kwenye taasisi hizi zote tatu ambazo zimeungana kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, tatu, nne, ninashukuru sana Serikali kwa ruzuku inayotoa. Tunampongeza Mheshimiwa Rais, kwani ametoa ruzuku kwenye mbolea, ametoa ruzuku kwenye mbegu hasa alizeti, mahindi, pamoja na viuatilifu. Tunashukuru sana wakulima wote hata wadogo, wadogo wanashukuru sana wanafurahia kupata ruzuku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, haya yote ni mawazo hasa mengine amebuni yeye na Mheshimiwa Rais yeye kwa pamoja tunawapongeza wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vituo vya zana za kilimo; vituo vya zana za kilimo ambavyo umesema kuwa matrekta yanaletwa pale na watu wanakuja kukodi ekari moja kwa shilingi 35,000, Mungu awape nini. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais hata mkulima mdogo mdogo ataweza kuchukua shilingi 35,000 na ataweza kulima angalau ekari yake akiweka mbolea, akafanya kanuni bora za kilimo anaweza akapata kwa ekari moja magunia zaidi ya 40 ya mahindi. Mungu awabariki kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazao mbalimbali; nikisema mazao mbalimbali yamepanda bei nianze na zao la kokoa ambalo tunalima katika Mkoa wetu wa Morogoro. Kilo moja imefikia shilingi ngapi mnajua? Imefikia shilingi 28,000 kilo moja ya kokoa, sasa kwa nini uende kulima mazao mengine. Kahawa na yenyewe imepanda mpaka shilingi 8,000, shiingi 6,000. Wakulima sasa hivi huwaambii nenda kulima, wanajituma wenyewe kwenda kulima kwa sababu soko lipo na bei ni nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Mkuu wetu wa Mkoa Mheshimiwa Adam Malima ambaye anasukuma pamoja na Wakuu wao wa Wilaya, pamoja na Maafisa Ugani kwa kazi nzuri wanayoifanya kwa upande wa kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema, kilimo Morogoro ni ghala la chakula. Morogoro ni ghala la chakula kwa sababu tunazalisha mpunga, sisi Mkoa wetu wa Morogoro ndiyo wa kwanza Tanzania. Tunashukuru sana Waziri Mheshimiwa Bashe, sekta ya umwagiliaji tumepewa skimu mbalimbali ambapo kwa kweli na wakulima wanajituma kwenye wilaya zote kwa wastani wanazalisha mpunga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, afisa ugani; maafisa ugani walikuwa wamesahaulika jamani, tunakushukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuwakumbuka. Tunashukuru sana Waziri Mheshimiwa Bashe, kwa kuwakumbuka na kuwapa vitendea kazi. Sasa hivi angalau wana vitendea kazi, mnawajengea nyumba mmesema ninyi wenyewe, wana vishikwambi, wana pikipiki, wana soil scanners ambazo zinaangalia afya ya udongo. Kwa hiyo, tunashukuru sana wafanye kazi, wafanye kazi kwa hivi vifaa wamevipata, kwa hiyo wamfikie hata mkulima mdogo mdogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye bajeti; bajeti imepanda imetoka kwenye shilingi bilioni 294 mpaka shilingi trilioni 1.2, kwa kweli haijawahi kutokea tunamshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa jambo hili kwa kuipa kipaumbele sekta ya kilimo na kuipandisha kuona kufikia hapo ilipofikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Tume ya Umwagiliaji, tumezunguka Tanzania nzima kuona umwagiliaji, mimi mwenyewe ninasema Tume ya Umwaguliaji inafanya vizuri, kuna scheme mbalimbali, kuna scheme kubwa ambazo Mheshimiwa Waziri umezitaja kwenye hotuba yako zinaendelea vizuri, Ndugu yangu Mndolwa ahsante kwa kazi unayoifanya pamoja na watu wako wa Tume ya Umwagiliaji, mnafanya vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushirika ulikuwa umekufa tunashukuru sasa hivi unafanya vizuri chini ya Mheshimiwa Waziri Bashe, hongera sana umefanya kazi kubwa Mheshimiwa Rais apewe maua yake kwa kuisimamia sekta ya kilimo na kutoa mchango mkubwa kwenye Benki ya Ushirika ambayo hii benki ya ushirika wataitumia wakulima wote wadogo na wakubwa, wanaweza kuitumia kwa sababu ni benki yao ambapo kuna vikundi mbalimbali vya wakulima tunashukuru sana kuona inakwenda vizuri ili mradi wachague viongozi wazuri, wawaongoze vizuri waende vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viwanda vya sukari, kuna viwanda vya sukari vinaenda vizuri...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja na Mwenyezi Mungu akubariki, abariki Wizara ya Kilimo na ambariki Mheshimiwa Rais na Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Bashe ubarikiwe na Mungu. (Makofi
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.(Makofi)