Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nami nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Kilimo. Ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa uzima na afya njema ambapo nimefanikiwa kupata nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Waziri wa Wizara hii ya Kilimo Mheshimiwa Hussein Bashe pamoja na Naibu Waziri wake Mheshimiwa Silinde pamoja na Wizara yote kwa ujumla, wakiongozwa na Katibu Mkuu na Naibu Makatibu Wakuu na watendaji wote kwa ujumla mnafanya kazi nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimpongeza sana Mheshimiwa Hussein Bashe na ninarudia tena kumpongeza, kwa namna ambavyo anafanya vizuri sana kwenye Wizara hii. Wizara hii ya Kilimo kiukweli kabisa umeitendea haki Mheshimiwa Hussein Bashe, mwaka jana ndiyo umetia fora moja kwa moja. Kwa sababu Siku ya Wakulima Tanzania Nanenane hapa Dodoma mambo uliyoyafanya ni makubwa sana, haijawahi kutokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, magari 40, matrekta 500, power tiller 800, pikipiki 6,444, vishikwambi 6,426, sare za wakulima yaani sijui niseme nini Mheshimiwa Hussein Bashe kwa kazi kubwa na nzuri unayoifanya, kwa kweli umeitendea haki Wizara hii. (Makofi)
Ndugu zangu Wana-Nzega Mjini hongereni sana kwa kumchagua Mheshimiwa Hussein Bashe kuwa Mbunge wenu, hamkufanya makosa na ninawaomba sana msikosee mwaka huu mumchangue kwa kishindo, mumpe kura za kutosha Mheshimiwa Hussein Bashe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami kwa sababu ni Mbunge wa Viti Maalum, nitafika huko ili niweze kumuombea kura kwa kumpigia magoti Mheshimiwa Hussein Bashe, ili aweze kurudi tena kwenye Bunge hili la Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameendelea kuwajali wakulima. Mheshimiwa Rais wetu alisikia kilio cha wakulima, mbolea ilikuwa ikiuzwa shilingi 150,000 akatoa ruzuku kwenye mbolea mpaka sasa hivi ni shilingi 75,000. Wakulima wanakushukuru sana Mheshimiwa Rais na shukrani yao utaiona tarehe 29 Oktoba, 2025 pale ambapo utapewa kura nyingi za heshima, za kishindo hasa kwenye Mkoa wangu wa Mbeya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kaka yangu Mheshimiwa Hussein Bashe anafanya kazi nzuri na njema sana, lakini Mkoani kwetu Mbeya Wilaya ya Rungwe kuna kilio kikubwa sana kaka, kuna kilio kikubwa mno, wakulima wa chai wamepata tatizo kubwa sana. Wakulima wa chai wa Kayuki, Chivanjee, Msekela na Masukuru kulikuwa kuna Kiwanda cha Chivanjee alipewa mwekezaji, mwekezaji huyo alikuwa akifanya vizuri sana Mo Dewji, alikuwa akifanya vizuri, lakini mwisho wa siku hatujui kulitokea nini. Kiwanda kilifungwa tangu tarehe 26 Machi, 2024; wakulima wale wanapata shida sana kwa sababu hilo zao limebeba watu wengi sana wa Wilaya ya Rungwe. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri Bashe, ninakuomba sana useme neno utakapokuwa unakuja ku-windup hapo, useme neno kwa ajili ya wakulima wa chai wa Wilaya ya Rungwe hasa wanawake wamekuwa wakipata shida mno. Walikuwa wakiamka saa 11 alfajiri wanajiandaa kwenda kuchuma chai pamoja na akina baba, lakini sasa hivi hawana kazi za kufanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba Mheshimwia Waziri Bashe, kulikuwa na kiwanda kile cha Katumba pale cha WATCO, kimefungwa rasmi tarehe 9 Mei, 2025, hawa wakulima wafanye nini? Na hao wakulima wa WATCO hapo wao tangu mwezi wa pili hawajalipwa fedha zao mpaka sasa, kiwanda kimefungwa na wao kwa kujidunduliza tu walinunua mbolea na hiyo mbolea hawana hata fedha za kulipa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba Mheshimiwa Waziri Hussein Bashe, kwa huruma yako wewe kaka una hekima, una busara ninakuomba utakapokuja kusema hapa useme neno kwa ajili ya wakulima wa chai wa Wilaya ya Rungwe. Mungu aendelee kukubariki na kukuongoza kama vile ambavyo tunaliombea Taifa hili la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nafasi hii uliyonipa acha nimpongeze sana Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan anavyolipenda Taifa hili la Tanzania kwamba liendelee kupata sifa kubwa. Ni juzi tu amefanya jambo kubwa ambalo limekwenda kumpitisha kiongozi wetu wa upande wa afya ndugu yetu Profesa Janabi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais wetu, kwa sababu anasimamia, anakuwa kipaumbele namna ya kuongea na mataifa mengine ili Watanzania tuweze kusikika kwa nafasi mbalimbali kwa kuwa ameendelea kuwa hapo, alianza na Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson ambaye alimpa nafasi kubwa kwa sababu alimuombea kule kwenye Mabunge ya Dunia akawa Rais wa IPU. Mungu akubariki sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajivunia sana na tunajisikia furaha na amani. Kwetu sisi ni dua kwako, Mwenyezi Mungu aendelee kukupa uzima na afya njema ili tufike salama Oktoba, 2025 mambo yote yaweze kwenda sawasawa kwenye kapu la kura ambazo utakuwa unazihesabu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa nafasi uliyonipa, Mwenyezi Mungu akubariki sana. Ninaunga mkono hoja Wizara hii na bajeti hii iende kupita sawasawa na Mheshimiwa Bashe alivyoomba, ahsante sana. (Makofi)