Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Josephine Johnson Genzabuke

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema, aliyenijalia afya na kunipa kibali cha kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kuunga mkono hoja na ninaunga mkono hoja hii kwa 100%. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwatumikia Watanzania. Hakika wote ni mashahidi, tumeona ni jinsi gani anavyojitaabisha usiku na mchana kwa ajili ya kututumikia sisi Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Bashe kwa moyo wa dhati kabisa, Mheshimiwa Bashe hongera sana, Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara yako. Kwa kweli Mheshimiwa Bashe, sote ni mashahidi wewe ni mnyenyekevu kwa kila mtu na unamsikiliza kila mtu, pengine ni kipaji ulichopewa na Mwenyezi Mungu, Mungu aendelee kukujalia hekima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niendelee kuishukuru na kuipongeza Serikali kwa namna ilivyoamua kwa dhati kabisa kukipandisha kilimo na kukipa kipaumbele, kwa sababu ni ukweli usiofichika, kilimo kimeajiri watu wengi sana, kimeajiri watu wengi sana wanawake kwa vijana na ukiangalia sasa hivi watu wengi wamejielekeza kwenye kilimo na hata Wabunge mliopo humu ndani wengi mna mashamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaendelea kuipongeza Serikali kwa namna ilivyoona kilimo kiweze kupewa kipaumbele kwa sababu kimeajiri watu wengi na bado wapo watu wanaomaliza vyuo wanarudi vijijini kwenda kujiajiri. Hivyo basi nipongeze kwa kazi kubwa ambayo Serikali imeifanya chini yako Mheshimiwa Bashe, kwa kupeleka mbolea ya ruzuku kwa wingi. Niombe tu mbolea iendelee kufika kwa wakati kwa sababu mvua za kwanza ni za kupandia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niendelee kuiomba Serikali ipeleke ruzuku kwenye mahindi, alizeti, mpunga na kwenye mbegu za muhogo, maeneo hayo nayo wanahitaji sana mbegu kwa sababu ukiangalia kwa mfano mahindi yanapatikana, lakini wakati mwingine bei inakuwa ni kubwa, kuna watu wengine hawawezi kuhimili bei hiyo. Kwa hiyo, tunaomba muendelee kupeleka ruzuku kwa wingi kwenye mbegu za mahindi, mpunga, mbegu za alizeti na mbegu za muhogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Mkoa wa Kigoma sisi zao letu la biashara ni pamoja na muhogo. Mheshimiwa Bashe nikuombe, mwaka juzi 2023, mwaka jana 2024 zao la muhogo limeporomoka sana kutoka kilo moja shilingi 800 kuja mpaka shilingi 200 wakati mwingine shilingi 300. Kwa hiyo, wakulima wanakata tamaa sana, tunaomba kama unavyofanya mambo mengine, uendelee kujitaabisha kutusaidia kututafutia soko la muhogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado mchikichi Kigoma unahitajika, tunaomba michikichi iendelee kupelekwa Kigoma ili wananchi waweze kupata mbegu zilizo bora waendelee kuzalisha zao hilo la mchikichi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali chini ya Mheshimiwa Rais na wewe mshauri kwa kuanzisha Benki ya Ushirika, benki hii itawasaidia sana wakulima, lakini mpeleke elimu ili watu waendelee kuelimishwa, wafahamu maana ya ushirika, waweze kuupenda ushirika na kuweka pesa zao kwenye ushirika na wakati mwingine sasa waanze kukopa kupitia kwenye benki yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, Mheshimiwa Waziri kule Kasulu kuna kampuni moja inaitwa Vod Sell, ilinunua tumbaku kwa wakulima, bado wakulima wale wanadai dola 208,503. Mheshimiwa Waziri, pesa hizo ni nyingi sana, tunaomba hao wakulima walipwe pesa zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu mmoja anadai kuanzia shilingi milioni 18, mwingine shilingi milioni 20 wengine mpaka shilingi milioni 15. Fikiria wanavyoshinda wanalima, wananyeshewa na mvua, wanajenga mabanda, lakini wameshindwa kulipwa. Tunaomba hao wenye Kampuni ya Vod Sell walipe pesa za wakulima mara moja. Mheshimiwa Waziri, nami kabla ya kuondoka kurudi Kigoma nitakuja ofisini kwako, ninaomba hiyo kampuni ilipe hizo pesa za wakulima mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dola 208,503 ndizo wanazodai hawa wakulima. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninarudia tena dola 208,503.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninarudia kuunga mkono hoja, lakini kwa kuleta kilio cha wakulima hao wanaodai pesa zao, ahsante. (Makofi)