Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninaungana na wenzangu kumshukuru Mungu kwanza, aliyetupa uweza, ametupa nguvu na mkono wake ulituatamia, leo tunasoma bajeti ya mwisho ya Bunge la Kumi na Mbili. Sifa na utukufu turudishe kwake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mambo aliyofanya kwa watumishi wa Serikali. Unajua mimi nikiamka ni watumishi, lakini kabla sijaenda huko ninakumbusha kidogo, nilikuwa mtumishi wa Wizara ya Fedha, wakati Tume ya Mipango inavunjwa watumishi wote tulichanganyikiwa. Kwa sababu, nilikuwa kiongozi wa wafanyakazi, nilitumwa nipeleke hoja kwenye Baraza la Wafanyakazi, wakati huo sijajua kama nitakuwa Mbunge, tuongelee kurudishwa kwa Tume ya Mipango, hatukufanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuja Bungeni nimeshirikiana na wenzangu kupaza sauti kuomba Tume ya Mipango. Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, hii ni bajeti ya mara ya pili tukiwa na Tume ya Mipango. Ukilinganisha bajeti za nyuma na bajeti hizi mbili ni mbingu na ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuja mpango wa maendeleo na bajeti vinaendana na hiyo ndio maana ya kuwa na Tume ya Mipango, lakini wakamkabidhi Waziri ambaye anajua kuchambua mambo. Mimi huwa namwambia Profesa Kitila yaani akishaanza mosi, ujue kinachofuata ni kitu cha mikakati. Kumekuwa na ushirikiano mzuri sana kati za Wizara ya Fedha na Tume ya Mipango, wanashirikiana kwa karibu sana. Ukiangalia mpango wa maendeleo, ukaangalia na bajeti, unaona hawa wataalam walikaa pamoja chini ya Mawaziri wanaonena jambo moja na wakatuletea bajeti ambayo ime-cover nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema hivi kwa sababu, nikianza na watumishi, kwa mara ya kwanza kwa miaka minne wakati naingia kuwa Mbunge wao humu watumishi walikuwa na miaka sita hawajapandishwa mshahara, lakini kwa miaka minne wamepandisha mshahara mara mbili. Mwaka wa Fedha 2022/2023 kima cha chini walikitoa kwenye shilingi 300,000 mpaka shilingi 370,000 sawa na 23.3%, lakini leo Mwaka wa Fedha 2025/2026 wamepandisha kutoka shilingi 370,000 mpaka shilini 500,000 sawa na 35.1%, sio jambo dogo na sio la kubeza. Niwaambie, watumishi wote wanasema Oktoba wao wana-tick, iwe mvua, iwe jua, kura zao ni kwa Mheshimiwa Rais kwa sababu, anawadai. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baraka walizofanya Mungu atawalipa. Kitabu Kitakatifu cha Biblia kinataja mistari ya kuwaenzi wazee na kuwatumia mara 100, tuwatumie wazee, tuwapende wazee, tuwasaidie wazee, tuwalee wazee. Leo wale wazee wastaafu wanaolipwa na Hazina, Naibu Waziri nimekusumbua sana, nilikuwa nakuja na wale wazee, lakini kila wakati alikuwa anawapa imani kwamba, Serikali itafanya na leo wamefanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupandisha kutoka shilingi 100,000 mpaka shilingi 250,000, sawa na 149.8%, sio jambo la kawaida. Bahati mbaya wakati Mheshimiwa Waziri anasoma bajeti aliruka kipengele chao, jirani yangu ni shahidi, simu zilikuwa zinaita hapa mpaka ninawawekea jamani niko Bungeni; “mbona Waziri katusahau na ulisema atatukumbuka?”
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipotoka nje nimewapigia nikawaambia, kiwango chenu kimepanda mpaka shilingi 250,000. Wale wazee wanasema wameamini hakika, kumbe mama kuwa kiongozi ni mlezi na anayejali. Ilikuwa ni miaka mingi sana hawajawahi kufanyiwa jambo la aina hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jumamosi tulikuwa na Mkutano Dar es Salaam na Vijana wa Temeke wanawaambia wana shaka na kura za Mama Samia kwa sababu, mikopo ya halmashauri ndiyo wanayotumia kununua bajaji, maguta na pikipiki. Leo wameenda wamewapunguzia ushuru, wamewagusa vijana wa Kitanzania, akinamama wa Kitanzania wamewagusa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wameenda kwenye Mifuko ya Jamii, Mwaka 1999 ndiyo tulibadilisha Sheria ya Kikokotoo. Kwa hiyo, wale waliokuwa wameanza toka miaka ya nyuma mpaka 1999 walikuwa hawachangii kikokotoo, lakini Serikali ikabeba, itawalipia na hili deni lilienda likataka kuangusha mifuko yetu, lakini leo ninaona wametoa hapo zaidi ya shilingi trilioni mbili kwenda kulipa deni hilo, si suala dogo, wameweza kuienzi, lakini hata waliokuwa na vyeti fake waliwalipa. Tunaishukuru sana Serikali hela waliyowapa si kidogo, imewasaidia kwenye maisha yao. Tuseme nini zaidi ya kurudisha ahsante kwa Serikali? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi uliopita nilikuwa naagana na Watumishi wa Serikali kwamba, sitaendelea kuwa Mbunge wa Wafanyakazi, walinipa tuzo, lakini niwaambie tuzo hii iende kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, iende kwa Baraza la Mawaziri. Mawaziri niliwasumbua sana na mambo ya watumishi, lakini hawakuniacha walikuwa na mimi kwa masuala ya watumishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaongea kwa uchungu sana, watumishi wa Tanzania walikuwa wanaumia sana, walikuwa wananyanyasika sana, lakini leo wamelipa madeni yao yote; wamelipa mishahara, wamewapandisha vyeo, Mungu awabariki sana Baraza la Mawaziri. Ninawaombea sana walio kwenye majimbo na Viti Maalum Mungu akawaguse wanaoenda kupiga kura wawarudishe, lakini mwenzangu wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Kitila, namwahidi iwe mvua iwe jua nitaweka kambi Ubungo, ili arudi na jicho la Mheshimiwa Rais limwone, ampe hii Tume na Wizara ya Mipango aendelee kufanya mambo yatakayosaidia nchi hii. Ninawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwaambia tuzo hii iwe ya Mheshimiwa Spika na wasaidizi wake kwenye Kiti pale; nilikuwa nikianza kuchangia mambo ya wafanyakazi, ukimwangalia Spika kama umechangia kitu cha maana huwa anacheka, ukiona ameshika kichwa kainama acha, hapo umeshapoteana. Kwa hiyo, nilikuwa nikianza kuchangia namwangalia, nikiona ametabasamu ninaendelea kukomelea mambo ya watumishi, lakini saa nyingine ananisaidia. Hata yeye alisaidia sana kwenye kuwaomba document watumishi wanapoenda kustaafu na leo wamejirekebisha. Sasa hivi wanaichukua kwa mfumo na mtumishi anapata pensheni yake muda mfupi baada ya kustaafu. Ninawashukuru na Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru wanawake wa Mkoa wa Dar es Salaam, mimi ni nani Janejelly, mtoto wa mnyonge, mkulima, ambaye nilikuwa sina jina, wanawake wa Dar es Salaam wakanipa jina. Ndiyo maana ninawaahidi na kuwaambia ninarudi, wasinichoke, wanitume sasa nikawafanyie wao kazi. Kwa watumishi nimefanya, sasa ninarudi kwao nikawafanyie kazi, niwalipe walichoniazima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza Watumishi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania maana inawezekana nisipate nafasi nyingine ya kuwapongeza. Watumishi wa Bunge Mungu awabariki sana, nimefanya kazi sehemu nyingi, nimefanya kazi Nishati, nimefanya kazi Wizara ya Fedha, kule kuna sifa ya kazi sana, lakini Bunge nimekuta sifa ya kazi na nidhamu iliyotukuka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sijawahi kuona mtumishi wa Bunge amekasirika na tunawakera saa zingine, lakini atakwambia Mheshimiwa samahani, unahitaji nini? Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtaona hata waliomo humu ndani Bungeni unaweza ukamwita, saa zingine huna sababu ya msingi, lakini unamnyooshea kikaratasi, anakuja na atacheka, ataondoka. Endeleeni hivyo hivyo na niwaambie, mtumishi wa Bunge akihama hapa akaenda Wizara nyingine kila mwaka atakuwa mfanyakazi bora. Wana nidhamu iliyotukuka, wana uvumilivu ambao umepitiliza, Mungu awabariki sana, lakini watuweke kwenye maombi yao, ili basi nasi turudi tuungane nanyi kwa sababu, tutawa-miss sana tusiporudi. Wanajua nilikuwa Kamishna wao, ninawapenda sana marafiki zangu sana, waniombee sana, ili nirudi tena tuendeleze gurudumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niseme tu ninaaga, lakini ninawaombea ninajua wote tutarudi. Mungu hajaacha kumwacha mja wake, wote tutarudi mahali humu. Mungu humpa ampendaye na humnyima ampendaye, usipopata usiumie, Mungu bado anakupenda na ukipata ufurahi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia muda huu kwa Mzee wangu Mkuchika, ametangaza hatarudi. Huyu ndiyo nilianzanaye kazi na siku ya kwanza niliyosema mshahara, aliniita akaniambia wewe bwana wewe mbona unakuja na speed kali sana bwana? Hayo si uje uniambie kule Wizarani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikamwambia hapana! Humu ndiyo nalindwa na ninachoomba ni mshahara wa watumishi, lakini aliniambia tutafanya. Bahati mbaya akaumwa, alivyorudi nikaendelea na Mheshimiwa Jenista, lakini kila Waziri niliyefanya naye kazi utumishi, leo hii ninapoaga hapa niko na Mheshimiwa Simbachawene, ninadhani ofisini kwake nilikuwa na kiti, pole sana kwa usumbufu. Ninamshukuru sana yote ilikuwa ni kuwatumikia Watumishi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)